*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN*47
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akaenda chumbani na kuchukua ile karatasi yake ya siri. Wakatoka nje na Seth. Hapo tu mlangoni wakakutana na Bozi akiwa ameambatana na kikosi cha wanaume watano.
Wanaume hao walikuwa wamebebelea silaha na kujivesha sura za ghadhabu.
ENDELEA
Haikuwa rahisi kwa Fluffy kupambana na watu hao. Alistaajabu wengine walikuwa ni walinzi wake wa karibu. Akawekwa chini ya ulinzi na kuchukuliwa kimya kimya kwa siri wakipita njia panya mpaka kwenye jengo lao walilomfungia Fluffy ndani.
Mbaya zaidi watu hawa walikuwa wamekwapua karatasi ile ya siri ya Fluffy. Karatasi ambayo ilikuwa inaeleza mambo ya siri ya kule Misri. Karatasi ambayo Fluffy alikuwa ameificha asimwambie mtu kuhusu, isipokuwa tu Seth.
Japokuwa alipambana kunusuru karatasi yake, hakufua dafu kwenye mikono ya wanaume watano, ukitazama Seth hakuwa mtu mwenye ujuzi wowote kwenye maswala ya kujilinda. Kweli hupewei vyote.
“Sasa mtakaa humo wapenzi. Bila shaka mlikumbukana sana,” Bozi akasema kwa kebehi kisha akaangua kicheko. Ingawa Fluffy alimtishia na kumwahidi atammaliza kwa mikono yake, Bozi hakuonekana kujali.
Zaidi akampungia mkono na kuufunga mlango akiwaacha wafungwa gizani.
“Bado na yule mwenzenu!” Sauti ya Bozi iliwafikia Fluffy na Seth waliokuwa ndani, gizani. Kisha ikafuatia kicheko kilichokuwa kinaishilia kadiri na muda.
“Sasa tunafanyaje, Seth,” Fluffy akauliza kwa hofu. Sauti yake ilikuwa ina ashiria anguko, huzuni.
Lakini kinyume chake, Seth akamwambia kuna tumaini. Alikuwa anaamini watatoka mule, na wataikomboa Sawaridi kwa mara nyingine tena.
“Maadui hawakuisha. Ni bora adui wa nje kuliko yule wa ndani unayeshirikiana naye sahani na kijuiko,” Seth alisema kwa sauti ya chini.
***
Baada ya hatua nzito, mlango wa nyumba ya mfanyabiashara Melkizedek unagongwa mara tatu, kisha mgongaji anatulia. Alikuwa ni mwanajeshi, yule aliyepewa kazi na mfalme ya kumfuatilia Tattiana katika mienendo yake yote.
Tattiana, binti wa Melkizedek ambaye alitokea kukamata jicho la mfalme. Binti mwenye macho mazuri, uso wa kistaarabu na nywele kama unyoya wa sufi.
Punde mlango ukafunguliwa na Fanty, kaka yake Tattiana, akauliza amsaidie nini mlinzi yule ambaye alisema anataka kuonana na baba yake kama yupo.
Haraka Fanty akaenda kumfikishia baba yake ujumbe, ndani ya muda mfupi akashuka kukutana na mwanajeshi.
“Karibu.”
Uso wa Melkizedek ulikuwa na wasiwasi. Siku zote ukiwa unajua kuna jambo baya umelifanya, basi ukutanapo na mhusika ama mtendwa, basi waanza kujitunuku mashaka.
Akili ya Melkizedek ilikimbia haraka na kuwaza kwamba ukute makubaliano yake na yule mzee wa baraza kuhusu biashara ya Cedar yamebumburuka, na sasa amefuatwa kukamatwa.
“Ahsante, sikaribii. Nina ujumbe toka kwa mfalme.” Mwanajeshi akamkambidhi Mlekizedek barua iliiyokuwa imefungwa na kamba ya madini ya fedha, ikichapwa na mhuri wa mfalme.
Mwanajeshi akaenda zake akimwacha Melkizedek anaikagua barua ile. Akazama ndani na kumwita mkewe kumjulisha kuhusu barua toka kwa mfalme.
“Itakuwa inamhusu binti yetu,” mama akasema upesi. Alikuwa amevalia gauni lake la thamani. Mkono wake ulinyaka barua toka mikononi mwa mumewe, haraka akafungua ujumbe huo na kuusoma.
Ulikuwa ni ujumbe wa mfalme akiomba kukutana na Tattiana.
“Si nilikuambia!” mama akalipuka. “Hii ndiyo hatua ya kwanza kuelekea ndoa. Endapo binti yetu akimkarimu vizuri mfalme, basi tutakuwa wakwe.”
Mama pasipo kupoteza muda akamwita mwanae na kwenda naye chumbani. Akamwandaa vema kwa kumkwatua na kumchagulia nguo iliyopendeza macho yake. Lakini zaidi akamhusia asimwangushe kwani hiyo ni nafasi adhimu sana kwake.
“Unaweza ukageuza familia na ukoo wetu kuwa wa kifalme. Tukaheshimika zaidi, na tukafanikiwa zaidi.”
Kisha akamfunda namna ya kuenenda.
“Mtazame mfalme kwa uso wa haya. Usimnyime tabasamu wala mkono wako. Hakikisha anakuwa wa moto kila anapokuwa karibu na wewe. Usiwe na papara, tulia na uzingatie kama paka mwitu awapo mawindoni.”
Likapita kama nusu saa hivi, mara farasi wawili toka kwenye kasri ya mfalme wakawasili nyumbani kwa Mlekizedek. Kwenye mgongo wa farasi mmoja alikuwa ameketi mwanajeshi, na mwingine alikuwa hana mtu mgongoni.
Huyu ambaye hakuwa na kitu mgongoni, alikuwa ni mweupe. Kamba yake iliyomshika shingo ilikuwa imeshikiliwa na mwanajeshi aliyekuja nao.
