JE, LISSU ANAPASUA JIPU WAKATI WA KULA?
Tundu Lissu anaambiwa na Hakimu awataje mashahidi wake. Lissu anawataja Rais Samia Suluhu Makamu wa Rais Philipo Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa! Lakini baada ya kusikia majina Hakimu anakataa kuyaandika na pia hatoi sababu ya kukataa kuyaandika majina na hatoi kifungu cha sheria kinachomuongoza asiandike majina ya mashahidi wa mtuhumiwa.
Hapa kuna maswali ya kujiuliza! Kama Hakimu alijua kuwa hataandika majina ya mashahidi, ni kwa nini alimtaka mtuhumiwa ataje majina ya mashahidi wake? Ni kwa nini Hakimu alikataa kuandika majina ya mashahidi hao? Je, katika kesi ya uhaini kuna watu hawana sifa ya kuwa mashahidi? Je, ni watu gani hao na ni kifungu gani cha sheria au cha katiba ya nchi ambacho kinawazuia baadhi ya watu kutoa ushahidi wa kesi inayowahusu na kuwa na madhara kwao?
Kama Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu atavamiwa na kuumizwa na ikatakiwa afike au awepo mahakamani kuthibitisha juu ya kuumia kwake hatakwenda? Na kama wakati tukio hilo linatendeka alikuwepo yeye na waliomuumiza na ikatakiwa awatambue mahakamani, hatafika kwenda kuwatambua? Je ni kwa nini sasa watu hao wasiandikwe kama mashahidi katika kesi hii ambayo kimsingi mmoja wao alilengwa kwa 'uhaini wa Tundu Lissu'?
Je, Tundu Lissu anataka kupasua jipu lililooza wakati ameketi mezani na wenzie kula chakula na je, watakubali kuona usaha wenye harufu?
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 19 Agosti 2025; saa 5:33 asubuhi