Namlilia jumanne mayoka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Namlilia jumanne mayoka

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by AHAKU, Feb 17, 2010.

 1. A

  AHAKU Member

  #1
  Feb 17, 2010
  Joined: Jan 28, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nawaamkia wana JF huku nikiwa na machungu makubwa kwa kuondokewa na mmoja wa magwiji wa Kiswahili hususan katika taaluma ya Ushairi Huyu si mwingine bali ni mzee Jumanne Mayoka. Hapa chini nawaletea tanzia yake iliyomo katika mtandao wa kampuni ya Mwananchi na pia gazetini (Mwananchi)
  Yaani angalau Mwananchi limeona umuhimu wa kumuandikia mtaalamu huyu, waandishi wengine katika magazeti mengine tena ya Kiswahili wamepiga kimya kizito ni aibu hii kwa waandishi wetu
  Someni Tanzia yake

  Mayoka: Ingawa kifo kina ogofya, hayuko atakaye kikwepa
  Na Abeid Poyo
  KWA wadau wa lugha ya Kiswahili, mwaka 2010 unaweza ukawa umeanza na nuksi kwao.

  Miezi minane tu baada ya kufariki kwa Sheikh Shaaban Gonga, wadau wa Kiswahili na ulimwengu wake wamempoteza mwanazuoni mwingine mahiri wa lugha hiyo.

  Huyu ni Jumanne Mrisho Mayoka, mmoja wa watunzi na washairi mahiri na maarufu nchini aliyefariki katika hospitali ya Mt Francis ya Ifakara alipokuwa amelazwa wiki iliyopita.

  Kwa mujibu wa familia yake Mayoka ( 66 ) alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifua. Alizikwa katika makaburi ya Chang’ombe Maduka mawili jijini Dar es Salaam.

  Wasomi wengi wa Kiswahili wanakiri alikuwa na umbuji na umahiri mkubwa katika fani ya ushairi iliyomtambulisha katika ulimwengu wa Kiswahili.

  Ni kwa sababu hii, wapenzi wa ushairi na wadau wa Kiswahili kwa ujumla wamempoteza mmoja wa watu muhimu tena katika kipindi ambacho fani hiyo ikiwa inachungulia kaburi.

  Kwa wanaomjua wanasema, licha ya kusoma kwa lugha ya Kiingereza karibu madaraja yote ya elimu aliyopitia, hakuwa mtumwa wa lugha za kigeni. Aliijua lugha ya Kiswahili, aliipenda, aliionea fahari na hata kuipigania.

  "Ni vigumu kuzungumzia maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania bila ya kulitaja jina la Jumanne Mrisho Mayoka aliyekuwa akijivunia lugha yake adhimu ya Kiswahili...

  Mara zote alikuwa akisema kwa fakhari kuwa asemaye lugha yake hana kigugumizi," anasema Sheikh Khamis Mataka, mtaalamu wa Kiswahili.

  Mataka aliyewahi kuwa mweka hazina wa Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), mwishoni mwa miaka ya 1980 anaendelea kumuelezea marehemu kama mdau mkubwa, mtaalamu, mpenzi wa lugha ya Kiswahili na mshairi farisi aliyetoa mchango mkubwa katika kukijenga, kukilinda na kukienzi Kiswahili.

  "Haya yanadhihirika unapoangalia mchango wake katika kipindi cha Mbinu za Kiswahili kilichokuwa kikirushwa na Redio Tanzania Dar es Salaam na ushiriki wake katika mihadhara na makongamano kadhaa ya lugha ya Kiswahili na Fasihi hususan Ushairi," anafafanua zaidi.

  Alikuwa mshairi wa kimapokeo na pale ulipozuka mgogoro mkubwa baina ya wateteao ushairi wa mapokeo unaozingatia kanuni za utungaji wa shairi hususan vina na mizani na wale watetezi wa ushairi huru ama matingiti, wakiongozwa na baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mzee Mayoka alishiriki vilivyo na kutoa mchango mkubwa akitetea ushairi wa mapokeo.

  Kwa mujibu wa Mataka, ushahidi wa mchango wake katika mgogoro huu ni kitabu alichokitoa mwaka 1984 na kukipa jina la Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka.

  Akiutetea ushairi wa kimapokeo kama anavyonukuliwa na Florence Ngesa Indede katika mada yake 'Mabadiliko katika umbo la ushairi na athari zake katika ushairi wa Kiswahili,’ (2008) Mayoka aliyejulikana kishairi kwa jina la Malenga wa Bara aliandika:

  "Ushairi ni mtungo wa kisanaa ulio na mpangilio maalum na lugha ya mkato ambayo ndani yake una vina, urari wa mizani na muwala maalum ambavyo kwa pamoja huwa na fani na maudhui yahusuyo hisi fulani na tukio juu ya maisha ya mtu au watu wa mazingira na wakati maalum."

  Kwa wanaofuatilia kipindi cha Ulimwengu wa Kiswahili kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) wanajua namna alivyokuwa mshiriki muhimu aliyechangia kwa kiwango kikubwa kukinogesha kipindi hicho ambacho aghlabu kimekuwa chuo chema kwa kutoa maana na maelezo ya maneno mbalimbali ya Kiswahili.

  Utamfurahia Mayoka pale anapofafanua maana na matumizi ya baadhi ya maneno ya Kiswahili kwa kurejea beti za mashairi ama tenzi zilizotungwa na magwiji wenzake miaka mingi iliyopita. Alikuwa na kifua cha kukariri na hili katu si jambo adimu kwa mshairi nguli kama yeye.

  Alikuwa mtetezi na mpiganaji wa lugha ya Kiswahili aliyeamua kukitumia kipindi hicho cha Televisheni kama silaha yake nyingine ya kukipigania Kiswahili.

  Amekufa akikitumikia Kiswahili, ulimwengu wa Kiswahili hauna budi kutambua mchango wake.

  Kwa mujibu wa Barnabas Maro, mwana safu maarufu katika gazeti la Habari Leo, alikuwa Mzee Mayoka aliyewapa tanbihi wazungumzaji wa Kiswahili kujua tafsiri sahihi ya neno la Kiingereza ‘Stake holder’.

  "Zamani kidogo, stake holder ilifasiriwa kuwa 'mshika dau’ hadi mwalimu Jumanne Mayoka, yule mtaalamu wa Kiswahili alipotanabahisha kwamba neno sahihi ni 'mdau' wengi ni wadau…" anasema Maro katika moja ya makala zake gazetini.

  Miongoni mwa watu watakaomkumbuka kwa kiasi kikubwa ni wanajopo wenzake katika vipindi vya televisheni aliokuwa nao bega kwa bega hadi siku za mwisho za umauti.

  Amezidi kutonesha donda la Mzee Suleiman Hegga, Mwalimu Mohammed Mwinyi, Maprofesa Abdallah Safari na David Massamba ambao mwaka 2009 walimpoteza mshiriki mwingine mahiri, Profesa Padri Zakaria Mochiwa.

  Aidha kuondoka kwake kumeongeza pengo la wataalamu waswahili waliokijua Kiswahili bila ya kuwa na vyeti vya madaraja ya kitaaluma kama vile Mzee Khamisi Akida, Pera Ridhiwan na wengineo.

  Baadhi ya wazee hawa wapo waliochangia kwa kiwango kikubwa kuwapandisha chati wasomi wa Kiswahili wanaosifika sasa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Nani wa kuwaenzi na vipi wataenziwa? Ni maswali yanayopaswa kupatiwa majibu na wale waliobaki katika medani ya lugha ya Kiswahili.

  Mayoka ameondoka, amekifuata kifo ambacho miaka mingi iliyopita aliwahi kukiandikia katika moja ya kazi zake, alisema:

  "Hako yeyote akwepe, ingawa kina ogofyo, Kijapo kisimnyape, afoke kisambe fyo! Kama yupo nimlipe, arudishwe Osagyefyo,
  Ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.

