MAJITA.
UFISADI MWINGINE CHADEMA.
Makala Habari nyingine zaidi!
Uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti na jinsi ulivyoitikisa CHADEMA
Theopista Nsanzugwanko
HabariLeo; Tuesday,January 08, 2008 @00:02
Makamu Mwenyekiti wa Chadema,Chacha WANGWE.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni moja ya vyama vikubwa vya siasa nchini. Kilianzishwa kwa juhudi za waasisi kadhaa wa chama hicho, ambao ni pamoja na Edwin Mtei na Bob Makani. Mkutano mkuu wake wa kwanza wa chama hicho, ulifanyika katika kituo cha Msimbazi Dar es Salaam kuanzia Desemba 15-17, 1992.
Mkutano huu ulihudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa yote ya Tanzania na ulichagua viongozi wa kwanza wa chama hicho, majina na vyeo vyao kwenye mabano ni: Edwin Mtei (Mwenyekiti), Ali Suleiman Ahmed (Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar), Brown Ngwilulupi (Makamu Mwenyekiti Bara), Bob Makani (Katibu Mkuu), Mustafa S. Simba (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar) na Eric Mchatta (Naibu Katibu Mkuu Bara).
Tangu mwaka huo 1992, chama hicho kimeendelea kukua na kufanya uchaguzi wa viongozi wake kila inapobidi. Pia, tangu mwaka huo kimekuwa kikishiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais. Matokeo ya kura katika chaguzi hizo yamekuwa ya kuridhisha na hali ya utulivu imekuwa pia inaridhisha.
Hata hivyo, hivi karibuni chama hicho kimetikiswa sana na suala la uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema upande wa Tanzania Bara. Hali hiyo ilijitokeza dhahiri katika vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu vilivyofanyika Dar es Salaam, ambapo baada ya mvutano wa muda mrefu hatimaye alipatikana mshindi, ambaye ni Mbunge wa Tarime kwa tiketi ya chama hicho, Chacha Wangwe.
Wakati wa kampeni ya kugombea nafasi hiyo, madai mengi yalitolewa na baadhi ya wanachama wao, kuhusiana na chama hicho hadi ikafika mahali Katibu Mkuu wao, Dk.Wilbrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, kudaiwa kutaka kujiuzulu nyadhifa zao. Wanadaiwa walitaka kujiuzulu baada ya kuchukizwa na kitendo cha Chacha Wangwe, ambaye alikuwa mgombea wa nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti, kukishutumu chama kupitia vipeperushi vilivyosambazwa nchi nzima.
Katika vipeperushi hivyo, Wangwe anadaiwa kusema kwamba chama kimegeuzwa kuwa mali ya ukoo na baadhi ya viongozi wa makao makuu. Vipeperushi hivyo vilisambazwa na wafuasi wa chama hicho, waliokuwa wakimuunga mkono Wangwe katika kinyang'anyiro hicho. Habari kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, zinadai Dk Slaa ambaye ni Mbunge wa Karatu na Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, walifikia uamuzi huo, baada ya hoja kuhusu vipeperushi hivyo kujadiliwa katika kikao hicho.
Hata hivyo, waasisi wa chama hicho, Edwin Mtei na Bob Makani walifanya kazi ya ziada kuwashawishi Dk Slaa na Zitto kubadili uamuzi wao wa kujiuzulu na kuendelea na nyadhifa zao ili kulinda chama kisigawanyike. Chanzo chetu kilichokuwa ndani ya kikao hicho cha Kamati Kuu, kilisema kuwa "Ni kweli Zitto na Slaa walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na vipeperushi vya Wangwe, lakini baada ya mambo kuwekwa sawa na waasisi hao wa chama, walikubali kurejea kwenye nyadhifa zao."
Kutokana na kitendo hicho, Kamati Kuu ilimuonya Wangwe na pia Kamati Kuu ilitishia kufuta uchaguzi huo. Hata hivyo, baadaye Kamati Kuu iliridhia kuwa uchaguzi huo ufanyike. Ilitoa uamuzi huo baada ya wajumbe wa kamati hiyo kupiga kura, ambapo 14 walisema ufanyike na 11 wakasema usifanyike.
Ndipo kikao hicho kilifanyika chini ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili kuandaa ajenda ambazo zingejadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu. Nalo Baraza Kuu baada ya kujadili ajenda hizo, liliendelea na ajenda ya kumchagua mwanachama atakayejaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti, iliyoachwa wazi na Amani Walid Kabourou, aliyejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana.
