Salamu zenu waheshimiwa mabibi na mabwana!
Nimekaa hapa na nimejikuta maswali yakizidi kujipanga kichwani mwangu utadhani mtu anayepanga matofali ya kuchoma kwenye tanuru nje kidogo ya mji wa Iringa, pembezoni mwa barabara iendayo Mbeya! Na kwa kadiri ninavyofikiria najikuta nashindwa kupata jibu la uhakika na kitu hicho kinanitia hofu kuwa tusipoangalia tumeendelea kukubali rushwa ya aina hii kiasi cha kuifanya ni kawaida. Fuatilia kisa hiki:
Mheshimiwa akiwa amevalia nguo za kawaida, yeye na dereva wake anateremshwa karibu na Duka la Bw. Bushiri. Wapita njia wanamtambua kuwa huyo ni mheshimiwa fulani. Hana lengo la kununua kitu isipokuwa kusalimia wafanyabiashara wachache. Anaingia dukani na mwenye duka kumuona anaingiwa na kiwewe na kuanza kujibamiza kwa "mwenye nchi huyo"
"Mheshimiwa!! karibu karibu" Bw. Bushiri anasema huku akiteremka kwenye kiti chake kikubwa kilichoko kwenye kona ya duka hilo.
"Asante sana Bw. Bushiri, habari za shughuli bwana" Mheshimiwa akajibu huku akinyosha mkono wake ambao ulikuwa umenona utadhani wale 'kuku' wa Salanda huku vinyweleo vya ngozi yake vikiwa vinameremeta kwa mafuta aliyojimwagia.
"Ni njema tu mzee, tumebahatika nini kutembelewa na mtu mzito kama wewe" Bushiri hakuchelewa kuuliza kwani alijua mheshimiwa anapokuja kwenye duka lake huwa anataka kitu.
"Ah! kukusalimia tu bwana, unajua tena mihangaiko ya hapa na pale" Kwa soni za uongo mheshimiwa akamjibu, huku macho yake yakiangaza angaza kila kona ya duka hilo. Bushiri, hakuchelewa kuelewa nini kinaendelea. Akaamua kumkaribisha mheshimiwa ofisini kwake kwenye kona nyingine ya duka hilo ambapo watu wengine hawaruhisiwi kupita. Walipoingia ofisini baada ya kuulizana hali za watoto na wake zao, Bw. Bushiri akamuuliza mheshimiwa
"Sasa mzee, unahangaika nini tena"
"Bwana we, unajua tena nilitarajia mzee angeniteua kwenye kaposition fulani lakini hakufanya hivyo. Hata hivyo nimehakikishiwa kuwa kwenye next reshuffle naweza nikaukwaa na mimi. Sasa nikasema ni bora nianze kuwajua rafiki zangu ni nani bwana" Mheshimiwa akajibu kwa uhakika huku unono wa mashavu yake ambao uliunganika hadi kwenye shingo ukitingishika tingishika utadhani ng'ombe wa maziwa wa pale Kange, Tanga.
"swadakta! na marafiki zako tupo mzee" Bushiri alijigamba huku akijigonda kifuo kwa mkono wake kuonesha na yeye ni mmoja wa marafiki hao.
"Nashukuru Bw. Bushiri, sasa hivi nahangaika kuinua kile kibanda changu kule Mbezi, ila hali ngumu bwana" Mheshimiwa akasema kana kwamba kwa mzaha. Bushiri alitamani aanze kumuuliza "hali ngumu gani" anayozungumzia kwani akianza kumhesabia pesa ambazo mheshimiwa huyo na wenzake wanamegewa na nchi yao, basi maana ya "hali ngumu" haipo tena. Lakini hakuthubutu.
"Sasa mzee tatizo nini nini kwenye kibanda?" Aliuliza Bushiri kwa unyenyekevu.
"Cementi bwana bei ghali kweli na mabati ndio usiseme, ila ningependa kuweka vigae, ndio nahangaika hapo" Mheshimiwa akajibu.
