Imetolewa mara ya mwisho: 15.06.2008 1320 EAT
•
Wabunge 'kususa' kikao cha bajeti kesho, Wahofia yaliyomsibu Dkt. Mwakyembe
sogeza Habari Zinazoshabihiana
• Demokrasia ndani ya Bunge kujadiliwa 13.06.2006 [Soma]
• Lowassa aokoa jahazi matumizi ya dola 11.08.2007 [Soma]
• Mbunge avunjika mguu akishuka kwenye lifti 28.03.2008 [Soma]
Na John Daniel, Dodoma
SIKU chache baada ya kugundulika kwa njama za kuwadhuru Mbunge wa Kyela Dkt. Herrison Mwakyembe, Spika wa Bunge Bw. Samwel Sitta, Naibu wake Bi. Anna Makinda, Mbunge wa Same Bi. Anna Kilango na baadhi ya Wabunge sasa hofu imetanda miongoni mwao na kutaka kufanyika kwa uchuguzi wa kina kwenye viti vyote na maeneo mbalimbali ya ukumbi wa Bunge, kabla ya kuendelea kutumia ukumbi huo kesho.
Sambamba na hilo, Taarifa zilizolifikia Majira Jumapili jana jioni zilisema watuhumiwa wanaodaiwa kutaka kuwadhuru Wabunge wameanza mkakati mahususi kuhakikisha kwamba ushihidi kuhusu uchunguzi wa kuwanasa unakwama kwa lengo la kumzushia Bw. Sitta na vyombo vya habari kwa kusema uwongo.
Taarifa hizo pia zilieleza kwamba tayari maofisa wa usalama na wataalamu wa kuchunguza aina mbalimbali za sumu waliwasili mjini hapa na kufanmya ukaguzi wa kutosha katika ukumbi huo usiku wa kuamkia jana ili kuhakikisha kwamba shughuli za Bunge zinaendelea kesho kama kawaida.
Wakizungumza na Majira Jumapili kwa nyakati tofauti mjini hapa jana, Wabunge hao walielezea kutokuwa na imani na usalama wa ukumbi huo na kudai kwamba huenda mtuhumiwa aliyeweka 'uganga' huo alichanganya na sumu maalum ya kuangamiza watu taratibu.
"Mimi binafsi nilikwenda kukaa karibu na Mhe. Mwakyembe siku alipopata matatizo ya kiafya na nilipotoka hapo niliharisha usiku kucha," alisema Mbunge mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
"Sikulala ingawa sasa najisikia vizuri lakini sina hakika kama niko kawaida, nina shaka na ule ukumbi na hata kama nitaenda bungeni, nitabadilisha kiti," alisema Mbunge huyo.
Mbunge mwingine ambaye pia hakutaka kutajwa jina gazetini alisema atamuomba Spika kusitisha kwa muda vikao Bunge Jumatatu kama wataalamu wa sumu hawatafanya uchunguzi wa kina kwenye viti.
Habari kutoka katika vyanzo vyetu zilieleza kwamba watuhumiwa hao wameanza mkakati wa kupoteza ushidi kwa kushirikiana na baadhi wachunguzi wa suala hilo.
"Mmoja wa Ofisa ambaye anatoka katika chombo nyeti ameanza kutaka kumsaidia mtuhumiwa yule kwa kutuambia kwamba hakuna kitu kama hicho, sasa sisi tunajiuliza yeye amepewa jukumu la kuchunguza suala hili sasa inakuaje anatangaza kwamba si kweli wakati uchunguzi haujakamilika?,"alihoji mmoja wa Wabunge.
Akizungumza na Majira kwa nijia ya simu Kaimu Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila alisema hana taarifa hizo na kwamba anachojua ni kwamba taratibu zote za Bunge zitaendelea kama kawaida.
Alipouliozwa kuhusu taarifa za ukumbi wa Bunge kufanyiwa uchunguzi wa kina juzi usiku na wataalam wa kuchunguza sumu waliokuwa na vifaa vya aina mbalimbali alisema hilo ni suala la kiusalama na si la umma hivyo hawezi kulizungumza.
"Nani amekwambia habari hizo, huenda yeye anayajua zaidi, hilo ni suala la kiusalama si Public, siwezi kulizungumza,"alisema Dkt. Kashilila.
Hata hivyo habari zaidi zilieleza kwamba ukaguzi huo wa kitaalaamu umefanywa hadi kwenye mavazi ya Spika na Naibu wake ili kuhakikisha kwamba havina madhara yoyote.
Habari hizo zilieleza kwamba kutokana na hali hiyo kutakwepo na mabadiliko makubwa ya ukaguzi na udhibiti wa usalama Bungeni kuhakikisha kwamba vitendo vyovyote vinavyoweza kuleta hofu ndani ya ukumbi huo havitokei tena.
Source: Majira Jumapili 15 June 2008