‘Ndoa' ya wapinzani inayumba -CUF
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema ushirikiano wa vyama vinne vya upinzani, unayumba kutokana na viongozi wakuu wa vyama hivyo vya TLP, Chadema, NCCR-Mageuzi na chama hicho, kukacha mikutano ya pamoja.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Juma Duni Haji aliyasema hayo alipozungumzia kampeni za chama hicho zilizotarajia kuanza jana kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini pamoja na masuala mengine yahusuyo muungano wa vyama vya upinzani.
Duni alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mara kwa mara amekuwa akiwaita viongozi wa vyama vingine kwa simu na barua ili wakutane, lakini wamekuwa wakishindwa kuhudhuria mikutano bila sababu za msingi na kusababisha vyama hivyo kukosa mwelekeo.
Alisema bila ya vyama vya upinzani kuungana, kamwe hawawezi kukiangusha Chama Cha Mapinduzi. "Siafu na sisimizi ili waweze kumwangusha tembo ni lazima waungane, wakati sisimizi akiingia kwenye mkonga wa tembo siafu anauma tumboni hadi tembo ataanguka," alisema Duni.
Aidha, Duni alipinga hoja ya Chadema iliyotaka wagombea wa vyama vilivyojitokeza katika uchaguzi huo wakutanishwe na kumpata anayekubalika kwa madai kuwa tamko la muungano wa vyama hivyo halisemi hivyo na kwamba wao walikiandikia barua chama hicho ili kiwaachie jimbo hilo.
Alisema CUF iliwaachia Chadema katika majimbo mbalimbali likiwamo Tarime mkoani Mara, lakini wanashangazwa na Chadema kutaka wakutane ili kumpata mgombea anayekubalika wakati wao hawakuwawekea masharti huko nyuma.
Katika hatua nyingine, Duni alisema wanaingia katika kinyang'anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini wakiwa hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokana na kuibiwa kura katika chaguzi zilizopita.
Alidai katika uchaguzi wa mwaka 2005, mgombea wao, Amina Ahmed alishinda lakini kutokana na wizi waliofanyiwa, marehemu Richard Nyaulawa alionekana kuibuka na ushindi na kumshinda mgombea wao. "Zanzibar tumeshinda mara tatu, lakini mara zote tumenyang'anywa na kila mtu anajua hilo, tutaendelea kupigania haki hadi mwisho," alidai Duni.
Alidai licha ya kuibiwa kura katika chaguzi mbalimbali wataendelea kushiriki katika chaguzi zinazofanyika nchini kwa kuwa lengo la chama hicho ni kuwakomboa wananchi kutoka katika fikra za kikoloni alizodai zimepandikizwa na CCM.
Hata hivyo wakati CUF ikidai kuwa iliiandikia barua Chadema, Mkurugenzi wa Vijana Taifa wa Chadema, John Mnyika alisema CUF iliandika barua ya kuomba kuachiwa nafasi katika kinyang'anyiro hicho na hawakuomba mazungumzo. Akizungumzia suala la Tarime, alisema CUF yenyewe haikusimamisha mgombea na kwamba NCCR-Mageuzi haikuwaunga mkono.
Katika hatua nyingine, hatima ya wagombea wa CCM, Chadema na DP waliowekewa pingamizi kutokana na kukiuka taratibu mbalimbali kisheria katika ujazaji wa fomu za kuwania kuteuliwa kuwania ubunge, inatarajiwa kujulikana leo.
Hadi kufikia jana majira ya saa 10 alasiri, wagombea wa vyama vilivyokuwa vimewekewa pingamizi walikuwa tayari wamerudishiwa majibu ya pingamizi walizowekewa na wagombea wenzao. Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Juliana Malange kupitia kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Damson Ntangu, aliwaeleza wanahabari saa 11:20 kuwa bado anapitia majibu yaliyotolewa na wagombea.
"Msimamizi amesema niwaambie kuwa bado anapitia maelezo ya wagombea, alitegemea atatoa maamuzi leo, lakini hatafanya hivyo na badala yake atawapa taarifa kesho saa tatu asubuhi," alisema Nthangu na kuongeza kuwa waandishi wanaweza kupata majibu kwa njia mbili, moja kwa kuwasiliana na wagombea wenyewe au kusubiri hadi kesho asubuhi.
‘HabariLeo' ilipata nakala ya majibu ya mgombea wa Chadema, Sambwee Shitambala aliyekuwa anajibu pingamizi alizowekewa na vyama vya CUF na CCM; la kwanza likihoji uhalali wake wa kugonga kuapa na kugonga muhuri wa wakili badala ya hakimu kama Sheria ya Uchaguzi inavyoelekeza.
Katika majibu yake, alisema Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuchukua fomu ni Desemba 27 na kurudisha ni Desemba 27, huku ikitambua fika kuwa Desemba 25 na 26 ni siku za sikukuu na Desemba 27 ni Jumamosi ambayo mahakama hazifanyi kazi. Aidha, Shitambala amemweleza Msimamizi wa Uchaguzi kuwa Sheria ya Uchaguzi haisomwi na wala haipaswi kusomwa peke yake na pia kiini cha kuapishwa na hakimu kieleweke.
Alisema kimsingi hakimu anapata uwezo wa kuapisha kisheria kutokana na Sheria ya Viapo (Judicial Proceedings) and Statutory Declarations Act 1996) katika kifungu cha 11 ikisomwa pamoja na Sheria ya Notaries Public and Commissioner for Oaths kifungu cha 10 kinachotaja nani wanaruhusiwa kuapisha. Kadhalika ametupilia mbali madai kuwa alijiapisha mwenyewe ofisini kwake pamoja na kutojaza kipengele cha kama amewahi kushitakiwa au la kwa kile alichodai wawekaji pingamizi hawajasoma vizuri taratibu za ujazaji wa fomu hizo.
Source: Habari leo