*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 32*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kukawa kimya. Sauti ya upepo pekee ndiyo ikivuma na kupuliza huku na huko.
Usiku ukazidi kusonga.
Zikiwa zimepita kama dakika thelathini tangu Ghaut amezwe na mchanga, Seth akawashtua tena wenzake baada ya kuona kitu cha ajabu kwa mbali.
Kilikuwa ni kile kiumbe kilichokuwamo ndani ya pango! Sasa jua lilikuwa kimetokomea, anaweza kuringa na kutamba. Sasa ulikuwa ni muda wake. Alikuwa amekuja kudai mifupa ya wageni wake.
ENDELEA
Kiumbe huyu alikuwa mwembamba mwenye rangi nyeupe ya kufifia. Kichwa chake kisichokuwa na nywele kilikuwa cha duara inayokaribia pembe tatu, macho yake makubwa rangi ya kijani, kifua chake kimechomoza mbavu, mikono mirefu na mipana.
Alikuwa anatembea kilevi lakini akionyesha mwenye nguvu. Miguu yake ilikuwa inatawanya michanga ya jangwa kana kwamba maji. Mdomo wake mdogo wenye meno ya paka ulikuwa wazi akiwatazama walengwa wake anaotaka kuwatia kinywani.
Na mate yalikuwa yanamchuruza.
Kiumbe gani hiki? Wakajiuliza wakina Malkia wakitumbua macho. Hawakuwa wanaamini wanachokiona. Hawakujua kiumbe hicho kinataka nini lakini kwa haraka wakaamini hakijaja pale kwa kheri.
"Wewe ni nani?" Seth akapaza sauti. "Unataka nini?"
Kiumbe kile wala hakikuongea, kikazidi kusonga kuwajongea kana kwamba hakijasikia. Seth akabadilisha lugha takribani nne akimuuliza kiumbe kile maswali hayohayo, hatimaye akafanikiwa!
Aliongea lugha anayoielewa. Lugha hii ilikuwa ni ki-injin, lugha inayozungumzwa na idadi ndogo sana ya watu waishio mabarafuni. Ilikuwa na maneno machache, na endapo ukiiskiliza vema utatambua inarudiarudia sana maneno lakini kumaanisha maana tofauti.
"Kukluf kazif tekop, meshan kabac tubuknova," akateta kiumbe yule akiwa anazidi kusogea.
"Anasema nini?" Zura akawahi kuuliza kwa hofu. Macho yake yalijawa woga, mikono yake ilikuwa inatetemeka.
Seth, kwa haraka, akawakalimania kwamba kiumbe yule anaitwa Kazif na amekuja hapo kuchukua kilicho chake.
"Kipi hicho?" Malkia akawahi kuuliza. Alimgeuzia uso Seth lakini macho yakiwa kwa yule mgeni wao anayezidi kujongea.
Seth akamuuliza tena yule kiumbe kwa lugha anayoielewa, hapo amekuja kufuata nini hicho kilicho chake? Kiumbe kile pasipo hiyana, akasema mifupa. Anahitaji kwenda kujaza pango lake zaidi.
Malkia akataka kunyanyua panga, Seth akawahi kumtazama na kumzuia kwa ishara ya kumwonyesha kiganja.
"Acha tuongee naye kwanza."
Kisha akamwomba kiumbe yule aketi chini wapate kuteta. Wao hawana maana ya kuzua shari. Kwa kusikia ombi hilo, kiumbe kile kikaketi kikiwatazama. Zura na Fluffy wakazidi kupata hofu. Kiumbe hicho hakikuwa kinavutia kukitazama hata kidogo.
Kadiri kilivyosogea basi kingekufanya tumbo likusokote kwa woga. Miguu ife ganzi. Na haswa kikikutazama, ungeweza kupata haja zote kwa mpigo!
Tangu kiumbe hichi kiliposogea hapo, hali ya hewa ikageuka na kuwa baridi zaidi. Ungemtazama vizuri ungebaini alikuwa anafuka moshi. Moshi wa barafu.
Si bure hakuwa anapatana jua maana angeweza kuyeyuka.
Basi Seth akamwomba awabakizie uhai wao, na watakaporejea toka safari yao ya mbali watampatia zawadi kama fadhila. Kiumbe hicho kikakataa na kusema:
"Habaq quatta kilim meshan, juata himas!" Akimaanisha kama wamemkatalia ombi lake basi wacheze naye mchezo. Seth akamuuliza mchezo gani huo, Kazif akamwambia unaitwa 'Yuaj si Kobil' - maji ama damu.
Akauelezea mchezo huo. Atawauliza mafumbo matatu na endapo wakiyakokotoa atawapatia maji, na endapo wakishindwa basi wao watampatia damu.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kuweka nao makubaliano.
"Hapana," Malkia akakataa. "Hatuwezi kucheza naye mchezo huo wa hatari kiasi hicho. Tupambane naye!"
"Lakini vipi kama tukapoteza zaidi kwa kupambana naye kuliko njia hii ya kidiplomasia?" Akauliza Seth. "Vipi kama tukashinda, tukabaki salama na maji akatupatia? Si rahisi kupambana na kiumbe hiki!"
Lakini bado Malkia akawa na woga. Seth akamsihi wachague mchezo huo, na kwa pamoja watashirikiana kufumbua mafumbo hayo. Vichwa vitano si sawa na kimoja.
Basi wakamruhusu kiumbe yule aanze kuuliza mafumbo yake. Hapa chini kama yalivyotafsiriwa:
La kwanza, kikapu kina matufaha matano na nina watoto watano. Nitayagawanyaje haya matufaha matano kwa watoto wangu na kwa wakati huo tufaha moja likabaki kapuni?
"Tumekwisha!" Akasema Fluffy akitoa macho. "Mbona anauliza maswali ambayo hayawezakani!"
Seth akasafisha koo lake kisha akafikiri kidogo. Akajibu atawapatia matufaha manne kwa wale watoto wa nne, alafu mtoto wa tano atampatia tufaha likiwa limebaki ndani ya kikapu.
Wakastaajabu mojawapo ya chupa yao imejawa na maji. Walikuwa wamepata!
La pili, anayekitengeneza, hakihitaji. Anayekinunua hakitumii. Anayekitumia hawezi kukiona wala kukihisi. Ni nini hicho?
Seth akatabasamu, haraka akajibu ni sanda. Basi chupa lao la pili likajawa na maji. Wakafurahi. Kile kiumbe kikang'ata meno yake kwa hasira. Sasa akadhamiria kuuliza fumbo gumu la mwisho ili angalau asiwe amepoteza muda wake bure.
La tatu, nyakati za mchana huzitumia dirishani, nyakati za chakula naenda mezani, nyakati za usiku najificha hamnioni. Mimi ni nani?
Seth akatabasamu tena, upesi akajibu ni nzi. Bobo lao moja lilio tupu likajaa maji! Alikuwa amepata! Sasa kiumbe huyu akawa ameshindwa kutimiza adhma yake. Lakini kwa ukaidi, akasema anaongezea swali moja la mwisho.
Seth na wenzake wakatahamaki. Malkia akasema yule kiumbe hakuwa anataka kuwaacha hai, inabidi wapambane. Lakini Seth akawatoa hofu, hawakuwa na haja hiyo. Wamwache huyo kiumbe atupe turufu yake ya mwisho.
La nne, kuna wadada wawili: mmoja anamzaa huyo wa pili, alafu naye huyo wa pili anamzaa huyo wa kwanza. Hawa wadada wawili ni wakina nani?
Seth akamtazama Malkia kisha Fluffy na baadae Zura. Akawauliza kama wana majibu, wote wakasema hawana. Wakajawa pia na hofu baada ya kuona Seth anawauliza wao. Walikuwa wanamtegemea yeye kwenye hili.
Lakini mara Seth akatabasamu, akamtazama kiumbe yule na kumjibu dada hao ni usiku na mchana.
Kiumbe kile kikakasirika mno. Alikuwa ameshindwa! Akasaga meno yake na kupiga ngumi kiganja chake. Akamwambia Seth kwamba ameshinda kwa leo lakini anajua itawachukua siku kadhaa kumaliza jangwa hilo kwahiyo kila siku usiku atakuwa anawatembelea na kuwauliza mafumbo kadhaa.
Hawatayapata siku zote hizo, aliamini na kuwaaminisha. Akaenda zake akiwa ameghafirika.
"Uliyajuaje mafumbo yote yale?" Fluffy akamuuliza Seth akiwa na kimuhe. Seth akamwambia baba yake alikuwa akimuuliza sana akiwa mtoto, vile vile vitabu vingi alivyovisoma. Wakampongeza sana kwani alisaidia kupata maji ambayo hawakujua wangeyapatia wapi.
Lakini kwa wakati huo, yule kiumbe, akiwa amepania kwa dhati, akaenda kukesha usiku mzima kupitia mafumbo yake aliyoyaandika kwenye kuta za pango. Hata kula hakutaka!
***