Viongozi wa Dini na Hatma ya Tanzania

Viongozi wa Dini na Hatma ya Tanzania

Kwa kuongezea alichosema Mushobozi, naomba pia tukumbushane mchango wa hayati Papa John Paul wa pili kwenye nchi yake menyewe ya Poland! nadhani mtakumbuka kuwa wapolish wanamuona kama mwanzilishi wa mapinduzi ambayo hatimaye yaliangusha ngoma ya Russia mwaka 1989, na hivyo kuondoa ukandamizaji nchini mwake na duniani kwa ujumla..na huyo alikuwa ni kiongozi mkuu wa wakatoliki wote duniani!

Kwa hiyo Kada na Binti senti 50, msikwepe historia kwa kisingizio cha kuwaogopa watumishi wa Mungu!

Mbona wanawaita hao wanasiasa kwenye harambee zao? Kwa nini wakati fulani Makamba alikuwa maarufu sana kwenye harambee za kikristo? Si kwa vile ana 'karisma' ya kupiga domo, akisema watu wanatoa? so what is the goal here..is it not money, and then dini inakuja baadaye?

Nadhani tunapaswa kuwaambia viongozi wetu kuwa ni wakati wa wao pia, kama wanavowaita kwenye harambee za kuchangia ujenzi nk, basi wawaite kwenye 'harambee' maalum, safari hii, kuwaaambia wasemeee japo kanisani kama wanaogopa kusemea kwenye majukwaa ya kisiasa, kujibu au kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali za kisiasa zinazojitokeza kwao!

waende misikitini, wakae kwenye mimbari, wajibie huko! Labda hawatazomewa, lakini angalau wanachiwatakuwawamepata ujumbe

Kama Raisi alisemea 'kanisani' juzi hapa kuhusu 'wanasiasa wachochezi', huku akiongoza harambee ya kuchangia kanisa, nawaomba viongozi wa dini pia wawaalike waje waseme, hali ikichafukia humo misikitini/makanisani labda inaweza kutulizwa kuliko ikianzia pale jangwani!
 
Naungana na Bi. Senti 50 kusema Mzee Mwanakijiji umechemsha. Wako Makasisi wengi (eg. Padre Baptiste Mapunda) ambao mara kwa mara wanakemea maovu unayosema. Kama huwasikii ni kosa lako, na haikupi ruhusa kuwashutumu.

Akienda leo Kardinali Pengo Parokia ya Mlandizi akakemea maovu utamsikia? Hutamsikia, na utabaki kusema hakemei maovu.

Viongozi wa dini hawapashwi kuwa wanasiasa. Wana haki kuchagua ni lini na ni yapi waseme. Si vema kuwashutumu kwa hilo, bila kuelewa vizuri maadili yao ya kazi.

Kwetu sisi, kuwasemea hovyo viongozi wetu wa kiroho ni tusi. Na kama umeandika haya makala kwenye Gazeti la Tanzania Daima, basi umelikosea haki hilo gazeti. Makala kama hiyo hushusha hadhi ya gazeti.
 
Kwanini Yesu hakuwaheshimu viongozi wake wa dini na akathubutu kuwaita "viongozi vipofu waongozao vipofu"?
 
Kusema vibaya namna gani? Viongozi wa dini wamekuwa wezi wa sadaka makanisani na pesa za ujenzi wa majengi ya kanisa, wamekuwa wanajirusha na mabinti na wake za watu.Wajiweke mbali na mauvu na kuukemea uovu sio kukaa na kusubiri sadaka za waumini.
 
Naungana na Bi. Senti 50 kusema Mzee Mwanakijiji umechemsha. Wako Makasisi wengi (eg. Padre Baptiste Mapunda) ambao mara kwa mara wanakemea maovu unayosema. Kama huwasikii ni kosa lako, na haikupi ruhusa kuwashutumu.

Akienda leo Kardinali Pengo Parokia ya Mlandizi akakemea maovu utamsikia? Hutamsikia, na utabaki kusema hakemei maovu.

Viongozi wa dini hawapashwi kuwa wanasiasa. Wana haki kuchagua ni lini na ni yapi waseme. Si vema kuwashutumu kwa hilo, bila kuelewa vizuri maadili yao ya kazi.

Kwetu sisi, kuwasemea hovyo viongozi wetu wa kiroho ni tusi. Na kama umeandika haya makala kwenye Gazeti la Tanzania Daima, basi umelikosea haki hilo gazeti. Makala kama hiyo hushusha hadhi ya gazeti.

Hilo ndo tatizo letu waumini tulio wengi, tumewapa heshima kubwa na kuwa amini mno kama vile si binadamu wenzetu!

Bado ni binadamu kama sisi wakiwa wamebeba udhaifu wote, pale tunapo jaliwa hekima ya kuona mapungufu yao hatuna budi kuwakumbusha na pengine kuwakemea inapo bidi!

Haiingii akilini watu wenye jukumu kubwa la kukemea dhambi wakae pembeni wakisubili nani afunge paka kengele wakati wanaona taifa lina teketea kwa dhambi ya ufisadi!

Mkijiji hajawakosea heshima bali ametumia hekima aliyo pewa na maulana kuwakumbusha madhaifu yao ya kibinadamu ili watimize wajibu wao!
 
