*MKUFU WA MALKIA II -- 52*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Lakini getini kulikuwa kuna walinzi. Wanaume watatu waliobebelea silaha. Wangefanyaje?
Na wakiendelea kukaa hapo, sebuleni wakiwa hawajui la kufanya, wale vijakazi wengine wawili watakawakuta. Watawaacha?
ENDELEA
Hakukuwa na namna. Iliwabidi waruke ukuta kwa kusaidiana wakatokea huko upande wa pili na kuanza kukimbia. Hawakujua wanapoelekea ila alimradi waondoke na kuacha mbali nyumba ya kuhani huyo.
Walipokimbia sana, wakasimama wapumzike. Mapafu yalikuwa yamekaukiwa. Wakashika magoti yao wakihema kama mbwa.
Walikuwa wanavuja jasho haswa. Macho yamewalegea kana kwamba wamepigwa na moshi. Ottoman hata akaketi chini baada ya kuhisi viungo vinamuuma haswa.
Hapa ndiyo akamuuliza mwenzake, nini kilimsibu kujaribu kumuua kuhani? Oragon akamwambia mwanaume huyo alimtaka kimapenzi.
Ottoman akatoa macho.
"Una maanisha nini?"
"Alitaka nimlale!" Oragon akajibu kwa midadi.
Ottoman akashika mdomo wake kwa mshangao. Ilikuwa ngumu kuamini mzee yule, mwenye nafasi yake kubwa ndani ya himaya, alikuwa na michezo hiyo.
Kumbe ndiyo maana hana mke wala mtoto! Wakang'amua. Lakini sasa tunafanyaje na wapi tunaenda? Swali lilikuwa hapa. Na wapi pia watapata chakula?
Wakakaa hapo kama kinda za ndege zilizompoteza mama yao. Na kwakuwa walitoka mbio kwa kuhani, hawakuwa wamebeba chochote kile mikononi mwao. Hata 'vituguo' vya kujihifadhi ama kujifunikia.
Wakalala wakiwa wamejikunyata, miili yao ikipambana na baridi kali. Wakisimamisha masikio yote kusikia ujio wa shari toka pande yoyote ya dunia.
**
"Mbona nakuita muda wote huo, hukunisikia?" Raam alifoka. Alikuwa yupo uchi chini sakafuni akiwa ameshikilia kichwa chake kinachomimina damu. Sakafu ilikuwa imetapakaa damu. Na mwili wake ulikuwa umeshika damu upande wake wa kushoto alioulalia.
Mbele yake alikuwa amesimama bwana Marimari mmoja wa vijakazi wake wa ndani.
"Sikukusikia, mkuu," akasema Marimari. Alikuwa amepigwa na butwaa kumwona mkuu wake katika hali ile aliyomkuta.
"Wako wapi wale vijana wapya?" Akauliza Raam. Kabla hajasubiria majibu akaagiza: "wakamateni na muwamalize mara moja!"
"Hawapo!" Marimari akampasha. "Sijawaona kwa muda sasa hapa ndani hata nikajua umewatuma huko nje."
Raam akashika kichwa chake kwa maumivu. Habari hizo zikamuumiza kichwa zaidi. Akajitahidi kunyanyuka akisaidiwa na Marimari, akajiveka joho jepesi na kutoka ndani kwenda kuonana na walinzi wake langoni.
Akamtaka abakie mlinzi mmoja tu, hao wengine wote, pamoja na wale ambao hawapo zamu, wajumuike wakawatafute wakina Oragon popote pale walipo.
"Mtakapowakamata, muwamalize asijue mtu yeyote yule. Sawa?"
"Sawa, mkuu!" Wakaitikia kwa ukakamavu.
"Ni wageni himayani hivyo hawatawasumbua kabisa. Mkiulizia mtawapata kwa urahisi, na hata wakichangamana na wenyeji mtaweza kuwachambua. Vilevile mkiwaua hakuna atakayewaulizia wala kusumbuka nao," Raam aliwapasha zaidi. Baada ya maelezo hayo, wanajeshi wakaenda zao kwenda kuwasaka vijana hao.
**
Kwa mbali wanaume wawili walionyeshea kidole upande wao wa kulia wakinong'onezana. Mmoja alikuwa mwanaume mfupi na mwingine mrefu. Kwakuwa ilikuwa giza, ilikuwa ngumu kuwatambua.
Baada ya kunong'onezana huko wakasogea kwa haraka na kusimama mbele ya wanaume waliokuwa wamejilaza chini.
Walikuwa ni wakina Oragon!
"Nyie!" Wakawaamsha wakiwasukuma na miguu. "Amka! Amka! Amka!"
Wakina Oragon wakamka kwa hofu kubwa wakidhani wameshatiwa nguvuni. Walipotazama vema wakagundua ni wale wanaume waliowakwapulia kila kitu chao. Wakataka kuzua ugomvi, lakini mara wanaume wale wakachomoa jambia zao na kuwatishia kuwanyofoa uhai.
"Tulieni hivyo hivyo kabla hatujawatoboatoboa!"
Wakanywea akama ukili majini. Wanaume hao wakawasachi mifukoni lakini hawakupata kitu. Badala yake wakina Oragon ndiyo wakawaomba wawafadhili kwani hawana mbele wala nyuma.
