Kimsingi hakuna tofauti kati ya vimondo na asteroidi:
ni suala la ukubwa tu. Violwa vidogo kuanzia ukubwa wa punje ya mchanga hadi kufikia kipenyo cha mita kadhaa huitwa vimondo. Vikubwa zaidi huitwa
asteroidi. Hivyo kimondo ni kidogo kuliko asteoridi na kikubwa kushinda vumbi la angani.
Njiamzingo (ing.orbit) ya kimondo unaweza kuingiliana na njiamzingo ya Dunia au sayari nyingine. Kimondo kikilikaribia kiolwa cha angani kikubwa zaidi kinavutwa na graviti yake. Kikikaribia mno dunia yetu kinaingia katika angahewa na kuanguka chini kwa kasi kubwa sana. Njiani kinapashwa moto kutokana na msuguano wa hewa dhidi yake. Kiasi cha joto kinatosha kuchoma kimondo kidogo kabisa hewani.
Hii inaonekana kwa macho matupu kama mstari wa moto angani unaowaka kwa sekunde 1-2. Hii ni hali inayoitwa pia "meteori". Waswahili wa Kale waliita "Vinga vya sheitani" walieleza miale hii ya moto angani kuwa malaika angani wanazuia masheitani kupanda juu kwa kuwarushia vipande vya kuni vya kuwaka
Kati ya vimondo kumi vikubwa kabisa duniani
ambavyo mabaki yake yanaonekana, kimojawapo ni Kimondo cha Mbozi nchini Tanzania.
Katika karne ya 20 kuna taarifa zifuatazo kuhusu watu walioathiriwa na vimondo:
-5 Septemba 1907 Weng-li, China - familia yote kufa
-28 Aprili 1927 Aba, Japan - binti kujeruhiwa
-8 Desemba 1929 Zvezvan, Yugoslavia - kimondo kugonga kwenye arusi, mmoja kufa
-16 Mei 1946 Santa Ana, Meksiko - nyumba kuharibiwa, watu 28 kujeruhiwa
-30 Novemba 1946 Colford, Ufalme wa Muungano - simu kuharibiwa, mvulana kujeruhiwa
-28 Novemba 1954 Sylacauga, Alabama, USA - kimondo cha kilogramu nne kugonga nyumba, mama kujeruhiwa
-14 Agosti 1992 Mbale, Uganda - vimondo 48 kuanguka, mvulana kujeruhiwa