  Hakichaguwi makupe, miti hufyekwa fyekefyo, Wenye hadhi na machepe, wote chawapa chachafyo, Vyote viumbe kichape, visende chafya si chefyo, ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.

  Tama na afe mapepe, akilize hofyo-hofyo, Ndugu hawapati lepe, hata hawasemi fifyo, Hawawezi wamtupe, mazishi yatukuzwafyo,
  Ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.

  Mbali ya Diwani ya Mayoka, alitoa kazi kadhaa kama vile Utenzi wa Vita vya Uhuru wa Msumbiji (1981), Vina na Mizani ni Uti wa Ushairi wa Kiswahili katika Mulika, Fasihi Simulizi na Nahau na Utangulizi wa Diwani ya Ustadh Andanenga (1997). Alitoa mashairi mengi katika magazeti ya Ngurumo, Kiongozi na Mfanyakazi.

  Mayoka aliyekuwa msomi wa elimu kitaaluma na mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Manchester, aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwemo Ukurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kuanzia mwaka 1991 hadi 2003 alipostaafu utumishi wa umma.

  Aidha aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri ya iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) na Mkuzaji mitaala katika iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni Kilipoanzishwa Chuo Kikuu cha Waislam cha Morogoro mwaka 2005 alikuwa Mkuu wa kwanza wa kitivo cha Sanaa na mhadhiri wa masomo ya Kiswahili na Saikolojia ya Elimu.

  Tarikhi yake inaonyesha alizaliwa mwaka 1944, Kaliua mkoani Tabora. Awali alisomea ualimu katika chuo cha Katoke Bukoba, na baadaye, Stashahada katika taaluma za Maendeleo ya Jamii na Elimu ya Watu Wazima kabla ya kwenda nchini Uingereza kusoma shahada ya Uzamili katika Elimu. Ameacha mjane na watoto watano.

  Sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
   
 2. Kiranga

  Kiranga JF-Expert Member

  #2
  Feb 17, 2010
  Joined: Jan 29, 2009
  Messages: 37,971
  Likes Received: 9,623
  Trophy Points: 280
  Huyu Mzee nilikuwa namsikiliza sana kwenye kipindi cha kiswahili RTD.Mmoja wa magwiji wa Kiswahili.
   
 3. A

  AHAKU Member

  #3
  Feb 17, 2010
  Joined: Jan 28, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Alikuwa mchangiaji mzuri hata mimi japo siku moja moja nilikuwa namcheki ila duh alikuwa deep
   
 4. SMU

  SMU JF-Expert Member

  #4
  Feb 17, 2010
  Joined: Feb 14, 2008
  Messages: 8,116
  Likes Received: 2,413
  Trophy Points: 280
  Upumzike kwa amani Mayoka.
   
 5. A

  AHAKU Member

  #5
  Feb 17, 2010
  Joined: Jan 28, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  nilikuwa namcheki pale runingani TVT sasa TBC1
   
 6. Sikonge

  Sikonge JF-Expert Member

  #6
  Feb 17, 2010
  Joined: Jan 19, 2008
  Messages: 11,524
  Likes Received: 576
  Trophy Points: 280
  Nilivyosoma Jumanne Mayoka (Majoka) nilifikiri ni ile familia ya kijijini kwetu. Jina lilikuwa limenikaa vizuri tu masikioni/machoni hadi nilipokuja kusoma ndani zaidi. Huyu Mzee namkumbuka sana ingawa sikuwa mpenzi wa lugha ila nilikuwa nawasikiliza mara moja moja. Nakumbuka siku moja wakawa wanabishana kuhusu jina la beberu wa kondoo anaitwaje kwa kiswahili. Baada ya mjadala mkubwa sana, wakaamuwa kumpa jina la Kisukuma/kinyamwezi yaani anaitwa NG'ONDI. Sijui kama watakuwa bado wanatumia hilo jina au wamebadili.

