Nimeshtushwa na taarifa za kifo cha Ndugu Peter Kalihose, mwanachama na kada hodari wa CCM mitandaoni ambaye alikua akikisaidia sana chama chake hasa kwenye propaganda. Lakini kifo cha Peter kitupe somo sisi tuliobaki hai.
Pamoja na umahiri wa Peter katika kujenga hoja lakini alikua bingwa wa kuattack personality. Matusi aliyoyatoa kwa Lowassa mengine hayaandikiki. Aliwahi kumuita mgonjwa, dhaifu, na marehemu mtarajiwa. Bahati mbaya hakuna kiongozi wa CCM aliyemkemea dhidi ya lugha hizo za matusi.
Leo Peter ametangulia amemuacha yule aliyemuita marehemu, maiti inayotembea, mgonjwa, na dhaifu akizidi kuimarika na kujenga chama chake. Ni vizuri tuishi tukijua maisha ya hapa duniani ni ya muda tu na siku moja sote tutatoweshwa. Hatuna mji udumuo hapa. Lakini jiulize utakapoondoka utaacha alama gani nyuma yako? Alama utakayoiacha itafuatana na matendo yako.
Usijivunie uzima ulionao. Uzima na ugonjwa ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Kama wewe ni mzima mshukuru Mungu na waombee walio wagonjwa. Katika malezi yangu nilifundishwa kila nisalipo nisisahau kuwakumbuka wagonjwa, yatima na wajane. Sio kuwadharau, kuwadhihaki, wala kuwapuuza. Huenda Peter alijiona ana nguvu kuliko Lpwassa, ni imara kuliko Lowassa, ana afya bora kuliko Lowassa akasahau kuwa aliyempa afya hiyo ni Mungu, tena kwa neema tu.
Simlaumu Peter, ya kwake yamepita na hatuna lolote la kubadilisha aliyosema. Tunachopaswa kujifunza kupitia Peter ni kwamba katika maisha yetu tusijivunie uzima tulionao, wala tusiwadhihaki tunaoona wana afya zilizodhoofu. Mpaji wa yote ni Mungu mwenyezi. Ayubu aliwahi kudhoofu mwili akabakia mifupa, akapoteza mali na watoto wake wote. Lakini hakufa. Waliokua na afya walikufa wakamuacha. Baadae Mungu akamnyanyua Ayubu na kumpa afya bora, mali na watoto wengine.
Tusiruhusu siasa kujenga chuki baina yetu. Sisi sote ni watanzania, tuulinde utaifa wetu. CCM, Chadema, ACT, CUF haiwezi kuwa muhimu kuliko utu wako na utaifa wako. Heshimu kila mmoja bila kijali ni wa chama chako au lah. Tujifunze kuwa na siasa za kujadili masuala badala ya kuattack personality.
Tukiwa na siasa za kujadili issues hatuwezi kuwa maadaui kwa wafuasi wa vyama vingine. Tutafanya siasa, tutabishana na kushambuliana kwa hoja, lakini nje ya siasa tutaheshimiana na kushirikishana mambo mbalimbali. Mimi ni mwanachama hai wa Chadema kwa miaka 9 sasa lakini nina ndugu na marafiki wengi ambao wapo CCM na vyama vingine. Wengine mawaziri, wengine wabunge, wengine viongozi wa kada mbalimbali na wwngine wanachama wa kawaida. Nje ya siasa tunakula pamoja, tunafurahi pamoja, tunashirikiana na kusaidiana.
Majuzi gari yangu ilipasuka tairi nikiwa mbele kdg ya Kibaigwa, na sikua na Spear tyre, nikampigia simu rafili yangu ambaye ni mwanaCCM na ni kiongozi wa serikali, akatuma gari ikaniletea spear tairi kutoka Dodoma. Siasa haipaswi kutufanya maadui, siasa haipaswi kutujengea chuki, dharau, au dhihaka dhidi ya wengine. Nje ya siasa sisi sote ni binadamu wenye usawa na tunastahili kuheshimiwa utu wetu.
By the way hapa duniani sote tutapita na hakuna atakayeishi milele. Rafiki yangu Dr.Christopher Cyrilo anapenda kusema hakuna atakayeondoka hapa duniani akiwa hai (Nobody will leave this world alive). Sote tutakufa siku moja, sote tunapita, sote ni mavumbi. Lakini je ukifa utaacha nini kwa waliobaki duniani? Watakukumbuka kwa lipi?
Kwa heri Peter. Upumzike kwa amani. Safari yako hapa duniani imefikia tamati. Sisi tuliobaki kwenye safari hii ni jukumu letu kujitathmini na kujipima kwa matendo yetu. Mungu atujalie kuwa na mwisho mwema.!
Malisa GJ
View attachment 455068