Mkufu wa Shani - Sehemu 1

raoka kubanda

Member
Jun 13, 2017
45
24
Na Beka Mfaume
[The Greatest]

MKUFU WA SHANI

Rika lake lilionekana kutozidi miaka arobaini. Alikuwa akiteremka kwa haraka sehemu ya mwisho ya ngazi huku mkono wake ukiwa umekamata kingo ya pembeni ya ngazi hiyo na kuwa mhimili wake uliomwezesha kuteremka kwa kasi aliyoitaka, begani akiwa na begi lililokuwa likining’inia. Hakuwa kwenye kasi kubwa, lakini pia hakuonekana kuwa na haraka sana. Alichokuwa akifanya ni kama kuuangalia wepesi wa miguu yake wakati akaziteremka ngazi hizo.

Alikuwa ametoka ghorofa ya pili ambako hakuona ulazima wa kupanda lifti wakati wa kwenda au hata alipokuwa akiteremka. Alizimaliza ngazi hizo kwa kasi aliyoshuka nayo na kuipokea kwa hatua chache za haraka kabla hajatulia na kutembea mwendo wa kawaida wenye hatua ndefu.

Maungoni alivaa fulana aina ya T. Shirt nyeupe iliyoonekana bado mpya kama si matunzo mazuri. Mbele ya shingo ya fulana kulikuwa na miwani ya jua iliyokuwa ikining’inia na kuchezacheza kifuani kwake wakati akitembea. Miguuni alivaa jeans iliyomkaa vema huku viatu vyake vyenye rangi ya kahawia visivyokuwa na kamba vikienda sambamba na hatua zake.

Aliitwa Rashid Othman Mgaya kwa uhalali wa jina alilopewa na wazazi wake. Hata hivyo mwenyewe alilibadilisha, akajiita Roche. Likatawala sehemu kubwa vinywani mwa watu kuliko jina lake halisi. Ni mchezaji wa mpira wa kikapu, na hata urefu wake uliendana na aina ya mchezo anaoucheza. Hakuwa na mwili wa kutisha, lakini kwa yeyote aliyemwangalia, alitambua mtu huyo yuko imara kimazoezi. Hakuwa na sura ya kuvutia ya kumwita jamali, lakini bado sura yake ilimkubalisha kukubaliwa na mwanamke yeyote mzuri. Aliishi Morogoro, lakini kila mwishoni mwa wiki alikuwa akija Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazoezi au kucheza mechi, akiichezea timu ya PAZI ya Upanga Dar es Salaam.

Alilimaliza jengo alilokuwa ametoka lililopo maeneo ya Posta jirani na Makumbusho ya Taifa. Hesabu zake zikawa ni kwenda Kituo cha Mwendokasi cha Kivukoni kwa ajili ya kupanda usafiri utakaompeleka Kituo Kikuu Cha Mabasi yanayokwenda Mikoani na Nje ya Nchi kwa ajili ya kurudi Morogoro. Siku hiyo ambayo ni ya Jumamosi, aliamkia Dar baada ya kuwasili katika jiji hilo usiku uliopita akitokea Morogoro kwa madhumuni ya kuja kucheza mechi siku inayofuata, yaani siku hiyo ya Jumamosi.

Hata hivyo, taarifa zilizomfikia akiwa tayari ameshawasili jijini Dar es Salaam, zilimtaarifu mechi hiyo isingeweza kuchezwa baada ya kutokea msiba wa ghafla wa kufariki mmoja wa viongozi wa timu pinzani waliyokuwa wacheze nayo. Hivyo Roche aliamua siku inayofuata ambayo ni hiyo, arudi zake Morogoro akaendelee na mambo yake mengine aliyoyaacha. Lakini kabla hajakwenda kutafuta usafiri wa kumrudisha huko, akataka kwanza afike katikati ya jiji amwone mtu aliyetaka kumwona kisha ndipo aende kutafuta basi litakalomrudisha nyumbani Morogoro.

Akiwa amemaliza kumwona mtu aliyetaka kumwona, ndipo Roche alipotoka ndani ya jengo hilo. Alipokuwa amesimama kandoni mwa barabara akitaka kuvuka ili aende ng’ambo ya pili aendelee na safari yake, akamwona mwanamke aliyekuwa ameingia eneo dogo linakoegeshwa magari akiwa analifuata gari dogo aina ya Benz la kisasa lenye rangi nyekundu ya metalic. Akiwa anamwangalia mwanamke huyo, nafsini mwake akakiri alikuwa akimwangalia mwanamke mzuri, lakini pia mwenye mwonekano ghali.

