Pokea Pole
Mpendwa Kinyau,
Pokea pole Kinyau, kaka'ko kuondokea
Muumba msisahau, mwenywe ameamua
kumbuka pia Kinyau, kaka'ko kumuombea
Kuondokewa Kaka'ko, Kinyau pokea pole
Nasema pokea pole, kwa sala nawaombea
Punguza pia kelele, mayowe kumlilia
kumbuka mengi ya kale, kaka'ko mlotendea
Kuondokewa Kaka'ko, Kinyau pokea pole
Mapenzi yake Muumba, kaka'ko kumchukua
Hakuna cha lambalamba, mganga wa kugangua
Avuta bila ya kamba, Muumba wetu wajua?
Kuondokewa Kaka'ko, Kinyau pokea pole
Ni kwake tulipotoka, na kwake tutarejea
Nimtajaye Rabuka, aliyeumba dunia
Na kila kiloumbika, mwenyewe kakiumbia
Kuondokewa Kaka'ko, Kinyau pokea pole
Nakuagia kwaheri, ya tano nina ishia
Kinyau uwe jasiri, mama'ko asubiria
Jikaze uwe ngangari, nduguzo wahitajia!
Kuondokewa Kaka'ko, Kinyau pokea pole
Wasalaam,
Nduguyo Choveki