“Tumesikia Kuhusu Ajali ya Precision Air, Wazembe Wawajibishwe”

Apr 24, 2011
29
542
April 2021, Egypt, Mkuu wa Shirika la Reli la nchi hiyo ya kaskazini mwa Baraa Afrika, alijiuzulu baada ya kutokea ajali ya treni. Ajali hiyo iliyotokea jioni katika mji wa Banha katika mkoa wa Qalyubia, ikapelekea kuuawa watu wasiopungua 16 na kujeruhi wengine 98. Waziri wa Usafirishaji wa Egypt, Kamel al-Wazir akaema kuwa wahusika wote wa ajali hiyo watachukuliwa hatua kali.

November 2016, Meneja Mkuu wa Shirika la Reli la nchi ya Iran, Muhsinpur Seyyid Agayi, alikubali kwamba kulikuwa na makosa katika sehemu ya usimamizi wa reli kutokana na ajali ya treni katika Mkoa wa Simnan, na kuua watu 40, na Muhsinpur akasema “ni wakati sasa mimi nijiuzulu rasmi, naomba radhi wananchi wa Iran kwa tukio hili chungu. Wasimamizi lazima wawajibike kwa matukio yaliyotokea.”

2013, Baada ya ajali ya meli South Korea serikali ilikosolewa kwa jinsi ilivyodili na ajali hiyo. Meli hiyo ilivyozama sehemu kubwa ya abiria walikuwa ni wanafunzi na watu kama 100 hawakupatikana. Kwenye hatua za ukoaji zilitumika meli 34 na helicopter 18 na njia nyingine lakini serikali ilikosolewa. Kutokana na hilo waziri mkuu Chung Hong-won alitangaza kujiuzulu baada ya wananchi kutoridhishwa na utendaji wa serikali kwenye hilo

Julai 20, 2012, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alijiuzulu wadhifa wake baada ya kuwepo kwa shinikizo la kuachia ngazi lilitoka kwa wananchi. Hatua hii ilikuja kufuatia madai ya wananchi kuwa ajali za meli zimekuwa zikiongezeka Zanzibar bila waziri kuchukua hatua. Baada ya kujiuzulu, Rais, Dkt Ally Mohammed Shein akamteua Rashid Seif Suleiman (CUF) kuchukua nafasi yake..

Taarifa (ambayo pia imesomwa na kuthibitishwa na waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa) 24/11/2022 ya Uchunguzi wa ajali ya ndege, Precision Air, 5H-PWF, ATR42-500 inatosha kabisa kuwaondoa watu katika majukumu yao, wakae pembeni, na ikiwezekana, washtakiwe kwa uzembe na kutowajibika na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine kujeruhiwa.

Taarifa (report) hiyo inaeleza baada ya ndege kutua kwenye maji (mita 500 kutoka ilipotakiwa kutua) boti ya uokozi haikuwepo Bukoba, ilifika baada ya saa 5 kupita (ingawa walipewa taarifa baada ya dakika 15 tangu ajali kutokea), na hata hiyo boti ilipofika haikufanya uokoaji kwa kuwa boti haikuwa na mafuta ya kutosha na mitungi haikuwa na gesi ya oksijeni kuwezesha wapiga mbizi kuzama kwenye maji.

Precision Air 5H-PWF, ATR42-500 ilianguka kwenye maji, ziwa Victoria saa 08:25 asubuhi. Boti mali ya Jeshi la polisi kitengo cha wanamaji haikuwepo bandarini au karibu na eneo la ajali. Ilikuwa kwenye majukumu mengine ya doria. Boti hiyo ilifika eneo la tukio saa 5 baadae (saa 13:49) hata hivyo wapiga mbizi walikosa oksijeni na mafuta kwenye boti. Nchi gani hii tunaishi? Ni kama wizara hizi hazina viongozi.

Waziri wa Uchukuzi bado yupo ofisini? Anafanya nini katika ofisi za umma? Watumishi wa Kitengo cha maafa - ofisi ya waziri mkuu bado wapo ofisini? Mkuu wa Polisi kitengo cha Wanamaji bandari ya Bukoba bado wapo ofisini? OCD wa Bukoba yupo ofisini? RPC wa Kagera bado yupo ofisini? Sababu gani za msingi zinawafanya waendelee kuwepo ofisini kama watumishi wa umma hadi sasa?

Kama hatuwezi kuwaokoa watu wetu katika ajali iliyotokea umbali wa mita 500 kutoka nchi kavu, katika maji yenye kina cha mita 5.4 (epipelagic zone) tunaweza kuokoa watu wetu wakipata ajali kwenye maji yenye kina cha kuanzia mita 200 hadi 1,000 (futi 660-3,300) chini ya uso wa bahari. Eneo hili wataalam wanaliita (mesopelagic zone). Tunaweza kutumks muujiza gani kufanya uokoaji?

Eneo hili (mesopelagic zone) linajulikana kama ukanda wa twilight (twilight zone), kwani linakaa kati ya eneo la epipelagic (mita 0-200) , ambalo hupokea mwanga zaidi, na eneo la bathypelagic, ambalo halipati mwanga. Mwanga unaofikia ukanda wa mesopelagic ni hafifu na hauruhusu photosynthesis. Fikiria, ndege imeanguka eneo hilo, binadamu hata mmoja ataokolewa hapo?

Umbali wa mita 500 ni sawa na urefu wa viwanja viwili vya mpira wa Miguu. Yaani Benjamin Mkapa Stadium au Kirumba Stadium (mara mbili). Polisi kitengo cha Wanamaji katika bandari ya Bukoba kilishindwa kuokoa watu katika ajali ya ndege ya Precision Air, 5H-PWF, ATR42-500 iliyoanguka kwenye maji, Ziwa Victoria.

Umbali huu kwa Askari aliyefundishwa vyema, anaweza kupiga mbizi. Tukubaliane kwamba Askari wetu hawana uzoefu wa kuokoa katika ajali za maji? Lakini hata kama wangelikuwa wanajua kupiga mbizi, wangewezaje kutekeleza majukumu yao ikiwa hawana vifaa vya kupigia mbizi? Mitungi haina gesi ya oksijeni na boti waliyonayo haina mafuta ya kutosha kusogea mita 500 kutoka nchi kavu.

Lakini pia hapa kuna mashaka. Kwanini? Taarifa hiyo ya Uchunguzi (ikiungwa mkono na waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa) inaeleza kwamba, boti ya uokozi mali ya Polisi kitengo cha Wanamaji kutoka katika bandari ya Bukoba, haikuwepo karibu na uwanja (zingatia uwanja upo mita 180 kutoka ufukweni) wakati ndege inapata ajali, boti hiyo ilikuwa katika shughuli zake nyingine za doria.

Tunaweza kukubaliana kwamba, ni kweli inafanya kazi za doria, lakini ilipaswa kuwepo bandarini wakati ndege inakaribia kutua kwa sababu ni boti ya uokozi (imetajwa hivyo katika ripoti na waziri alifafanua), ili kujiandaa na lolote kuzuia maafa kama litatokea janga, ukizingatia uwanja huo upo karibu sana na Ziwa na mvua zilzoambatana na upepo mkali, ngurumo na radi ilikuwa inanyesha.

Zingatia, kama uwanja wa ndege wa Bukoba hakuna mnara wa udhibiti anga (Air Traffic Control Tower) Ndege zinazofanya safari uwanja huo hutumia huduma hiyo kwa njia ya MWANZA masafa ya 122.8MHz hadi zitakapoleta taarifa za ufahamu kutoka Bukoba, unafikiri bandari ya Bukoba watakuwa na Mawasiliano ya kitaalam na boti ya uokoaji (isiyokuwa na mafuta) kwamba wasitoke eneo la uwanja kusubiri ndege zitue?

Lakini, kama kweli ni boti ya uokozi, kwanini saa tano ilipofika eneo la tukio haikuwa na mafuta ya kutosha kufika umbali wa mita 500 kutoka kwenye kizingiti cha njia ya kutua ndege? Mafuta waliyatumia katika doria, sawa, hawana mafuta ya ziada kwa ajili ya kufanya kazi rasmi ya boti hiyo, uokozi majini? Sawa, na hiyo mitungi ya gesi ya oksijeni kwanini haikuwa na gesi? Boti hii ilijiandaa kufanya uokoaji wa kitu gani?

Nia ni kuwatahadharisha wasomaji wote wa makala hii dhidi ya jaribio lolote linalokusudia kutufanya watu wote timamu tuache kufikiri. Juhudi za watawala zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutufanya kuwa “mabwana-ndiyo”, watu wa kumezeshwa maneno, dhana, fikra na imani zisizokuwa na maana kwetu kama wananchi, na tukazikubali bila kusaili lolote. Tukikubali, utakuwa ushindi mkubwa sana kwa watawala wazembe.

Taifa la “mabwana-ndiyo” haliwezi kupiga hatua yoyote ya maendeleo hata kama lingesimikwa katika machimbo ya rubi, dhahabu na almasi. Mifumo yetu mbalimbali imetumika, kujaribu kutufanya sote tuwe mazuzu. Tusikubali hilo jaribio la kutufanya kuwa “mabwana-ndiyo”.

Juhudi kubwa zinafanywa ili tukubali kuacha kutumia bongo zetu timamu na badala yake tutumie bongo za kuazima kutoka kwa watawala wazembe wanaodhani kwamba jinsi wanavyofikiri wao ndivyo kila mmoja wetu anatakiwa afikiri, na asiyefikiri kama wao anakuwa ni zwazwa.

Maswali ni mengi, na hakuna majibu, ajali ya Precision Air, 5H-PWF, ATR42-500 imetokea, 6/11/2022 hadi sasa naandika hapa (25/11/2022) ni siku 19 baadae, hakuna anaejali, hakuna aliyewajibika au kuwajibishwa, watanzania wanafanywa mazuzu tu, wanahamishwa mijadala, na hawawezi kamwe kuwajibisha wahuni, wazembe waliopo serikalini na wamesababisha maafa. Kamwe, tusikubali kuwa Taifa la mabwana ndiyo.

#MMM, Martin Maranja Masese, Mtikila
25/11/2022
 
Kwa jinsi Mungu alivyo fundi, Ipo siku ndege zao zitahusika ndio watatia akili.

Halafu wakawaletea igizo la Bashiru kuwatoa kwenye reli. Hata kama alikuwa igizo, CCM wakalishikia bango lengu likiwa ni lile lile la kuwatoa kwenye reli.
 
Ccm ni kikundi cha kigaidi, lakini wapinzani ndio mazombie kabisa.

Haiwezekani watu wenye akili timamu eti kubishania Majaliwa hakufunguwa mlango wa ndege hilo lina tija gani?

Kitu cha msingi wahusika wote ambao hawakutimiza majukumu yao wawajibishwe, na siyo kumuonea gere kijana maskini ambaye Mungu amemdoshea zali la mentali kwa kuhusika kwake katika uhokowaji.

Mfunguwaji wa mlango siyo issue, kama walifunguwa mlango wenyewe mbona hawakuogelea mpaka nchi kavu?

Hapa ndio nimemdharau sana Zitto Kabwe na Sugu kwa kushikia bangi hoja za kipuuzi kabisa na kuacha hoja za msingi za kuwajibishwa waliohusika na uzembe.
 
Mkuu

Tangu Baba wa taifa atuache huo utamaduni ulikufa Rasmi!

Anaepaswa kujiuzulu ni nani!?

Je ni Waziri mkuu PEKEE!?je ni Nani!?

Mungu ibariki Tanzania NCHI yangu!
 
Kwa jinsi Mungu alivyo fundi, Ipo siku ndege zao zitahusika ndio watatia akili.
Cha kushangaza, watu wa aina hii hata uwaombee mabaya kiasi gani; hayawakuti eti! Na hata siku ikitokea, basi kuna watu hufanya mpaka sherehe kama ilivyotokea mwaka 2021.
 
Back
Top Bottom