Akiwa anatimiza Siku 283 gerezani, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amevunja rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza wa juu kabisa wa chama cha upinzani nchini kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
Lissu ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Januari 22 mwaka jana, alikamatwa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma Aprili 9 mwaka jana na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam alikofunguliwa shtaka la uhaini ambalo hali dhamana kwa mujibu wa sheria.
Lissu alikamatwa alipokuwa akiendelea na mkutano wa hadhara wa chama chake katika operesheni yao iliyojulikana kama 'No reforms no election' ambayo ilikuwa ikiendelea katika kanda ya kusini baada ya kumalizika katika kanda zingine ikiwamo kanda ya ziwa.
Licha ya kwamba wapo baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani waliowahi kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekaa gererezani kwa zaidi ya siku 220 lakini hakuna aliyefikia rekodi ya Tundu Lissu aliyefikisha siku 283.
Kama ilivyokuwa kwa Lissu ,Mbowe alikamatwa mkoani Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 na kisha kusafirishwa hadi Jijini Dar es Salaam alikounganishwa na wenzake katika kesi ya Ugaidi kesi iliyoendelea hadi Machi 4,2022 baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali kusema hana nia ya kuendelea na kesi hiyo hivyo kuachiwa huru.
Makosa ya Ugaidi na Uhaini yote hayana dhamana kwa mujibu wa sheria jambo lililofanya viongozi hao wawili kusota gerezani kwa muda mrefu. CHADEMA ipo katika kumbukumbu ya miaka 33 tangu kuanzishwa kwake wakati huu ambapo kiongozi wao mkuu bado yupo gerezani.
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
HUYU HAPA