Nawaamkia wana JF huku nikiwa na machungu makubwa kwa kuondokewa na mmoja wa magwiji wa Kiswahili hususan katika taaluma ya Ushairi Huyu si mwingine bali ni mzee Jumanne Mayoka. Hapa chini nawaletea tanzia yake iliyomo katika mtandao wa kampuni ya Mwananchi na pia gazetini (Mwananchi)
Yaani angalau Mwananchi limeona umuhimu wa kumuandikia mtaalamu huyu, waandishi wengine katika magazeti mengine tena ya Kiswahili wamepiga kimya kizito ni aibu hii kwa waandishi wetu
Someni Tanzia yake
Mayoka: Ingawa kifo kina ogofya, hayuko atakaye kikwepa
Na Abeid Poyo
KWA wadau wa lugha ya Kiswahili, mwaka 2010 unaweza ukawa umeanza na nuksi kwao.
Miezi minane tu baada ya kufariki kwa Sheikh Shaaban Gonga, wadau wa Kiswahili na ulimwengu wake wamempoteza mwanazuoni mwingine mahiri wa lugha hiyo.
Huyu ni Jumanne Mrisho Mayoka, mmoja wa watunzi na washairi mahiri na maarufu nchini aliyefariki katika hospitali ya Mt Francis ya Ifakara alipokuwa amelazwa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa familia yake Mayoka ( 66 ) alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifua. Alizikwa katika makaburi ya Changâombe Maduka mawili jijini Dar es Salaam.
Wasomi wengi wa Kiswahili wanakiri alikuwa na umbuji na umahiri mkubwa katika fani ya ushairi iliyomtambulisha katika ulimwengu wa Kiswahili.
Ni kwa sababu hii, wapenzi wa ushairi na wadau wa Kiswahili kwa ujumla wamempoteza mmoja wa watu muhimu tena katika kipindi ambacho fani hiyo ikiwa inachungulia kaburi.
Kwa wanaomjua wanasema, licha ya kusoma kwa lugha ya Kiingereza karibu madaraja yote ya elimu aliyopitia, hakuwa mtumwa wa lugha za kigeni. Aliijua lugha ya Kiswahili, aliipenda, aliionea fahari na hata kuipigania.
"Ni vigumu kuzungumzia maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania bila ya kulitaja jina la Jumanne Mrisho Mayoka aliyekuwa akijivunia lugha yake adhimu ya Kiswahili...
Mara zote alikuwa akisema kwa fakhari kuwa asemaye lugha yake hana kigugumizi," anasema Sheikh Khamis Mataka, mtaalamu wa Kiswahili.
Mataka aliyewahi kuwa mweka hazina wa Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), mwishoni mwa miaka ya 1980 anaendelea kumuelezea marehemu kama mdau mkubwa, mtaalamu, mpenzi wa lugha ya Kiswahili na mshairi farisi aliyetoa mchango mkubwa katika kukijenga, kukilinda na kukienzi Kiswahili.
"Haya yanadhihirika unapoangalia mchango wake katika kipindi cha Mbinu za Kiswahili kilichokuwa kikirushwa na Redio Tanzania Dar es Salaam na ushiriki wake katika mihadhara na makongamano kadhaa ya lugha ya Kiswahili na Fasihi hususan Ushairi," anafafanua zaidi.
Alikuwa mshairi wa kimapokeo na pale ulipozuka mgogoro mkubwa baina ya wateteao ushairi wa mapokeo unaozingatia kanuni za utungaji wa shairi hususan vina na mizani na wale watetezi wa ushairi huru ama matingiti, wakiongozwa na baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mzee Mayoka alishiriki vilivyo na kutoa mchango mkubwa akitetea ushairi wa mapokeo.
Kwa mujibu wa Mataka, ushahidi wa mchango wake katika mgogoro huu ni kitabu alichokitoa mwaka 1984 na kukipa jina la Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka.
Akiutetea ushairi wa kimapokeo kama anavyonukuliwa na Florence Ngesa Indede katika mada yake 'Mabadiliko katika umbo la ushairi na athari zake katika ushairi wa Kiswahili,â (2008) Mayoka aliyejulikana kishairi kwa jina la Malenga wa Bara aliandika:
"Ushairi ni mtungo wa kisanaa ulio na mpangilio maalum na lugha ya mkato ambayo ndani yake una vina, urari wa mizani na muwala maalum ambavyo kwa pamoja huwa na fani na maudhui yahusuyo hisi fulani na tukio juu ya maisha ya mtu au watu wa mazingira na wakati maalum."
Kwa wanaofuatilia kipindi cha Ulimwengu wa Kiswahili kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) wanajua namna alivyokuwa mshiriki muhimu aliyechangia kwa kiwango kikubwa kukinogesha kipindi hicho ambacho aghlabu kimekuwa chuo chema kwa kutoa maana na maelezo ya maneno mbalimbali ya Kiswahili.
Utamfurahia Mayoka pale anapofafanua maana na matumizi ya baadhi ya maneno ya Kiswahili kwa kurejea beti za mashairi ama tenzi zilizotungwa na magwiji wenzake miaka mingi iliyopita. Alikuwa na kifua cha kukariri na hili katu si jambo adimu kwa mshairi nguli kama yeye.
Alikuwa mtetezi na mpiganaji wa lugha ya Kiswahili aliyeamua kukitumia kipindi hicho cha Televisheni kama silaha yake nyingine ya kukipigania Kiswahili.
Amekufa akikitumikia Kiswahili, ulimwengu wa Kiswahili hauna budi kutambua mchango wake.
Kwa mujibu wa Barnabas Maro, mwana safu maarufu katika gazeti la Habari Leo, alikuwa Mzee Mayoka aliyewapa tanbihi wazungumzaji wa Kiswahili kujua tafsiri sahihi ya neno la Kiingereza âStake holderâ.
"Zamani kidogo, stake holder ilifasiriwa kuwa 'mshika dauâ hadi mwalimu Jumanne Mayoka, yule mtaalamu wa Kiswahili alipotanabahisha kwamba neno sahihi ni 'mdau' wengi ni wadauâ¦" anasema Maro katika moja ya makala zake gazetini.
Miongoni mwa watu watakaomkumbuka kwa kiasi kikubwa ni wanajopo wenzake katika vipindi vya televisheni aliokuwa nao bega kwa bega hadi siku za mwisho za umauti.
Amezidi kutonesha donda la Mzee Suleiman Hegga, Mwalimu Mohammed Mwinyi, Maprofesa Abdallah Safari na David Massamba ambao mwaka 2009 walimpoteza mshiriki mwingine mahiri, Profesa Padri Zakaria Mochiwa.
Aidha kuondoka kwake kumeongeza pengo la wataalamu waswahili waliokijua Kiswahili bila ya kuwa na vyeti vya madaraja ya kitaaluma kama vile Mzee Khamisi Akida, Pera Ridhiwan na wengineo.
Baadhi ya wazee hawa wapo waliochangia kwa kiwango kikubwa kuwapandisha chati wasomi wa Kiswahili wanaosifika sasa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Nani wa kuwaenzi na vipi wataenziwa? Ni maswali yanayopaswa kupatiwa majibu na wale waliobaki katika medani ya lugha ya Kiswahili.
Mayoka ameondoka, amekifuata kifo ambacho miaka mingi iliyopita aliwahi kukiandikia katika moja ya kazi zake, alisema:
"Hako yeyote akwepe, ingawa kina ogofyo, Kijapo kisimnyape, afoke kisambe fyo! Kama yupo nimlipe, arudishwe Osagyefyo,
Ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.
Hakichaguwi makupe, miti hufyekwa fyekefyo, Wenye hadhi na machepe, wote chawapa chachafyo, Vyote viumbe kichape, visende chafya si chefyo, ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.
Tama na afe mapepe, akilize hofyo-hofyo, Ndugu hawapati lepe, hata hawasemi fifyo, Hawawezi wamtupe, mazishi yatukuzwafyo,
Ingawa kina ogofya, hako kifo akiepe.
Mbali ya Diwani ya Mayoka, alitoa kazi kadhaa kama vile Utenzi wa Vita vya Uhuru wa Msumbiji (1981), Vina na Mizani ni Uti wa Ushairi wa Kiswahili katika Mulika, Fasihi Simulizi na Nahau na Utangulizi wa Diwani ya Ustadh Andanenga (1997). Alitoa mashairi mengi katika magazeti ya Ngurumo, Kiongozi na Mfanyakazi.
Mayoka aliyekuwa msomi wa elimu kitaaluma na mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Manchester, aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwemo Ukurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kuanzia mwaka 1991 hadi 2003 alipostaafu utumishi wa umma.
Aidha aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri ya iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) na Mkuzaji mitaala katika iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni Kilipoanzishwa Chuo Kikuu cha Waislam cha Morogoro mwaka 2005 alikuwa Mkuu wa kwanza wa kitivo cha Sanaa na mhadhiri wa masomo ya Kiswahili na Saikolojia ya Elimu.
Tarikhi yake inaonyesha alizaliwa mwaka 1944, Kaliua mkoani Tabora. Awali alisomea ualimu katika chuo cha Katoke Bukoba, na baadaye, Stashahada katika taaluma za Maendeleo ya Jamii na Elimu ya Watu Wazima kabla ya kwenda nchini Uingereza kusoma shahada ya Uzamili katika Elimu. Ameacha mjane na watoto watano.
Sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.