Nimempoteza kaka

Kinyau

JF-Expert Member
Joined
Nov 24, 2006
Messages
818
Likes
151
Points
60

Kinyau

JF-Expert Member
Joined Nov 24, 2006
818 151 60
Hodi hodi ninabisha, jukwaani kuingia
Kwa simanzi kuwapasha,yale yalonitokea
Mtima una mashaka,jinsi ya kuelezea
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Ilikuwa ni jioni, nikaipokea simu
Haraka fika nyumbani,mpeleke kaka sehemu
Hali yake mashakani, matibabu ni muhimu
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Tukafika kwa tabibu,kueleza yake hali
Tukamuomba amtibu,ampunguzie makali
Nyingi dawa ajaribu,atibu kila mahali
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


Dawa akampatia, kasikia ahueni
Mganga katuambia,nyumbani nyi rejeeni
Andelee kutulia, na maji mengi mpeni
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Tukapakia garini, kaka alikaa mbele
Tukarejea nyumbani, na matumaini tele
Tukakaa ukumbini, tukicheka kwa kelele
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


Uji tukampikia na maji akajinywea
Kisha kajipumzikia,ubavu kuulalia
Magoti tukampigia,kwa mola kumuombea
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Akasema asanteni, kwa nzuri yenu huduma
Nimepata ahueni,mwaweza enda salama
Mola awabarikini,dada kaka na mama
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

***** akahiari, kukaa pembeni yake
Apate Sali rozari,pamoja na mwana wake
Mafungu kutafakari, kumuomba mola wake
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


***** akamaliza, kasogea sikioni
Apate mnong’oneza,neno lake la moyoni
Mkono akasogeza, Ambariki usoni
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Ghafla akashituka, alipomgusa kichwani
Moyo ukamruka,kajihisi hayawani
Ni wa baridi hakika, usoni na miguuni
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Na Mama akaniita, upesi kaka muamshe
Pembeni kanivuta,kwa hofu nimuegeshe
Kaka nilimuita,japo neno anipashe
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


Macho aliyafumba, Mwiliwe ulizizima
Wala hayakuyumba, ukatoweka uzima
Tumbo kake lilivimba,baridi mwili mzima
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Roho yake ilitoka,Bila ya sisi kujua
Malaika alifika, pumzi yake kuchukua
Machozi yalinitoka,mkono nikimshika
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Nilimwangalia sana, kufikiri ni uongo
Nilimlilia sana, moyo lipata msongo
Maumivu yalibana, kichwani hata mgongo
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


Uende kwa usalama,uende kwako nyumbani
Malaika wa salama, wakupokee mbinguni
Mola wetu maulana,akulaki mlangoni
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


Naamini siku moja,tutaonana peponi
Siku mwokozi akija, kuhukumu duniani
Hapo tutakuwa pamoja, tukiimba furahani
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana

Kwaheri kaka yangu, kwaheri wetu kijana
Kwaheri rafiki yangu,kwaheri wetu mwana
Kwaheri nguzo yangu kwaheri ya kuonana
Nimempoteza Kaka, Niliyempenda sana


shairi hili nimeliandika kwa simanzi kubwa baada ya kuondokewa na kaka yangu mpenzi,aliyenifia mikononi ghafla wiki mbili zilizopita. Namuomba Mola Amlaze salama Peponi.
 

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Messages
31,747
Likes
7,616
Points
280

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined Mar 10, 2006
31,747 7,616 280
Nimeshindwa kuandika, kinyau nasikitika,
Majonzi yalowafika, moyoni yamenishika,
Machozi yatiririka, msiba umewafika,
Poleni mwana wa kwetu, kwa kumpoteza kaka.

Ujumbe uloandika, mtima umeshtuka,
Na huzuni kunishika, uchungu umegubika,
Nami nikalikumbuka, la kaka uloandika,
Poleni mwana wa kwetu, kwa kumpoteza kaka.

Ni makubwa kwa hakika, mauti yaliyofika,
Kinyau nimegusika, rambirambi naandika,
Rehema zake rabuka, mbele zake natambika,
Poleni mwana wa kwetu, kwa kumpoteza kaka.

Mengine sitotamka, moyoni nimeyashika,
Maulana mtukuka, faraja kuwafunika,
Nawaombea baraka, uponyaji wa hakika,
Poleni mwana wa kwetu, kwa kumpoteza kaka.

NB: Kinyau poleni sana kwa msiba na tafadhali pitisha salamu zangu za pole kwa wazee.
 

IsayaMwita

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2008
Messages
1,123
Likes
11
Points
135

IsayaMwita

JF-Expert Member
Joined Mar 9, 2008
1,123 11 135
Kinyau,

Msiba hauna hodi, kinyau tambueni, mungu ameratibu maisha yetu kiganjani kwake,siku zetu zahebika mithiri ya punje za haradari,pole kwa hayo yaliyokufika, anza na wewe maandalizi, usijeshitukizwa ukawa haujajiandaa, pole sana ndugu yangu Kinyau haya yote ni dunia
 

BAK

JF-Expert Member
Joined
Feb 11, 2007
Messages
80,439
Likes
117,237
Points
280

BAK

JF-Expert Member
Joined Feb 11, 2007
80,439 117,237 280
Pole sana kwa msiba uliokufika. Tunamuomba Mwenyezi Mungu apokee sala na maombi yetu ya kuilaza roho ya marehemu mahali pema peponi~AMEN.
 

Kithuku

JF-Expert Member
Joined
Nov 19, 2006
Messages
1,395
Likes
107
Points
145

Kithuku

JF-Expert Member
Joined Nov 19, 2006
1,395 107 145
Pole sana Kinyau, yote ni mapenzi ya Mungu. Nakuombea kwa Mungu akujalie moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, wewe na familia yako na wote walioguswa na msiba huu.
 

Zitto

MP Kigoma Urban
Joined
Mar 2, 2007
Messages
1,273
Likes
1,708
Points
280

Zitto

MP Kigoma Urban
Joined Mar 2, 2007
1,273 1,708 280
Habari nimezipata, hivi punde nimesoma
Msiba umewapata, kachukuliwa kwa mema
Pole umeziapata, Mola akupe rahima
Inna Lillah, Wainna illaih Raajiuna
 

Single D

JF-Expert Member
Joined
Feb 27, 2007
Messages
459
Likes
5
Points
35

Single D

JF-Expert Member
Joined Feb 27, 2007
459 5 35
Kwa msiba ulopata,Kinyau umesisika,
Pole zangu nazileta,kwa ndugu na wahusika,
Ujumbe tumeupata,Hapa si pa kukalika,
Mdau Kinyau pole,Mwenyezi Mungu akupe nguvu.

Twasafiri kwake mola,Hapa si makao yetu,
Kifo hakina kabila,Hakijali vyeo vyetu,
Hata kwao watawala,hakina wakili katu,
Mdau kinyau pole,Mwenyezi Mungu akupe nguvu.
 

Forum statistics

Threads 1,203,210
Members 456,663
Posts 28,104,693