Stories of Change - 2022 Competition

Moselyn11

New Member
Aug 23, 2022
1
0
Screenshot_2022-09-08-10-08-44-70.jpg


Mambo vipi? Nimekuja kukuambia machache kuhusu mimi mpenzi wangu.
Mimi ndiye ninayekufahamu wewe kuliko hata unavyojifahamu wewe, Naam.

Mimi ndiye ninamjua mpenzi anayekufaa kuliko hata wazazi wako wanaokushauri kila siku, umesahau juzi ulikuwa una-gugo sifa za mpenzi bora?

Ni mimi huyuhuyu ambaye nina sifa za kitunguu, Kila siku nakutoa machozi lakini bado unanihitaji, hata jana mimi ndiye nilitumika kusambaza "koneksheni" yako na bado leo unanitaka tena...

Kwani umenichukia?

Mimi ni ajira kwa vijana wengi sasa, hakuna mtu asiye na kazi sasa, huku nikiukuza msemo wa kujiita jobless kwa vijana, hata shemeji yako si anauza simu online? Au hukumbuki kwamba dada yako kila siku anaposti kuhusu platform?

Mimi ndiye ninawapa ulaji na kuvimba wasanii wenu, Kila siku wanakomaa kunitumia kujitajirisha, mnawashabikia huku mnalala njaa
Ndio, ni Mimi

Hey, subiri usiondoke kwanza bado sijamaliza

Mimi naweza kukupa umaarufu kama ukitaka na naweza kukupoteza vilevile, kwani hukumbuki kuhusu Wasanii na wanasiasa Ninachowafanya?

Uongo sio jadi yangu, nakwambia ukweli mtupu.

Mimi ndiye chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika kwa kuwa mimi ninawaonesha kwamba wapo wanaume wanaenda muda mrefu kwenye zile pilau zangu.

Ndio, Mimi nawafanya mabinti wengi wanarahisisha maisha kwa kutafuta wapenzi wasiowasaliti Wala wasiochoka... Na mashuti ya Bakari Nondo Mimi ndo ninayakuza kwa kaka zenu...

Kwangu Mimi kila mtu ni tajiri, hakuna anayeweza kuwa masikini kwangu, angalia vizuri status za rafiki yako yule anayekuomba vocha kila siku, ila status zake zinaonyesha ni Fogo

Mimi ndiye chanzo cha watu wengi kupoteza ajira zao, kwani hukumbuki wale vijana waliopoteza kazi zao kwa kuwa walikuwa wanashuti klipu ya TikTok?

Ninakiri kuhusika moja kwa moja na matendo ya ulawiti wa watoto, ndio kwani si nawaonyesha kaka zenu kwamba ni rahisi kupata utelezi? Na wanapogundua sio rahisi wanaishia kumalizia haja zao kwa wadogo zenu.

Kwani hujui kwamba mimi nimefanya hata usiende ibadani? Unasali online siku hizi na sadaka unatuma kwenye simu kwa kutumia ile lipa namba ya kwenye dhehebu lako.

Mimi ni waziri wa habari sasa, hakuna nisichojua, hata ambacho hukikuti kwenye taarifa ya habari pale ITV kwangu hukosi kupata.

Mimi ndiye nimewafunga vijana kwa wazee kwa minyororo mizito na hawawezi kunikataa Wala kuacha kunitumia

Nimeamua nikwambie kila kitu kunihusu ili kama utanitumia unitumie na ukiamua pia uniache.....

Naitwa MTANDAO

Nina madhara yote hasi na chanya pia, nitumie upendavyo.

MTANDAO

Matumizi ya mtandao yameshamiri sana kwa maisha ya sasa, ni wakati ambapo kila kitu kinachofanyika ni lazima kipitie kwenye mtandao kwa namna moja ama nyingine, aidha kwenye uandaaji wake au kwenye uwasilishaji wake, kuna namna ambayo hatuwezi kuishi tukikosa matumizi ya mtandao.

Matumizi ya mtandao yameshamiri sana, tangu Karne ya 21 ilipoingia tumeshuhudia mageuzi makubwa kwenye suala la mtandao karibia Kila kitu sasa kinategemea mtandao, sekta zote zimejikita kwenye matumizi ya mtandao

Aidha matumizi ya mtandao yamekuwa na tija kubwa kwa dunia kwa kurahisisha mambo mengi ambayo kwa kawaida yangetumia gharama kubwa sana (muda na pesa) kuyakamilisha, kwa mfano, SI ajabu sasa kuona vikao mbalimbali vinafanyika kwa njia ya mtandao, badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda kuhudhuria kikao, kwa kutumia mtandao tu mambo yanafanyika.