Ninapokaa chini kuwaandikia waraka huu wapendwa watumishi wa Mungu, ninajihisi kutostahili na kutofaa kusema nitakayosema. Mikono yangu yanitetema na vidole vyangu kama vina ganzi kwa hofu lakini moyo wangu unadunda kwa shauku. Kwenu nyote msimamao katika nyumba zetu za ibada na kuwaongoza watu wetu katika safari ya kiroho, ninyi ambao mnajua mmeitwa kumtumikia Mungu Mwenyezi katika makundi ya imani zenu mbalimbali, ninyi ambao watu huwaita “wahudumu wa Bwana” na Watendaji kazi katika shamba la Mungu, kwenu nyote Saalam!

Ninapozungumzia “wachungaji” simaanishi wale tu wa Wachungaji wa Kilutheri au makanisa ya Kiprotestanti au wale ambao wanaongoza parokia na sharika mbalimbali; na sina maana ya wale tu ambao ni viongozi wa dini ya Kikristu. “Wachungaji” ninaowazungumzia hapa ni wale ambao kwa maana ya msingi kabisa ya neno hilo, wanajukumu la kuchunga na kutoa mafunzo ya kiroho kwa waamini wao. Hapa najumlisha viongozi wote wa kidini wa dini zote na madhehebu yote, wale ambao jukumu lao la kwanza ni katika kuwaongoza watu katika mafundisho na maadili ya kidini. Wale wenye kukiri Imani ya Mitume na wale wenye kukiri Shahda, wale wenye kusimama makanisani na wale wenye kusimama misikitini. Nina maana ya wale wote ambao kimsingi wanachunga maisha ya kiroho ya watu kwa kutoa maongozo, maelekezo na mausia ya kiroho ili waamini wao waweze siku moja kufika mbinguni. Hawa ndiyo wachungaji ambao ninakusudia waraka huu.

Kwenu nyote Mashehe, Mapadre, Maimamu, Wachungaji n.k bila ya shaka mnafahamu wajibu wenu mkubwa katika maisha ya kiroho ya waamini wenu na bila ya shaka mmekuwa mkijitahidi kila kukicha kuwapatia waamini wenu mafundisho na maelekezo ambayo mna uhakika yatawasaidia kiroho. Hata hivyo ni kwa masikitiko makubwa niseme wazi kuwa kwa kiasi kikubwa mmewaangusha Watanzania. Sauti yenu haisikiki kama inavypaswa katika kuongoza “kondoo” wenu, na matokeo yake badala ya nyinyi kuwa katika kundi la wanaoongoza, sasa hivi mnajikuta mnafuata.

Ninayasema haya hasa baada ya kusoma Tamko la Baraza Maaskofu Katoliki lililotolewa hivi karibuni. Niliposoma tamko hilo nilijikuta natikisa kichwa kwa mashaka kwani walichotaka kukisema hawakukisema na wasichotakiwa kukisema walijaribu kukisema, na matokeo yake walitumia herufi na maneno mengi waliyoyapanga vizuri kwa lugha “endelevu” lakini bila kusema kitu! Ni ubutu huu ambao ninawaandikia ili muunoe na viongozi wengine wa madhehebu mengine ya dini watakapotoa tena matamko wafikirie vizuri.

Viongozi wetu wa dini mmekuwa butu! Mnameremeta kama kisu kwenye ala, na mnang'aa kama sime iliyoinuliwa. Mnapendeza kwa kanzu na majoho yenu na kwa hakika mnavutia mnapozungumza kwa maneno yaliyopangwa. Hata hivyo hamna tena makali ya kukata kwani mmekuwa butu kwa muda mrefu na sasa mmbakia kama ishara ya “kile kilichowahi kuwepo”.

Mlikuwa wapi wakati watanzania 900 walipokufa kwenye ajali ya MV. Bukoba? Mlikuwa wapi wakati wa ajali ya MV. Kilombero, ajali ya treni Dodoma, na ajali ya basi kule Singida? Leo hii Rais Joseph Kabila amemtimua Waziri wake wa Usafiri baada ya ajali nyingine ya ndege iliyoua watu zaidi ya thelathini. Hivi hapa Tanzania ni hadi watu wangapi wafe kwenye ajali zisizo za lazima ndipo wachungaji wetu mtaungana na wanaharakati kutaka viongozi goi goi wawajibishwe? Zilipotokea vurugu Mwembechai na baadaye mauaji ya kisiasa kule Pemba, mbona hatukuwaona mkiikemea serikali, vyama vya kisiasa na wananchi kwa ujumla na mkaliacha jambo hilo kwa watu wachache? Wakati serikali inanunua ndege ya bilioni 50, rada ya bilioni 50, magari mawili ya milioni mia mbili, na kuingia mkataba wa Richmond, wachungaji wetu mlikuwa wapi? Hata hili suala la sasa linaloendelea la Buzwagi na Karamagi, mbona mmechelewa kuamka na mnafumbua macho kama mliolazimishwa au kukatishwa usingizi?

