Mambo yalizidi kuwa magumu mule ndani....Naam... hali ilikuwa ya taharuki. Katika kile chumba cha jikoni, Tjedi aliendelea kutega sikio, jicho lake likiwa limekodoa kwenye mlango mdogo wa kuingilia jikoni.
--London, Miaka 25 Nyuma---
Gari la Bwana Aesh lilikuwa likisafiri kwa kasi barabarani za jiji la London, likielekea hospitali. Bi. Nadira alikuwa katika maumivu makali ya kujifungua pia akiwa ameshikwa na wasiwasi.
"Tunafika hivi karibuni, mpenzi kuwa na imani" alimtuliza Bwana Aesh huku dereva wake akiendelea kusonga mbele kwa kasi ya ajabu
Ghafla watu wawili wakiwa kwenye pikipiki wakawapita kwa kasi na kuachia risasi tatu ambazo zilipenya kwenye kioo cha gari, moja kati ya hizo ikimgonga Bi. Nadira kifuani!
"NADIRA! HAPANA!" Bwana Aesh alipiga kelele kwa mshangao na huzuni. Damu ilimwagika kwa kasi ndani ya gari.
Dereva alizungusha usukani kupiga msele na kubadili mwelekeo na kuanza kukimbizaa gari kwa kasi zaidi kuelekea hospitali ya karibu.
"Endelea kuwa nami mpenzi! Usiniache" Bwana Aesh alimwambia mke wake huku akiwa ameziba jeraha la risasi kwa mkono wakati damu ikiendelea kuvuja kwa kasi
Walipofika hospitalini, wakunga walimchukua Bi. Nadira kwa haraka na kumpeleka kwenye chumba cha dharura.
"Mtoto anahitaji kutolewa sasa hivi, vinginevyo wote wawili watakufa!" daktari alisema kwa msisitizo.
Bwana Aesh alikuwa amesimama nje ya chumba hicho akiomba Mungu amwokoe mke wake na mtoto wake.
Baada ya Masaa kadhaa daktari alitoka huku uso wake ukionekana na huzuni.
"Samahani, Bwana Aesh... tumefanya kila tunachoweza, Bi. Nadira amepoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi. Lakini mtoto wako ni mzima, na ni msichana."
Bwana Aesh alimuangalia mtoto wake mchanga, akamwita 'Zara', jina alilopendekeza mke wake kabla hajafa.
Wote wanaliohusika na tukio hili watalipa!" alipaza sauti huku akikandamiza meno yake kwa hasira kali. Alijua kuwa ana maadui wengi wa biashara lakini hakujua ni nani alikuwa nyuma ya shambulizi illo na alijitoa moyo kwamba anafahamu tu.
-----
Mbweni, dar es salaam
Ghafla, mlango wa jikoni ulianza kufunguliwa taratibu. Tjedi alinyanyuka kimya kama kivuli na kushika kisu kilichokuwa mezani. Emmy na Zara walijificha nyuma ya kabati kubwa la chuma lililokuwa pembeni, wakitetemeka kwa hofu.
Mlango ulipofunguka kidogo, kivuli cha mguu kilionekana. Kabla jambazi hajaingiza mwili wote ndani, Tjedi alimrukia kwa kasi na kumchoma kisu kwenye koromeo
Pah! Pah!
Yule jambazi aliachia risasi mbili zilizomkosa kosa Tjedi na kupiga ukutani huku damu zikitoka kwa kasi kwenye koromeo lake akajikuta akiishiwa nguvu, na kudondosha bunduki huku mwili wake ukianguka kwa kishindo kwenye sakafu
"Wapo huku chini!" Mmoja wa majambazi alipiga kelele baada ya kusikia milio ya risasi.
"Haraka, inabidi tuondoke hapa", Tjedi alisema kwa sauti ya haraka lakini tulivu. "Kuna mlango wa dharura unaotokea kwenye njia ya chini ya ardhi. Njooni!"
Wakiwa na hofu na mioyo ikidunda kwa kasi, Zara na Emmy walimfuata Tjedi kwa haraka kupitia korido ya siri iliyo nyuma ya friji kubwa la jikoni. Njia hiyo Ilijengwa na bwana Aesh kwaajili ya dharura kama hizi, lakini haijawahi kutumika, hadi leo.
Walitembea kwa haraka kwenye njia hiyo hadi walipofika kwenye mlango mwingine wa chuma. Tjedi alitoa funguo kwenye shingo yake, akauufungua. Mlango ulifunguka kuelekea kwenye msitu mdogo nyuma ya nyumba.
"Hatuwezi kutumia gari. Tutasonga kwa miguu hadi tutakapoona usalama. Tutampigia Bwana Aesh baadaye, Zara" Tjedi alisema.
Zara aliangalia nyuma, machozi yakimtoka. “Wameua mtu nyumbani kwetu... Kwa ajili yangu.”
Tjedi alimwekea mkono begani. “Tutalipa kisasi Lakini kwanza ni lazima tuishi”
....Zara, Tjedi na Emmy walizidi kusonga mbele gizani, huku wakisindikizwa na sauti za vyura waliokuwa wanashindana kukoroma ndani ya kibwawa kidogo kilichokuwa pembeni ya kinjia walichopita.
"Jamani, mimi mpaka hapa nimechoka mpigie baba simu ili alete gari linibebe....miguu inauma" Zara aliwaambia Tjedi na Emmy.
"Jikaze, kuna kinjia cha vumbi kiko pale mbele, nadhani tukikaribia pale tunaweza kupata msaada, ila kupiga simu haitawezekana maana huenda bado tunafuatiliwa na hao watu nyuma, kuwasha simu ni hatari kwani wataona mwanga...." Tjedi aliongeza.
Walizidi kusonga mbele huku wakikatiza ndani ya vichaka, maana kwa wakati ule maeneo ya Mbweni yalikuwa bado hayajajengeka kama wakati huu.
"Tjedi nakufaaaaa..." Emmy alipiga kelele baada ya mguu wake kunasa ndani ya kifungu cha miba.
"Mungu wangu, hivi hio kelele uliyopiga hatujasikika kweli?" Zara alisema kwa jazba kidogo.
Mguu wa Emmy ulikuwa umeingia ndani ya kifungu cha miti ya miiba na kunasa, na alipojaribu kuuchomoa mguu, akajikuta anapiga ukelele wa maumivu.
Ilibidi Tjedi aanze kumtoa miba taratibu huku Zara kamziba mdomo ili asiendelee kupiga kelele za maumivu.
Hakika Tjedi alikuwa na kibarua kizito usiku huo.
Walifanikiwa kumtoa Emmy miiba na safari ikaendelea mpaka wakajikuta wanatokea sehemu moja inaitwa Boko Magengeni.
Walikuta wauza chips, bodaboda na mama ntilie wakimalizia malizia kufunga biashara zao.
Walikuwa wamechafuka miili yao, wako peku huku Emmy na Zara wakiwa wamechoka sana.
"Braza, vipi boda?" dereva mmoja wa bodaboda aliwauliza.
"Hapana, tunaenda hapo mbele mara moja..."
Tjedi alimjibu yule bodaboda.
Walizidi kusonga mbele bila kujua wanaelekea wapi,
Ghafla mbele yao ilipaki gari ndogo nyeupe aina ya Crown
Kioo kikashushwa na mdada wa makamo aliwauliza...."...usiku huu mnaelekea wapi maana kwa sasa daladala hakuna"
"Tunaelekea maeneo ya mjini, Masaki jirani na Club AB....unaweza kutupeleka?" Tjedi alimuuliza yule dada wa makamo.
"Hakuna tabu, ingieni maana mimi naelekea Magomeni maeneo ya Flomi bar, nitawapitisha..."
Zara, Tjedi na Emmy waliingia kwenye gari na safari ikaanza taratibu.
Moyoni Emmy alikuwa anawaza vingi...."
laiti nisingekuwa muhudumu wa basi siku hiyo huenda nisingeonana na Tjedi na haya yote yasingetokea...au Majaliwa asingeshukia Mlandizi huenda ningekuwa salama mpaka leo...."
Walikaribia Club AB huku wote wakiwa kimya, ghafla yule dada aliyewapa lifti akavunja ukimya na kusema..."laiti marehemu baba asingedhulumiwa hili jengo, na mimi leo ningekuwa nakula matunda ya baba yangu..." akaanza kulia kwa sauti ya chini.
"Samahani dada, mbona umeongea hayo maneno?" Tjedi aliuliza.
"We acha tu kaka, dunia ina mengi sana, mmiliki wa hili jengo alimdhulumu baba yangu hili eneo na kujipa umiliki wake, na baada ya siku 5 baba yangu aliokotwa ufukweni mwa bahari ya Hindi akiwa ameuawa...."
"Nina kisasi mpaka leo na huyu mwenye eneo na nitakuja kulipa kisasi hata kwa watoto wake.....shukeni nadhani mmeshafika"
Wakati huo wote Zara alikuwa kimya maana lugha ya kiswahili kwake kidogo ilimpiga chenga.
Emmy na Tjedi walitazamana kisha wakaunga matukio yote tangu mwanzo hadi kufikia hapa, wakajisemea moyoni..."
kazi ipo"
Walifungua mlango wa gari na kushuka kisha walizunguka nyuma ya Club AB ili watokezee kwenye vyoo vilivyopo nyuma ya Club hiyo.
Upande wa vyoo vya nyuma walikutana na wahudumu waliokuwa wanasafisha vyoo, walipomuona Tjedi na wale wadada, kwanza walishtuka kisha wakawauliza mbona mmechafuka hivyo?
"Tjedi leo naona umekumbuka kazi yako ya zamani ya ubaunsa, umekuja kutulinda....na mbona mmechafuka hivi?"
"Heee! Mbona mikononi una damu?" Aliuliza mfanya usafi mmoja
"Kaniitie Mukheef, au alishaacha kazi hapa?"
Aliongea Tjedi huku akielekea kwenye sinki la kunawia mikono lililoko karibu na vyoo vya kiume.
"Hapana, yuko kazini bado na sasa amekuwa meneja wa Club....tupeni na sisi dawa mnazotumia ili nasi tupandishwe vyeo..." aliongea yule mfanya usafi wa kike
"Hakuna cha dawa wala nini, ni utendaji wa kazi mzuri tu ndio maana vyeo vinapanda, ....au acha nikamfuate mwenyewe ndani"
Aliongeza Tjedi huku akipiga hatua kuingia ndani ya Club kupitia mlango wa nyuma.
Baada ya maongezi yale mafupi, Emmy na Zara walielekea maliwatoni ili kujisafisha na Tjedi alimfuata meneja Mukheef ili aweze kuwasiliana na Bw. Aesh ili kumsimulia mkasa mzima....
Lakini wakati Emmy na Zara wanatoka maliwatoni, ghafla walishangaa kuiona ile gari iliyowapa lifti ile Crown nyeupe ikiwa imeegeshwa nyuma ya vyoo vya Club ile na yule mdada akiwa nje ya gari lake akivuta sigara.
Wakahisi kuna jambo, kwani yule dada alisema anaelekea Magomeni Flomi bar, lakini hapa sasa anafanya nini?
Na kwa wakati huu muziki ndani ya Club ulikuwa umepamba moto kwani kama unavyojua siku za Jumamosi watu wengi hupendelea kwenda sehemu za starehe ili kupata burudani na kupunguza mawazo kidogo.
Emmy na Zara wakaingia kwa kasi ndani ya Club kumfuata Tjedi.....