*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN*47
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akaenda chumbani na kuchukua ile karatasi yake ya siri. Wakatoka nje na Seth. Hapo tu mlangoni wakakutana na Bozi akiwa ameambatana na kikosi cha wanaume watano.
Wanaume hao walikuwa wamebebelea silaha na kujivesha sura za ghadhabu.
ENDELEA
Haikuwa rahisi kwa Fluffy kupambana na watu hao. Alistaajabu wengine walikuwa ni walinzi wake wa karibu. Akawekwa chini ya ulinzi na kuchukuliwa kimya kimya kwa siri wakipita njia panya mpaka kwenye jengo lao walilomfungia Fluffy ndani.
Mbaya zaidi watu hawa walikuwa wamekwapua karatasi ile ya siri ya Fluffy. Karatasi ambayo ilikuwa inaeleza mambo ya siri ya kule Misri. Karatasi ambayo Fluffy alikuwa ameificha asimwambie mtu kuhusu, isipokuwa tu Seth.
Japokuwa alipambana kunusuru karatasi yake, hakufua dafu kwenye mikono ya wanaume watano, ukitazama Seth hakuwa mtu mwenye ujuzi wowote kwenye maswala ya kujilinda. Kweli hupewei vyote.
“Sasa mtakaa humo wapenzi. Bila shaka mlikumbukana sana,” Bozi akasema kwa kebehi kisha akaangua kicheko. Ingawa Fluffy alimtishia na kumwahidi atammaliza kwa mikono yake, Bozi hakuonekana kujali.
Zaidi akampungia mkono na kuufunga mlango akiwaacha wafungwa gizani.
“Bado na yule mwenzenu!” Sauti ya Bozi iliwafikia Fluffy na Seth waliokuwa ndani, gizani. Kisha ikafuatia kicheko kilichokuwa kinaishilia kadiri na muda.
“Sasa tunafanyaje, Seth,” Fluffy akauliza kwa hofu. Sauti yake ilikuwa ina ashiria anguko, huzuni.
Lakini kinyume chake, Seth akamwambia kuna tumaini. Alikuwa anaamini watatoka mule, na wataikomboa Sawaridi kwa mara nyingine tena.
“Maadui hawakuisha. Ni bora adui wa nje kuliko yule wa ndani unayeshirikiana naye sahani na kijuiko,” Seth alisema kwa sauti ya chini.
***
Baada ya hatua nzito, mlango wa nyumba ya mfanyabiashara Melkizedek unagongwa mara tatu, kisha mgongaji anatulia. Alikuwa ni mwanajeshi, yule aliyepewa kazi na mfalme ya kumfuatilia Tattiana katika mienendo yake yote.
Tattiana, binti wa Melkizedek ambaye alitokea kukamata jicho la mfalme. Binti mwenye macho mazuri, uso wa kistaarabu na nywele kama unyoya wa sufi.
Punde mlango ukafunguliwa na Fanty, kaka yake Tattiana, akauliza amsaidie nini mlinzi yule ambaye alisema anataka kuonana na baba yake kama yupo.
Haraka Fanty akaenda kumfikishia baba yake ujumbe, ndani ya muda mfupi akashuka kukutana na mwanajeshi.
“Karibu.”
Uso wa Melkizedek ulikuwa na wasiwasi. Siku zote ukiwa unajua kuna jambo baya umelifanya, basi ukutanapo na mhusika ama mtendwa, basi waanza kujitunuku mashaka.
Akili ya Melkizedek ilikimbia haraka na kuwaza kwamba ukute makubaliano yake na yule mzee wa baraza kuhusu biashara ya Cedar yamebumburuka, na sasa amefuatwa kukamatwa.
“Ahsante, sikaribii. Nina ujumbe toka kwa mfalme.” Mwanajeshi akamkambidhi Mlekizedek barua iliiyokuwa imefungwa na kamba ya madini ya fedha, ikichapwa na mhuri wa mfalme.
Mwanajeshi akaenda zake akimwacha Melkizedek anaikagua barua ile. Akazama ndani na kumwita mkewe kumjulisha kuhusu barua toka kwa mfalme.
“Itakuwa inamhusu binti yetu,” mama akasema upesi. Alikuwa amevalia gauni lake la thamani. Mkono wake ulinyaka barua toka mikononi mwa mumewe, haraka akafungua ujumbe huo na kuusoma.
Ulikuwa ni ujumbe wa mfalme akiomba kukutana na Tattiana.
“Si nilikuambia!” mama akalipuka. “Hii ndiyo hatua ya kwanza kuelekea ndoa. Endapo binti yetu akimkarimu vizuri mfalme, basi tutakuwa wakwe.”
Mama pasipo kupoteza muda akamwita mwanae na kwenda naye chumbani. Akamwandaa vema kwa kumkwatua na kumchagulia nguo iliyopendeza macho yake. Lakini zaidi akamhusia asimwangushe kwani hiyo ni nafasi adhimu sana kwake.
“Unaweza ukageuza familia na ukoo wetu kuwa wa kifalme. Tukaheshimika zaidi, na tukafanikiwa zaidi.”
Kisha akamfunda namna ya kuenenda.
“Mtazame mfalme kwa uso wa haya. Usimnyime tabasamu wala mkono wako. Hakikisha anakuwa wa moto kila anapokuwa karibu na wewe. Usiwe na papara, tulia na uzingatie kama paka mwitu awapo mawindoni.”
Likapita kama nusu saa hivi, mara farasi wawili toka kwenye kasri ya mfalme wakawasili nyumbani kwa Mlekizedek. Kwenye mgongo wa farasi mmoja alikuwa ameketi mwanajeshi, na mwingine alikuwa hana mtu mgongoni.
Huyu ambaye hakuwa na kitu mgongoni, alikuwa ni mweupe. Kamba yake iliyomshika shingo ilikuwa imeshikiliwa na mwanajeshi aliyekuja nao.
Mwanajeshi huyo akasema amekuja kumtwaa Tattiana. Tattiana akatoka ndani na kumwea farasi, wakatimka kwenda kasrini kwa mfalme.
Ni muda mchache ukapita, na mara akatokea kijana fulani hapo nyumbani kwa wakina Tattiana. Kijana huyu alikuwa mwembamba mwenye nywele ndefu rangi ya kahawia na ndevu zilizojaa kwenye taya.
Akamuulizia Fanty kwa walinzi, Fanty akaitwa na kuja kujumuika naye hapo nje ya uzio.
“Nimemwona Tattiana akiongozana na mwanajeshi. Kuna nini?” akauliza mwanaume huyu ambaye kwa mujibu wa maongezi ya Fanty, alikuwa anaitwa Roboth. Macho yake yalikuwa madogo yanayong’aa.
Fanty akamwambia kwamba Tattiana amepelekwa kasrini kukutana na mfalme na kama mambo yakiwa vema basi ataolewa na mkuu huyo wa nchi. Roboth akastaajabu sana. akaishiwa na nguvu akiuliza:
“Kuolewa? Na vipi husumu mimi?”
Fanty akamsikitikia. Japokuwa Roboth alikuwa ni rafiki yake, na anajua fika alikuwa ana mahusiano na Tattiana, ambaye ni dada yake, hakuwa na fursa ya kumzidi mfalme.
Akamwambia amsahau Tattiana, kwani atajiumiza tu. hata familia yake haiwezi kumwelewa. Roboth akapinga hilo jambo kwa nguvu zake zote. Fanty asimjalli, akarudi zake ndani.
Na kumbe mama yake alikuwa anaushuhudia mchezo wote huo. Akamfuata Fanty na kumuonya.
“Sitaki yule kifaranga akanyage tena hapa kwangu, wala amsogelee Tatty. Sawa?”
Fanty akaitikia, kisha akaenda zake.
---
“Karibu,” Akasema Phares akimpatia mkono Tattiana. Tattiana akashuka wakaenda zao ndani.
Walifikia sebuleni wakakaketi katika umbali wa kunyoosha mkono kumfikia mwenzako. Mfalme akamsifia Tattiana amapendeza. Tattiana akiwa ameinamisha uso wake akashukuru.
Wakakaa kwa muda wa kama dakika mbili pasipo kuongea. Tattiana alikuwa anafinyaga vidole vyake wakati Phares akifurahia kutazama uso wa binti huyo mrembo akiwa anatabasamu mwenyewe.
Mwishowe Phares akamtaka Tattiana amwandalie chakula cha usiku. Angependa kula mkono wake. Na zaidi akataka abaki naye kwa siku hiyo.
“Sawa, mfalme wangu,” Tattiana akaitikia.
***
Farasi alipolia, Bonas akamwambia Rhoda:
“Ni muda mrefu sasa twatembea. Huoni kama itakuwa vema tukipumzika.”
Walikuwa wametimiza kama masaa sita hivi wakitembea. Watu wote walionekana kuchoka isipokuwa Rhoda mwenyewe. Bado macho yake yalikuwa makavu na mwenye nguvu.
Alikuwa anaangaza angaza huku na kule japo haoni jambo isipokuwa giza.