Ninyi mnaojitambua kuwa ni watumishi wa Mungu, mbona mmekuwa kimya na mnagwaya mbele ya watawala wetu? Mbona hivi karibuni kiongozi mmoja wa ngazi za juu alitamka mbele ya viongozi wa dini kuwa taasisi za dini zinapojenga mahospitali n.k zinashiriki katika utekelezaji wa ilani ya CCM, mbona hamkukosoa, au zile hisia kuwa kanisa ni sehemu ya CCM zina ukweli? Kuna wakati lazima muwe mashahidi wa ukweli!

Wako wapi kina Sheikh Khalifa Bin Khamisi watetezi wa “mali” za waislamu? Je na wao wamekuwa kama CCM kuwa mali za Watanzania wote zikipotea kama zilivyopotea Benki Kuu haziwaumi, ila zile za Waislamu na za CCM ndizo huwauma? Iko wapi ile Shura ya Maimamu ambao kila baada ya muda wanatishia maandamano ili kuishinikiza serikali kufanya hili au lile? Mbona hadi leo hawajatishia maandamano kutaka kujua ukweli wa Benki Kuu, Buzwagi, Richmond, n.k ? Au ndio huo uongozi wa kidini mambo leo ambao wapendwa watumishi wa Mungu mnauendeleza? BAKWATA wako wapi wakati nchi yetu iko katika wakati mgumu?

Wako wapi wale wahubiri wa Injili, wahubirio miujiza? Yuko wapi Mchungaji Kakobe ambaye yuko tayari kukemea “mapepo” wakati watu wanatoana upepo? Ni lini ataacha kwa dakika chache kuhubiri miujiza na badala yake aje kuwajuza watu, kuhusu udhambi wa maisha ya kujikuza, na ya kutweza wengine? Haitoshi kuimba mapambio, haitoshi kusikiliza kasida, na haitoshi kushika vitabu vya dini mikononi, huku nchi na wananchi wanakosa mwelekeo katika maisha yao ya kawaida. Sala nyingine za miujiza zinaweza kuwa si za lazima endapo watu watakua na matumaini wanapoenda mahospitalini, wanapata huduma nzuri serikalini n.k

Wapendwa wachungaji wetu, ninahofu kuwa inawezekana hamkemei na kupiga vita uovu wazi wazi na pasipo utata kwa sababu ninyi nanyi mnanufaika kwa namna moja au nyingine na uongozi mbovu na tabia za kifisadi. Je yawezekana ni kwa sababu baadhi yenu wamelala kitanda kimoja na ufisadi, wakijifunika mablanketi ya unafiki, huku wanajipepea upepo wa uzandiki? Inawezekana ni kwa sababu baadhi ya miradi yenu (binafsi na vinginevyo) isingewezekana isipokuwa kwa baraka za “walio katika viti vya enzi vivunjikavyo”?

Ni wazi mara nyingi mna hofu ya kutotaka kuichukiza serikali. Tunatambua kuwa mkipiga kelele sana viongozi watawanyoshea vidole na kuwaonya, na watawaambia “fanyeni kazi zenu za dini, msiingilie serikali” Tunajua hilo linaweza kuwafanya mgwaye, kwani wanaweza wakaanzisha uchunguzi dhidi yenu au kujaribu kuwaumbua kutokana na madhaifu yenu mbalimbali kama ilivyomkuta Askofu Ncube wa Zimbabwe. Je ni hilo ndilo mnaloogopa, kiasi cha kwamba mikataba mibovu inasainiwa na hakuna mwenye ujasiri wa kuitisha Waziri Karamagi ajiuzulu au awajibishwe?

Tunafahamu pia kuwa wakati mwingine hamna ujanja isipokuwa kula sahani moja na watawala wetu alimradi mkiwaalika kwenye harambee zenu watokee, vinginevyo mnahofu kuwa michango yenu na makusanyiko yenu hayatafanikiwa. Lakini kama kilichotokea Burma hivi karibuni ni fundisho, basi kuna wakati ambapo viongozi wa dini ni lazima wafanye uchaguzi aidha kufumba macho na kuendelea kufurahia hisani ya watawala, au kuwa majasiri na kuongoza mapambano ya kifikra ili kuamsha dhamira za wananchi wetu ili tuweze kujenga taifa lile la kimaadil mnalolihubiri kila siku.

Ni kiongozi gani kati yenu ambaye atakuwa tayari kusimama juani, kuandamana, na kushika mabango na sisi wanakijiji kuihoji na kuikemea serikali? Ni nani kati yenu ambaye atakuwa tayari hata kwenda kifungoni katika harakati za kutetea haki za raia na wananchi? Itakuwa ni siku ya uamsho mkubwa tukimuona Kardinali Pengo mtaani, Mufti Simba mtaani, kina Kakobe, Mwakasege, Mwaipopo na wengine mtaani wakiongoza kelele za kutaka serikali iwajibike. Katika Tanzania ambayo viongozi wa dini na serikali hawawezi kufanya kazi pamoja isipokuwa hadi wakubaliane, na ambao hawawezi kupingana bila kuvunjiana mahusiano, ni vigumu kwa viongozi wetu wa dini kwenda kinyume na serikali na hicho ndicho kiini cha ubutu wenu.

