KUTOKA KATIKATI YA KUTA ZA MAGEREZA UKONGA, ANAANDIKA TUNDU ATIPHAS LISU:
Mwaka 1988 mto Vaal huko Free State ulifurika na kujaza bwawa kubwa la kuzalisha umeme la Vaal Dam. Bwawa likazidiwa maji na kutapika. Sehemu kubwa ya maji yakaenda kuathiri mashamba ya makaburu huko Free State na Gauteng. Nyumba za wakulima wa kizungu zikabomoka, na vifo 11 vikaripotiwa.
Wakati huo kulikuwa na mapambano makali ya watu weusi kudai uhuru kutoka kwa makaburu. Baada ya makaburu kupata majanga hayo ya mafuriko, maelfu ya watu weusi walishangilia mitaani na wengine wakifanya sherehe kama ishara ya kushukuru "miungu" yao kwa kuwalipia kisasi.
Rais Pieter Willem Botha, mmoja wa Marais katili mno wa Kikaburu, akalaani kitendo cha Waafrika kushangilia vifo vya makaburu. Huyu ni yule aliyewahi kusema Waafrika hawana akili za kujitawala, wanapaswa kutawaliwa milele. Baada ya mafuriko hayo P.W Botha akasema serikali yake haitawavumilia walioshangilia vifo vya makaburu kwa sababu huo si ubinadamu.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha ANC, Walter Sisulu, akamjibu P.W Botha kwa maneno ambayo yanaishi hadi leo. Sisulu alisema:
"Kama makaburu hawaumizwi na vifo vya watu weusi, wasitegemee kwamba weusi wataumizwa na vifo vyao. Weusi wameuawa kinyama na makaburu, na wengine hawakupewa hata heshima ya kuzikwa; walifukiwa kwenye makaburi ya halaiki kama wanyama. Leo, makaburu wakifa wanataka weusi waomboleze? Huku ni kujipa haki kubwa kuliko hata malaika.
Hamuwezi kuua watu weusi, muwafukie kama mizoga, halafu mkifa nyie mnataka watu haohao wasikitike. Binadamu ni yule yule, awe mwenye ngozi nyeusi au nyeupe. Kama wewe kaburu unaumizwa na kifo cha kaburu mwenzako; unapaswa kuumizwa na kifo cha mtu mweusi pia. Kuwa mweupe au kuwa na madaraka hakukufanyi kuwa binadamu kuliko wengine. Utu wetu haupo kwenye rangi za ngozi zetu wala
vyeo vyetu.”