SoC01 Namna Bora na Endelevu ya Kutatua Tatizo la Mrundikano wa Machinga Katika Maeneo Yasiyo Rasmi kwa Biashara

Stories of Change - 2021 Competition

Mwadilifu Mdhulumiwa

JF-Expert Member
Jul 22, 2021
418
630
Utguanlizi:

Machinga ni jina maarufu wanaloitwa wafanya biashara ndogondogo wa mijini na vijijini kote nchini. Wafanyabiashara wa kundi hili wanatabia ya kuhamahama kutembea huku na kule kutafuta maeneo wanayoona wanapata wateja wengi wanaowaungisha bidhaa zao.

Utamaduni huu wa kuhamisha hamisha biashara zao ndio hasa huwafanya wajikute wamepeleka biashara zao katika maeneo yasiyo rasmi kama vile kwenye hifadhi za barabara zinazojengwa kwaajili ya wananchi wanaotembea kwa miguu na sehemu nyingine hujikuta wameziba kabisa njia au kuziba wateja wanaokwenda kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wakubwa wenye flemu za maduka.

Hatua hii ndio huwafanya wajikute wanaingia katika migogoro na mamlaka za serikali au kulalamikiwa na wafanyabiashara wakubwa.

Pamoja na hatua kadhaa ambazo huchukuliwa na serikali lakini tatizo hili limekuwa likijirudia rudia kila wakati na hivyo kuonekana ni tatizo sugu lililokosa ufumbuzi wa kudumu. Pengine ni njia zinazotumika na serikali kutatua tatizo hili au wadau na jamii kukosa utashi wa kulimaliza tatizo hili.

Katika mada hii nitajadili sababu zinazofanya tatizo la machinga kuendelea kukuwa na namna bora ya kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu.

Je nini kinasababisha tatizo la machinga kuibuka kila wakati?

Tunaweza kuwa tunalitazama tatizo la machinga kama kwamba ni tatizo dogo au ni tatizo la sehemu moja au la kundi flani tu, lakini kiuhalisia tatizo hili linachangiwa na mambo mengi sana ikiwemo hata mifumo yetu ya elimu, uchumi, siasa na kijamii. Miongoni mwa mambo yanayochangia ongezeko la tatizo la machinga mtaani ni pamoja na haya yafuatayo;-

Ukosefu wa ajira:

Ukosefu wa ajira ni moja ya sababu kubwa za ongezeko la machinga mtaani, Katika kundi hili wapo wanafunzi wanaomaliza shule za msingi na sekondari na vyuo mbalimbali kila mwaka ambao huamua kujiajiri katika biashara ndogondogo baada ya kukosa ajira ya serikali.

Mara wamalizapo masomo wanafunzi hawa tayari hufikia hatua ya kujiona ni watu wazima na hivyo huanza kuwajibika kimajukumu kama baba au mama au hata kujitegemea yeye binafsi kujikimu kimaisha wakiwa nje ya ajira ya serikali.

Hivyo kundi hili ni lazima litaendelea kuwepo hasa ikizingatiwa na uwezo mdogo wa serikali katika kutoa ajira kwa wananchi wake wa makundi mbalimbali ya wahitimu wa shule na vyuo. Hapa ndipo makundi ya machinga huzaliwa na kuongeza familia mtaani kila mwaka.

Kudorora kwa sekta mama ya kilimo:

Kutokufanya vizuri kwa sekta nyingine za ajira ambazo zingeweza kutoa ajira kwa wananchi wa makundi mengi kama sekta ya kilimo ni sababu nyingine inayochangia kuongezeka kwa machinga mtaani. Vijana wengi wamekuwa hawavutiwi katika kuwekeza nguvu zao kwenye kilimo sababu ya kuyumba kwa soko lamazao ya kilimo kama mahindi, pamba na korosho.

Kukosekana soko la uhakika kwa mazao ya sekta ya kilimo kumefanya vijana wengi kuamini kuwa kilimo hakina faida katika kujikwamua kimaisha kwani wanaona namna wakulima wetu wanavyohangaika na masoko ya mazao waliyoyazalisha.

Ukosefu wa mfumo bora wa kuwaingiza vijana katika biashara:

Vijanana wengi wamekuwa wakijiingiza katika kufanya biashara bila kuwa na elimu thabiti kuhusu aina ya biashara anayotaka kufanya na mazingira ya bishara husika. Elimu hii ingetolewa tangu mashuleni ingekuwa ni mwongozo bora kwa wale wanaokuja kujiajiri kama machinga.