Niwakumbushe kuhusu kiongozi mwingine wa dini ambaye alionesha kilele cha “Uchungaji Bora” siyo tu kwa kwenda jela na kufungwa, bali kutoa uhai wake mbele ya risasi muuaji. Dr. Martin Luther King Jr, alipokuwa amefungwa kwenye jela ya Birmingham kule Alabama Marekani, baadhi ya viongozi wa dini walimshangaa kwanini amekuwa anapiga kelele sana, na walimshauri apunguze makali yake kwani yeye ni kiongozi wa dini. Akiwa kifungoni, Dr. King aliandika barua yake maarufu ijulikanayo kama “Barua toka Jela ya Birmingham” (Letter from Birmingham Jail) ambayo ndani yake alieleza ni kwanini yeye kama kiongozi wa kidini hakuweza kukaa kimya. Na hata alipouwa kule Memphis, alikuwa tayari moyoni amejua kuwa ameshafika “kilele cha mlima”!

Alisema jambo moja ambalo natumani litawasha moto ya uzalendo na kusababisha mlipuko wa utumishi wa umma ndani yenu. Alisema “ukandamizaji mahali popote, ni tishio la haki mahali pote.” Haiwezekani viongozi wa dini wakakaa katika kisiwa cha mahekalu yao, huku watu wanataabika, wananyimwa haki au kwa namna moja au nyingine kufanywa duni. Ndio maana ninawauliza, mlikuwa wapi wakati vijana zaidi ya ishirini wa Kitanzania wamekwama Ukraine na kupigwa na ubaridi nje ya ubalozi wa Uingereza kisa serikali imejifanya mbabe? Mbona hamjauliza hatima yao ikoje? Na kwa nini hamkuibana serikali kutoa majibu ya kina badala ya majibu ya kibabe iliyoyatoa?

Leo hii mnaposimama na kutuhubiria maadili, hivi mnaweza kweli kusimama mbele ya Mungu mnayemtumkia na kusema ninyi ni mawakili wazuri wa maadili mnayotuambia tuyafuate? Wapendwa viongozi wa dini, wakati uko mbioni na sasa umefika ambapo mnatakiwa mfanye uchaguzi, tena uchaguzi wa haraka na wa makusudi. Nina mapendekezo machache kwenu kufikia uchaguzi huo.

Kwanza kabisa mtakapotoa matamko mengine huko mbeleni na hasa yale yaliyokusudiwa kutuma ujumbe kwa watawala wetu, acheni kuzunguka mbuyu, semeni mnachotaka kusema badala ya kutumia maneno mengi kutosema kitu! Kuweni kama Yohana Mbatizaji (Nabii Yahya A.S) na watangazieni watawala wetu kwamba wakati wa toba umefika na ya kuwa shoka limekwishainuliwa juu ya shina! Pili, vunjeni hii ndoa haramu ambayo mlijifungisha na watawala wetu na muwe huru kweli kweli. Leo hii mnashindwa kukemea maovu moja kwa moja kwa sababu mnaowakemea ni watu ambao wanawanufaisha!

Ndio maana leo mmekuwa bubu kukemea tabia ya Rais kufanya biashara Ikulu, na mmekuwa bubu mabilioni ya fedha kupotea Benki Kuu, na kwenye taasisi mbalimbali na halmashauri mbalimbali nchini. Mnashindwa kunyosha kidole kwani mkinyosha kimoja mnaogopa vitatu vinawaelekea nyinyi wenyewe na gumba linashuhudia mbinguni! Mnatetemeka mbele ya saluti na mnagwaya mbele ya vimulimuli!

Na mwisho, muwe tayari kusimama upande wa haki si kwa matamko yasiyokwisha na mausia yasiyokoma bali kwa hatua dhahiri na za makusudi. Muwe tayari kufanya kile ambacho Yesu wa Nazareti (Nabii Issa Bin Maryam A.S) alikisema kuhusu Mchungaji Mwema kuwa “Mchungaji Mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake”. Kuna siku (Mungu aiepushie mbali) ambapo Taifa letu litapitia ile “Saa ya Mjaribu” na mtatakiwa wakati huo kuchagua uhai wenu au hatima ya kondoo, natumaini mtafuata mifano ya wale walioenda mbele yenu, mifano ya kina Oscar Romero, Martin Luther King, Malcom X, na watawa wa Kibudha kule Burma ambao wiki chache zilizopita baadhi yao wamekwenda kwenye vifo vyao wakitetea haki za wananchi wenzao. Siku ambapo Taifa lenu litawaita kutoa sadaka kubwa mtakuwa tayari au mtaandika barua nyingine ya kichungaji au kuitisha vyombo vya habari?

Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu mnayemtumikia mpate ujasiri wa kusimama kama manabii na kunyosha mikono ya haki mbele zake, na kuwaongoza watu wetu siyo tu katika “malisho ya majani mabishi” ya mbinguni, bali katika kupata mana itokayo mbinguni hapa hapa duniani kwanza. Ni matumaini yangu hatamjaribu kujenga ufalme au paradiso mpya mbinguni bali mtaanza kushiriki katika kujenga paradiso ya Bongo hapa hapa duniani! Msipofanya hivyo, kama kile kinachowakuta CCM leo na nyinyi mjiandae kitawakuta, nacho ni kuwa mkianza kutuyeyusha na kutupiga soga za kizamani, Watanzania watawahesabu kuwa na ninyi hamna mpango (you'll become irrelevant) . Natumaini, hilo halitatokea. Myakumbuke maneno ya Nabii Yeremia kuwa “Ole wenu Wachungaji, wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu” Yer. 23.1

Ni mimi msafiri mwenzenu katika safari ya Kiroho,

mwanakijiji -at-jamboforums.com


....Mzee mwanakijiji umetoa mada safi sana sasa sijui kama Waheshimiwa mawebofya na kujionea nini maoni ya wafuasi wao?
Mimi nikileta kumbukumbu zangu hasa wakati wa kampeni niliwahi kusikia kuwa mzee JK "alikuwa ni chaguo la Mungu" kutokana na maelezo ya Viongozi wetu...

Hili lilikuwa Jambo la kutafuta "Cheap Popularity"..kwa viongozi wa Dini kuwa na wao wamewakumbuka wakumbwa hapo watakapopita wawakumbuke katika enzi zao.....

Matokeo ya Viongozi wetu wa madhehebu kutokutetea haki na kupiga vita rushwa na wizi ni hapo Taifa zima la Mungu linapoangukia kuzikanyanga Amri kumi.... amri sita ...nguzo tano.... na mengineyo mengi.

Hata pale Viongozi wenzao wanaume waliopoamua kufunga Ndoa sijasikia jitihada za makusudi toka kwao kuwatenganisha na huku tunaambiwa ile in dhambi sasa kweli ya Buzwagi na BOT..yatapata kukemewa kama lile limebaki...

Katika Dunia Hii sijui safari yetu ya kuelekea katika uzima ule wa milele itakuwaje?.........

Hebu fikiri kidogo hawa waliotajwa kuwa ni wala rushwa na
'Mafisadi" na wao wanazo DINI!!! na wanasali na kutoa sadaka kubwa kubwa na kuchangia kanisa fedha zile zile zilizopatikana Buzwagi na BOT.... na hapo hupewa baraka tele na sisi kuambiwa tuige mfano huu wa kujitolea lakini kutoka wapi....

Ukiangalia bei za mazao yetu wakulima asilia 80% hoi.....

Basi hayo ndiyo mambo yalivyo katika safari yetu hii ya kuelekea katik amaisha ya umilele...

Asante .....
 
comrade mwanakijiji!

Kwanza nikupe hongera sana kwa kuibua issue ambayo imekuwa inanisumbua kwa siku kitambo. Umenikumbusha suala zima la 'liberation theology' which focuses on Jesus as not only the redeemer but also the liberator of the poor. Ni nini wajibu wa kanisa/taasisi za dini? The mission is to bring justice to the poor and the oppressed, particularly through political activism. Sala pekeyake hazitoshi!

Taasisi zetu za dini na viongozi wake katika kukabiliana na suala la umaskini wameishia tu kugawa unga na maharage 'kwa walio maskini' bila kujihusisha na tatizo la ki-mfumo lilalosababisha mamilioni ya watanzania waendelee kuwa maskini.

The rev Martin Luther King Jr hakuishia kutoa tu hotoba...he had to organise politically! Karibu kabisa na nyumbani africa tunao mfano mzuri wa Bishop Desmond Tutu. Huyu sio askofu wa kawaida, kupambana na makaburu kama alivyofanya, na kuendelea kutetea haki za wanyonge hadi leo sio jmbo la mchezo.

Na siyo wakristu peke yao. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (circa 1979) ni mfano bora kabisa wa 'liberation theology' ambapo viongozi wa dini walionyesha kukwerwa na vitendo vya ufisadi, dhuluma na ubadhirifu ulikuwa unafanywa na Shah wa Iran akisaidiwa na wamarekani.

Hata mapinduzi ya Cuba, yaliyomuondoa Dikteta Batista madarakani yaliongozwa na castro kwa kuungwa mkono kwa hali na mali na makasisi wa kanisa katoliki (The Jesuit Fathers) who trained castro at Dolores and owned several other catholic schools in cuba that were fiercely nationalistic and anti- american.

Bado Tunamkumbuka Bishop Alexander Muge wa Kenya ambaye alikuwa kinara wa kudai mfumo wa vyama vingi...hatimaye Moi alihakikisha anauawa. Pia hapo jirani yetu Congo, alikuwa ni Cardinal Pasinya na kanisa waliosimama kidete kupinga ubadhirifu na udhalimu wa mobutu consistently! Viongozi wa upizani kama Nguza, Tshisekendi, Bemba kwa nyakati tofauti waliingia ubia na mobutu kuifilisi nchi in the spirit of if you cant beat them join them.

Back to Tanzania. Tunategemea kwamba Baraza la Maaskofu, CCT, BAKWATA wawe mstari wa mbele kabisa katika kupinga dhuluma na ubadhirifu. Lakini ndio hao hao kila kukicha wanakabiliwa na tuhuma za kufuja mali ama z kanisa ama za msikiti. Sidhani kama hawa ni watu wa kutegemewa.

