19.08.2008 0101 EAT
Ahukumiwa kunyongwa kwa kuchinja kichanga
Na Anita Boma, Iringa
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, imemhukumu Julio Makombe
(47), adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kukichinja kichanga cha wiki mbili, kutokana na mkewe kuzaa nje ya ndoa.
Jaji Fakhi Jundu, alitoa hukumu hiyo jana, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani, ukiwemo wa Stella Mbata (38) mama wa kichanga icho, Mwamvita Kiyeyeu.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Jundu alisema anatoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kukatisha maisha ya wengine, hususan watoto ambao hawana hatia.
"Nimezingatia ushahidi uliotolewa mahakamani, pia ushahidi wako katika Mahakama ya Wilaya ulikubali kuwa ulikichinja kitoto hicho eti kwa sababu ulimchukia kwa kuwa mkeo hakuzaa na wewe. Hukuwa na sababu ya kuchukua uamuzi huo," alisema Jaji Jundu.
Jaji Jundu alisema kitendo hicho ni cha kinyama, ikizingatiwa mshitakiwa alimkimbia mkewe kwa miaka miwili na yeye katika kipindi hicho alizaa nje ya ndoa.
Stella akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya alidai waliishi na Makombe kama mke na mume kwa muda mrefu na walizaa watoto sita, wawili kati yao walikufa.
Alidai mwaka 2002, Makombe alisafiri kwenda wilayani Kilolo, ambako alikaa kwa miaka miwili bila ya kuwa na mawasiliano na hakuwa akitoa huduma zozote. Katika kipindi hicho alipata mwanaume mwingine, Pangalas Kiyeyeu aliyezaa naye.
Stella alidai Machi, 2004 Makombe alirudi na kumkuta akiwa na mimba na alijifungua mtoto wa kike Agosti 13, 2004, aliyempa jina la Mwamvita.
Alidai Agosti 30, 2004, Makombe alimtaka waende Kilolo akisema kuna mgonjwa, lakini kwa masharti akichinje kichanga hicho. Stella alidai hakukubali ushauri huo.
Stella alidai asubuhi ya Agosti 31, 2004, Makombe alikichukua kichanga hicho na kwenda nacho jikoni akiwa ameshika kisu, ambako alikilaza chini na kukichinja.
Mama huyo alidai baada ya unyama huo, alimtaka kukiweka kwenye mfuko wa rambo na kukitupa choo cha shuleni, lakini alikataa na alipiga kelele za kuomba msaada.
Makombe katika utetezi wake, alidai hakumuacha mkewe na mimba, lakini aliporudi alimkuta akiwa mjamzito na alikiri kwamba si yake.
"Nilichukua mtoto na kumchinja na nilipomaliza nilimwambia akamtupe ******, lakini nichukua uamuzi huo kwa sababu ya hasira, kwa nini mke wangu azaea na mume mwingine," alidai.
Kwa mara ya kwanza Makombe alifikishwa mahakamani Septemba 3, 2004 na kusomewa shitaka la mauaji yaliyotokea Agosti 31, 2004 katika kijiji cha Mgima.