Mwanajeshi huyo akasema amekuja kumtwaa Tattiana. Tattiana akatoka ndani na kumwea farasi, wakatimka kwenda kasrini kwa mfalme.
Ni muda mchache ukapita, na mara akatokea kijana fulani hapo nyumbani kwa wakina Tattiana. Kijana huyu alikuwa mwembamba mwenye nywele ndefu rangi ya kahawia na ndevu zilizojaa kwenye taya.
Akamuulizia Fanty kwa walinzi, Fanty akaitwa na kuja kujumuika naye hapo nje ya uzio.
“Nimemwona Tattiana akiongozana na mwanajeshi. Kuna nini?” akauliza mwanaume huyu ambaye kwa mujibu wa maongezi ya Fanty, alikuwa anaitwa Roboth. Macho yake yalikuwa madogo yanayong’aa.
Fanty akamwambia kwamba Tattiana amepelekwa kasrini kukutana na mfalme na kama mambo yakiwa vema basi ataolewa na mkuu huyo wa nchi. Roboth akastaajabu sana. akaishiwa na nguvu akiuliza:
“Kuolewa? Na vipi husumu mimi?”
Fanty akamsikitikia. Japokuwa Roboth alikuwa ni rafiki yake, na anajua fika alikuwa ana mahusiano na Tattiana, ambaye ni dada yake, hakuwa na fursa ya kumzidi mfalme.
Akamwambia amsahau Tattiana, kwani atajiumiza tu. hata familia yake haiwezi kumwelewa. Roboth akapinga hilo jambo kwa nguvu zake zote. Fanty asimjalli, akarudi zake ndani.
Na kumbe mama yake alikuwa anaushuhudia mchezo wote huo. Akamfuata Fanty na kumuonya.
“Sitaki yule kifaranga akanyage tena hapa kwangu, wala amsogelee Tatty. Sawa?”
Fanty akaitikia, kisha akaenda zake.
---
“Karibu,” Akasema Phares akimpatia mkono Tattiana. Tattiana akashuka wakaenda zao ndani.
Walifikia sebuleni wakakaketi katika umbali wa kunyoosha mkono kumfikia mwenzako. Mfalme akamsifia Tattiana amapendeza. Tattiana akiwa ameinamisha uso wake akashukuru.
Wakakaa kwa muda wa kama dakika mbili pasipo kuongea. Tattiana alikuwa anafinyaga vidole vyake wakati Phares akifurahia kutazama uso wa binti huyo mrembo akiwa anatabasamu mwenyewe.
Mwishowe Phares akamtaka Tattiana amwandalie chakula cha usiku. Angependa kula mkono wake. Na zaidi akataka abaki naye kwa siku hiyo.
“Sawa, mfalme wangu,” Tattiana akaitikia.
***
Farasi alipolia, Bonas akamwambia Rhoda:
“Ni muda mrefu sasa twatembea. Huoni kama itakuwa vema tukipumzika.”
Walikuwa wametimiza kama masaa sita hivi wakitembea. Watu wote walionekana kuchoka isipokuwa Rhoda mwenyewe. Bado macho yake yalikuwa makavu na mwenye nguvu.
Alikuwa anaangaza angaza huku na kule japo haoni jambo isipokuwa giza.
Wakapumzika. Na wale wenye chakula wakatoa kula.
“Unaweza ukaona lolote tukiwa hapa?” Rhoda akamuuliza Tretho.
“Sijajua,” Tretho akamjibu. “Ni mpaka tufanye huo msako.”
Basi Rhoda akasogea kidogo kando apate kumaliza haja yake ndogo. Alipomaliza, kabla hajajirejesha kule walipo wenzake, akaangaza kushoto na kulia kwake. Akaona taa moja kwa mbali upande wake wa kaskazini.
Aliporejea akamwambia Tretho na Bonas.
“Kwahiyo tutaelekea huko?” Bonas akauliza.
“Ndio,” Rhoda akajibu. “Ila ni sisi wenyewe siyo na kikosi kizima.”
Bonas na Tretho walipomaliza kula, basi wakatoka na Rhoda kwenda kule walipoona taa. Baada ya mwendo wa dakika ishirini na, wakawa wamekaribia kufika. Ilikuwa ni nyumba ya wale wabibi walozi watatu.
Ila punde, wakaanza kuona maajabu!
Kwanza walisikia sauti ya popo na mvumo wa upepo tokea kushoto mwao. Kutazama wakaona rundo kubwa la popo wakubwa. Popo hao walikuwa wanakuja upande waliopo.
Wakawavamia katika mtindo wa kuwazunguka. Japokuwa Rhoda alishikilia kizingiti chake alichopewa na Venin kama kinga. Hakikumsaidia. Wakajikuta wananyanyuliwa na kimbunga kile cha popo na kusafirishwa wakielekea wasipopajua.
Ndani ya hekalu kubwa, kubwa mno, popo wakaingiza watu hao ndani na kuwamwaga kwenye ukumbi. Ndani ya ukumbi huo wakawakuta wenzao, yaani kile kikosi cha watu waliokuja nao wakiwa tayari wameuawa!
Kila waliyemwamsha, hakusikia wala kufurukuta. Walikuwa wamekauka ngozi yao ikiwa nyeupe pe!
“Wamenyonywa damu,” akasema Tretho. “Hawajabakiziwa hata tone moja.”
Wakiwa hapo wanabung’aa. Hawaoni pa kuingilia wala kutokea. Yule mtu aliyekuwa anamtazama Rhoda kwenye rada, akaangua kicheko kisha akatia kidole chake kwenye rada na kukoroga.
Mara Rhoda na wenzake wakaanguka chini kwa kizunguzungu. Wakapoteza fahamu.
***
“Malkia, hakuna aliyemwona,” askari alifikisha ripoti kwa ukakamavu.
“Umeulizia vizuri lakini?”
“Ndio, nimeuliza kila eneo na kila mtu. Hakuna aliyesema amemwona jenerali kamanda.”
Malkia akanywea. Aliminya mdomo wake akitazama kushoto. Akafikiri kwa muda kidogo kabla hajauliza:
“Na kaimu?”
“Yu njiani yuaja,” akajibu mwanajeshi na kisha akaondoka. Malkia akarejea sebuleni kukutana na Zura aliyekuwa ameketi kwenye kiti akifuma kitambaa kikubwa kizito.
“Hamna anayejua wapi alipo,” Malkia akamwambia Zura huku akinyanyua gauni lake zito lililofumwa na nyuzi za dhahabu apate kukaa kochini.
“Sasa atakuwa ameenda wapi?”
“Sijui. Tangu aliporejea toka kwa mama yake, nilionana na kuongea naye kwa muda mchache sana. Sijui amekumbwa na nini.”
Punde si nyingi, akaja mwanaume mrefu mwenye mwili mpana, Benadi. Mwanaume huyu alikuwa makamu wa Fluffy. Malkia akamuuliza kama amemwona Fluffy ama ana taarifa zozote kuhusiana naye.
“Hapana, sijui alipo,” akajibu Benadi akitikisa kichwa.
“Umeongea naye karibuni?”
“Hapana, sijaongea naye.”
“Unadhani atakuwa wapi?”
Benadi akatikisa kichwa chake. Basi Malkia akamruhusu aende zake.
Benadi alipotoka nje, akatembea kwa umbali mfupi kabla hajasikia jina lake linaitwa na sauti tokea nyuma. Alikuwa ni Bozi akiwa amejiveka shuka moja kubwa jekundu.
“Naweza nikapata wasaa wa kuongea na wewe?”
“Kwa sasa, hapana. Malkia amenituma kumtafuta Jenerali.”
“Oooh, huwezi jua labda naweza nikasaidia,” akasema Bozi kwa tabasamu.
LAKO JICHO.....
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN (MWISHO WA MSIMU WA KWANZA)*
*Simulizi za series*48
ILIPOISHIA
Benadi alipotoka nje, akatembea kwa umbali mfupi kabla hajasikia jina lake linaitwa na sauti tokea nyuma. Alikuwa ni Bozi akiwa amejiveka shuka moja jekundu.
“Naweza nikapata wasaa wa kuongea na wewe?”
“Kwa sasa, hapana. Malkia amenituma kumtafuta Jenerali.”
“Ooh, huwezi jua labda naweza nikasaidia,” akasema Bozi kwa tabasamu.
ENDELEA
Basi wakasogea kando, mahali ambapo hamna watu, wakateta ambapo Bozi akamshirikisha Benadi juu ya mpango wao wa siri. Benadi akashtuka sana. Akahofia mwanzoni. Ila Bozi akamwambia kwamba wapo wengi nyuma yao.
“Kuna wenzako ambao tayari wameshajiunga nasi. Tuna jeshi kubwa na watu wenye ushawishi.” Bozi akasema na kuwataja watu kadhaa. Kidogo, Benadi akapooza. Ila bado tu alikuwa na chembe za mashaka kwani jambo aliloambiwa halikuwa dogo hata kidogo.
“Hakikisha inakuwa siri. Hili ni jambo ambalo linafanyika chini kwa chini.”
Benadi akaomba apewe muda. Akaenda zake akisindikizwa na macho ya Bozi mpaka ndani, kisha Bozi akaenda zake. Akaenda kukutana na wanajeshi fulani ambao aliwapa kazi ya kumtazama Benadi.
Ilitakiwa wajue sasa harakati zote za Benadi asije akamwaga mchele kwenye kuku wengi. Kama akikataa, basi amalizwe mapema.
“Hakikisha mnajua wanaoingia na wanaotoka ndani ya nyumba yake. Kila mtu anayeongea naye na kuwasiliana naye. Sawa?”
“Sawa,” wakaitikia wanajeshi na kwenda zao kutekeleza agizo.
***
Usiku ukazidi kujongea na kuwa mzito. Kwa majira ya sasa, tungesema ni saa nne ya usiku. Na ilikuwa ndani ya Kasri ya mfalme wa Phares.
Kila kitu kilikuwa mezani kikiwa kimepangiliwa vema. Mabakuli yaliyobebelea vyakula vya kila aina na vinywaji, ambavyo vingi vilikuwa ni mvinyo mwekundu. Basi Tattiana akamwita mfalme na kumwambia kwamba chakula tayari na hivyo ajongee.
Lakini wakati huo si kwamba Mfalme alikuwa tumbo tupu, lah! Alikuwa tayari ameshapewa ka chakula ka kusogezea muda. Kale cha kumfanya asipige mihayo.
Akanyanyuka na kujongea mezani. Siku hiyo hakukuwa na kijakazi yoyote yule wa kumhudumia mfalme isipokuwa Tattiana peke yake. Mwanamke huyo aliwaonba vijakazi wote wapumzike na ni yeye ndiye atahusika na kila kitu.
Akampakulia chakula mfalme kisha kabla hajaketi akabakia kusimama apate majibu yake. Mfalme akang’ata na kutafuna. Na akanywa pia. Hakika akapenda chakula kile. Kilikuwa kitamu haswa.
Akatabasamu akimtazama Tattiana.
“Unaweza ukakaa?”
Tattiana akaketi akiweka mikono yake mapajani. Mfalme akamsifia kwa chakula chake kitamu na amekifurahia sana.
“Ni nani aliyekufundisha kupika hivi?”
“Mama yangu.”
“Ni ajabu kuona binti wa familia kama ya kwako akijua kupika hivi.”
Tattiana akatabasamu pasipo kusema kitu. Alitazama tu chini. Basi mfalme akala chakula mpaka akashiba. Akafurahia sana maana hakuwahi kula chakula kitamu vile.