Viongozi wetu wa dini wametulia kwenye mahekalu yao, wakiendesha magari ya kifahari kama wabunge wetu, in short wanakula kuku kwa mrija na hawaoni sababu kwanini 'sytem ibadilike', kwani wamekaribishwa kula meza moja na watawala.

Nuff Respect kwako mwanakijiji.
 
hata yesu alitoa kodi kwa serikali ya Kaisari, ndiyo maana aliwalaumu watoza ushuru na wanasheria wanafiki maana yake aliona fedha yake ilikuwa inatumika vibaya.

sasa iweje viongozi wa dini wanaotoa kodi kwa serikali ya Kikwete wakae mabubu pale ela na sheria za nchi zikitumika vibaya?

kama viongozi wanapigia kura viongozi wanchi iweje waambiwe wakae kimya na wakubali?

kama yesu alisema,"duniani mtakutana na masumbuko mengi, ila jipeni moyo, mimi nimeyashinda, nanyi mtayashinda". kwa nini wayaogope masumbuko hayo, ya kulaumiwa na kupelekwa jela na hata kufa kama yesu.

wana JF nikosoe nikikosea; yesu alibeba msalaba begani na kusulubishwa nao; je unaweza kujilinganisha naye eti sababu unavaa msalaba mkubwa na mrefu njiani? au umeuweka juu ya kiti unachokalia kanisani kama njia ya kujisulubisha na kumfata yesu. la hasha.....huko ni kumsulubisha mara mbili bwana yesu. tunataka matendo

ni mara ngapi SiSiEM iliidhinisha dhambi ya Takrima, na Viongozi wetu wakakaa kimya.si mliona. eti hawataki kuikosoa serikali.....wanataka serikali isiwachukie. lakini yesu si alisema serikali(ulimwengu lazima uwachukie?.

yesu alisema, ulimwengu lazima uwachukie wote waliowangu. ulimwengu ukiwapenda ninyi ni wana wa ibilisi, na mkiona umewachukia basi ninyi ni wa Mungu.

NAWAULIZA WALE WALIOMPINGA MWANAKIJIJI,

1. IPI NI AMRI KUU KULIKO ZOTE, SI NI UPENDO?......SASA UTASEMAJE KUWA UNAMPENDA MUNGU LAKINI UNAMCHUKIA RAFIKI YAKO?. MBONA HAWA WACHUNGAJI WANAWACHUKIA AKINA kARAMAGI KWA KUTOWAAMBIA UKWELI ILI WAACHE DHAMBI YAO NA WAMRUDIE MUNGU ILI WAUONE UFALME WAKE

2. HIVI AMRI ZA ULIMWENGU ZINAWEZA KUZIDI AMRI ZA MUNGU?........JE SERIKALI INAWEZA KUTUNGA SHERIA ZA KUWALIMIT HAWA VIONGOZI KITU GANI WAFUNDISHE NA KINGINE WASIFUNDISHE NA WAKAKUBALI.
 
sehemu fulani inasema usimnyoshee mkono wako "mpakwa mafuta wa Bwana" ninyi ni nani kufanya hivyo!? Vinginevyo na nyini muwe wachungaji na mashehe tuwaone kama mtakuwa na ujasiri huo.

shukrani.
 
sehemu fulani inasema usimnyoshee mkono wako "mpakwa mafuta wa Bwana" ninyi ni nani kufanya hivyo!? Vinginevyo na nyini muwe wachungaji na mashehe tuwaone kama mtakuwa na ujasiri huo.

shukrani.

unakumbuka ilikuwa katika 'context' gani, LOL,..na je kilimpata nini baadaye huyo 'mpakwa mafuta wa Bwana' hata kama hakunyooshewa mkono wakati ule ule?
 
Yesu alisema kama wao watakaa kimya atayaamsha mawe nayo yatasema.

Mwanakijiji ni jiwe lililoamshwa kusema.

Viongozi wa dini ni jukumu lao kukemea dhambi na maovu yote bila kujali yametendwa na nani hayomaovu, hapa kwetu maovu yakitendwa na watu wa hali ya chini wanakemewa sana ila yakitendwa na viongozi hakuna wa kuwakemea ,

Kumbukeni mbele za muumba wote tutakuwa sawa na hakuna atakayekwenda na kuingia kwa sababu ya cheo chake hapa duniani ila wote tutahukumiwa kulingana na matendo yetu ya hapa ulimwenguni.

Kama MUNGU aliweza kumkataa saul asiendelee kuwa mfalme aliyechaguliwa na wana wa israel kwa nin i basi asiweze kumkataa JK aliyechaguliwa na watanzania?

Wana wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa........
Ole wenu ninyi muangamizao taifa langu asema bwana wa majeshi maana iko siku sio mbali mtalia na kusaga meno.

Mwanakijiji timiza wajibu wako wa kuwakumbusha viongozi wa kiroho kuwa kama wataacha miili hii iendelee kuteseka kwa wao kukaa kimya ipo siku muumba atawadai .
 
Nasikia Baraza la Makanisa wameitikia wito na sasa wametoa Waraka wa Kichungaji... sijui kama ni kweli au wanauchanga huo na ile barua ya TEC?
 
