Bunge, serikali vyashutumiwa kwa kumkingia kifua mfanyabiashara
Zitto Kabwe
na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa serikali na wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wameshutumiwa kumlinda mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia, anayedaiwa kupora fedha za mifuko ya jamii nchini.
Wameshutumiwa kuwa wameshindwa kumchukulia hatua mfanyabiashara huyo na kumlinda asijadiliwe ndani ya Bunge, hata baada ya kubainika kuwa ametumia pesa za umma vibaya.
Madai hayo yalitolewa juzi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa vyama vya upinzani uliofanyika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, kulaani mpango wa ununuzi wa rada unaodaiwa kugubikwa na rushwa.
Kabwe alisema tayari Mtanzania huyo mwenye asili ya kiasia amekwishaweka kibindoni kiasi cha sh bilioni 83, fedha za wafanyakazi wanazokatwa kuchangia mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii.
Ndani ya mwaka mmoja, kuna skendo ya ubadhirifu wa sh bilioni 83 katika Serikali ya Rais Kikwete na ameshindwa kutoa maelezo kuhusu skendo hiyo
hili linatia shaka.
Mwaka jana serikali ilikwenda kuomba msaada wa fedha za kufanikisha bajeti yake katika Jumuiya ya Ulaya (EU), ikapewa sh bilioni 80, wakati kuna Muasia amechukua sh bilioni 83 za Watanzania, amekaa nazo, lakini serikali haina pesa, inalazimika kwenda kuomba kwa wafadhili, hii ni akili gani? alihoji Kabwe.
Alisema kashfa ya kuliwa kwa fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii, ilianza mwaka 2004, ambako Tanzania ilianza kukithiri kwa matumuzi mabaya ya fedha za wananchi, huku wahusika wa kashfa wakionekana kuwa na kinga maalumu kutoka kwa wakubwa, ya kutokamatwa au kuchunguzwa na taasisi yoyote ya serikali.
Akizungumzia jinsi pesa hizo zilivyochukuliwa, Kabwe alisema, Februari 2004, Muasia huyo alikopa sh bilioni sita kwa ajili ya kununua maghala yaliyokuwa yakimilikiwa na NSSF.
Alisema, siku chache baada ya kununua maghala hayo, aliyauza tena kwa NSSF kwa gharama ya sh bilioni 47, jambo ambalo linatia shaka kuwa, huo ni mpango uliopagwa kwa ajili ya kuihujumu NSSF pamoja na wanachama wake.
Aidha, hakuna Mtanzania anayejua kama hizo bilioni 47, bado ziko nchini au zimekwishahamishiwa nje ya nchi. Serikali inalijua jambo hili vizuri, lakini imekaa kimya, hata rais hathubutu kuhoji, inashangaza, alisema Kabwe.
Alisema, muda mfupi baadaye, Muasia huyo alikwenda PSPF na kudai kuwa ana jengo la ghorofa mbili analiuza na kwamba ndani ya muda wa wiki moja, bodi ya PSPF ilikaa na kukubali kulinunua jengo hilo.
Kabwe alisema, anazo taarifa kuwa bodi ya PSPF ilikubali kununua kampuni nzima ya Quality Plaza badala ya jengo la ghorofa mbili na siku kumi kabla ya kununuliwa kwa kampuni hiyo, thamani yake ilipanda kwa sh bilioni sita zaidi.
Sijui wajumbe wa bodi ya PSPF walitumia vigezo gani kukubali kununua kampuni nzima bila kufanya tathmini na kubaini ilikuwa na madeni kiasi gani, pamoja na mambo mengine ya msingi kabla ya kuinunua kampuni kama hiyo, alisema Kabwe.
Alisema baada ya kugundua kashfa hiyo, wabunge walijaribu kuhoji ndani ya bunge jinsi fedha za mifuko hiyo zinavyoishia kwa Muasia huyo, lakini Spika wa Bunge aliupiga stop mjadala huo, kwa maelezo kuwa suala hilo liko mahakamani.
Tulipogundua kashfa hiyo, tulihoji ndani ya bunge kulikoni, ajabu, tukapigwa zengwe, tukaambiwa kesi iko mahakamani. Tulipofuatilia tukagundua kesi iliyoko mahakamani ni ya kuvunjiana heshima baina ya wafanyabiashara wawili.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour, Augustine Mrema, alisema anamuonea huruma Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo kwa kuibua kashfa ya rushwa ambayo inawagusa viongozi wakuu wa serikali.
Mrema alisema ingawa Ndesamburo ameonyesha ujasiri wa hali ya juu, lakini anamuonea huruma, kwa sababu ana hakika atakiona cha mtema kuni kwa kuwatuhumu wabunge wenzake kuwa, wamehongwa ili wapindishe ukweli katika kesi inawayowakabili Adamu Malima na Reginald Mengi.
Ninamuonea huruma Ndesamburo, ingawa amepasua ukweli kuwa ziwa la mama linanyonywa na mtoto wa kambo, lakini nina hakika atakiona cha mtema kuni!... nchi inateketea hii
inakwisha, na mimi nitaendelea kulia na CCM, alisema Mrema.