12/25/2007
Maaskofu: Ufisadi ni janga la kitaifa
* Wasema unaipeleka nchi pabaya
* Washauri mikataba ya madini ifutwe
* Wasema haiwanufaishi Watanzania
* Wawahimiza wananchi kufanya kazi
Na Waandishi Wetu
Mwananchi
MAASKOFU wamesema ufisadi, rushwa, mikataba feki ya kuuza rasilimali za nchi na wimbi la wageni wanaoingia nchini na kuhodhi mali na ajira za wazawa ni janga linaloendekezwa na kuachwa likiwatafuna Watanzania.
Maaskofu hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti kwenye mkesha na ibada ya maadhimisho ya Sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, katika makanisa tofauti nchini juzi na jana.
Akihubiri katika misa ya mkesha wa Krismasi juzi usiku, uliofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa alisema utajiri wa madini wa nchi unasombwa na wageni huku raia wakibaki wanaogelea kwenye lindi la umaskini.
Askofu Mokiwa alisema alitembelea baadhi ya migodi na kushuhudia jinsi utajiri wa nchi hii unavyowanufaisha wageni, huku raia wakiendelea kutaabika.
Alisema suala hilo ni nyeti na linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la pekee na viongozi wa kitaifa.
"Ningekuwa na uwezo, ukiniuliza leo kuhusu mikataba ya madini, nitakwambia ifutwe mara moja na iandikwe upya ili kuwanufaisha wazawa...," alisema.
Aliongeza kuwa hata kwenye Biblia imeandikwa kwamba, mgeni asinywe mvinyo kwenye shamba ambalo hajashiriki kulitayarisha, hivyo akahoji iweje, wageni wafaidike na madini ilhali wazawa wakiendelea kutaabika.
Askofu Mokiwa alisema suala la madini linatakiwa liangaliwe kwa jicho kali ili liweze kupatiwa ufumbuzi kusudi madini yawasaidie wananchi kuondokana na umaskini, badala ya kuwaacha wageni kuzoa utajiri huo.
Kuhusu kutelekeza watoto, Askofu Mokiwa alisema sio mafundisho ya Yesu Kristo, haiwezekani watoto wakaadhibiwa na kuitwa majina yasiyofaa kwa kosa la wazazi wao.
"Mara waitwe watoto wa mitaani na mengineyo mengi lakini mitaa haikuzaa! Watoto wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la huruma na hayo ndio mafundisho ya Yesu Kristo," alisema Askofu Mokiwa.
Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alisema rushwa na ufisadi ni tatizo la kitaifa ambalo linahitaji watu kujikana ili kupambana nalo.
Malasusa alisema hayo wakati akihubiri kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika jana katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam,
Alisema ili kupambana na tatizo hilo, Watanzania hawana budi kushiriki kikamilifu katika kumaliza tatizo hilo.
Alisema sasa wakati umefika kwa wananchi kutimiza wajibu wao wa kupambana na tatizo hilo ili kuinusuru nchi kuendelea kupoteza rasilimali zake.
Ni lazima kila mmoja aone kuwa ni jukumu lake kupambana na rushwa na si kusubiri viongozi wawasukume, la sivyo tatizo hilo litaendelea kuwa sugu na kubadilishwa majina kila kukicha. Kwa mfano sasa hivi wameipa msamiati mwingine kwa kuiita ufisadi,� alisema Malasusa.
Alisema pamoja na kupambana na rushwa ili uchumi wa nchi uweze kukua ni lazima wananchi wajue umuhimu wao katika kuinua uchumi kwa kufanya kazi kwa bidii.
"Kazi ni uhai, suala hili linatakiwa kuingizwa kwenye mitaala ya shuleni ili kujenga vijana wenye moyo wa kupenda kazi," alisema Malasusa.
Aliyataka mataifa tajiri duniani kuacha utaratibu wa kuzinyonya na kuzikandamiza kiuchumi nchi maskini.