"Sasa" Bw. Bushiri akadakia, "Mzee usiwe na wasiwasi, nitamtuma dereva siku ya jumamosi na mifuko 50 ya saruji na vigae 5000 hivyo vya kukusaidia kidogo" Alimalizia huku akiandika kwenye kijitabu chake cheusi ambacho kurasa zake nyeupe zimeanza kugeuka na kuwa za rangi ya udongo.
"hayo maneno sasa" Mheshimiwa akajibu huku akisimama kuagana na Bw. Bushiri.
"Mzee na wewe ukifika katika ufalme wako usitusahau mzee" Bw. Bushiri alisema kwa upole lakini akiwa anatoa ujumbe ulio dhahiri.
"Bila ya shaka, umenifaa leo, na siku moja nitakufaa bwana" Mheshimiwa alisema huku akimuelekeza dereva wake aliyekuwa bado anang'aa ng'aa macho kuwa muda umefika waondoke.
Walipotoka kwenye duka la Bw. Bushiri, waliendelea na 'kaziara' hako kafupi kwenye maduka ya Bw. Minja, duka la Mzee Sudi, duka la vifaa vya umeme la Patel na duka kubwa la samani la Bw. Abdalah Fundi lililoko eneo la Keko gerezani karibu na barabara ya kwenda Chang'ombe. Mwisho wa siku, Mheshimiwa alikuwa amepata ahadi ya saruji, vigae, mabomba ya maji, samani za ndani ya nyumba, mafjiri mawili, viyoyozi sita na mazuria toka Uchina. Aliporudi nyumbani mheshimiwa alienda kujipongeza kwenye Baa ya "Sisi kwa Sisi" iliyoko kwenye kona ya mtaa wake ambapo huko nako hata bia alipewa ya dezo!
Miezi sita baadaye, mheshimiwa wetu alikuwa anamalizia kujenga 'hekalu' lake kubwa eneo la Mbezi ya Kimara upande ule mwingine kutoka upande wa nyumba ya jenerali Musuguri. Ilikuwa baada ya mabadiliko ya mawaziri ya hivi karibuni Mheshimiwa akapewa na yeye unaibu wa wizara moja nyeti, na haikuchukua muda kwa yeye kuanza kuwarudishia fadhila wafadhili wake. Kwa vile sasa kaupata na ujiko mkubwa kidogo mheshimiwa wetu ameanza tena kufanya viziara vya hapa na pale kwa wafanyabiashara wa mikoani na pole pole ameanza kujenga "vibanda" vingine karibu kila mkoa katika mihangaiko yake ya kila siku, kwani "hali ngumu". Na wakati haya yote yanaendelea, mheshimiwa ameendelea kunawiri na kunenepa! Wale wafanyabiashara wote waliomsaidia sasa hivi wanaweza kupiga simu wakati wowote na kutaka hisani ya aina yoyote toka kwa Naibu Waziri na mara nyingi wanapata!
Mfano mzuri ni kuwa hivi karibuni Bw. Bushiri alikuwa afanyiwe uchunguzi na TRA lakini kwa neno zuri la Naibu Waziri uchunguzi huo umezimwa baada ya Bw. Bushiri kulipa kodi ya shilingi milioni moja tu wakati kodi aliyotakiwa kulipa kwa halali ilizidi shilingi milioni 40! Huu ndio uzuri wa "kujuana na mkubwa".
M W I S H O
Kikanusho: Kisa hiki ni cha kubuni. Mlingano wowote na watu, majina, au matukio halisi ni wa kinasibu. Haki zote za kunakili zimeachiliwa na M. M. Mwanakijiji
NB: Kisa hiki kinamhusu mheshimiwa mmoja tu kati ya wengi, kama wengi wanafanya tabia ya aina hii, athari zake ni kubwa kiasi gani? Je kuna ubaya wowote kwa viongozi kutafuta na kupokea zawadi za aina hii? Kama raia anataka kumsaidia kiongozi kuna kosa gani hapo? Je hii nayo ni rushwa, takrima, zawaida au ukarimu tu wa Watanzania? Maswali yameanza tena kichwani mwangu.