Huenda na sura ya Tattiana ilichangia kwake kuona chakula kitamu. Uso wa binti huyo ulikuwa ni kielelezo tosha cha namna gani Mungu alivyo hodari wa kuumba.
Mpaka anamaliza chakula, mfalme alikuwa anamtazama tu Tattiana. Huku naye binti huyo akitazama chini na kutabasamu mwanana.
Binti akatoa vyombo ambavyo mfalme amekula navyo kisha akareja na kuketi na mfalme. Akamuuliza:
“Kuna kingine ambacho ningeweza kukuhudumia mfalme wangu?”
Mfalme asiwe na kauli, akatikisa kichwa chake. Kabla muda mfupi hawajaenda kupumzika wote. Huko mfalme akapata kujua mwili wa Tattiana. Alikuwa ni msichana ambaye hakumjua mwanaume hapo kabla.
Baada ya kumaliza tendo, mfalme akapitiwa na usingizi mzito akimwacha Tattiana mkavu asiye hata na lepe.
Alikuwa anatafakari siku nzima ilivyoenda. Namna ambavyo alivyokuwa anachakarika na hatimaye akafanikiwa kumfurahisha mfalme. Akajiuliza sana, vipi kama akija kuwa malkia itakuaje? Atafanya nini?
Hakujua. Ni kitu ambacho hakuwahi kukitarajia maishani mwake. Kulala na mfalme, tena ndani ya chumba cha kasri! Haikuwa kawaida.
Basi akanyanyuka na kwenda mpaka dirishani mwa chumba. Akafungua dirisha na kutazama nje. Kama haitoshi akatoka chumbani na kwenda kuzurura kasri nzima.
Alifurahia sana mazingira ya mule.
Ila akiwa anazurura zurura, akajikuta anamkumbuka Roboth, mpenzi wake wa enzi. Alienenda dirishani upande ule ambao makazi ya Roboth yalikuwepo, akatazama kana kwamba anamwona.
Alijitahidi kumpuuzia maana alikuwa anaelekea maisha mapya. Maisha ambayo yangewafanya wazazi wake wajivunie. Maisha ambayo yangempatia heshima tele kwenye uso wa himaya ya Goshen.
Kukosa huko usingizi kukamfanya awaze mawazo mengi sana, yenye tija na yasiyo na tija. Alirejea chumbani kwa mfalme akaendelea kutafakari, lakini haikupita muda mrefu sana, akataka sasa kulala.
Akalaza mgongo wake kitandani na kumwekea mkono mfalme. Akagundua mwanaume huyo ni wa baridi kupitiliza. Akashangaa sana maana haikuwa kawaida. Ndani kulikuwa kuna joto, na hata blanketi walilokuwa wamejifunika lilikuwa zito.
Sasa baridi limetokea wapi? Ama mfalme anaumwa?
Tattiana akamtazama mfalme, mbona haonekani kama anayeumwa! Mbona hakumwona kama ana dalili zozote za kuumwa?
Akaondoa mkono wake mwilini mwa mwanaume huyo maana kadiri alivyokuwa anauweka hapo ndivyo na yeye akawa anahisi baridi mwili mzima. Alijigeuzia kando alale.
***
“Sasa tunafanyaje? Ndiyo hatutatoka humu?” sauti ya kike iliuliza ndani ya lupango.
“Unajua kwa mara ya kwanza, hawakuwa wameweka ulinzi maradufu kiasi hiki. Sasa hata mlango wameufunga huko nje kwa komeo si chini ya tatu,” sauti ya kiume ikajibu.
“Endapo tusipotoka humu, basi Malkia ataisha. Hakuna mtu mwingine wa kumwamini huko nje.”
“Basi inabidi tufikirie namna ya kujichoropoa humu.”
“Lakini kivipi? Mawazo yangu yamegoma kabisa. Au una wazo lolote?”
“Hapana, ila ntalipata tu tena karibuni.”
Mara wakasikia sauti za watu wakiingia chumbani. Basi wakakaa kimya kusikiliza. Lupango waliyomo iliwaruhusu wao kufanya hivyo maana ilikuwa inapakana na sehemu ambapo wakina Bozi walikuwa wanapenda kukutana kufanyia majadiliano.
Wakasikia sauti ya mwanaume mmoja, na punde ikakaribishwa na ya Bozi kuketi chini.
Kadiri sauti hiyo mpya masikioni mwao ilivyokuwa inaongea, basi Fluffy akaitambua. Ilikuwa ni ya Benadi. Akamnong’oneza Seth, sauti hiyo anaijua. Wakasikiliza na kugundua kuwa Benadi alikuwa naye amesilimu na kujiunga na wakina Bozi.
“Lakini mtanipangia nyadhifa gani?” Sauti ya Benadi ikauliza.
“Usijali,” Seth akajibu. “Wewe sasa hivi ni kaimu, ila kwenye serikali mpya, wewe ndiye utakuwa jenerali.”
Sauti ya Benadi akicheka ikavuma. Kisha sauti ya meza ikikitwa. Bila shaka kicheko kilikuwa kipana.
“Basi tupo pamoja. Hilo halina wasi kabisa,” Benadi akasema.
“Sawa sawa. Basi kuna kazi moja ambayo tunataka uitekeleze. Kazi hiyo itakapokwisha, basi na filimbi ya kuhitimisha mchezo itakuwa imepuluziwa papo.”
“Ipi hiyo?”
“Kummaliza Malkia.”
Sauti ya mguno ikaita. Kisha Benadi akasema:
“Ila si rahisi.”
“Kwako ni rahisi kuliko kwetu,” Bozi akasema. Kukawa kimya kwa muda. Kisha sauti ya mtu akishusha pumzi ndefu.
“Vipi, kuna shida yoyote? Kama kuna tatizo ama mahali umekwama tunaweza kusaidiana.”
“Vipi lakini haitasababisha namna yoyote ya kuwatia watu hofu, na pengine nikaonekana msaliti?”
“Benadi, hakuna namna ya kukimbia maneno ya watu siku zote. Ila labda cha kukuarifu ni kwamba, tunataka mambo haya yafanyike kimya kimya. Hatutaki mtu yeyote afahamu mpaka pale tutakapokuwa tumekamilisha kila jambo. hivyo tungeshauri ukatumia sumu kummaliza. Na ni bora ikawa chakulani.”
“Sumu?”
“Ndio. Tayari ipo, ni swala la kutiwa tu kwenye chakula.”
“Sawa, ntajitahidi.”
Sauti ya makofi mawili ikasikika, na mara vishindo vya miguu vya mtu vikasikika. Punde kidogo.
“Hii hapa. Utatia kidogo tu. itammaliza chini ya siku tatu.”
“Sawa. Naweza nikaenda sasa.”
“Ndio. Utatupa mrejesho.”
Zikasikika vishindo vya miguu na kisha ikafuatiwa na sauti ya mlango kufungwa. Mara ikasikika tena sauti ya makofi na vishindo vya watu wasiopungua wawili.
“Kaendeleeni kutekeleza kazi yenu,” sauti ya Bozi ikasema. “Hakikisheni mnajua kila nyendo zake. Kila anapotoka na kurudi asije akatuchoma.”
Baada ya hiyo kauli, vikasikika vishindo vya miguu vikipotelea. Kisha kukawa kimya kabisa. Basi sauti ndani ya lupango zikadakia.
“Seth, wanaenda kumuua Malkia.”
Kimya kidogo. Mara sauti ikauliza:
“Unaweza kuchimba?”
Hakukuwa na majibu. Ila mara sauti ya mtu akifukua gizani ikaanza kusikika. Na ilikuwa inaongezeka kadiri na muda.
“Tusaidiane, tufanye upesi. Hii ndiyo njia pekee ya kututoa nje.”
***
Walipokuja kuzinduka, wakajikuta mbele ya kiti kikubwa cha rangi nyekundu. Hakuna aliyeelewa hapo wamefikaje, wakabak kutazamana: Rhoda, Tretho na Bonas.
Vichwa vilikuwa vinawauma vikiwagonga haswa. Walitazama huku na huko hawakuona kitu isipokuwa giza. Ni pale tu walipokuwa wamejilaza, na mbele kidogo penye kiti ndipo palikuwa na mwanga. Huko kwengine kote macho hayakuweza kuona jambo.
Na pale kwenye kiti kile chekundu palikuwa patupu. Hawakujua nani alikuwa amekaa pale. Na ameenda wapi. Wakatazamana. Na pengine wakaulizana maswali ambayo hakuna kati yao aliyekuwa na majibu.
Ila haikupita muda mrefu, wakasikia sauti ikitokea pale kitini. Ikiwaambia:
“Nimewapa muda ili mnipe sababu za kuwaachia uhai wenu.”
Hawakujua anayenena ni nani. Wakauliza ila hawakujibiwa. Walitawaliwa na hofu kubwa. Ukapita kama dakika tatu, na mara popo wakavamia eneo hilo. Wakatanda kiti na mara akatokea mtu hapo!
Popo wale wote walipotelea ndani ya mwili wa huyo mtu. Yaani yeye ndiye aliyekuwa popo hao wote.
***
TUKUTANE WEEK END HII KWENYE MUENDELEZO WA MSIMU WA PILI MBARIKIWE SANA KWA KUWA WOTE PAMOJA [emoji120]
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 32*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kukawa kimya. Sauti ya upepo pekee ndiyo ikivuma na kupuliza huku na huko.
Usiku ukazidi kusonga.
Zikiwa zimepita kama dakika thelathini tangu Ghaut amezwe na mchanga, Seth akawashtua tena wenzake baada ya kuona kitu cha ajabu kwa mbali.
Kilikuwa ni kile kiumbe kilichokuwamo ndani ya pango! Sasa jua lilikuwa kimetokomea, anaweza kuringa na kutamba. Sasa ulikuwa ni muda wake. Alikuwa amekuja kudai mifupa ya wageni wake.
ENDELEA
Kiumbe huyu alikuwa mwembamba mwenye rangi nyeupe ya kufifia. Kichwa chake kisichokuwa na nywele kilikuwa cha duara inayokaribia pembe tatu, macho yake makubwa rangi ya kijani, kifua chake kimechomoza mbavu, mikono mirefu na mipana.
Alikuwa anatembea kilevi lakini akionyesha mwenye nguvu. Miguu yake ilikuwa inatawanya michanga ya jangwa kana kwamba maji. Mdomo wake mdogo wenye meno ya paka ulikuwa wazi akiwatazama walengwa wake anaotaka kuwatia kinywani.
Na mate yalikuwa yanamchuruza.
Kiumbe gani hiki? Wakajiuliza wakina Malkia wakitumbua macho. Hawakuwa wanaamini wanachokiona. Hawakujua kiumbe hicho kinataka nini lakini kwa haraka wakaamini hakijaja pale kwa kheri.
"Wewe ni nani?" Seth akapaza sauti. "Unataka nini?"
Kiumbe kile wala hakikuongea, kikazidi kusonga kuwajongea kana kwamba hakijasikia. Seth akabadilisha lugha takribani nne akimuuliza kiumbe kile maswali hayohayo, hatimaye akafanikiwa!
Aliongea lugha anayoielewa. Lugha hii ilikuwa ni ki-injin, lugha inayozungumzwa na idadi ndogo sana ya watu waishio mabarafuni. Ilikuwa na maneno machache, na endapo ukiiskiliza vema utatambua inarudiarudia sana maneno lakini kumaanisha maana tofauti.
"Kukluf kazif tekop, meshan kabac tubuknova," akateta kiumbe yule akiwa anazidi kusogea.
"Anasema nini?" Zura akawahi kuuliza kwa hofu. Macho yake yalijawa woga, mikono yake ilikuwa inatetemeka.
Seth, kwa haraka, akawakalimania kwamba kiumbe yule anaitwa Kazif na amekuja hapo kuchukua kilicho chake.
"Kipi hicho?" Malkia akawahi kuuliza. Alimgeuzia uso Seth lakini macho yakiwa kwa yule mgeni wao anayezidi kujongea.
Seth akamuuliza tena yule kiumbe kwa lugha anayoielewa, hapo amekuja kufuata nini hicho kilicho chake? Kiumbe kile pasipo hiyana, akasema mifupa. Anahitaji kwenda kujaza pango lake zaidi.
Malkia akataka kunyanyua panga, Seth akawahi kumtazama na kumzuia kwa ishara ya kumwonyesha kiganja.
"Acha tuongee naye kwanza."
Kisha akamwomba kiumbe yule aketi chini wapate kuteta. Wao hawana maana ya kuzua shari. Kwa kusikia ombi hilo, kiumbe kile kikaketi kikiwatazama. Zura na Fluffy wakazidi kupata hofu. Kiumbe hicho hakikuwa kinavutia kukitazama hata kidogo.
Kadiri kilivyosogea basi kingekufanya tumbo likusokote kwa woga. Miguu ife ganzi. Na haswa kikikutazama, ungeweza kupata haja zote kwa mpigo!
Tangu kiumbe hichi kiliposogea hapo, hali ya hewa ikageuka na kuwa baridi zaidi. Ungemtazama vizuri ungebaini alikuwa anafuka moshi. Moshi wa barafu.
Si bure hakuwa anapatana jua maana angeweza kuyeyuka.
Basi Seth akamwomba awabakizie uhai wao, na watakaporejea toka safari yao ya mbali watampatia zawadi kama fadhila. Kiumbe hicho kikakataa na kusema:
"Habaq quatta kilim meshan, juata himas!" Akimaanisha kama wamemkatalia ombi lake basi wacheze naye mchezo. Seth akamuuliza mchezo gani huo, Kazif akamwambia unaitwa 'Yuaj si Kobil' - maji ama damu.
Akauelezea mchezo huo. Atawauliza mafumbo matatu na endapo wakiyakokotoa atawapatia maji, na endapo wakishindwa basi wao watampatia damu.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kuweka nao makubaliano.
"Hapana," Malkia akakataa. "Hatuwezi kucheza naye mchezo huo wa hatari kiasi hicho. Tupambane naye!"
"Lakini vipi kama tukapoteza zaidi kwa kupambana naye kuliko njia hii ya kidiplomasia?" Akauliza Seth. "Vipi kama tukashinda, tukabaki salama na maji akatupatia? Si rahisi kupambana na kiumbe hiki!"
Lakini bado Malkia akawa na woga. Seth akamsihi wachague mchezo huo, na kwa pamoja watashirikiana kufumbua mafumbo hayo. Vichwa vitano si sawa na kimoja.
Basi wakamruhusu kiumbe yule aanze kuuliza mafumbo yake. Hapa chini kama yalivyotafsiriwa:
La kwanza, kikapu kina matufaha matano na nina watoto watano. Nitayagawanyaje haya matufaha matano kwa watoto wangu na kwa wakati huo tufaha moja likabaki kapuni?
"Tumekwisha!" Akasema Fluffy akitoa macho. "Mbona anauliza maswali ambayo hayawezakani!"
Seth akasafisha koo lake kisha akafikiri kidogo. Akajibu atawapatia matufaha manne kwa wale watoto wa nne, alafu mtoto wa tano atampatia tufaha likiwa limebaki ndani ya kikapu.
Wakastaajabu mojawapo ya chupa yao imejawa na maji. Walikuwa wamepata!
La pili, anayekitengeneza, hakihitaji. Anayekinunua hakitumii. Anayekitumia hawezi kukiona wala kukihisi. Ni nini hicho?
Seth akatabasamu, haraka akajibu ni sanda. Basi chupa lao la pili likajawa na maji. Wakafurahi. Kile kiumbe kikang'ata meno yake kwa hasira. Sasa akadhamiria kuuliza fumbo gumu la mwisho ili angalau asiwe amepoteza muda wake bure.
La tatu, nyakati za mchana huzitumia dirishani, nyakati za chakula naenda mezani, nyakati za usiku najificha hamnioni. Mimi ni nani?
Seth akatabasamu tena, upesi akajibu ni nzi. Bobo lao moja lilio tupu likajaa maji! Alikuwa amepata! Sasa kiumbe huyu akawa ameshindwa kutimiza adhma yake. Lakini kwa ukaidi, akasema anaongezea swali moja la mwisho.
Seth na wenzake wakatahamaki. Malkia akasema yule kiumbe hakuwa anataka kuwaacha hai, inabidi wapambane. Lakini Seth akawatoa hofu, hawakuwa na haja hiyo. Wamwache huyo kiumbe atupe turufu yake ya mwisho.
La nne, kuna wadada wawili: mmoja anamzaa huyo wa pili, alafu naye huyo wa pili anamzaa huyo wa kwanza. Hawa wadada wawili ni wakina nani?
Seth akamtazama Malkia kisha Fluffy na baadae Zura. Akawauliza kama wana majibu, wote wakasema hawana. Wakajawa pia na hofu baada ya kuona Seth anawauliza wao. Walikuwa wanamtegemea yeye kwenye hili.
Lakini mara Seth akatabasamu, akamtazama kiumbe yule na kumjibu dada hao ni usiku na mchana.
Kiumbe kile kikakasirika mno. Alikuwa ameshindwa! Akasaga meno yake na kupiga ngumi kiganja chake. Akamwambia Seth kwamba ameshinda kwa leo lakini anajua itawachukua siku kadhaa kumaliza jangwa hilo kwahiyo kila siku usiku atakuwa anawatembelea na kuwauliza mafumbo kadhaa.
