Na Geofrey Nyang'oro
HAKUNA shaka kwamba utawala wa Rais Jakaya Kikwete sasa uko katika majaribu kutokana na mvutano uliopo baina ya taasisi kubwa mbili za dini, huku kila moja ikivutia kwake katika suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania bara.
Wakati Waislamu wakiwa wameweka msimamo wao wa kushinikiza suala hilo, Wakatoliki wamependekeza kinyume chake katika ilani yao ya uchaguzi iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa kushirikiana na chama cha wasomi wa kanisa hilo (CPT).
Katika ilani hiyo iliyotolewa na idara ya Kichungaji, Tume ya Haki na Amani-TEC na kubatizwa kama 'Mapendekezo ya vipaumbele vya kitaifa', wameeleza kuwa wangependa katiba ya nchi iheshimu kanuni ya kuwa serikali haina dini na kutoruhusu taasisi za kidini kama vile Mahakama ya Kadhi na Uanachama wa OIC kuwa sehemu ya mfumo wa nchi.
Hoja za pande hizo mbili zinamweka kati Rais Kikwete na kumfanya akune kichwa kutoa maamuzi ya busara ambayo yataungwa mkono na pande zote.
Hali hii imekuwa tete zaidi baada ya serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba kuanika bungeni mpango wake wa kutoanzisha mahakama hiyo inayodaiwa kuahidiwa kwenye ilani ya CCM mwaka 2005, badala yake ikataka kuhuisha sheria za kiislamu katika sheria za nchi kama inavyofanyika Afrika Kusini.
Lakini Waislamu ambao tayari wamekwenda mbali zaidi na kutishia kuinyima kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao endapo mahakama hiyo haitaanzishwa bara, wanapinga kufuatwa mfano wa Afrika Kusini, badala yake wanataka ufuatwe mfano wa nchi za Kenya, Uganda na Zanzibar zilizopo Afrika Mashariki ambazo zina mahakama ya kadhi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amesema kuwa Waislamu hawana sababu ya kukinyima kura chama hicho kwa kuwa kimeshatimiza ahadi yake inayodaiwa kuchangia Rais Kikwete kupata ushindi wa kishindo mwaka 2005.
Katika ahadi hiyo iliyopo kwenye ibara ya 108 (b), CCM ilipanga "Kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania bara", hatua ambayo Makamba anasema wameifikia, lakini Waislamu kupitia Baraza lao Kuu (Bakwata) na taasisi nyingine za dini hiyo bado wananung'unika.
Watu mbalimbali waliozungumza na gazeti hili na wengine kukaririwa na vyombo vingine vya habari nchini, wameonekana kwamba kila kundi linavutia kwake, Waislamu wanataka ofisi hiyo huku Wakristo wakiwa hawaoni umuhimu wake, hatua ambayo imelalamikiwa kuwa inahatarisha amani ya nchi.
Mkuu wa zamani wa Majeshi, Jenerali Robert Mboma amekaririwa na gazeti moja akionya hali hiyo na kushauri serikali kuwaruhusu Waislamu kuanzisha mahakama hiyo, na kujiwekea utaratibu wa namna ya kumlipa kadhi wa mahakama hiyo.
Mboma alifafanua kuwa kulihusisha bunge katika suala hilo ufumbuzi hautapatikana, kwani kila kundi litakuwa linavutia kwake, na kwamba kama mahakama hiyo itakuwa inajitegemea Wakristo wakizidi kulalamika watakuwa wendawazimu.
Mvutano huo umeibuka katika kipindi ambacho TEC kwa upande wake inasambaza Mpango wa Kichungaji Kuhamasisha Jamii kuelekea Uchaguzi wenye ilani inayoeleza vipaumbele vya kitaifa na mada za kuongoza maandalizi ya uchaguzi ujao, likiwamo suala la Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC na jinsi ya kupata kiongozi mwadilifu anayejali matatizo ya wananchi.
"Kiongozi, huduma kwa umma ni dhima muhimu kwa jamii yeyote ya wanadamu, ndio maana lazima pawepo uangalifu mkubwa kwa jamii yoyote katika njia na namna inavyochagua viongozi wake na namna inavyoweka taratibu za kusimamia na kudhibiti mienendo ya viongozi wao," inasomeka sehemu ya ilani hiyo.
Ilani hiyo inasisitiza kuwa mamlaka iliyopo mikononi mwa wanadamu inahitaji uangalifu ili pasiwe na madaraka yanayoegemea upande mmoja, yawe na uwiano na yasitumike vibaya na hata kuwa na rushwa.
Wakatoliki katika ilani yao wamezungumzia umuhimu wa kufanyika kwa mapitio ya mamlaka ya rais katika kuwateua mawaziri na idadi yao; pia uwezo na uhuru wa bodi za usimamizi wa mashirika ya huduma za umma na kuwaondoa wale wote wanaothibitika kutumia vibaya nafasi zao.
Pia wamekosoa sera ya uchumi ya sasa ambayo imeelezwa kuwa imelalia upande mmoja wa kuangalia matajiri na ikiacha maskini katika mazingira magumu.
Padri Baptist Mapunda amelieleza Mwananchi Jumapili kuwa ilani hiyo imelenga kukuza uelewa wa elimu ya uraia kwa Watanzania, kwa kuwa wengi wao hawajui maana ya demokrasia.
Alisema wamependekeza iundwe Tume Huru ya Uchaguzi ili kusaidia kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki kwa kuwa haiwezekani tume ikaundwa na kiongozi wa CCM halafu ikatoa maamuzi yasiyopendelea upande wowote.
"Tume yetu huru tunayopendekeza ivihusishe vyama vyote vya siasa hapa nchini,wanazuoni kutoka vyuo mbalimbali na hilo ndilo litakalowezesha Watanzania kuingia kwenye demokrasia ya kweli," alisema.
Padri Mapunda alisema mabadiliko ya katiba na Tume ya Uchaguzi hapa nchini ni muhimu katika kuleta demokrasia ya kweli.
Alisema ilani hiyo inapaswa kuibua mijadala miongoni mwa wananchi, kuhoji na kujua maana ya uraia na mapendekezo ya Tume ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, marehemu Francis Nyalali.
Kwa mujibu wa Mapunda serikali imelifumbia macho pendekezo la Jaji Nyalali kuhusu mabadiliko ya katiba.
Jambo jingine linalozungumziwa kwenye ilani hiyo ni upendeleo katika kuwaletea wananchi maendeleo, hali ambayo inaathiri mahusiano mema ya kibiashara na kikazi.
Pia wanadai wamebaini udhaifu mkubwa katika mfumo wa mahakama, na kuitaka serikali kuboresha mazingira ya mahakama ili kuzifanya ziweze kufanya kazi zake kutoa haki bila ya kuingiliwa.
Viongozi hao wa dini na wataalamu wao mbalimbali, wamekemea mchezo mchafu katika utoaji haki kama vile nyaraka muhimu kunyofolewa kwenye mafaili ya kesi na kuathiri mwenendo wake.
Wakizungumzia ufisadi, wameitaka serikali iongeze uwazi katika kuingia mikataba mikubwa, kwa kuwa si vyema mikataba hiyo kuendelea kuwa siri wakati inahusu Watanzania wote.
Vile vile wameonyesha kuchukizwa kwao na kasi ndogo ya kuchukua hatua na kutolea mfano wa kashfa za Buzwagi, EPA na Richmond, ambazo licha ya mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja, serikali ilitumia kanuni zuizi za bunge kudhibiti hali isichafuke zaidi.
Source: Mwananchi.
Nakubaliana na Mboma. Kama mahakama ya kadhi itaji tegemea na si sheria hizo kuingizwa kwenye katiba ya nchi then by all means they should go ahead. Cha muhimu ni ijitegemee na iwa affect wenye imani yao tu. Ila kama serikali itaamua kuingiza sheria hizi kwenye katiba basi hapo kutahitajika debate zaidi kujua namna itakavyo fanya kazi.