Alisema nchi tajiri za duniani zinazikandamiza nchi masikini kutokana na uwezo wao wa kiuchumi waliojiwekea tangu zamani, hivyo kutawala masoko na kuweka mfumo wa kuendelea kuzinyonya nchi zinazoendelea.
Pia aliwataka Watanzania wa dini zote kutumia muda huu kuombea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho nchini Kenya.
Alisema uchaguzi huo ukifanyika kwa amani ni jambo la heri kwa Watanzania kutokana na ujirani uliopo baina ya nchi hizi mbili, kwani yatatokea machafuko nchini humo kutokana na matokeo ya uchaguzi huo, Watanzania pia wataathirika.
Imeshazoeleka kwa nchi za Kiafrika unaposikia uchaguzi, mara nyingi maana yake ni fujo, heka heka na machafuko. Sisi na Kenya ni watu wa nyumba moja, vyumba vinavyofuatana, lolote litalotokea kwa wenzetu linatuhusu pia. Tuwaombee ili wafanye uchaguzi wao kwa amani,� alisisitiza Askofu Malasusa.
Katika ibada hiyo, Askofu Malasusa alifanya maombi maalum kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwaombea Watanzania waweze kubadilika na kusimama kikamilifu kwenye maadili ili waweze kupata neema ya Mungu wanapojiandaa kuingia mwaka mpya wa 2008.
Kutoka Geita, Mwanza, Askofu Mkuu Damian Denis Ndalu wa Kanisa Katoliki, akihubiri katika ibada ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Mama Bikira wa Phatimo, Jimbo la Geita jana, aliwataka viongozi na wananchi kuacha vitendo vya ufisadi na rushwa.
Alisema vitendo vya ufisadi na rushwa vimekuwa vikiendelezwa na watu kutokana na ubinafsi ambao umewafanya walazimishe kuomba rushwa bila kuogopa.
Siku hizi watu hawaombi rushwa bali wanalazimisha rushwa, wanasema leta rushwa ili waweze kutoa huduma. Sasa sijui tunakwenda wapi?� alisema na kuhoji Askofu Ndalu.
Alisema ili taifa na watu wake waweze kuondokana na vitendo vya rushwa na ufisadi wanapaswa kusali na kuwa waaminifu katika sehemu zao za kazi.
Askofu huyo alisema mbali ya Wananchi na Serikali kupambana na rushwa, Watanzania wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kujenga tabia ya kujisimamia wenyewe kwa ajili ya kuongeza pato la taifa.
Alisema kufanya hivyo, Watanzania watakuwa na sauti ya kuitaka Serikali iwaongezee mishahara kwa kuwa pato la taifa litakuwa limeongezeka.
Watu wajijengee tabia ya kujisimamia wenyewe na wasichague kazi ya kufanya. Tupende kazi kwa sababu kwa kufanya kazi, Watanzania watakuwa na uwezo wa kuiambia serikali iwaongezee mishahara. Sasa unataka serikali ikuongezee mshahara wakati kazi hufanyi kwa bidii na uzalishaji unakuwa hafifu...,� alisema askofu huyo.
Akizungumzia ugonjwa wa ukimwi, Askofu Ndalu aliwataka Watanzania kuacha kufanya ngono kwa kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kuepukana na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) kwa asilimia 100.
Acheni ngono. ,Utasikia wanasema ngono zembe, acheni kabisa kufanya ngono, jiheshimuni muweze kuishi kwa amani. Kutokana na watu kutokuwa makini na watu wengi kuendeleza zinaa kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wengi wa mitaani, alisema askofu huyo.
Kutoka Zanzibar, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Zanzibar, Augustine Shao, alishutumu utandawazi usiokuwa na usimamizi wa dola kuwa unaua Utamaduni wa Mtanzania.