  Hawa wazee wamefanya kazi moja safi sana ingawa kwa sasa naona kuna mengine hawa jamaa wanaharibu kabisa. Kwa nini kwa mfano TV isiitwe tu TV na badala yake wanaitwa eti Luninga? Kwa nini computer issitwe kompyuta na badala yake wanaita sijui nini? Kuna maneno kama Miundombinu nakubaliana nalo maana kwa kiingereza linawapa shida sana hasa wazee.

  Rip Mzee Mayoka!!!!!
   
 7. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #7
  Feb 17, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,737
  Likes Received: 7,507
  Trophy Points: 280
  Kwetu siye wapenzi wa lugha ya Kiswahili kwa hakika tumempoteza mwalimu na gwiji wa lugha hiyo kwa hakika tutamkosa sana. Mungu ailaze roho yake pema peponi. Amina
   
 8. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #8
  Feb 17, 2010
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 25,641
  Likes Received: 23,839
  Trophy Points: 280
  Hata mimi namkumbuka enzi zile za RTD kwenye kipindi cha Mbinu za Kiswahili, kikiendeshwa na Suleiman Hegga, wakati huo akiwa na Abdulbary Diwani, Salim Ali Kibao na wengine wawili ambao majina yamenitoka. Mghanii wa wakati huo akiwa ni Athumani Khalfani, wana mashairi maarufu akiwemo Amiri A.S Adanenga, (Sauti ya Kiza)

  Enzi hizo redio ni moja tuu, ikiwashwa asubuhi ni mpaka usiku.

  RIP Jumanne Mayoka, kaungane na mdogo wako Nadhir Mayoka.
   
 9. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #9
  Feb 17, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  kweheli ndugu Mayoka,
  ni kweli umetutoka,
  machungu kutuachia
  daima tutakulilia

  umetuacha Mayoka
  kama mti na shoka
  kuomboleza hatutachoka
  daima tutakulilia

  daima tutakkulilia
  kipenzi chetu Mayoka
  pengo ulilo liacha
  hakuna wa kuliziba

  kweheli mayoka kwaheri
  jamii twakutakia heri
  Mungu iweke pema mahari
  roho yake mayoka
   
 10. C

  Choveki JF-Expert Member

  #10
  Feb 18, 2010
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 35
  Buriani bin Mayoka;  Buriani e mayoka, kwa heri umetutoka
  Twakuombea Rabuka, peponi uje kufika
  kwa mengi twakukumbuka, na yale uloandika
  Jumanne umetutoka, buriani bin Mayoka


  Buriani we Mayoka, machozi yanatutoka!
  Amekuita Rabuka, Muumba alotukuka
  kwa heri baba Mayoka, kwa heri babu Mayoka
  Jumanne umetutoka, buriani bin Mayoka


  Kwa heri bwana Mayoka, kwaheri umeondoka
  Ghafula umetutoka, wakati wahitajika
  Mapenzi ya Mtukuka, ingawa twasikitika
  Jumanne umetutoka, buriani bin Mayoka


  Kwa heri gwiji Mayoka, ni wengi tumeshituka
  Habari zikazunguka, Dunia kusikitika
  Mwalimu hukuamka, Yarabi amekuita
  Jumanne umetutoka, buriani bin Mayoka


  Kwa heri ndugu Mayoka, simanzi imetushika
  Ni wengi tunatamka, waenda kupumzika
  Wafiwa mjekumbuka, kwa sala twamkumbuka
  Jumanne umetutoka, buriani bin Mayoka
   
 11. The Boss

  The Boss JF-Expert Member

  #11
  Feb 18, 2010
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 37,852
  Likes Received: 22,944
  Trophy Points: 280
  buriani mayoka...
   
