SoC02 Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, chanzo cha maovu na kupoteza uelekeo kwa vijana

Stories of Change - 2022 Competition

Tino Pissy

New Member
Sep 14, 2022
1
0
Habari ndugu mwana Jamii Forum, haswa wa Jukwaa la ‘Stories of Change’ ni matumaini yangu u mzima wa afya, karibu katika chapisho hili. Andiko hili litajikita katika kuelezea jinsi gani matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yameweza kuleta athari pamoja na matokeo hasi katika jamii zetu, bila kusahau nini kifanyike ili kuweza kunusuru kizazi hiki kisiangamie na tuweze kujenga taifa lenye tija na maendeleo bora.

Mitandao ya kijamii ni wavuti ama huduma za mawasiliano kupitia mitandao ambapo watu huwasiliana ama kujumuishwa pamoja na watu wengine, mijumuiko hii inaweza kuwa ndani ya nchi au mahali pengine popote ulimwenguni. Huduma hizi za mitandao ya kijamii kutokana na kukua kwa utandawazi, imeweza kuleta na kuunganisha Pamoja watu mbalimbali wenye fikra tofauti ulimwenguni kote, mfano wa mitandao hiyo ya kijamii ni kama vile whatsapp, facebook, Instagram, twitter pamoja mitandao mingineyo mingi.

Maendeleo ya teknolojia Habari na mawasiliano, yamekuwa na mchango mkubwa sana katika huduma hii kuwafikia vijana wengi. Uwepo wa vifaa kama simu janja,kompyuta mpakato,vishkwambi pamoja na intaneti imeifanya mitandao ya kijamii iweze kuwafikia vijana wengi zaidi ulimwenguni kote na maendeleo hayo yameleta athari kubwa sana na kuacha alama kwa watumiaji wa mitandao hiyo ambapo wengi wao ni vijana. Sehemu kubwa ya mitandao hii inawapa vijana fursa ya kutengeneza machapisho katika kurasa zao pamoja na kusambaza mawazo, picha ama maudhui mbalimbali, ambapo pia vijana wengi sana wameishia kujifunza na kuiga tamaduni nyingi za kigeni ambazo hazina tija wala msaada wowote katika maendeleo ya jamii zetu.


Athari na matokeo ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kama vile:

Kumomonyoka kwa misingi bora ya maadili na utu wema kwa vijana;
vijana wengi ambao hutumia mitandao ya kijamii vibaya huishia kujifunza mitindo mipya ya maisha, mfano kuiga mavazi yasio na heshima kwa jinsia zote mbili hasa jinsia ya kike, ambayo vijana wanaweza kujifunza na kuyaona kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao hiyo ya kijamii, matokeo yake hupelekea vijana wengi kuingia kwenye wimbi kubwa la kuuza miili yao(ushoga na ukahaba).

Athari nyingine ni picha za ngono na usambazaji wa picha za utupu; vijana wengi hasa wa jinsia ya kiume hupata madhara makubwa kisaikolojia na kiafya ambayo ni matokeo ya kuangalia machapisho yasiofaa,picha za utupu ama video za ngono ambazo hupatikana katika mitandao ya kijamii pamoja na tovuti mbalimbali katika intaneti, hapa kijana hujifunza mambo mengi sana yasiomsaidia chochote na baada ya kuzitazama chapisho hizo vijana huishia kufanya ngono zembe, na vitendo vingine kama kujichua maumbile yao ya uzazi ili kuridhisha mihemuko walioipata kutokana na kutazama machapisho hayo.

Kuongezeka kwa wizi na utapeli kupitia mtandaoni. Mitandao ya kijamii imechangia sana uhalifu wa kimtandao kuongezeka kutokana na vijana wengi kupata ujuzi huo na kuutumia vibaya ujuzi huo katika kujinufaisha wenyewe na si kunufaisha jamii zinazowazunguka.

Kuzalisha ajira zisizo rasmi mfano ‘uchawa’, udangaji nk.
Kumekuwa na wimbi kubwa sana la vijana kuwa na ajira zisizo rasmi kama vile uchawa, ambapo vijana huwa na kazi ya kuwasifia na kuwatukuza vijana wenzao ama watu mbalimbali ambao ni maarufu, wana nyadhifa mbalimbali za uongozi ama wana uwezo mkubwa wa kifedha kuzidi wao kwa matarajio ya kupata malipo ama umaarufu fulani ambapo hupelekea ndoto nyingi na ubunifu wa vijana hao kupotea, pia vijana wa kike kudanga kumekuwa ni kama ajira japo isiyo rasmi, yaani ni kawaida leo kumkuta binti mdogo akiwa na mahusiano kimapenzi na mtu mwenye umri sawa ama zaidi ya mzazi wake kwa lengo tu la kujipatia kipato, tena waweza kukuta ni mzee mwenye mke na watoto wenye umri kama wake. Hali hii huchangia sana ongezeko la magonjwa hatarishi katika jamii kama vile UKIMWI hivyo kupoteza vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Suluhisho na Mapendekezo
Kutokana na matokeo hayo ya matumizi mabaya ya mitandao, yafuatayo yanaweza kufanyika ili kupunguza ama kumaliza kabisa athari hizo.

Kwanza kabisa ni kwa vijana wenyewe ambao ndio watumiaji na wadau wakubwa wa mitandao ya kijamii kuchagua maudhui yanayofaa katika kujifunza na kusambaza machapisho yanayo elimisha ili vijana wengine waweze kupata elimu ya vitu mbalimbali, hii itasaidia kuongeza ubunifu kwa vijana na kuwawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii zetu mfano changamoto ya ukosefu wa ajira n.k.

Pili ni kwa mamlaka husika, hapa naongelea mamlaka zote kama vile TCRA, Pamoja na mihimili mingine ya serikali, kutunga sheria na kanuni mbalimbali zitakazo waongoza na kuwalinda watumiaji wa mitandao hiyo ya kijamii kutokufanya uhalifu ama kutodhurika na wahalifu hao wanaoitumia mitandao hiyo vibaya pia POLISI TANZANIA kusimamia vema utekelezaji wa sheria na kanuni hizo.

Tatu na mwisho ni serikali kupitia wizara zake kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa pamoja kutoa elimu juu ya jinsi gani matumizi haya mabaya yanaweza kuliangamiza taifa la vijana pia ni nini faida kwa kijana, jamii na taifa kwa ujumla endapo kila kijana akaweza kutumia mitandao ya kijamii kwa kujiendeleza na kupata maendeleo.

Kwa kuhitimisha ningependa kuwaasa vijana pamoja na watumiaji wote wa mitandao ya kijamii na intaneti kutumia vizuri mitandao hiyo kwani kuna faida kubwa sana, kwani ubunifu mkubwa unaofanywa na vijana katika kurahisisha na kutatua changamoto mbalimbali umeweza kufanyika na kuleta matokeo chanya. Mfano wa vijana kama Benjamin Fernandes, mtanzania alieweza kubuni njia ya kutuma na kupokea pesa moja kwa moja kutoka Uingereza nk. ni mfano halisi kwamba vijana tunaweza kufanya chochote na kitaleta matokeo chanya katika jamii yetu.
 
Back
Top Bottom