Akihubiri kwenye ibada ya mkesha wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili Unguja, alisema ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania haiwezi kuwa kisiwa bila ya kuingia kwenye utandawazi, lakini akaonya kuwa utandawazi usiokuwa na usimamizi unaleta matatizo kwa jamii
Siamini kwamba tunahitaji wageni kuwa wauza maduka, kioski, wapishi na watandika vitanda katika mahoteli yetu. Ndugu zangu Watanzania, hivi sasa wapo wageni wengi nchini kihalali, kwa sababu ya ndugu zetu tuliowakabidhi ofisi za uhamiaji wameshindwa kusimamia ipasavyo wajibu wao,� alisema.
Askofu Shao alisema ubinafsishaji wa sehemu muhimu za uchumi ni jambo linalowasononesha wananchi kwani hakuna manufaa yoyote wanayopata zaidi ya kushuhudia bidhaa nyingi zikitoka nje na kuletwa hapa nchini na mali zao kupelekwa nje kinyemela.
Askofu Shao pia alizungumzia tatizo la uwajibikaji katika jamii kwani shida nyingi katika taifa hili ni watu kupenda vyeo na madaraka bila ya kuwajibika.
Dhambi kubwa iko kwenye mikataba feki ya kuuza rasilimali za nchi. Hii ni dhambi kubwa ambayo itazaa mateso kwa vizazi vingi vijavyo kwa hiyo lazima ipigwe vita kikamilifu,� alionya Askofu Shao.
Aidha, aliwasihi viongozi kuwa makini katika kushughulikia kero mbali mbali za wananchi hasa katika suala la uwekezaji na ukosefu wa ajira.
Alisema mara nyingi mishahara na marupurupu ya watu kutoka nje ya nchi ni makubwa zaidi ya mishahara ya Watanzania wanaotumikishwa katika kazi ngumu zaidi ya zao za usimamizi.
Alitoa mfano kuwa kwenye hoteli zote za kitalii Zanzibar hakuna chumba kinachotozwa chini ya dola za Marekani 50 kwa siku, lakini Mtanzania anayefanya kazi katika hoteli hizo hulipwa mshahara wa kati ya dola 50 na 80 kwa mwezi.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, akihubiri katika ibada ya Krismasi jana, alikemea uzinzi na kuitaka jamii kuachana na uasherati na utoaji mimba kwa kuwa vitendo hivyo ni vya aibu na vinamkasirisha Mungu.
Kwetu sisi tunaotambua kuwa Neno (Yesu) alifanyika mwili na akakaa katikati yetu, tusiidhalilishe miili yetu kwa uasherati, uzinzi na kutoa mimba kwani huko ni kumdhalilisha Mungu, alisema Kadinali Pengo.
Alisema waumini wa dini ya Kikristo wanatakiwa kumuenzi Mungu kwa kuthamini miili yao na kuepuka vitendo vya kuidhalilisha kwani ndani ya mwili wa mwanadamu ipo roho inayoungana na Mungu.
Kwa mujibu wa Kadinali Pengo jamii inatakiwa kulitangaza fumbo la sherehe za Krismasi kwa kuishi maisha ya kuheshimu miili yao na kuwa chachu ya mema badala ya kutumia sherehe hizo kufanya anasa na kumkosea Mungu.
Alisema tofauti na imani za watu wa kale kwamba mwili ni tunda la shetani hivyo kuamua kuidhalilisha kwa lengo la kumkomoa, lakini kwa Mkristo mwili ni hekalu la Mungu linapaswa kuheshimiwa na kulindwa wakati wote.
Alisema roho na mwili siku zote vinashirikiana katika kumjengea mtu utakatifu hivyo aliwataka Wakristo kuwa safi roho na mwili ili kuweza kuwa karibu na Mungu.
Imeandaliwa na Salma Said kutoka Zanzibar, Andrew Msechu, John Stephen, Midraji Ibrahim na Kizitto Noya.