Walijikuta wameamka saa tano asubuhi,huku wakiwa na uchovu wa mwili kutokana na "shughuli pevu" waliyoshughulika nayo usiku kucha. Usingizi ulijua mtamu, lakini bado walijua kuwa siku mpya ilikuwa inawangojea na walihitaji kujiandaa. Emmy aliketi kitandani akimwangalia Haduri kwa macho ya shauku, akimwambia, "Leo tutaanza rasmi, nakuahidi nitafanya kila liwezekanalo kukusaidia kupata kazi." Haduri alitabasamu kwa kutambua kuwa alikuwa na mtu wa kumsaidia katika safari yake ya mabadiliko. Walijua kuwa safari hiyo ilikuwa ngumu, lakini walikuwa tayari kushirikiana na kupambana kwa pamoja ili kufikia malengo yao. Baada ya kutimiza majukumu ya asubuhi, walijipanga na kuondoka kwenda kwa rafiki wa Emmy ili kuanza mchakato wa kumtafutia Haduri kibarua.
...na breki ya kwanza ilikuwa ni Magomeni kwa fundi ujenzi aitwaje Abdalla, huyu alikuwa ni rafiki wa kaka ake Emmy.
Abdalla alisema vibarua wamejaa ila nafasi itakapopatikana basi atapigiwa simu kujulishwa.
Wakaelekea mpaka mitaa ya Magomeni Kagera pale kuna ofisi ya kukatisha tiketi za mabasi na Emmy akamwambia Hedaru kuwa hii kazi haitakufaa....kumbe Emmy aliona wivu asije akanyang'anywa Haduri wake na abiria.
Basi walizunguka siku nzima, huku Emmy akimtia moyo Haduri kuwa kazi zipo ni kupambana tu.
Na ilipofika jioni walirudi nyumbani kuendelea na ratiba zao huku Emmy akimueleza kuwa kesho ni siku ya kuhudumu ndani ya basi, hivyo itabidi akamkodie gesti kwa maana kuonana siku moja tu si kigezo cha kumuamini kiasi cha kumuachia chumba chake abaki nacho.
Haduri alijiapiza kuwa yeye si mwizi wala kibaka kwanini hamuamini
"Wazazi wangu wamenilea vyema, na sikuwahi kuiba na wala sina hiyo tabia..., hiyo pesa ya kunilipia gesti siku mbili kwanini tusifanye ya kula? Huoni kama unachezea pesa?"
Haduri alimuuliza Emmy
"Sawa, nakuamini, ila itabidi kesho nikitoka nawe utoke ukatafute kazi, omba kazi kama mwanaume, usichague kazi...nakuombea kila la kheri ufanikiwe...nakupenda"
Emmy alimjibu Haduri huku akitabasamu na kumkumbatia.
Hakika penzi lao lilichipua ghafla mithili ya tawi jipya la mgomba.
Emmy, binti wa miaka 23 aliyechanganywa kimapenzi vilivyo na Haduri, kijana shababi wa miaka 30.
Hakika ungethubutu kuwaona kwa siku hiyo ungedhani labda penzi lao lina miaka 5 au 8...kumbe ndio kwanza wana siku 2 tu tangu waonane na kujuana.
Kweli mapenzi upofu....