Wakapumzika. Na wale wenye chakula wakatoa kula.
“Unaweza ukaona lolote tukiwa hapa?” Rhoda akamuuliza Tretho.
“Sijajua,” Tretho akamjibu. “Ni mpaka tufanye huo msako.”
Basi Rhoda akasogea kidogo kando apate kumaliza haja yake ndogo. Alipomaliza, kabla hajajirejesha kule walipo wenzake, akaangaza kushoto na kulia kwake. Akaona taa moja kwa mbali upande wake wa kaskazini.
Aliporejea akamwambia Tretho na Bonas.
“Kwahiyo tutaelekea huko?” Bonas akauliza.
“Ndio,” Rhoda akajibu. “Ila ni sisi wenyewe siyo na kikosi kizima.”
Bonas na Tretho walipomaliza kula, basi wakatoka na Rhoda kwenda kule walipoona taa. Baada ya mwendo wa dakika ishirini na, wakawa wamekaribia kufika. Ilikuwa ni nyumba ya wale wabibi walozi watatu.
Ila punde, wakaanza kuona maajabu!
Kwanza walisikia sauti ya popo na mvumo wa upepo tokea kushoto mwao. Kutazama wakaona rundo kubwa la popo wakubwa. Popo hao walikuwa wanakuja upande waliopo.
Wakawavamia katika mtindo wa kuwazunguka. Japokuwa Rhoda alishikilia kizingiti chake alichopewa na Venin kama kinga. Hakikumsaidia. Wakajikuta wananyanyuliwa na kimbunga kile cha popo na kusafirishwa wakielekea wasipopajua.
Ndani ya hekalu kubwa, kubwa mno, popo wakaingiza watu hao ndani na kuwamwaga kwenye ukumbi. Ndani ya ukumbi huo wakawakuta wenzao, yaani kile kikosi cha watu waliokuja nao wakiwa tayari wameuawa!
Kila waliyemwamsha, hakusikia wala kufurukuta. Walikuwa wamekauka ngozi yao ikiwa nyeupe pe!
“Wamenyonywa damu,” akasema Tretho. “Hawajabakiziwa hata tone moja.”
Wakiwa hapo wanabung’aa. Hawaoni pa kuingilia wala kutokea. Yule mtu aliyekuwa anamtazama Rhoda kwenye rada, akaangua kicheko kisha akatia kidole chake kwenye rada na kukoroga.
Mara Rhoda na wenzake wakaanguka chini kwa kizunguzungu. Wakapoteza fahamu.
***
“Malkia, hakuna aliyemwona,” askari alifikisha ripoti kwa ukakamavu.
“Umeulizia vizuri lakini?”
“Ndio, nimeuliza kila eneo na kila mtu. Hakuna aliyesema amemwona jenerali kamanda.”
Malkia akanywea. Aliminya mdomo wake akitazama kushoto. Akafikiri kwa muda kidogo kabla hajauliza:
“Na kaimu?”
“Yu njiani yuaja,” akajibu mwanajeshi na kisha akaondoka. Malkia akarejea sebuleni kukutana na Zura aliyekuwa ameketi kwenye kiti akifuma kitambaa kikubwa kizito.
“Hamna anayejua wapi alipo,” Malkia akamwambia Zura huku akinyanyua gauni lake zito lililofumwa na nyuzi za dhahabu apate kukaa kochini.
“Sasa atakuwa ameenda wapi?”
“Sijui. Tangu aliporejea toka kwa mama yake, nilionana na kuongea naye kwa muda mchache sana. Sijui amekumbwa na nini.”
Punde si nyingi, akaja mwanaume mrefu mwenye mwili mpana, Benadi. Mwanaume huyu alikuwa makamu wa Fluffy. Malkia akamuuliza kama amemwona Fluffy ama ana taarifa zozote kuhusiana naye.
“Hapana, sijui alipo,” akajibu Benadi akitikisa kichwa.
“Umeongea naye karibuni?”
“Hapana, sijaongea naye.”
“Unadhani atakuwa wapi?”
Benadi akatikisa kichwa chake. Basi Malkia akamruhusu aende zake.
Benadi alipotoka nje, akatembea kwa umbali mfupi kabla hajasikia jina lake linaitwa na sauti tokea nyuma. Alikuwa ni Bozi akiwa amejiveka shuka moja kubwa jekundu.
“Naweza nikapata wasaa wa kuongea na wewe?”
“Kwa sasa, hapana. Malkia amenituma kumtafuta Jenerali.”
“Oooh, huwezi jua labda naweza nikasaidia,” akasema Bozi kwa tabasamu.
LAKO JICHO.....