Dodoma
HALI si shwari mjini Dodoma, wabunge sasa wanaonekana kuogopa kuusogelea ukumbi wa Bunge, baada ya kupatikana taarifa za mmoja wa wabunge kuingia ndani ya ukumbi huo na kufanya vitendo vya kishirikina.
Wabunge kadhaa waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili juzi na jana, walieleza wasiwasi wao kuhusu suala hilo na kudai kuwa iwapo hatua za haraka kudhibiti vitendo vya aina hiyo hazitachukuliwa, uwezekano wa kuwapo mahudhurio hafifu ya wabunge katika vikao vinavyofuata ni mkubwa.
Hili tukio limetutia hofu, tunadhani kuna kila sababu ya kukamilisha uchunguzi wa tukio hili mapema. Spika ameeleza kuwa tukio hili linachunguzwa, tunaomba lichunguzwe kweli, tena kwa haraka, ili kutuondolea hofu tuliyonayo sasa, alisema mmoja wa wabunge kutoka Mkoa wa Mwanza.
Mbunge mwingine ambaye pia hakutaka kutaja jina lake liandikwe gazetini, alilieleza gazeti hili kuwa Spika anapaswa kutoa taarifa ya tukio hili bungeni na kulitolea ufafanuzi badala ya kuendelea kulizungumza kwenye vyombo vya habari.
Hizi taarifa zipo, wabunge wengi wanazijua, lakini Spika analizungumzia kwenye vyombo vya habari. Mimi nadhani suala hili linagusa maisha yetu, ni bora akalieleza Bunge nini kilitokea, alisema mbunge huyo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ofisi yake imekabidhi picha za video zilizomnasa mbunge huyo akiwa ameambatana na Ofisa Mwandamizi wa Bunge kwa siri, waliokuwa wakiweka vitu vinavyoaminika kuwa vya kishirikina au aina fulani ya sumu kwenye kila kiti cha mbunge.
Sitta alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo ambalo hivi sasa limewachanganya baadhi ya wabunge kiasi cha kuhofia kuingia na kukalia viti vyao ndani ya ukumbi wa Bunge kabla ya uchunguzi kubaini kitu kilichowekwa.
Kwa mujibu wa Sitta, picha za mkanda huo zilizonaswa na kamera za usalama zilizomo ndani ya jengo hilo la kisasa, zimefifia kiasi cha kushindwa kubaini kwa haraka watu wanaoonekana ndani ya mkanda huo.
Kutokana na hali hiyo, Sitta alisema ofisi yake imeamua kuukabidhi mkanda wa picha hizo kwa maofisa usalama wa taifa na kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi zaidi.
Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa 12 wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, mbunge mmoja akiandamana na Ofisa Mwandamizi wa Bunge (jina limehifadhiwa kwa sasa), wanadaiwa kuingia ndani ya Bunge na kupita kwenye kila kiti cha mbunge, huku wakinyunyizia vitu vinavyoaminika kuwa sumu au aina fulani ya dawa za kishirikina, kwa sababu ambazo hadi sasa hazijaeleweka.
Baadhi ya wabunge na vyanzo vyetu vya habari, vilisema kuwa mbunge anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo la aina yake ni mmoja kati ya mawaziri waliojiuzulu nyadhifa zao kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi. Jina la mbunge huyo kwa sasa pia linahifadhiwa.
Hata hivyo mawaziri waliojiuzulu hivi karibuni kutokana na tuhuma za ufisadi ni pamoja na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha (wote walikuwa Nishati na Madini) na Andrew Chenge (Miundombinu).
Akizungumzia tukio la kuugua ghafla kwa Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, Sitta alisema taarifa ya daktari aliyemtibu Dk. Mwakyembe imeonyesha kuwa halina uhusiano na aina hiyo ya dawa inayodaiwa kuwekwa ndani ya viti vya wabunge.
Alisema Dk. Mwakyembe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza mkataba tata wa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, aliugua ghafla bungeni kutokana na sababu za kawaida na si vinginevyo.
Wakati Spika akitoa ufafanuzi wa tukio hilo, baadhi ya wabunge wamekuwa katika mjadala huku wakiwa na hofu ya kuendelea kukalia viti vyao bungeni, kwa hofu ya kudhurika kwa sumu au dawa hiyo inayodaiwa kuwa ya kishirikina.
Hata hivyo wapo baadhi ya wabunge wanaopuuza tukio hilo, kwa madai kuwa hakuna suala la ushirikina linaloweza kumdhuru mtu katika karne hii.
Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana ilikuwa na semina iliyokuwa na lengo la kujadili hali ya uchumi, hususan mfumuko wa bei na jinsi ya kurekebisha hali hiyo.
Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM, Kapteni John Chiligati, alisema semina hiyo ambayo itaendelea leo, ilikuwa na ajenda kubwa juu ya hali ya uchumi, ambapo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Beno Ndullu, alitoa mada ndefu juu ya hali ya uchumi nchini.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vya habari ndani ya semina hiyo, vilidai kuwa NEC pia ilijadili suala la ufisadi na hatua zinazochukuliwa kwa mafisadi, ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa sababu ya kudidimiza hali ya uchumi nchini.
Hata hivyo, Chiligati aliahidi kutoa taarifa kamili leo baada ya kumalizika kwa semina hiyo inayoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete