Mkufu wa Shani - Sehemu ya 2

raoka kubanda

Member
Jun 13, 2017
45
24
MKUFU WA SHANI (2)
IMETUNGWA NA BEKA MFAUME
[The Greatest]

ILIPOISHIA

Kabla hajateremka kutoka kwenye gari ambalo tayari lilishaegeshwa kwenye maegesho ya nyumbani na mume wake aliyekuwa akiliendesha, Shani akaingiwa na hisia kuwepo na hitilafu shingoni kwake. Hisia hizo zikaenda sambamba na kuupeleka mkono wake kifuani. Akapapasa kwa papara kama aliyekuwa akitarajia kuna kitu kimetokea, papohapo akauinamisha uso kuangalia miguuni kwake. Alichokihisi, akakiona kimetokea kweli. Mkufu wake ulikuwa haupo shingoni.

“Mungu wangu!” alisema kwa sauti iliyotaharuki huku mkono wake ukiwa bado kifuani.

SASA ENDELEA…

Mume wake aliyekuwa tayari ameufungua mkanda wa kiti na kujiandaa kutoka kwenye gari, akasita kufanya hivyo baada ya kushtushwa na sauti ya mkewe. Akamwangalia na papohapo kuuliza, “Vipi?”
“Mkufu wangu!” Shani alisema huku akiangalia chini na miguu yake kuisogeza sogeza kama atauona mkufu wake.

Mume wake anayejulikana kwa jina la Abdu Mgiriki mcheza mpira wa miguu wa zamani, palepale naye akaangalia chini ilipo miguu ya mkewe kana kwamba angeuona mkufu huo. Pekua pekua ya haraka ikaanza. Shani akateremka kutoka kwenye gari na kupiga magoti nje ya mlango uliokuwa wazi akichungulia chini ya kiti na wakati huohuo mkono wake ukisaidia kupapasa.

“Una hakika ulikuwa umeuvaa?” mumewe alimuuliza.
Shani hakujibu. Hakutaka kujibu swali lililomkwaza. Hakuamini yeye na mumewe waliotoka pamoja nyumbani, tena wakitoka chumba kimoja walichokitumia kuvalia nguo, kisha wakazungumza mara kadhaa kabla ya kupanda gari na kuelekea mjini na kisha kurudi wote pamoja, halafu mumewe awe hajauona mkufu aliokuwa ameuvaa kifuani kwake? Swali gani la kijinga! Shani aliwaza.

“Turudi!” Shani alimwambia mumewe bila kujibu swali aliloulizwa.
Uso wa Abdu ukaonekana kama vile umeota jipu. Hakuamini alichokisikia, kwa sababu alijua kilichomaanishwa na mkewe ni kumtaka warudi tena mjini. “Turudi wapi?” aliuliza huku sauti yake ikiwa na hamaki.
“Mjini tulipokuwa tumeliegesha gari. Nahisi pale ndipo ulipoanguka,” Shani alisema huku akisimama.
“Turudi tena mjini kwa ajili ya mkufu tu?” Abdu alijibu kwa sauti ya kulidhihaki swali la Shani. “Una mikufu mingapi ya dhahabu? Naamini hata mingine umeisahau ilivyo!” Akajenga kituo. Kisha akamalizia kwa kusema. “Mi sirudi mjini!”

Shani akionekana mtulivu usoni akawa kama aliyegandishwa na jibu la Abdu. Akamwangalia mumewe kana kwamba anaisoma akili yake. “Umejuaje kama nimepoteza mkufu wa dhahabu?”
“Si ndio uliokuwa umeuvaa? Ule wenye jina lako!” Abdu alijibu huku hamaki ingalipo.
“Mbona umeniuliza kama nina uhakika nilivaa mkufu?”

Swali hilo likaonekana kumpiga Abdu. Hata hivyo hakukubali kushindwa. “Kwa hiyo ndio unataka turudi mjini kwa ajili ya huo mkufu?” alijitetea. “Unayo mikufu mizuri mingapi niliyokununulia? Leo huu mmoja uturudishe mjini? Na una hakika gani kama utaukuta?”

“Sisemi kama nina hakika ya kuukuta, nataka tu kwenda kujiridhisha. Wangapi walishaangusha vitu vya thamani na waliporudi kuviangalia walivikuta?”

Abdu akionekana kutokubaliana na mawazo ya mkewe ya kurudi tena mjini, aliangalia pembeni huku akionekana kukwazwa na dai la mkewe. “Nitakununulia mwingine kama huo!” alisema.
“Tatizo si kuupata kama huo!”

Abdu akayarudisha macho na kumwangalia Shani. “Kwa hiyo tatizo ni nini?”
“Huu mkufu nimepewa na mama, Abdu!” Shani alisema kwa sauti iliyoonesha kutaka kulia. “Mama aliniomba niutunze na uwe kumbukumbu yake pindi atakapokufa. Na alininunulia zawadi hii baada ya kupata mafao yake ya kustaafu. Leo mama amekufa, na hii ndiyo kumbukumbu kubwa ninayomkumbuka nayo. Leo Abdu unaniambia nipotezee kama vile hakuna kitu kilichopotea. Kufanya hivyo najiona kama ninayempuuza mama yangu. Angalau nimwonyeshe kujali kwa kwenda kuutafuta ili hata huko kuzimu alipo atajua nimehangaika kuutafuta. Suala la kuninunulia mwingine hilo ni chaguo la pili endapo nitaukosa, lakini kwanza wacha nikautafute!”

“Acha na fikra za kiitikadi Shani, eti mama yako ataona umemdharau huko aliko. Twende katika uhalisia wa jambo. Kubali mkufu umeshapotea! Hizo fikra eti ukienda kuutafuta utakuwa ndiyo umemthamini mama yako, hizo ni fikra potofu. Kwani nani asiyemthamini mama yake Shani? Hata mimi mama yangu amekufa. Ni kukubali tu mama amekufa, full stop! Hizo stori za sijui mama huko alipo atakuona humthamini kwa sababu hukuutafuta mkufu aliokununulia ulipopotea, hayo ni mawazo ya kijinga!”

Shani aliyekuwa amesimama nje, akasogea hadi pembeni mwa boneti la gari. “Naomba hiyo swichi!” alisema kwa sauti iliyoonyesha kuumizwa na kauli ya mumewe.

“Nikupe swichi ili uendeshe gari urudi mjini? Halafu ukipata ajali? Twende ndani ukapumzike! Unaonekana umeshachanganyikiwa kwa kuupoteza huo mkufu na hutaki kukubali kama umeshapotea. Halafu unataka nikuachie uendeshe gari? Usije ukaleta msiba mwingine hapa!”

“Hauko fair Abdu!” Shani alisema machozi yakionekana kuelea kwenye mboni zake.

“Nimeshakwambia, nitakununulia mkufu mwingine unaofanana na huo ulioupoteza, tatizo ni nini?” safari hii Abdu alisema akionekana kuwa na hamaki.

Sauti ya Abdu ikamwonya Shani ambaye alijua akikazania kutaka apewe swichi ya gari huenda mambo yakabadilika hapohapo walipo na kuwa mabaya zaidi. Akarudi ndani ya gari na kuchukua mkoba wake na kuelekea nyumbani akiwa mnyonge.

Akaanza kulia bila kutoa sauti.

__________

Jioni wakati Abdu ameshatoka maliwatoni kuoga, ndipo alipotambua mkewe hayupo tayari kutoka kwenda safari waliyokuwa wamepanga waende. Safari hiyo ambayo hata asubuhi walipoamka kabla ya kwenda mjini, na hata walivyokuwa wakirudi kutoka mjini, njiani waliizungumzia kwa furaha kabla ya Shani kugundua ameupoteza mkufu wake.

Safari hiyo ilikuwa ya kwenda harusini.
Tokea walivyoyapoteza maelewano baada ya kurudi na kugundua kupotea kwa mkufu, tangu walivyoingia nyumbani baada ya kuteremka kwenye gari, amani ya watu hao wawili ikawa haipo. Shani aliyekuwa amelia na kununa, hakumsemesha tena Abdu wakiwa ndani ya nyumba.

Abdu alitarajia kukutana na hali hiyo mara baada ya majibizano yale yaliyofanyika kwenye gari. Haikuwa mara yao ya kwanza kuwa na hali hiyo inayosababishwa na mifarakano tofauti kati yao, yenye akili na isiyo na akili. Ipo ambayo Abdu aliweza kuituliza kwa kumsemesha mkewe hili na lile kisha mambo yakakaa sawa, lakini pia, yapo yaliyowafanya kufika hata siku tatu, wakiwa hawasemezani. Na kama kulikuwepo la kuzungumza kati yao, basi ni kuulizana mambo ya msingi na huku kila mmoja akimjibu mwenzake kwa sauti yenye ubaridi.

Kwa siku hiyo, Shani akiwa amenuna kwa kukataliwa kurudi mjini, Abdu aliyekuwa ametoka maliwatoni, akamwangalia mkewe huyo aliyekuwa amejilaza kitandani, uso akiwa amefudikiza kwenye mto. Kwa kiasi fulani, Abdu alijiona ana haki ya kumbembeleza Shani ili ampatie faraja kutokana na kile kilichotokea cha kupoteza mkufu wake. Akamfuata Shani aliyekuwa amelala kitandani huku akiwa amempa mgongo.

Akakaa upande wa uchagoni ambako Shani aliulalia mto. Abdu akaupandisha mguu mmoja juu ya kitanda na kisha kulilalisha begi lake karibu na mgongo wa Shani. “Shani,” aliita huku akilikamata bega la mkewe.
“Abdu, naomba uniache!” Shani alijibu bila kugeuka.

Kwanza Abdu alitulia baada ya kupewa jibu hilo. Kisha akashusha pumzi na baadaye kujiondoa taratibu kitandani. Akaondoka na kuelekea sebuleni ambako alikaa kwenye kochi na kuupandisha mguu mmoja juu ya mwingine akiwa na taulo kiunoni. Hakupendezwa na katazo la mkewe wakati alivyokuwa amekwenda kwa nia ya kumbembeleza. Akajitahidi kadri alivyoweza kuidhibiti hasira iliyokuwa ikimchemka kichwani.

Pamoja na kuwa na ghadhabu, lakini bado Abdu alihitaji kujua, kama Shani angekuwa tayari kwenda naye harusini. Jambo hilo kidogo lilimpa shida. Hakutaka aonekane anambembeleza mkewe, lakini na pia kama angetoka bila kumuuliza mkewe kuhusu safari hiyo, angekuwa bado hajatimiza jukumu lake kama mume.
Alijua asingembembeleza Shani endapo ataamua kutokwenda harusini. Lakini pia haitamfanya yeye ashindwe kwenda harusini kwa sababu mkewe amekataa kwenda. Alichotaka ni kupata jibu, Shani atakwenda, au hatakwenda! Ingawa alikuwa na uhakika, Shani hatakwenda!

Abdu akasimama kutoka kwenye kochi alilokuwa amelikalia. Akarudi chumbani. Mara tu alipoingia, akasimama na kumwangalia Shani aliyekuwa bado amelala kitandani, uso akiwa ameufudikiza vilevile kwenye mto. Akapiga hatua na kwenda kusimama kando ya kitanda. Akaita, “Shani!”
Shani hakujibu.

Abdu akaita tena, “Shani!”
“Unasemaje?” Shani aliuliza kwa ukali kama asiyetaka kusumbuliwa.
Abdu akasita kidogo kama aliyekuwa anajiuliza. Kisha akauliza, “Utaenda harusini?”
“Siendi!” Shani alijibu kwa mkato.

Abdu hakuendelea kuhoji. Akajivalia nguo zake alizopanga aende nazo harusini. Kisha akajipuliza manukato na baadaye akamwangalia tena Shani. Akajiuliza, aage au aondoke kimya kimya?

“Mi nakwenda!” hatimaye Abdu alimwambia kwa sauti isiyoonyesha kubembeleza huku akielekea mlangoni.
“Nenda!” Shani alijibu kwa kisirani bila kugeuka kumwangalia mumewe.

Jibu hilo likamfanya Abdu asimame ghafla. Akageuka kumwangalia Shani kwa sekunde kadhaa huku akipambana kuidhibiti hasira iliyokuwa ikimpanda kwa kasi. Kisha akapiga kite cha mara moja kama aliyekuwa akifikiria jambo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom