Duh! kwa hiyo ndo siolewi tena hivyo. Huyu Mungu nae kwa nini anidanganye? Najua hakuna dhambi isiyo na consequences lakini rehema zake ni za milele. Mi keshaniambia " hata sasa nirudie kwa moyo wako wote kwa kufunga, kulia na kuomboleza. Rarua moyo wako na si mavazi yako. Rudi kwa Bwana Mungu wako kwa kuwa ana neema na huruma, si mwepezi kukasirika na mwingi wa upendo......................... Nitafidia miaka yako iliyoliwa na nzige (nzige wakuu na nzige wadogo na nzige wengine na jeshi la nzige ambalo nililituma miongoni mwenu.............. (hii ni tafsiri yangu toka Joel 2: 12, 13..25 NIV).
Halafu hata katika kuwa na VVU na kuwa na m/watoto bado kuna kitu kikubwa kinatendeka katika maisha ya mhusika kama atachukulia kuwa hakuna dhambi isiyo na matokeo, na adhabu au majaribu ni sehemu ya kuadabishwa na kujengwa ili kuendea utu wema zaidi. Kuna watu tunawafahamu kabla ya kupata VVU walikuwa watu wa hovyo nikimaanisha waliishi maisha yasiyo na malengo. Baadhi yao walikuwa wana-anasa, kero kwao wenyewe, kwa familia na taifa lakii baada ya kukwaa VVU wakatulia chini wakatafakari upya maisha na kupatana na Mungu. Baada ya hapo wakaanza kufanya mambo ya maana ikiwemo kuwafariji wenzao wenye VVU waliokata tamaa, kuwasiadia wenye maisha duni, kupenda familia zao n.k. Kuna silver line kwenye kila wingu zito. Kila kitu ni namna unavyokiangalia.
Kwa hiyo niwatie moyo wadada na wakaka wote mnaopitia mambo magumu kwa sababu ya matendo yenu ya nyuma kuwa mpatane na nafsi zenu na Mungu wenu. Mkifanya hivyo mtapita kwa wepesi kwenye lolote mnalopitia. Maoni ya wengine hayana umuhimu kwenu kwani nao ni wadhaifu kama nyie na wana matatizo pia kwa kuwa ni wanadamu na pengine makubwa kuliko yenu ila kwa kuwa wanaogopa kuyakabili basi hutafuta mahali pa kupeleka maumivu yao. Kila mwanadamu yuko kwenye nafasi sawa ya kuanguka. Ndo maana tunaambiwa tusijiapize wala kuhukumu kwa sababu kuhukumu kunatukosesha fursa ya kujitathmini sisi wenyewe.
Mwisho, unapoamua kumhusisha Mungu (wa Israel) unatakiwa ujue kwa Mungu neema (grace) ndo inafanya kazi na si ukamilifu wetu. Ndo maana kuna mabikira hawajaoa wala kuolewa japo wanataka, kuna malaya wameoa na kuolewa, kuna wenye watoto wameolewa wengine hapana, kuna wasio na watoto lakini hola, yaani kuna watu wana vigezo vyote vya kupata vitu fulani na hawajapata lakini wasio na vigezo wamepata. Mwanadamu yeyote anayeamua kuamini mambo ya Mungu hatakiwi kusononeka akikosa kitu. Kazi yake ni kumcha Mungu tu. Kumcha Mungu ni pamoja na kushukuru kwa kila jambo.