"Naomba mtupatie fedha kidogo," akasema Oragon. "Hatuna hata cha kutia mdomoni."
Wale wanaume wakatazamana, alafu yule mfupi akarudishia jambia lake kiunoni na kuwaambia kama wanataka kula basi waungane nao la sivyo waozee hapo.
"Mnafanya shughuli gani?" Ottoman akauliza.
Wanaume hao wakacheka alafu mrefu akasema:
"Yani mpaka sasa hamjajua tu tunafanya shughuli gani?"
Kisha wakacheka tena.
**
"Mwambie ntalizingatia, anipatie muda tafadhali," alisema Phares akimwambia mwanaume mgeni aliyekuwa ameketi naye. Mwanaume huyu alikuwa ana ndevu za wastani, nywele nyeusi ti ndefu mpaka begani, na kwenye kifua chake upande wa kushoto alikuwa ametundika alama ya ndege, ishara ya himaya ya Maam.
Mwanaume huyo, mjumbe wa Maam, akanyanyuka na kumpatia mkono mfalme.
"Nitamfikishia habari hizo, lakini nisiwe muongo, hamna muda wa kungoja tena. Keshokutwa anaapishwa kuwa mfalme na hawezi akaapishwa pasipo kuwa na mke."
Mjumbe huyo akashusha pumzi ndefu na kutengenezea nguo yake.
"Kwahiyo kiuhalisia muda ulionao ni kesho tu mpaka majira ya jioni," akasema mjumbe kisha akaondoka zake mfalme akimsindikiza kutoka naye nje. Mjumbe huyo alipoyoyoma mfalme akarudi zake ndani akiwa na mawazo.
Sasa ni rasmi kijana wa mfalme alikuwa anamtaka Tattiana akawe malkia wake. Harid alishampasha habari kijana huyo kuwa Tattiana ndiye mrembo himaya nzima.
Na ubaya zaidi, hata mjumbe huyu aliyetumwa kuja hapo himayani, alikutana na Tattiana akasadiki hayo maelezo. Akasema Alah! Kweli huyu afaa.
Sasa afanyaje?
Mfalme akahisi kichwa kinamuuma. Hakuwa radhi kumpoteza Tattiana hata kidogo.
**
Ni usiku sasa. Tattiana hakuwa katika chumba kimoja na mfalme kama inavyotakiwa, bali katika kile chumba alimokuwa anaishi malkia Vedas.
Humo alikuwa tayari ameshafungua kabati na kuchukua chupa ile ya maajabu. Anaitazama na kujiuliza maswali kichwani.
Anaisikiliza chupa hiyo na kusikia ikidunda mapigo ya moyo. Anasikiliza tena na kuhakiki kweli, yalikuwa ni mapigo ya moyo.
Leo anapata wazo na kuanza kung'amua kitendawili hiki. Alijiuliza:
"Nimelala na mfalme kwa muda wote huo, amekuwa baridi mpaka nashindwa kulala. Lakini pia sijawahi kusikia mapigo yake ya moyo, hata nilipolaza kichwa changu kifuani mwake.
Ina maana hana moyo?" Akajiuliza akitazama chupa ile.
"Au moyo wake ndiyo huu chupani?"
Habari hiyo ikaleta mantiki.
"Lakini nani kauweka moyo huo humo? Inawezekanaje mfalme akaishi na huku moyo wake upo chupani?" Maswali hayo yalimpasua kichwa. Na kama haitoshi basi, yule kiumbe anayetoka nje ya chupa pale ifunguliwapo, ni nani?
Akakumbuka yale maneno yake: "Nefil njhami khatu habab?" Anamaanisha nini?
Ikiwa ni usiku sasa mkali, akiwa ndani ya mawazo haya, mara anasikia harufu ya ajabu. Akanusanusa kuhakiki. Hakuijua harufu hiyo ni ya nini. Na kadiri na muda ilikuwa inaongezeka!
Akashindwa kuipuuzia. Akaificha chupa kabatini na kuanza kuifuatilia harufu hiyo. Akafungua milango na kutembea akikatiza korido kadhaa akiacha pua ifanye kazi yake.
Mwishowe akajikuta amefika kwenye kingo ya kasri. Kwenye kakona kidogo alikuwa amesimama Bella akiwa ameshikilia miti kadhaa mikononi mwake. Miti hii ilikuwa inafuka moshi mweupe.
"Bella," Tattiana akaita. "Unafanya nini hapo muda huu?"
Bella hakujibu. Akawa anamtazama Tattiana kana kwamba alikuwa anamtarajia. Tattiana akasogea karibu zaidi. Kuangaza akaona askari kadhaa wakiwa wapo chini.
Hakuelewa kilichokuwa kianendelea pale.
"Bella, unafanya nini hapa? Na hao maaskari mbona wapo chini?"
Tattiana akawatazama vema wale maaskari. Akagundua walikuwa wamekufa. Macho na midomo yao ilikuwa wazi!
Akamezwa na hofu. Lakini kufumba na kufumbua, kabla hajatenda hata jambo, akasukumizwa kwanguvu na mtu tokea nyuma. Akajigonga na kizuizi cha kibaraza, akabinuka na kudondokea chini!
Bella na Lucy, aliyetokea nyuma, wakamtazama. Lucy akabinua mdomo wake na kusema:
"Amekwisha."
Bella akamalizia.
"Tufanye upesi!"
**