Lakini, pamoja na kuonywa, Wangwe aliendelea kushikilia msimamo wake ulioko kwenye vipeperushi vyake katika kikao hicho pia. Vipeperushi hivyo vinawatuhumu baadhi ya viongozi wa Chadema kuendesha chama kwa upendeleo, hasa katika mgawo wa ruzuku. Pia, kinawatuhumu viongozi wa Chadema kwa ubaguzi wa misingi ya kidini na Kikanda. Katika vipeperushi hivyo, Wangwe anadai kuwa kutokana na kasoro hizo, atahakikisha analeta mabadiliko ya kweli ndani ya chama ili kukiepusha kuendeshwa kama shirika lisilo la kiserikali (NGO).
"Tunataka kiwe chama cha siasa chenye lengo la kuking'oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010," anasema Wangwe. Anasisitiza kuwa jambo kubwa linalokitia dosari CHADEMA ni ofisi za wilaya na kata kutokuwa na mawasiliano na makao makuu, hasa katika mgawo wa ruzuku na uteuzi wa wabunge wa viti maalumu.
Wangwe anadai mgawo wa ruzuku na uteuzi wa wabunge wa viti maalumu, vimekuwa vikitolewa na uongozi wa Chadema kwa kuangalia upande mmoja wa wanachama wanaotoka Kanda ya Kaskazini hapa nchini. "Chama kimekuwa mali ya koo na familia fulani. Tunataka kiwe cha wanachama," anadai Wangwe, ambaye baadaye alifanikiwa kupata nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti. Alimshinda Mbunge wa Mpanda Kati kwa tiketi ya Chadema, Said Arfi.
Wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Wangwe katika kinyang'anyiro hicho, waliendelea kusambaza vipeperushi hivyo vinavyotuhumu kuwapo na upendeleo katika mgawo wa ruzuku za chama na ubaguzi wa kidini na kikanda katika chama hicho. Vipeperushi hivyo vilitawanywa makao makuu ya Chadema, mikoani, wilayani na katika eneo ambalo Kamati Kuu ilikutana na vinadai kwamba chama hicho kimekuwa kikipata ruzuku ya Sh milioni 60 kila mwezi, lakini fedha hizo zimekuwa zikiishia makao makuu huku matumizi yake hayawekwi bayana.
"Tunasema inawezekana kila mkoa ukapata Sh milioni 1.5 kila mwezi na makao makuu itabaki na zaidi ya Sh milioni 10 ambazo zinawatosha kwa shughuli za chama," inaeleza sehemu ya kipeperushi hicho. Kipeperushi kinadai kuwapo kwa "ubinafsi" katika chama, ambao umesababisha karibu wabunge wote wa viti maalumu kuteuliwa kutoka katika mkoa mmoja uliopo eneo la Kaskazini mwa nchi.
"Tumchague Chacha ili aweze kubeba majukumu hayo na kuyavalia njuga ili ruzuku igawanywe katika mikoa yote. Chacha pambana kama unavyopambana na CCM katika Jimbo lako la Tarime," kinaeleza kipeperushi hicho. Kipeperushi hicho kinawataka wajumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu kutoingia kwenye mtego wa kidini, kwa madai kwamba chama hicho siyo msikiti wala kanisa.
"Ni chama cha siasa kinachotaka kuendelezwa na kiongozi jasiri kama Chacha (Wangwe). Hatusemi kwa ushabiki, angalia ukweli hapo makao makuu. Chadema ni chama chetu siyo kampuni ya watu binafsi, tubadilishe hali hii," kilieleza kipeperushi hicho. Baada ya kutolewa kwa malalamiko hayo yaliyopo katika vipeperushi, Dk.Slaa alikanusha madai yaliyotolewa na kusema kuwa pesa zote za ruzuku, hutumika kutokana na maamuzi ya vikao vya chama.
Pia, alizungumza kuhusu wabunge wa viti maalumu karibu wote kutoka upande mmoja wa Kaskazini, ambapo alisema kutokana na chama hicho kuwa na wabunge wachache, inawabidi kutafuta wenye uwezo katika kutoa hoja za msingi bungeni. Wabunge huteuliwa kwa kuangalia utendaji wa kazi zao ambazo zinaonekana wakiwa bungeni. Kule bungeni hatupeleki sura, bali watendakazi ambao ndio jeuri ya chama chetu, anasema.