Pia mtandao umekuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwa jamii, maana sasa jamii inaishi kwa utamaduni mmoja kwa kuwa matumizi ya mtandao yamechagiza sana kuwa na utamaduni mmoja duniani na kufanya maisha ya Dunia kuwa kitu kimoja bila matabaka ya kitamaduni.

Ni dhahiri kwamba mtandao unasaidia sana kuleta hamasa kwa watu wengi kutengeneza ajira, siku hizi kwa njia ya mtandao kuna solo huria, ni rahisi sana mtu kupata ajira au pia kufanya biashara kwa njia ya mtandao tu, kwa hivyo mtandao unarahisisha maisha kwa namna moja ama nyingine.

Mataifa nayo yanapata faida kubwa sana kupitia matumizi ya mtandao, kwa kuwa yanatumia mtandao kutangaza mambo yake ambayo yanakuja kuleta faida kwa jamii zetu, mfano hai ni matumizi ya mtandao kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana kwenye nchi fulani, jambo ambalo linasaidia sana kukuza uchumi wa nchi kwa utalii wa kigeni na WA ndani pia.

Aidha, matumizi ya mtandao yana madhara hasi pia mengi ni muhimu tuyaangazie pia.....

Kuongezeka kwa uhalifu wa kimtandao. Matumizi mabaya ya mtandao yamepelekea kuzaliwa kwa vitendo viovu vya uhalifu wa kimtandao (cyber crime) ambapo watu wanaotumia vibaya mtandao wanafanya udukuzi (hacking) na wizi mwingine wa kimtandao.

Pia matumizi ya mtandao yanasababisha watu wengi kukosa kazi na ajira zao kutokana na mambo mengi hivi sasa hufanyika kwa mtandao hivyo kupunguza soko la ajira kwa watu ambao wangeweza kuajiriwa kwenye baadhi ya kazi zilizokaimiwa ma mtandao.

Moja kati ya changamoto kubwa sana zinazoletwa na mtandao ni mmomonyoko wa maadili ya
jamii. Jamii ya ulimwengu hivi leo inapitia changamoto kubwa sana ya mmomonyoko wa maadili kutokana na mambo ambayo watu wanayaona kwenye mtandao. Masuala ya mapenzi ya jinsia moja, kuvaa mavazi yasiyo na stara, pia matumizi ya lugha chafu husababishwa na matumizi mabaya ya mtandao kwa kuangalia watu wa kuigwa (role models) wanavyofanya na wengine wanaofanya hayo.

Kuongezeka kwa matukio ya kihalifu na ujambazi ni matokeo ya matumizi mabaya ya mtandao, watu wengi hivi sasa wanajiingiza kwenye makundi ya kihalifu kutokana na kuona video na picha chafu kwenye mitandao zikiwaonesha wahalifu jinsi wanavyofanya na hivyo baadhi wanavutika na kuanza uhalifu.

Mitandao pia imeleta ugonjwa mkubwa sana wa "ulevi wa mtandao", ninauita ulevi kwa sababu hivi sasa watu hawawezi kuishi bila mtandao (Internet addiction), watu wanaharibu kazi kwa sababu ya mtandao, wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ipasavyo kwa sababu ya matumizi ya mtandao.

FUNZO:
Mtandao ni mzuri sana hasa ukitumika kwa umakini na uangalifu mkubwa, watu wote wanaotumia mtandao ni muhimu waangalie madhara yote hasi na chanya ya mtandao kabla hawajajiingiza kwenye matumizi ya mtandao.

Mtandao ukitumika vizuri unafaa sana na una faida kubwa mno ila bila uangalifu, matumizi ya mtandao yatasababisha kizazi kijacho kuharibika kabisa.

"Tumia mtandao kwa maamuzi yako mwenyewe"
"Use internet at your risk"
Sikuambii utumie au usitumie mtandao.






Imeandikwa na:
Moses Kaponda
University of Dar-Es-Salaam student.
Bachelor of science with Education
+255767244436
mokp0220@gmail.com
 

Attachments

  • Screenshot_2022-09-08-10-08-44-70.jpg
    Screenshot_2022-09-08-10-08-44-70.jpg
    311.5 KB · Views: 4
Back
Top Bottom