Aina na namna ya hatua ambazo huchukuliwa na serikali hazileti ufumbuzi endelevu:

Mara nyingi na katika mikoa mingi nchini hatua za kuthibiti machinga zimekuwa zikichuliwa kikatili ikiwemo kuwaamrisha kufunga biashara zao na kuondoka katika maeneo walipoweka biashara hizo au kuvunja vunja kabisa meza na vibanda vyao vya bishara na kuwafukuza kwa nguvu.

Utaratibu wa nanma yoyote unaohusisha matumizi ya nguvu ama amri za kimamlaka kamwe hauwezi kulipatia tiba ya kudumu tatizo hili, zaidi utasaidia tu kulituliza kwa muda lakini ni lazima litaibuka tena kwa ukubwa na athari zinazozidi za awali.

Utatuzi wa suala hili kimsingi unapaswa ufanyike kwa kuzingatia sababu zilizofanya wamachinga hao kupeleka biashara zao katika maeneo walipowakuta! Sababu kubwa huwa ni kufuata wateja wa bidhaa zao, kwamba wanapeleka biashara zao maeneo ambako wanaona kuna wateja.

Hivyo basi kuwaondoa kwa nguvu na kuwapeleka maeneo ambako hawana uhakika wa kuuza bidhaa zao, ni dhahiri hawata kubali kukaa huko. Hatakama watakaa basi itakuwa ni kwa muda tu, lakini baadaye lazima watarudi tena kwenye maeneo yaleyale walikoona kuna wateja wengi.

Tozo kubwa za kodi na utaratibu wa malipo usio rafiki kwenye biashara rasmi:

Wafanya biashara wengi wamekuwa wakiogopa kujisajili katika mfumo rasmi wa ulipaji kodi ya serikali kutokana na mfumo mbovu wa ukadiriaji wa kodi za biashara husika.

Mathalani mfanya biashara anaweza kwenda TRA kwaajili ya kupata namba ya mlipa kodi (TIN) ili akaiwasilishe kwenye mamlaka nyingine kwaajili ya kusajiliwa au kupewa vibali kabla kuanza biashara husika ambayo hata hana uhakika kama vibali husika atapata au la! Lakini jambo la kushangaza ukienda TRA kuomba tu hiyo namba ya mlipa kodi, Kwanza unakadiriwa kodi kubwa isiyolingana na faida unayotegemea kupata.

Pili unaamrishwa na TRA kwenda kuanza kuilipa hiyo kodi saa hiyo hiyo hata kabla hujaanza biashara husika! Je hii kodi mfanyabiashara analipa kutoka kwenye mapato ya biashara ipi ambayo hajaanza kuifanya? Utamaduni huu mbovu wa TRA nao umekuwa chanzo cha wafanyabiashara wengi kukimbia mfumo rasmi wa ufanyaji biashara na kuamua kuwa machinga.

Uwekezaji mdogo wa serikali katika kuliinua kundi la vijana kiuchumi:

Serikali imekuwa ikijaribu kuwainua vijana kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri za miji, majiji na manispa kwa makundi ya kina mama , vijana na wenye ulemavu.

Hata hivyo kiasi cha fedha kinachotengwa na halmashauri nyingi ni kidogo mno ukilinganisha na mahitaji halisi ya vijana katika maeneo husika.

Pia kumekuwepo na udanganyifu na ubabaishaji mwingi unafanywa na watendaji wa halmashauri hizo. Mathalani kuna halmashauri za miji na Manispaa tangu mwaka huu uanze hazijatoa mikopo hata mara moja kwa makundi ya vijana , kina mama na wenye ulemavu ilihali kanuni ya serikali inazielekeza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya kila robo mwaka kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo.

Lakini hapohapo utakuta kwenye zile taarifa zao za kila robo mwaka wameripoti kuhusu kutoa mikopo hiyo na hata katika mpangokazi wameainisha kitu hicho. Uwekezaji huu wa wasiwasi ndio unachangia vijana wengi kushindwa kukuza mitaji yao na kufungua biashara rasmi na badala yake kujiunga na machinga.

Je nini kifanyike ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la machinga nchini?

Ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo la machinga mijini serikali na wadau hawana budi kuchukua hatua zifuatazo;-

Serikali iimarishe mifumo ya kiuchumi kwa kuongeza fungu la bajeti katika Nyanja zote za uzalishaji ili kupanua wigo wa fursa za ajira kwa makundi mbalimbali ya wananchi wake wanaomaliza shule na vyuo.

Serikali na wadau wa kilimo na viwanda waboreshe mazingira ya uwekezaji na kupanua masoko ya bidhaa za kilimo ili kuboresha kipato cha mkulima na hivyo kuwavutia vijana wengi zaidi kujiajiri katika sekta hiyo.