Dk Slaa anasema shutuma zilizotolewa na Wangwe, ambaye alikuwa anagombea umakamu mwenyekiti, ni maneno tu ya kumtaka apate nafasi hiyo. Alizungumzia baadhi ya matumizi yaliyoamuliwa katika vikao vya chama, kuwa ni pamoja na kuzunguka nchi nzima kukitambulisha chama kwa Watanzania, ambazo ukiacha usafiri na gharama nyingine zimetumika zaidi ya Sh milioni 200 kutengeneza bendera, kadi na vipeperushi.
Dk. Slaa anasema matumizi kama hayo siyo kwa manufaa ya makao makuu pekee, bali kwa mikoa yote waliyotembelea, ukiacha Mtwara na Lindi, ambayo bado hawajaitembelea kwa lengo la kuwajulisha Watanzania walioko mikoani sera za chama hicho. Hakuna chama kingine cha siasa ukiacha chama tawala kilichoweza kuzunguka mikoani na kujitambulisha kwa wananchi kama tulivyofanya sisi kwa shilingi milioni 60 kila mwaka, anasisitiza.
Akifungua Baraza Kuu la chama hicho, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alidai suala la kusitishwa kwa mjadala wa Katiba ni ukiritimba. Anasema katiba inapaswa kujadiliwa wakati wowote kwa kuwa ni mali ya wananchi. Pia, alisema baada ya kutimiza miaka miwili, Rais Jakaya Kikwete inabidi afanyiwe tathmini ya uongozi wake na pia alidai kuwa wananchi wamechoka na kauli za kutia matumaini huku hali ya maisha ikizidi kuwa ngumu.
Pia, Mbowe anawataka Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, kutoa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwani kampuni iliyopewa kazi ya kuichunguza ilipewa siku 28 tu kukamilisha uchunguzi na kutoa ripoti. Anadai kuwa siku zimeisha, lakini wananchi bado hawajapewa ripoti hiyo. Baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha Baraza Kuu, Mbowe alikanusha kuwa kuna migogoro katika chama chake hicho.
Pia, alisema kuwa Chadema itaendelea kutumia helikopta katika awamu nyingine ya ziara zake, baada ya kutafakari gharama za ziara za helikopta. Baraza Kuu limetafakari gharama za ziara za helikopta na kuwianisha na ziara nyingine na kuazimia kwa kauli moja kuendelea kutumia usafiri huo katika awamu nyingine ya ziara, anasema.
Mbowe anasema maazimio mengine waliyoyafikia ni pamoja na kuweka hadharani hesabu ya mapato na matumizi, kwani kila mwanachama wa chama hicho ana uhuru wa kufahamu hilo. Alitaka wengine wanaotaka kujua hesabu hizo wafike makao makuu. Pia, Baraza Kuu liliamua kuendeleza ushirikiano wa vyama kwa lengo la kudumisha demokrasia nchini na kuunganisha nguvu katika kutetea maendeleo na hatimaye upinzani uweze kuchukua dola. Baraza hilo lilipitisha azimio la kutangaza ratiba ya uchaguzi wa chama hicho, utakaofanyika kuanzia mwezi Januari hadi Desemba.
Anasema uchaguzi huo utaanzia katika vitongoji, kata, jimbo, wilaya, mikoa na Kanda. Pia, kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa. Katika uchaguzi wa Makamu wa Mwenyekiti upande wa Tanzania Bara, Baraza Kuu lilimchagua Chacha Wangwe kushika nafasi hiyo, baada ya kupata kura 56 kati ya 94 zilizopigwa.
Mpinzani wake Mbunge wa Mpanda Kati, Said Amour Arfi, alipata kura 38. Akitoa shukrani zake baada ya kutambulishwa rasmi kuwa Makamu, Wangwe anasema atatumia nafasi hiyo kurudisha demokrasia iliyoanza kupotea katika chama hicho. Anasema atafanya hivyo kwa kutumia vikao vya viongozi wa ngazi za juu. Wangwe anasema kutokana na chama hicho kuwa cha kidemokrasia, mambo yote yaliyotokea ni harakati za kuimarisha demokrasia, hivyo yalikuwa ni sehemu ya midahalo tu; na wala sio migogoro, kama wengi walivyodhania.