Huyu ndiye ‘the real’ Kikwete!

Huyu ndiye ‘the real’ Kikwete!

Jamani kwa wapenzi wa kikwete, kipi amabcho kikwete ameboresha tangu ameingia madarakani. kitu alicho initiate mwenye sio mikakati aliyoacha mkapa yeye kafanya kuendeleza? tuanzie kwenye ilo
 
Murangira

Swali la Asha Abdala mbona unalirukia? Mwenyewe alisema hajaliona.
 
Hapa hakuna wapenzi wa rais, kuna wananchi wenye mitizamo tofauti kwa namna nchi inavyoendeshwa,

nafikiri ukirudia threads nyingi zilizoko humu utayaona hayo maoni ya pande nyingi tofauti, kuhusu urais wa Muuugwana, unless una swali specific kuhusu urais wake!
 
Kuna wapenzi na wapambe wa Kikwete hapa . Ni bora swali likajibiwa .
 
Kama vile walivyo wapenzi na wapambe wa Freman, Lipumba, Seif, na Mtikila, and what is wrong with that?
 
Hapa hakuna wapenzi wa rais, kuna wananchi wenye mitizamo tofauti kwa namna nchi inavyoendeshwa,

nafikiri ukirudia threads nyingi zilizoko humu utayaona hayo maoni ya pande nyingi tofauti, kuhusu urais wa Muuugwana, unless una swali specific kuhusu urais wake!

Okay, Kipi alichofanya Kikwete ndani ya miezi 12 ambacho anaweza kukaa na kujivunia leo hii?
 
nimesoma mjadala jinsi unavyokwenda nimeonelea nami nichangie,jk ni rais wa awamu ya nne,uongozi ni kama mnyororo ama kama alivosema mwenyewe awali kuwa ni kama mbio za kupokezana vijiti,kwanini naanza hivi ? katika awamu yake JK lengo siyo kuanza jipya bali kupeleka kwa kasi yale yote yanayolega-lega,kama mtakumbuka kazi kubwa ya awamu ya kwanza ya jkn ilikuwa kujenga utaifa,awamu ya pili ya mzee ruksa ilikuwa kubadilisha sera na awamu ya tatu ya bm ilikuwa kutekeleza na kuboresha sera ikiwemo ya kuimarisha ukusanyaji kodi na mengineyo mengi,mikakati mingi inajukuwa zaidi ya miaka 15 mpaka 20,mingi aliyoiacha bm bado haijafikia kikomo,ingawa baada ya muda jk naye atakuwa na yake,katika kipindi chake cha mwaka mmoja na ushee jk amepambana na njaa kuhakikisha hakuna mtanzania anayekufa,akaja kupambana na tatizo la umeme,sasa mvua imeanza kunyesha kwa fujo na mabarabara yameharibika aidha kuna mafuriko ya wanafunzi waliofaulu na wanahitaji kuendelea na sekondari na kwa bahati nzuri hilo pia limefanikiwa,ajira kwa vijana wengi bado wazururaji kwa kuanzia jk ameaanza kubuni njia ya kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kutoa shilingi bilioni moja kwa kila mkoa,mimi kwa mtazamo wangu jamaa atakwenda vizuri tu
 
ingawa baada ya muda jk naye atakuwa na yake,katika kipindi chake cha mwaka mmoja na ushee jk amepambana na njaa kuhakikisha hakuna mtanzania anayekufa,akaja kupambana na tatizo la umeme,sasa mvua imeanza kunyesha kwa fujo na mabarabara yameharibika aidha kuna mafuriko ya wanafunzi waliofaulu na wanahitaji kuendelea na sekondari na kwa bahati nzuri hilo pia limefanikiwa,ajira kwa vijana wengi bado wazururaji kwa kuanzia jk ameaanza kubuni njia ya kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kutoa shilingi bilioni moja kwa kila mkoa,mimi kwa mtazamo wangu jamaa atakwenda vizuri tu

bigman
endelea kuishi kwa matumaini, hakika imani yako kwa jk itakuponya
 
mshikaji kwa namba zilizopo sasa,labda tuongozwe na malaika lakini jk anajitahidi kwa kadiri ya uwezo wake ingawa nakiri kuwa amezungukwa na manyang'au na uso umeumbwa na haya na wahenga walinena zimwi likujualo halikuli ukakwisha,tatizo kubwa ninaloliona na ile hali ya kuendelea kutumia falsafa ya kupokezana vijiti hata katika kulindana,boronga utandawazi unapelekwa viwanda,chemsha utalii na mazingira unapelekwa mifugo,haribu mifogo unapelekwa maji na piga dili madini unapelekwa jumuiya ya afrika ya mashariki,angeweza kuwa na ujasiri wa kumwambia aliyeboronga kaa pembeni tumpe mwingine mwenye uwezo angezoa 100% lakini labda aje malaika ama kizazi cha wenetu...................hapooooooooooo ndipo panapoua tz
 