Askofu Kilaini: Kikwete ameelemewa na mafisadi

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini, anasema baadhi ya viongozi wa serikali wanapokea pesa kutoka kwa wawekezaji wa nje, na hivyo kumfanya Rais Jakaya Kikwete awe na wakati mgumu katika kuongoza vita dhidi ya ufisadi wa kimataifa.

Askofu Kilaini aliiambia Raia Mwema katika mahojiano maalum, yaliyofanyika wiki iliyopita, kwenye ofisi yake iliyoko katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.

Alisema kwamba anamwonea huruma Rais Kikwete kwa kuwa lengo lake jema, la kupambana na rushwa kubwa au ufisadi wa kimataifa, linahujumiwa na baadhi ya viongozi walioko chini yake, wenye dhamana za kusaini mikataba na wawekezaji wa nje, ambao hupewa pesa nyingi ili kuwapendelea wageni hao.

Alisema kwamba wawekezaji hao wa kigeni huja nchini na pesa nyingi kwa lengo la kuwekeza, lakini huwa na malengo mengine zaidi na hivyo kuwahonga pesa baadhi ya viongozi walioko madarakani, ili walinde maslahi yao.

"Wanakuja na vitu vyao na mapesa mengi sana. Sasa wanapofika hapa wanayatumia mapesa haya kuwapa viongozi walioko madarakani.

Viongozi wa aina hii, ambao ndio walipaswa kumsaidia Rais Kikwete, ndio hao hao wanakuwa wa kwanza kumkwamisha.

"Hao ndio wanaofanya dhamira nzuri ya Rais Kikwete, ya kupambana na rushwa hii kubwa, iwe ngumu kuitekeleza. Inabakia tu kusikia kelele za rushwa kwenye mahakama zetu hizi ndogo, ikiwahusu watu wadogo.Hii haitoshi," anasema.

Kilaini anasema kwamba, ufisadi huu wa kimataifa (rushwa kubwa) unalindwa sana na viongozi hao waliohongwa, kiasi kwamba mtu akijaribu kulinda maslahi ya taifa, hushurutishwa na wakubwa wake kwamba anapaswa kunyamaza.

"Ufisadi wa kimataifa, ambao ndio unaolisumbua taifa hivi sasa, unalindwa sana na walioko madarakani. Mtu akijaribu kuingilia kati anaambiwa 'nyamaza' na walioko juu yake. "Kwa hiyo serikali yetu ina kazi kubwa sana, na hasa Rais wetu Kikwete, ambaye ameonyesha moyo wa kutaka kupambana na tatizo hilo.

Ana kazi kubwa kwa sababu kuna watu wanashirikiana na wawekezaji hawa wa nje ili kujinufaisha wao. Ni kazi ngumu sana kwake. Mafanikio yako mbali sana nasi."

Askofu anasema kwamba vita dhidi ya ufisadi wa kimataifa inakuwa ngumu sana kwa sababu mikataba yenyewe ina usiri mkubwa, kiasi kwamba hata wale ambao wanatarajiwa kuwa wa kwanza kuupiga vita, wanajikuta hawana taarifa mapema kutokana na mazingira ya kificho.

"Wale ambao wanapaswa kuwa wa kwanza kupiga vita suala hili, na wenye dhamana hiyo, wanashindwa kupata taarifa na hata wanapokuja kuzipata, wanakuwa wamechelewa sana na mambo yamekwisha kufanyika na kuleta athari.

"Kutokana na usiri huu, kazi ya kupigana vita na ufisadi inakuwa ngumu sana. Hapa ndipo dhamira ya Rais Kikwete inakuwa vigumu kutekelezeka.

Hata hivyo, Askofu Kilaini anasema suala la ufisadi wa kimataifa halikujitokeza wakati wa utawala wa Rais Kikwete, bali lilianza kujitokeza wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu, wakati Rais Benjamin Mkapa alipofungua zaidi milango ya uwekezaji wa nje.

Mara kadhaa wabunge wamekuwa wakilalamika ndani ya Bunge, kwamba mikataba hiyo ingekuwa inawekwa wazi mbele yao, lakini upande wa serikali umekuwa ukipinga dhana hiyo kwa madai kuwa mambo mengi ni ya siri baina ya wale wanaoingia kwenye makubaliano ya mkataba.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni, Rais Kikwete alionyesha kuguswa na mikataba mbalimbali na hivi karibuni amebainisha kwa kusema kwamba mikataba aliyoizungumzia wakati ule ilikuwa ni ile kati ya serikali na makampuni ya madini na tayari amechukua hatua kwa kuunda tume ya serikali na baadaye kamati ya kupitia upya mikataba ya madini.

Hata hivyo, Mkapa alipoingia madarakani kwa 'gia ya Mr Clean' aliunda Tume ya Kero za Rushwa mara tu alipoingia madarakani, tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, lakini matokeo ya tume hiyo ya kihistoria hayajaonyesha kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Badala yake imekuja kubainika kwamba kipindi cha utawala wa awamu ya tatu kilisheheni rushwa kubwa kubwa ambayo imeliingiza taifa katika matatizo makubwa.

Kabla hata ya kuanza kwa kipindi cha pili cha utawala wake, Mkapa alijiingiza katika biashara akiihusisha familia yake na baadaye mawaziri wake na mfano maarufu ni ule wa kujihusisha kwake na ununuzi wa mradi mkubwa wa mkaa wa mawe wa Kiwira.

Mkapa kupitia kampuni yake ya ANBEM Limited alianzisha kampuni (kabla ya kujitoa) iitwayo TANPOWER kwa kushirikiana na kampuni ya Waziri wake, Daniel Yona, kampuni iliyonunua hisa za mradi wa Kiwira, mauziano ambayo yamezua gumzo kubwa hasa ikizingatiwa kwamba kwa wakati huo wote walikuwa madarakani kama Rais na Waziri wa Nishati na Madini.

Hivi karibuni, wanasiasa wa kambi ya upinzani na zaidi Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, waliibua kile kilichoitwa 'orodha ya mafisadi' ambayo pamoja na mapungufu yake, iliibua mjadala mkubwa katika siasa za Tanzania kiasi cha kuwachanganya viongozi na watendaji wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Tuhuma hizo, mbali ya kutaja majina ya baadhi ya watu, ziliibua hoja kadhaa ambazo baadhi zimejibiwa na baadhi hadi leo hazijatolewa maelezo, angalau ya kubabaisha. Baadhi ya mawaziri na watendaji walitishia kwenda mahakamani lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi za kufunguliwa kesi mahakamani.


Source: Raia Mwema
 
Viongozi wa dini kwa unafiki tu??

Sasa hapa we Kilaini si useme ukweli tu!!

Raisi kama anaangushwa na mafisadi walioko chini yake wanao kula rushwa toka kwa wachotaji wa mali zetu, kwanini asi wawajibishe wakati uwezo huo anao???

Hapa ni uswahili wa pwani kujuana kwa vilemba, raisi ndo kinara akiwatumia hao swahiba zake, tuwaonao na kumuacha yeye pembeni kama vile ni malaika! Na ndo maana hawagusi na hafanyi chochote!

Kitakacho tukomboa watz ni sisi wenyewe wala si Jk wala swahibazake, pale tu tutakapo fanya kweli kwenye masanduku ya kura na kukata huu mzizi wa umwenzetu na kulindana.. na himaya za kitawala zilizo dumu takribani nusu karne sasa,ndo tutakapo jikomboa. Pale tu tutakapo pata mawazo mapya na damu mpya tukajinasua kwenye mawazo mgando yaliyo tufikisha hapa tulipo!vinginevyo mpaka Yesu arudi maisha bora kwa kila mtanzania zitabaki ndoto za mchana!
 
Wakinyea kazi watu waliopo chini ya JK (na ambao ni chaguo lake) yeye anaajibika. Kiongozi mzuri hateui wasaidizi waovu wengi hivyo.

Naona Mhashamu Askofu Kilaini ameogopa kumhusisha JK kwenye yale anayohusika nayo. Baadhi yametajwa kwenye ripoti ya Slaa. Ujasiri kama huo anao Slaa peke yake?
 
Wakinyea kazi watu waliopo chini ya JK (na ambao ni chaguo lake) yeye anaajibika. Kiongozi mzuri hateui wasaidizi waovu wengi hivyo.

Naona Mhashamu Askofu Kilaini ameogopa kumhusisha JK kwenye yale anayohusika nayo. Baadhi yametajwa kwenye ripoti ya Slaa. Ujasiri kama huo anao Slaa peke yake?

Ndo maana nasema ni unafiki,
Mtu kama huyu anapaswa aiiite a spade a spade not.., anapaswa amueleze ukweli kwamba kama ahusiki ajipambanue nao kwa kuwa wajibisha! lakini kuwakumbatia manake ni mwenzao!.. hiyo ingempa message kubwa Jk,

Na watu kama hawa ambao jamii ina waheshimu wasipo sema kweli nani aseme?? Slaa tu??

Na si hivo tu, wao pia huo ni wajibu wao kama viongozi wa kiroho na maadili ya jamii!! Ina maana maadilia ya dini yake yanasema uwe mnafiki?? usiseme ukweli kwa ajili ya kumplease mtu??
 
Askofu Kilaini analeta siasa za dini. Mwambie Kikwete unahusika vinginevyo wafukuze hao mafisadi uliowateua. Hivi kweli kawateua yeye mwenyewe halafu wanaiangamiza nchi nayeye amekaa tu anaangalia! naye si mhusika? maana hao ni mawakala (wasaidizi)wake.
 
Kilaini,
Ya Kaisari mpe Kaisari, na ya Mungu mwachie Mungu. Ndio nyie ambao mlisema kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu mwaka 2005 wakati wa kampeni,kwa hiyo apewe kura, leo hii mnatamka vingine tena!
 
Namsifu Askofu Kilaini kwa ujasiri huu, sikumbuki lini nilimsikia akizungumza siasa kwa boldness aliyoonesha hapa. Mzee Pengo ndie tuliyemzoea ni mwanasiasa (wa CCM), lakini si huyu mwenzie. Natumaini Baba Askofu Kilaini hajaacha mwanya wa kusababisha yamkute yale ya Baba Askofu Pius Ncube wa Bulawayo! Mchezo mchafu huu baba, usichezee tope ilhali umevaa vyeupe!
 
Back
Top Bottom