Papa Benedict XVI kuzuru Tanzania
*Asifu amani na upendo, ataka viendelee kudumu
Na Godfrey Lutego, Vatican City
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedict XVI amekubali mwaliko wa Rais Jakaya Kikwete kutembelea Tanzania baadaye na akasifu wananchi wake kwa amani na utulivu licha ya tofauti za kidini na kutaka waendelee kuishi hivyo.
Alisema hayo jana alipozungumza na Rais Kikwete kwenye maktaba yake binafsi makao makuu ya Vatikani, alikomwalika ikiwa ni sehemu ya mwaliko aliompa awali kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa madhehebu ya dini duniani utakaofanyika Napoli, Italia kesho, ulioandaliwa na taasisi ya Mt. Egidio inayojihusisha na masuala ya amani duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari walio kwenye msafara wake baada ya kutoka kwa Papa Benedict XVI, Rais Kikwete alisema katika hoteli ya Exedra alikofikia, kuwa kiongozi huyo alimweleza kufurahishwa kwake na amani na utulivu uliopo Tanzania na jinsi watu wake wanavyoishi kwa upendo, licha ya tofauti za dini mbali mbali zilizopo ( hivi kweli bado JK ana amini Tanzania bado ina AMANI na UTULIVU?).
Rais alisema kiongozi huyo wa Wakatoliki duniani, alimweleza kuwa Vatikani inafurahia uhusiano wa kiserikali na kidini uliopo kati yake na Tanzania, kwani ni kati ya nchi ambazo haziisumbui kuhusu masuala ya amani kutokana na watu wake kuishi vizuri ingawa ni wa madhehebu tofauti ya dini na vyama tofauti vya siasa.
Alisema kiongozi huyo alisema amefurahishwa kuona kuwa viongozi wa Serikali waliomfuatia Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere, wameendelea kudumisha misingi ya amani iliyowekwa naye wakati wa uongozi wake na yeye alimhakikishia kuwa ataendeleza ya watangulizi wake ( si aseme anaendeleza uporaji alioanzisha Mkapa pamoja na ufisadi!), na akamwomba aendelee kuibariki ibaki na amani, naye akaahidi Kanisa litaendelea kuiombea idumu katika amani, upendo na umoja ilionao.
Rais Kikwete alisema walizungumzia pia masuala ya afya na elimu ambapo Papa Benedict XVI alisema Kanisa limeona umuhimu wa elimu ya UKIMWI kujikinga na maambukizi na akaahidi kuendelea kusaidia Serikali katika hilo na elimu kwa jumla.
Alisema katika kuimarisha zaidi uhusiano na Kanisa na hasa Kiongozi huyo ambaye ni mpya akiwa amemrithi marehemu Papa Yohanne Paulo II aliyewahi kuzuru Tanzania, alimwalika Papa Benedict XVI na akakubali, lakini akasema atapanga ziara hiyo wakati atakapopanga kuzuru Afrika baada ya kumaliza ziara ya Marekani aliyokwishaipanga.
"Tumemwomba atutembelee na amekubali. Anasema anajua umuhimu wa Afrika lakini akasema anapanga kwanza ziara ya Marekani. Tunatarajia akipanga ya Afrika, atakuja pia Tanzania. Tulimkumbusha pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatikani kuhusu ombi letu tulipokutana naye na akasema lazima Papa atatembelea Tanzania, kwani ina sifa ya pekee katika Kanisa Katoliki duniani, kutokana na kutoa Kardinali wa kwanza Mwafrika, marehemu Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa na Naibu wa Waziri huyo sasa ni Mtanzania, Padri Novatus Rugambwa, anayeshughulikia uhamiaji, hivyo alisema watatufikiria kuwamo kwenye ziara yake," Rais aliwambia waandishi wa habari.
Rais Kikwete alisema alimpatia Papa Benedict IXVI zawadi ya meza ya mchezo wa chess ya mti wa mpingo naye akampa zawadi ya medali ya dhahabu ya Upapa yenye picha yake kwa mbele na maandishi kwa nyuma huku mkewe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe, Waziri wa Chakula na Kilimo, Bw. Stephen Wassira, Waziri wa Utalii Zanzibar, Samia Suluhu Hassan na viongozi waliokuwa kwenye msafara huo wa Rais wakipewa zawadi pia na kusalimiana naye.
Source: Majira