Date::8/4/2008
Babake mzazi wa Mallya azidi kuchanganya mambo
Francis Matey Mallya, baba mzazi wa Deus Mallya akiwa katika ofisi za Mwananchi, mjini Moshi kumtetea mwanae jana.
Na Daniel Mjema, Moshi
BABA mzazi wa kijana aliyekuwa na Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe (Chadema) kwenye gari lililosababisha kifo chake, amezidi kuchanganya mambo baada ya kueleza kwamba, mwanaye hakuwahi kusoma sekondari Nairobi, nchini Kenya, kama mwanaye huyo alivyodai.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili mjini hapa jana, Francis Matey Mallya, ambaye ni baba mzazi wa Deus Mallya, alisema mwanaye hakuwahi kabisa kujiunga na shule yoyote ya sekondari ndani au nje ya nchi kwa vile hakuwa na uwezo wa kumsomesha masomo hayo.
Kijana huyo (27), ambaye ameshitakiwa kwa tuhuma za kuendesha gari bila leseni na kwa mwendo kasi uliosababisha kifo cha Wangwe, wiki iliyopita, alikaririwa na gazeti hili akidai kwamba, ana fani ya usanifu aliyoipata Nairobi katika Chuo cha Mtakatifu Hubert baada ya kumaliza sekondari kidato cha nne.
Hata hivyo, katika maelezo yake aliyoyatoa jana, Francis alisema anakumbuka kwamba, mwanaye alizaliwa mwaka 1983 katika Kijiji cha Kichare na kubatizwa kisha kusoma shule ya msingi Umbwe hadi darasa la saba.
"Kwa sababu mimi sikuwa na uwezo wa kumpeleka sekondari aliendelea kujisomea akawa ananunua vitabu vya kujisomea, lakini baadae akaondoka kwenda Dar es Salaam alikojifunza kozi ya kompyuta," alisema Francis.
Francis alisema mwanaye alipita tu Nairobi alipokuwa akirejea kutoka nchini Libya, ambako hadi sasa hafahamu hasa shughuli iliyompeleka huko (Libya).
Mzee huyo, alisema aliporejea kutoka Libya, alishukia Nairobi ambako alikutana na rafiki yake waliorejea wote jijini Dar es Salaam.
Alisema anachofahamu ni kwamba kulikuwa na mtu ambaye hamfahamu, ambaye alikuwa akiwasiliana na mwanae kwa ajili ya kwenda Libya na alipokwenda hakufikisha wiki alirejea nchini.
Francis alisema mwanae aliweza kumudu vyema mafunzo ya kompyuta baada ya kupata mtu wa kumfundisha na baada ya kumudu mafunzo hayo alijishughulisha na kazi ya kutengeneza fulana, ambayo anaendelea kuifanya hadi sasa.
Alishutumu mwelekeo unaoanza kujitokeza wa kutaka kuhalalisha kuhusika kwa mwanae na kifo cha Wangwe.
"Kumuita mtoto wangu ni jasusi bila kumpa nafasi ya kumsikiliza wala vyombo vya dola havijathibitisha hilo ni kumhukumu, jambo ambalo ni kinyume cha katiba…wanamhukumu vipi kwa hisia?," alihoji Francis.
Alidai kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ya kumuita mwanae ni jasusi, ina lengo la kuushawishi umma uamini mwanae anahusika na kifo cha Wangwe.
Francis ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kichare katika kijiji cha Umbwe Sinde alisisitiza kilichotokea ni ajali kama ajali nyingine na suala hilo sasa liachiwe mahakama ambayo itachambua ushahidi na kujua lipi la kweli na lipi halina ukweli.
"Kwa muelekeo huu ninaouona, naomba taasisi zinazotoa msaada wa kisheria zisaidie kulinda haki ya mwanangu, ambaye tangu akamatwe hatuna mawasiliano naye na ndugu wamezuiwa kuonana naye," alidai.
Akielezea tabia ya mwanae, alisema anamfahamu vyema na kwamba hajawahi kushika bunduki wala kisu achilia mbali kutembea na wahuni, bali alikuwa akifuata maadili mema ya Kanisa Katoliki.
Alisema anamfahamu mwanae kama mtu anayejishughulisha na kazi ya kuchapisha maandishi na picha kwenye fulana na kazi hiyo ndio ambayo amekuwa akiifanya kwa ajili ya shule, makanisa na vyama vya siasa.
Alifafanua kuwa mara tu baada ya ajali, mwanae alimpigia simu akimuarifu kuwa alikuwa akitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam akiwa na mbunge mmoja, lakini kwa bahati mbaya gari imepata ajali na mbunge amefariki dunia.
"Aliniambia kuwa gari imepinduka mara sita na kujikuta nje ya gari akiwa hana simu yake ya mkononi huku akiwa na majeraha miguuni na kichwani na mbunge alifariki dunia papo hapo," alidai Francis.
Aliendelea kusema kuwa: "Alinitaka nisiwe na wasiwasi sana kwani hajaumia sana ila masikitiko yake ni kwamba mbunge amefariki…nilimuuliza nani alikuwa anaendesha gari akasema ni mbunge mwenyewe."
Kwa mujibu wa Francis, hata wakati anakwenda kwake Dodoma mwanae alimpigia simu na kumjulisha kuwa anakwenda huko kikazi kwa wiki moja na baadae atarejea Dar es Salaam kabla ya kwenda tena Dodoma kwa kazi ya fulana.
Katika hatua nyingine, Ramadhan Semtawa anaripoti kutoka Dodoma kuwa Deus Mallya anayedaiwa kuwa dereva wa marehemu Wangwe, amezidi kugonganisha vichwa vya watu baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Juma Kilimba, kusema hamjui wala hana urafiki na kijana huyo.
Kauli hiyo ya Kilimba inapingana na ile aliyotoa Mallya kwamba anafahamiana vema na mbunge huyo kwani walikuwa wote katika safari yao ya kwenda Libya mwaka jana.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge mjini hapa jana, Kilimba alisema licha ya kutomfahamu pia alishangaa na hadi sasa hajui kijana huyo aliingiaje katika msafara wao wa kwenda Libya hapo mwaka jana.
Kilimba alifafanua kwamba, alisikia Mallya kwamba anamfahamu yeye (Kilimba), alishangaa na kuongeza kwamba: "Siyo urafiki tu, simjui na sijawahi kuwa na ukaribu naye."
Hata hivyo, Kilimba aliongeza kwamba baada ya kusikia taarifa hizo alikumbuka kwamba wakati wakiwa uwanja wa ndege wa Zurich, Uswisi, katika safari hiyo kuelekea Libya mwaka jana, kijana huyo aliwahi kusahau hati yake ya kusafiria kwenye ndege.
Alisema kwa kuwa walikuwa katika msafara mmoja, yeye (Kilimba), alishauri asaidiwe baada ya kuzuka tafrani ndipo kiongozi aliyeshughulikia safari hiyo akamsadidia kijana huyo na wala si yeye.
"Niliposikia huyo kijana ana nifahamu mimi, kwanza sikuwa na fikra kabisa kwamba kuna kijana kama huyo aliwahi kuwa rafiki yangu au namfahamu, nikakumbuka kumbe ahaa, ni yule ambaye aliwahi kusahau pasi ya safari yake ndani ya ndege tukiwa Zurich,"alisema Kilimba na akaongeza:
''Mimi nilikuwa Bussines Class yeye alikuwa Economy, sikuwa nikimfahamu, nilishangaa hata mimi pale Zurich kumuona yuko katika msafara, nilihoji na hadi sasa sijajua, aliingiaje katika msafara ule, ndiyo maana nakwambia simfahamu kabisa zaidi ya kuonana pale.''
Aliongeza kwamba, watu aliokuwa nao na aliowafahamu ni pamoja na Makongoro Nyerere ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara, Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mamuya, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Simba, Shehe Seleman Kilemile na Hebron Mwakagenda, ambaye ni kutoka Leadership Forum.
Mallya alifunguliwa kesi namba TR 103/08, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa, kwa makosa ya kuvunja sheria za usalama barabarani, ambayo ni kuendesha gari kwa mwendo kasi na kusababisha kifo cha Wangwe na kuendesha gari bila leseni.
Tuma maoni kwa Mhariri