Hawatayapata siku zote hizo, aliamini na kuwaaminisha. Akaenda zake akiwa ameghafirika.
"Uliyajuaje mafumbo yote yale?" Fluffy akamuuliza Seth akiwa na kimuhe. Seth akamwambia baba yake alikuwa akimuuliza sana akiwa mtoto, vile vile vitabu vingi alivyovisoma. Wakampongeza sana kwani alisaidia kupata maji ambayo hawakujua wangeyapatia wapi.
Lakini kwa wakati huo, yule kiumbe, akiwa amepania kwa dhati, akaenda kukesha usiku mzima kupitia mafumbo yake aliyoyaandika kwenye kuta za pango. Hata kula hakutaka!
***
*MKUFU WA MALKIA II -- 52*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Lakini getini kulikuwa kuna walinzi. Wanaume watatu waliobebelea silaha. Wangefanyaje?
Na wakiendelea kukaa hapo, sebuleni wakiwa hawajui la kufanya, wale vijakazi wengine wawili watakawakuta. Watawaacha?
ENDELEA
Hakukuwa na namna. Iliwabidi waruke ukuta kwa kusaidiana wakatokea huko upande wa pili na kuanza kukimbia. Hawakujua wanapoelekea ila alimradi waondoke na kuacha mbali nyumba ya kuhani huyo.
Walipokimbia sana, wakasimama wapumzike. Mapafu yalikuwa yamekaukiwa. Wakashika magoti yao wakihema kama mbwa.
Walikuwa wanavuja jasho haswa. Macho yamewalegea kana kwamba wamepigwa na moshi. Ottoman hata akaketi chini baada ya kuhisi viungo vinamuuma haswa.
Hapa ndiyo akamuuliza mwenzake, nini kilimsibu kujaribu kumuua kuhani? Oragon akamwambia mwanaume huyo alimtaka kimapenzi.
Ottoman akatoa macho.
"Una maanisha nini?"
"Alitaka nimlale!" Oragon akajibu kwa midadi.
Ottoman akashika mdomo wake kwa mshangao. Ilikuwa ngumu kuamini mzee yule, mwenye nafasi yake kubwa ndani ya himaya, alikuwa na michezo hiyo.
Kumbe ndiyo maana hana mke wala mtoto! Wakang'amua. Lakini sasa tunafanyaje na wapi tunaenda? Swali lilikuwa hapa. Na wapi pia watapata chakula?
Wakakaa hapo kama kinda za ndege zilizompoteza mama yao. Na kwakuwa walitoka mbio kwa kuhani, hawakuwa wamebeba chochote kile mikononi mwao. Hata 'vituguo' vya kujihifadhi ama kujifunikia.
Wakalala wakiwa wamejikunyata, miili yao ikipambana na baridi kali. Wakisimamisha masikio yote kusikia ujio wa shari toka pande yoyote ya dunia.
**
"Mbona nakuita muda wote huo, hukunisikia?" Raam alifoka. Alikuwa yupo uchi chini sakafuni akiwa ameshikilia kichwa chake kinachomimina damu. Sakafu ilikuwa imetapakaa damu. Na mwili wake ulikuwa umeshika damu upande wake wa kushoto alioulalia.
Mbele yake alikuwa amesimama bwana Marimari mmoja wa vijakazi wake wa ndani.
"Sikukusikia, mkuu," akasema Marimari. Alikuwa amepigwa na butwaa kumwona mkuu wake katika hali ile aliyomkuta.
"Wako wapi wale vijana wapya?" Akauliza Raam. Kabla hajasubiria majibu akaagiza: "wakamateni na muwamalize mara moja!"
"Hawapo!" Marimari akampasha. "Sijawaona kwa muda sasa hapa ndani hata nikajua umewatuma huko nje."
Raam akashika kichwa chake kwa maumivu. Habari hizo zikamuumiza kichwa zaidi. Akajitahidi kunyanyuka akisaidiwa na Marimari, akajiveka joho jepesi na kutoka ndani kwenda kuonana na walinzi wake langoni.
Akamtaka abakie mlinzi mmoja tu, hao wengine wote, pamoja na wale ambao hawapo zamu, wajumuike wakawatafute wakina Oragon popote pale walipo.
"Mtakapowakamata, muwamalize asijue mtu yeyote yule. Sawa?"
"Sawa, mkuu!" Wakaitikia kwa ukakamavu.
"Ni wageni himayani hivyo hawatawasumbua kabisa. Mkiulizia mtawapata kwa urahisi, na hata wakichangamana na wenyeji mtaweza kuwachambua. Vilevile mkiwaua hakuna atakayewaulizia wala kusumbuka nao," Raam aliwapasha zaidi. Baada ya maelezo hayo, wanajeshi wakaenda zao kwenda kuwasaka vijana hao.
**
Kwa mbali wanaume wawili walionyeshea kidole upande wao wa kulia wakinong'onezana. Mmoja alikuwa mwanaume mfupi na mwingine mrefu. Kwakuwa ilikuwa giza, ilikuwa ngumu kuwatambua.
Baada ya kunong'onezana huko wakasogea kwa haraka na kusimama mbele ya wanaume waliokuwa wamejilaza chini.
Walikuwa ni wakina Oragon!
"Nyie!" Wakawaamsha wakiwasukuma na miguu. "Amka! Amka! Amka!"
Wakina Oragon wakamka kwa hofu kubwa wakidhani wameshatiwa nguvuni. Walipotazama vema wakagundua ni wale wanaume waliowakwapulia kila kitu chao. Wakataka kuzua ugomvi, lakini mara wanaume wale wakachomoa jambia zao na kuwatishia kuwanyofoa uhai.
"Tulieni hivyo hivyo kabla hatujawatoboatoboa!"
Wakanywea akama ukili majini. Wanaume hao wakawasachi mifukoni lakini hawakupata kitu. Badala yake wakina Oragon ndiyo wakawaomba wawafadhili kwani hawana mbele wala nyuma.
"Naomba mtupatie fedha kidogo," akasema Oragon. "Hatuna hata cha kutia mdomoni."
Wale wanaume wakatazamana, alafu yule mfupi akarudishia jambia lake kiunoni na kuwaambia kama wanataka kula basi waungane nao la sivyo waozee hapo.
"Mnafanya shughuli gani?" Ottoman akauliza.
Wanaume hao wakacheka alafu mrefu akasema:
"Yani mpaka sasa hamjajua tu tunafanya shughuli gani?"
Kisha wakacheka tena.
**
"Mwambie ntalizingatia, anipatie muda tafadhali," alisema Phares akimwambia mwanaume mgeni aliyekuwa ameketi naye. Mwanaume huyu alikuwa ana ndevu za wastani, nywele nyeusi ti ndefu mpaka begani, na kwenye kifua chake upande wa kushoto alikuwa ametundika alama ya ndege, ishara ya himaya ya Maam.
Mwanaume huyo, mjumbe wa Maam, akanyanyuka na kumpatia mkono mfalme.
"Nitamfikishia habari hizo, lakini nisiwe muongo, hamna muda wa kungoja tena. Keshokutwa anaapishwa kuwa mfalme na hawezi akaapishwa pasipo kuwa na mke."
Mjumbe huyo akashusha pumzi ndefu na kutengenezea nguo yake.
"Kwahiyo kiuhalisia muda ulionao ni kesho tu mpaka majira ya jioni," akasema mjumbe kisha akaondoka zake mfalme akimsindikiza kutoka naye nje. Mjumbe huyo alipoyoyoma mfalme akarudi zake ndani akiwa na mawazo.
Sasa ni rasmi kijana wa mfalme alikuwa anamtaka Tattiana akawe malkia wake. Harid alishampasha habari kijana huyo kuwa Tattiana ndiye mrembo himaya nzima.
Na ubaya zaidi, hata mjumbe huyu aliyetumwa kuja hapo himayani, alikutana na Tattiana akasadiki hayo maelezo. Akasema Alah! Kweli huyu afaa.
Sasa afanyaje?
Mfalme akahisi kichwa kinamuuma. Hakuwa radhi kumpoteza Tattiana hata kidogo.
**
Ni usiku sasa. Tattiana hakuwa katika chumba kimoja na mfalme kama inavyotakiwa, bali katika kile chumba alimokuwa anaishi malkia Vedas.
Humo alikuwa tayari ameshafungua kabati na kuchukua chupa ile ya maajabu. Anaitazama na kujiuliza maswali kichwani.
Anaisikiliza chupa hiyo na kusikia ikidunda mapigo ya moyo. Anasikiliza tena na kuhakiki kweli, yalikuwa ni mapigo ya moyo.
Leo anapata wazo na kuanza kung'amua kitendawili hiki. Alijiuliza:
"Nimelala na mfalme kwa muda wote huo, amekuwa baridi mpaka nashindwa kulala. Lakini pia sijawahi kusikia mapigo yake ya moyo, hata nilipolaza kichwa changu kifuani mwake.
Ina maana hana moyo?" Akajiuliza akitazama chupa ile.
"Au moyo wake ndiyo huu chupani?"
Habari hiyo ikaleta mantiki.
"Lakini nani kauweka moyo huo humo? Inawezekanaje mfalme akaishi na huku moyo wake upo chupani?" Maswali hayo yalimpasua kichwa. Na kama haitoshi basi, yule kiumbe anayetoka nje ya chupa pale ifunguliwapo, ni nani?
Akakumbuka yale maneno yake: "Nefil njhami khatu habab?" Anamaanisha nini?
Ikiwa ni usiku sasa mkali, akiwa ndani ya mawazo haya, mara anasikia harufu ya ajabu. Akanusanusa kuhakiki. Hakuijua harufu hiyo ni ya nini. Na kadiri na muda ilikuwa inaongezeka!
Akashindwa kuipuuzia. Akaificha chupa kabatini na kuanza kuifuatilia harufu hiyo. Akafungua milango na kutembea akikatiza korido kadhaa akiacha pua ifanye kazi yake.
Mwishowe akajikuta amefika kwenye kingo ya kasri. Kwenye kakona kidogo alikuwa amesimama Bella akiwa ameshikilia miti kadhaa mikononi mwake. Miti hii ilikuwa inafuka moshi mweupe.
"Bella," Tattiana akaita. "Unafanya nini hapo muda huu?"
Bella hakujibu. Akawa anamtazama Tattiana kana kwamba alikuwa anamtarajia. Tattiana akasogea karibu zaidi. Kuangaza akaona askari kadhaa wakiwa wapo chini.
Hakuelewa kilichokuwa kianendelea pale.
"Bella, unafanya nini hapa? Na hao maaskari mbona wapo chini?"
Tattiana akawatazama vema wale maaskari. Akagundua walikuwa wamekufa. Macho na midomo yao ilikuwa wazi!
Akamezwa na hofu. Lakini kufumba na kufumbua, kabla hajatenda hata jambo, akasukumizwa kwanguvu na mtu tokea nyuma. Akajigonga na kizuizi cha kibaraza, akabinuka na kudondokea chini!
Bella na Lucy, aliyetokea nyuma, wakamtazama. Lucy akabinua mdomo wake na kusema:
"Amekwisha."
Bella akamalizia.
"Tufanye upesi!"
**
Shunie hii nayo ilikuwepo kwa story kumbe! HahaaaaaaNguvu ya papuchi
Nipo dadangu, mizunguko tu ya maisha.Upooooo nani kakuteka jamani
Usijali tuko pamoja.Pole sana kaka nimekumiss tu mm