Simu yake ikaita. Akaacha kumwangalia mwanamke huyo aliyekuwa ameelekea mlango wa mbele wa kiti cha abiria cha gari hilo. Roche akajipinda na kuichomoa simu kutoka kwenye mfuko wa mbele wa jeans ambayo ilikuwa ikiendelea kuita. Akaiweka sikioni baada ya kuipokea. Akamwona yule mwanamke akifungua mlango na kuingia kwenye gari hilo ambako upande wa dereva kulikuwa na mwanamume.

Lakini wakati akiongea na mtu aliyempigia simu na wakati huohuo akielekea mwelekeo ambao gari hilo lipo, Roche akaona kama kuna kitu kidogo kilichotoka mwilini mwa mwanamke huyo na kuangukia chini. Hata hivyo hakukitilia maanani baada ya kumwona mwanamke huyo akiufunga mlango wa gari na gari hilo kuondoka.
Akiwa bado na simu sikioni huku akiendelea kuongea, Roche akalikaribia eneo ambalo mwanamke yule alikuwa ameingia kwenye gari. Akaangalia ile sehemu iliyoangukiwa na kitu alichokiona ambacho hakujua ni nini. Akakiona kitu kidogo kilichojisambaza na kujinyonga kwa pamoja kama nyoka mdogo. Kikamvutia. Akainama na kukiokota.
Ulikuwa mkufu wa dhahabu.

___________

Aliutoa mfukoni baada ya kupanda basi litakalompeleka Morogoro. Mara tu baada ya kutambua alichokiokota ulikuwa ni mkufu wa dhahabu wakati akiwa kule mjini, Roche aliamua kuutia mfukoni mkufu huo kabla watu waliokuwa pembezi mwa barabara kumtilia wasiwasi huenda ameokota kitu cha maana, hasa pesa. Na hakuutoa tena kuuangalia ingawa ndani ya basi la mwendokasi angeweza kufanya hivyo. Lakini kwa kuwa alitaka utulivu wakati atakapokuwa anauangalia, aliona bora afanye hivyo akishaingia ndani ya basi litakalomsafirisha kwenda Morogoro. Na ndipo alipoutoa baada ya kupata basi hilo na kukaa kiti cha dirishani.
Basi lilikuwa likisubiri abiria wajae ndiyo lianze safari ya kuelekea Morogoro, Roche akiwa amekaa peke yake huku kiti mwenza kikiwa hakijapata abiria, akaitumia nafasi hiyo kuutoa mkufu huo na kuuangalia kwa mapana. Hakuwa na utaalam wa kujua aina tofauti za dhahabu, lakini kwa mwonekano aliokuwa akiuona katika dhahabu hiyo, aliamini ulikuwa ni mmoja wa mkufu wa daraja la juu. Haukuwa mnene kama ile inayovaliwa na wasanii ambayo mingi inakuwa na rangi ya dhahabu, lakini mkufu si wa dhahabu.

Uliokuwa mkononi mwake haukuwa na chembe ya mashaka. Ilikuwa dhahabu safi, uking’aa na kumeremeta kama gamba la nyoka. Haukuwa mrefu wa sifa. Ulikuwa ni mmoja wa mikufu inayotulia shingoni na kumpendezesha mwanamke. Mwembamba wenye kidani cha ukubwa mdogo lenye umbo bapa kama hirizi ya kihindi. Pande zote mbili za kidani hicho kulikuwa kumeandikwa kwa maandishi yenye migongo iliyotuna yakiwa na jina la SHANI.

Roche alikipindua pindua kidani hicho na wakati mwingine kuburuza kidole chake kwenye migongo ya maandishi hayo huku akitafakari. Kwanza alijua mkufu huo ni bei ghali. Ughali uliofanana na mwanamke aliyeuangusha. Hakuwa na uhakika kama ulikuwa shingoni mwa mwanamke huyo wakati ukianguka au ulikuwa sehemu nyingine ya maeneo ya mwili wake. Aliamini endapo ataupeleka kwa sonara angeuuza kwa bei kubwa, lakini hilo halikuwa lengo lake.

Hakuwa tayari kusutwa na nafsi yake dhidi pesa ambayo angeipata kutokana na mauzo kuwa si ya halali. Nafsi yake ingekuwa tayari kumwambia, huo ungekuwa wizi. Hivyo hakuona sababu ya kukimbilia kuuza kabla ya kuvuta subira ili pengine mwenye mkufu huo angejitokeza. Alikuwa tayari kuurudisha. Akajiuliza kama angeweza kumjua mwanamke yule endapo atamwona tena. Akajaribu kuivuta kumbukumbu ya sura yake, lakini hakuna kilichompa ukakika, zaidi ya kujua alikuwa ni mwanamke mzuri. Hata hivyo alijihisi kama aliyekuwa amelikariri kwa kiasi fulani umbile la mwanamke huyo lililokuwa limejigawa vyema kimahaba.

Wazo jingine lililokuwa likimsukuma ni kutaka kumzawadia rafiki yake wa kike mkufu huo. Lakini angempaje ukiwa na jina la Shani? alijiuliza. Akawaza kama angeupeleka kwa sonara ili alibadilishe jina la kwenye kidani na liandikwe jina la rafiki yake wa kike? Halafu nimwambieje? alijiuliza. Kwamba nimemnunulia mkufu wa dhahabu? Roche akajiona huko ni kujidanganya mwenyewe. Na kwa nini aishi maisha ya kujidanganya?

Ingawa kwa kiasi fulani aliona bora kumzawadia rafiki yake huyo wa kike endapo mwenye mkufu hatajitokeza, lakini angefanya hivyo bila ya kumwambia alikoutoa mkufu huo. Hata hivyo kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimsitisha kuchukua uamuzi huo. Kulikuwa na tatizo lililokuwa likimkabili mbele yake, tatizo ambalo hakutaka kujidanganya nalo. Kuna mtu aliyekuwa akimzengea demu wake huyo kwa kipindi hicho!

Hakuwa na uhakika kama rafiki yake huyo wa kike ataendelea kumkatalia huyo jamaa. Jamaa mwenyewe ni mtu mwenye pesa na anayejulikana! Siku zote Roche alikuwa hamwamini mwanamke mbele ya mwanamume mwenye pesa. Ni siku za karibuni alipojua habari hizo kama jamaa anamwinda demu wake. Na habari hizo alizipata kupitia rafiki yake huyo wa kike baada ya kumwarifu kuwa anafuatwa na huyo jamaa!

Kauli za kujimwambafai alizokuwa akimsikiliza huyo rafiki yake, eti kwamba jamaa anajisumbua na kupoteza muda wake kwa kumfuata yeye, kamwe zilikuwa hazimwingii akilini Roche, au kumfanya amwamini. Alijua tu ipo siku rafiki yake huyo ataingia kwenye mtego wa jamaa. Alikuwa akiwajua vizuri wanaume wenye pesa wanapomtaka mwanamke. Ni mwanamke mmoja au wawili kati ya wanawake mia wanaoweza wakabaki kwenye misimamo yao. Wengi hulegeza misimamo yao baada ya kuingizwa kwenye mitego rahisi itakayowatamanisha kuwaaminisha kwamba, watatimiziwa wanachokihitaji.

Wazo hilo likamfanya Roche ajikute akiuondoa uwezekano wa kumzawadia rafiki yake huyo wa kike kumzawadia mkufu huo, kwa hofu asije baadaye akaumizwa.

Alipofika Morogoro, akauihifadhi mkufu huo sehemu ambayo alihakikisha rafiki yake wa kike hatauona.

_____________

Kabla hajateremka kutoka kwenye gari ambalo tayari lilishaegeshwa kwenye maegesho ya nyumbani na mume wake aliyekuwa akiliendesha, Shani akaingiwa na hisia kuwepo na hitilafu shingoni kwake. Hisia hizo zikaenda sambamba na kuupeleka mkono wake kifuani. Akapapasa kwa papara kama aliyekuwa akitarajia kuna kitu kimetokea, papohapo akauinamisha uso kuangalia miguuni kwake. Alichokihisi, akakiona kimetokea kweli. Mkufu wake ulikuwa haupo shingoni.

“Mungu wangu!” alisema kwa sauti iliyotaharuki huku mkono wake ukiwa bado kifuani
Itaendekea......
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom