MARIDHIANO HAYAJI KWA NJIA ZA UTAPELI!
Mtu aliyetambulishwa kama Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA (BAZECHA) Kanda ya Kati (Morogoro, Singida na Dodoma, Acquilin Magalambula amenukuliwa akisema CHADEMA waingie maridhiano na serikali hata kama Lissu hajatoka gerezani.
Mtu ambaye aliyetambulishwa kama Katibu wa CHADEMA wa Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola amenukuliwa akiwashambulia Mhe. Jaji Joseph Warioba na Mhe. Anna Tibaijuka.
Lakini uchambuzi wa picha mjongeo (video) na mazingira ya mikutano yote miwili insonyesha kuwa ni mkutano mmoja kwa sababu mavazi ya wahudhuriaji yanafanana na watu wengine nyuso zao ni zile zile na kipaza sauti ni kile kile na hata wasambazaji wa video hizo ni watu au media zenye mrengo wa CCM.
Lakini waandaji wa mkutano huo ni watu wa ajabu sana. Wanasukuma maridhiano lakini hawataki Lissu atoke gerezani. Wanasukuma maridhiano lakini wanawashambulia Mhe. Jaji Joseph Warioba na Prof. Tibaijuka.
Lakini jambo lingine ni kuwa mikutano yote ya CHADEMA ina muktadha unaojulikana na hata hupambwa na bendera za chama chao na hukuwa wanachama wao wakivalia mavazi ya chama chao.
Pia, hata viongozi wa CHADEMA wakiwa katika mikutano yao lazima waseme kauli mbiu zao kama 'People's Power', nk. Lakini muktadha na mazingira ya mkutano huo au mikutano hiyo ni kinyume kabisa.
Sisi askofu tunataka kuwaeleza watu ambao wako nyuma ya mkakati huo wa kurubuni watu kwa kuwatumia watu ambao hujinasibu kama viongozi wa CHADEMA. Ujumbe wetu ni kuwa maridhiano ya kweli hayajengwi kwa kutumia njia za ulaghai, utapeli au udanganyifu. Kama CCM na serikali yake wanataka kweli kufanya maridhiano ya kweli waache kulaghai watu au kudanganya watu kwa njia hizo.
Kwa nini kauli za watu wanaohujumu ukweli na kukihujumu CHADEMA na viongozi wake pia zipate nafasi katika media za watu ambao ni wale walio karibu na CCM na serikali yake?
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 9 Septemba 2026; Saa 5:55 usiku.