Serikali na wadau wote wawashirikishe machinga kikamilifu kabla ya kuwaondoa sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyingine. Maeneo ya kuwahamishia yasiwe ni maeneo mapya yasiyo na wateja wa kuwahakikishia soko bali yateuliwe maeneo rasmi jirani na masoko makubwa kwani wao pia hutega biashara zao kufuata wateja wanaokwenda kwenye masoko hayo.

Serikali na wadau wa bishara waunde mfumo rafiki wa namna ya kuwaingiza vijana katika kufanya biashara kwa mtindo na mbinu za kisasa lakini pia katika mfumo utakaowafanya watambuwe mazingira bora na salama ya kufanyia biashara zao. Elimu rasmi ya biashara na ujasiriamali itolewe kwa wanafunzi wetu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa biashara ianzishe mpango kabambe wa kuyaboresha na kuyapanua masoko ya vitongoji vya miji nchini kote ili mengine yatumike kama vituo maalumu kwa ajili machinga badala ya kuwapeleka nje ya miji kwenye maeneo mapya yasiyo na wateja wa kutosha.

Eidha mamlaka zinazohusika na tozo za kodi kwa biashara mbalimbali ziangalie upya taratibu zake za ukadiriaji wa tozo hizo na kuziboresha ili kuvutia wafanyabiashawengi kujisajili katika mfumo rasmi wa kulipa kodi na hivyo kusaidia kupunguza machinga na kuzalisha walipakodi wengi zaidi.

Serikali iboreshe fungu la bajeti na iimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha hizo kwenye halmashauri zake ili ziache kukwepa kutoa mikopo kwa vijana na badala yake ziongeze fungu na kasi ya utoaji wa mikopo hiyo ili kuwezesha vijana wengi zaidi kukuza mitaji na kujisajili katika bishara rasmi ili kupunguza machinga mtaani.

Hitimisho:

Tatizo la kutapakaa kwa machinga katika maeneo mbalimbali nchini ni matokeo ya ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira rasmi za serikali . Hivyo katika kulishughulikia suala hili serikali na wadau hawana budi kutambua kuwa machinga hawa popote walipo huwa wapo kazini kujitafutia riziki za maisha ili kujikimu kimaisha wao binafsi na familia zao au wategemezi wao.

Hivyo basi, njia zinazotumika kuwaondoa katika maeneo wanayofanyia biashara zao ni vyema zikatoa ufumbuzi wa kuwahakikishia masoko mbadala ya bidhaa zao yatakayowafanya waendelee kujipatia riziki za maisha yao. Lakini kinyume na hivyo ndio chanzo cha tatizo hili kuendelea kudumu siku zote kwani mfanyabiashara hawezi kukubali kuendelea kuwepo mahala ambapo biashara zake hazitoki.
 
Wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mikoa pitieni uzi huu mpate madini ya kukabiliana na tatizo la machinga bila vurugu!
 
You don't want me to comment I have totally different take on this....

Kuna Suluhisho la kudumu sustainable na kuna suluhisho la muda mpaka hapo baadae yaani delaying the inevitable...,

Kwanza kabisa machinga inabidi iwe state ya mtu kupitia na sio state ya kudumu (maisha haya ni magumu yasiyojulikana kesho yake na hayana security); ni maisha ya kimasikini..., Kwahio hata tukijenga sehemu ni kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ambao wanapanga bidhaa zao (sio machinga tena) kwa kufuata sheria na watu hao kuingia kwenye mfumo unaotambulika hivyo kuchangia pato..., ila biashara zilivyo na mzunguko wa pesa mgumu na vilevile watu buying power yao ni ndogo utajikuta hata wafanyabiashara hao (potentially) na wa sasa wanaolipia maduka wote ni one step away from ufukara. Ingawa ni hatua nzuri kuwaingiza watu hawa kwenye mfumo unaotambulika.....

Lakini je mfumo huo tunaowaingiza ni sustainable for 21st century ? watu tunaelekea kwenye delivery services na watu kufanya shopping online alafu bado tunajenga kesho yetu kwa watu kuchuuza mali ?, kwahio badala ya kufanya mipango ya kuendelea kuwa na machinga kesho na keshokutwa mipango ya kufanya ni kuhakikisha waliopo wanaondoka kwenye umachinga na wanaokuja hawaingii kwenye umachinga.... Wanyonge ni wengi Tanzania..., ila wanyonge ni kina nani ?

 
Back
Top Bottom