 12. Tusker Bariiiidi

  Tusker Bariiiidi JF-Expert Member

  #12
  Feb 18, 2010
  Joined: Jul 3, 2007
  Messages: 4,986
  Likes Received: 419
  Trophy Points: 180
  RIP Jumanne Mayoka... Mkuu Pasco sikujua kama Nadhir Mayoka hatunaye hapa duniani... RIP Nadhir Mayoka Pasco nashukuru kwa taarifa...
   
 13. MwalimuZawadi

  MwalimuZawadi JF-Expert Member

  #13
  Feb 18, 2010
  Joined: Sep 1, 2007
  Messages: 643
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
  Tutakosa sana mchango wako wa lugha hii tamu, RIP Mayoka
   
 14. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #14
  Feb 19, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,649
  Likes Received: 117
  Trophy Points: 160
  1
  Bismillaahi Naanza, salaam zipokeeni
  Tutakaa tukiwaza, machozi tele Machoni,
  Mwenzetu ameshaanza, nasisi tupo mbioni,

  Ametutoka mpenzi, Mayoka hayupo tena

  2
  Yanabaki simulizi, amekwenda kwa manani
  Katuachia simanzi, ushairi mashakani
  Kigogo wetu wa tenzi, mrithi wake ni nani

  Ametutoka mpenzi, Mayoka hayupo tena

  3
  Kiswahili alikienzi, akipa tele thamani
  Mashughuri kwenye tenzi, sote tulimuamini
  Alikuwa ni muhunzi, kwa tungo zake za fani

  Ametutoka mpenzi, Mayoka hayupo tena

  4
  Alikuwa ni mtetezi, akulala asilani
  Kiswahili kukienzi, tunampa shukurani
  Alikuwa mkombozi, afananaye ni nani

  Ametutoka mpenzi, Mayoka hayupo tena

  5
  Alikuwa ni jahazi, akwenda mbio majini
  Akuwa mkimbizi, wa lugha asilani.
  Kuendelea siwezi, kalamu naweka chini

  Ametutoka mpenzi, Mayoka hayupo tena
   
 15. m

  maikomjd New Member

  #15
  Feb 19, 2010
  Joined: Oct 30, 2008
  Messages: 1
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nimepokea taarifa hii kwa mshituko, sikuwa na taarifa. Msiba huu unanigusa sana kwani huyu aliwahi kuwa mkurugenzi wa Taasisi ya elimu ya Watu wazima katika miaka ya 90 wakati nikiwa mwanafunzi katika Taasisi hiyo.

  Hili ni pigo katika fani ya Kiswahili na kwa wadau wengine!
   
 16. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #16
  Feb 21, 2010
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,632
  Likes Received: 634
  Trophy Points: 280
  Mola aiweke roho ya marehemu Mayoka peponi. Mimi binafsi nilijifunza mengi sana kutokana na kusikiliza MBINU ZA KISWAHILI kipindi ambacho marehemu alikuwamchangiaji mahili sana hasa pale walipokuwa wanabishana na magwiji wenzie ambao pia ni marehemu Prof. Zakaria Mokiwa na Mzee Akida.. R.I.P. magwiji wetu
   
 17. Balantanda

  Balantanda JF-Expert Member

  #17
  Feb 21, 2010
  Joined: Jul 13, 2008
  Messages: 12,359
  Likes Received: 1,084
  Trophy Points: 280
  Mkuu Pasco nadhani hapo mmojawapo unamzungumzia mzee Hamis Akida

  R.I.P Mzee wetu Nguli wa Kiswahili Jumanne Mayoka
   
 18. Mphamvu

  Mphamvu JF-Expert Member

  #18
  Dec 29, 2011
  Joined: Jan 28, 2011
  Messages: 10,709
  Likes Received: 970
  Trophy Points: 280
  Aliandika shairi la 'Ningekuwa na Sauti' lililokuwa likipatikana katika Diwani ya Fungate ya Uhuru ya Mohamed Seif Hatibu(Ph.D)...
  Alikuwa mfuasi wa ushairi wa Kimapokeo huyu!
   
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
Loading...