Maaskofu, masheikh wakemea mikataba mibovu
*Wataka serikali ijibu hoja za Dk Slaa.
*Wasema kinachofanyika sasa ni kuwahadaa Watanzania
*Wataka ufisadi ukemewe kwenye nyumba za ibada
*Mtaalam akiri mikataba haiwanufaishi wazawa
Na Kizitto Noya
Mwananchi
VIONGOZI wa dini za Kikristo na Kiislam nchini, wameisihi serikali kutoa tamko linaloeleweka na la wazi kuhusu tuhuma za ufisadi zinazowakabili baadhi ya watendaji wake badala ya kuendelea kukaa kimya.
Wakizungumza jana katika warsha ya kuelimishana kuhusu faida na hasara za mikataba mbalimbali nchini, maaskofu, masista, mapadri na viongozi kutoka Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), walisema serikali inapaswa kujibu hoja za Mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa badala ya kumnyamazisha kwa kumtishia kumshtaki.
Askofu Dk Peter Mwamasika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, alisema sura ya ufisadi katika baadhi ya mikataba ipo na serikali haina budi kujibu hoja hiyo kwa vielelezo badala ya kumnyamazisha Dk Slaa kwa maslahi ya kisiasa.
"Serikali itoe tamko linaloeleweka kuhusu utata wa mkataba wa mgodi wa Buzwagi, wasimtishe Dk Slaa kwa kukimbilia mahakamani maana yeye hawezi kutoa hoja za kitoto kwani ni msomi kama wao," alisema askofu Mwamasika.
Alisema sasa umefika wakati ambapo serikali inatakiwa ieleze bayana namna mgodi wa Buzwagi unavyomnufaisha Mtanzania au hata Wasukuma na Wanyamwezi wenye ardhi yao katika mgodi huo.
Alizitaka taasisi mbalimbali kusimama kidete na kutoa matamko kuikumbusha serikali wajibu wake katika kutetea maslahi ya taifa na watu wake, badala ya maslahi ya kikundi kidogo cha watu.
"Tutawezaje kuondokana na viongozi wabovu wanaowatumikisha wananchi badala ya kuwatumikia, kama si mashirika na wadau wa maendeleo kupiga kelele?" alihoji askofu huyo.
Naye Askofu Isaac Nicodemo wa Kanisa la Morovian la Tabora, alionya tabia ya watu wachache kunufaika na rasilimali za nchi huku wengine wakibaki kuwa maskini na kuipeleka nchi pabaya.
Alisema tabia hiyo sio tu inaliongezea taifa umaskini bali pia inaleta utumwa kwa taifa mbele ya mataifa mengine na isipodhibitiwa ni hatari.
Mkuu wa Shirika la Masista la Mbeya, Immaculate Mirambo, alielezea kukosekana kwa uwiano wa matumizi ya rasilimali za taifa baina ya wazawa na wageni kuwa ni sehemu ya ufisadi unaolalamikiwa na jamii.
"Mimi siyo mtaalam, nazungumza kama mtu wa kawaida kwamba kwa nini kusiwe na uwiano wa matumizi ya rasilimali za nchi kati ya wazawa na wageni?" alihoji.
Alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikizuia matumizi ya baadhi ya rasilimali kwa wazawa na kuruhusu rasilimali hizo zitumike na wageni jambo ambalo limesababisha umaskini kwa mwananchi wa kawaida.
Naye Mchungaji John Magofu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), aliwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya taifa badala ya kuwaachia wanasiasa ambao hata kama hoja zao zina ukweli, zinapokelewa kisiasa na kupuuzwa.
Alisema hoja nzito kama za ufisadi zinatakiwa kusimamiwa na viongozi wa dini kwa kuzihubiri katika sehemu zao za ibada ambako wahusika wanaabudu ili wabadili tabia.
"Mafisadi wana imani zao na wanaabudu, viongozi wa dini wakihubiri hoja hizo huenda zikafika kwa walengwa mapema zaidi kuliko wanasiasa," alisema Mchungaji Magofu.
Alisema kuna haja kwa serikali kujichunguza na kuanza kufanya utafiti wa kina kabla ya kuingia mikataba mbalimbali kwani uzoefu unaonyesha kuwa mikataba mingi haiwanufaishi wananchi.
Akizungumza katika ibada ya ufunguzi wa warsha hiyo, Askofu Charles Salala wa Kanisa la African Inland (AICT) Dayosisi ya Pwani, alisema viongozi wa kanisa ndio dira iliyobaki na kuweza kutoa matamko yanayoheshimika katika jamii.
Alisema jamii imeanza kupoteza imani na wanasiasa badala yake inahitaji viongozi wa kiroho kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi yao.
"Viongozi wa kanisa wanatakiwa kuishauri serikali na kutoa matamko ya utetezi wa wananchi badala ya kuwaachia wanasiasa,"alisema.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kasuto na Mshauri Mkuu wa masuala ya Uchumi na Biashara, Mikubuka Shimwela, alibainisha kuwa tafiti zilizofanywa hivi karibuni zimeonyesha kuwa asilimia 38 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini ni bandia.
Hata hivyo, alisema kuwa serikali imefanya jitihada za makusudi kudhibiti tatizo hilo kwa kupeleka bungeni muswada unaotaka kuipa nguvu za kisheria Tume ya Ushindani wa Biashara nchini kukamata na kuwafikisha watuhumiwa wa bidhaa bandia mahakamani.
Alisema baada ya kujadiliwa katika Bunge la Bajeti mwezi Juni, Muswada huo utapitishwa katika Bunge la Mwezi Novemba mwaka huu.
Akizungumza katika warsha hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtaalam wa masuala ya mikataba ya biashara za Kimataifa, Profesa Francis Matambalya, alisema ni ukweli usiopingika kwamba mikataba mingi nchini haiwanufaishi wananchi.
Alisema tofauti na nchi za Magharibi nchini mikataba mingi inawanufaisha wageni badala ya wazawa jambo ambalo linaathiri uchumi wa nchi na kusababisha umaskini kwa wananchi wake.
Kwa mujibu wa Profesa Matambalya, mbali na ubovu wa mikataba, woga wa watendaji katika kusimamia ukweli na tabia yao ya kujikomba kwa serikali na kusahau maslahi ya wananchi pamoja na maamuzi ya kushitukiza ni baadhi ya mambo yanayoleta umaskini nchini.
Alisema watendaji wengi wanatumikia matakwa ya serikali badala ya wananchi na hawana uchungu wa kutetea maslahi ya nchi, zaidi ya kujilimbikizia mali na kutafuta madaraka.
"Inakuwaje nchi ina polisi, usalama wa taifa, Takukuru, wataalam na viongozi wa ngazi zote ishindwe kudhibiti ufisadi kama siyo kutokuwa na moyo wa kizalendo?" alihoji.
Alisema umasikini nchini hautakoma endapo viongozi wa dini hawataingilia kati suala hilo na kuwasemea wananchi kwani hii ni sehemu ya kazi yao waliyopewa na Mungu.
Kauli za viongozi hao zimekuja baada ya Dk Willibrod Slaa kuibua tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali.
Tayari maaskofu wa Kanisa Katoliki ambao ni sehemu ya washiriki katika warsha hiyo wameonya kuhusu ufisadi kwamba ni hatari kwa taifa.
Viongozi hao wa dini leo wanatarajia kutoa tamko la pamoja kuhusu mjadala wa mikataba mbalimbali ikiwapo nafasi ya Tanzania katika mkataba wa Contonou.