hapo bigman umenena, JK anajitahidi sana ila amezungukwa na manyang'au,
lakini tujiulize hawa manyang'au amelazimishiwa?? si amejichagulia mwenyewe? kama kweli uso umeumba na haya basi asingejichagulia wasaidizi ambao atawaonea haya pindi wakoseapo.
La ajitahidi saaaana kuzuia hiyo soni maana kwenye uongozi yabidi uwe mkakamavu, usieyumbishwa na ukubali lawama hata toka kwa marafiki (japo ni ngumu)
Lakini kwa kuwabadili badili jamaa zake toka wizara moja hadi nyingine loh atakuwa anacheza pata potea.Mikakati yooote aliyoweka haiwezi kwenda.
 
Mr/Mrs kinyau, kama nilivyokueleza labda tz iwe na rais malaika aliteremla kutoka heaven, lakini kwa namba tulizonazo, labda watoto na wajukuu zetu, tunashindwa kufahamu kiti hicho hata tungempa sas, Mwandosya taja jina lolote mambo yangekuwa mabaya zaidi, ni kweli kuwa wasaidizi kateua mwenyewe lakini mbio za kupekezana vijiti bado bomu kwa watz, kinachotakiwa aamke siku moja na kuwapiga chini manyang'au wote na kuweka hadharani yote mabaya, kuna mengi tunayafahamu ikifika wakati tutayaweka ndani ya jf
 
bigman,
Hawezi kuwapiga chini manyang'au kwa sababu na wao wanayajua madhambi yake. Amegandana nao.
 
nafasi aliyonayo ni mungu tu ndiye yupo above him lakini hata kama mtu anafahamu madhambi yake kwani hatamfanya nini ? kwani Waingereza hawafahamu madhambi ya Mugabe ? lakini kwa kuwa ana kipande chake cha kutawala ni lazima kuheshimiana
 
Jamani kwa wapenzi wa kikwete, kipi amabcho kikwete ameboresha tangu ameingia madarakani. kitu alicho initiate mwenye sio mikakati aliyoacha mkapa yeye kafanya kuendeleza? tuanzie kwenye ilo

Hivi wewe Unataka nini!!? yaani...Hufikirii kabisa...Ni vizuri Kama Unge tueleza Ni mambo yapi Ungefanya endapo wewe Ungekua Kikwete!!?- Katika muda huo Uanao U- uliza( uzungumzia)?
 
Hivi wewe Unataka nini!!? yaani...Hufikirii kabisa...Ni vizuri Kama Unge tueleza Ni mambo yapi Ungefanya endapo wewe Ungekua Kikwete!!?- Katika muda huo Uanao U- uliza( uzungumzia)?

Kama angekuwa Kikwete au Rais?
 
bigman,
Hawezi kuwapiga chini manyang'au kwa sababu na wao wanayajua madhambi yake. Amegandana nao.

Sasa hivi Hana Ujanja!!.....Ila Hana wasi wasi sana!! Lakini...ana vuta vuta Muda !! Ila Sijui kwasa babu gani!!...

Kuwapiga chini sio suluhisho!!-- suluhisho Ni kuumbuana[/B]!!Kuzinguana....
Hakuna ujanja tena zaidi Ya Ukweli!!!
 
hapo bigman umenena, JK anajitahidi sana ila amezungukwa na manyang'au,
lakini tujiulize hawa manyang'au amelazimishiwa?? si amejichagulia mwenyewe? kama kweli uso umeumba na haya basi asingejichagulia wasaidizi ambao atawaonea haya pindi wakoseapo.
La ajitahidi saaaana kuzuia hiyo soni maana kwenye uongozi yabidi uwe mkakamavu, usieyumbishwa na ukubali lawama hata toka kwa marafiki (japo ni ngumu)
Lakini kwa kuwabadili badili jamaa zake toka wizara moja hadi nyingine loh atakuwa anacheza pata potea.Mikakati yooote aliyoweka haiwezi kwenda.

Hakulazimishwa na kibaya zaidi aliwachagua wengi halafu akawapa na Rungu la wasikae ofisini waende sana Mikoani.......................Sasa wameitikia wito si kwa kufanyakazi kidhati bali kulimbikiza miposho,Kichekeshoi cha askari wa mwavuli mmoja anaenda kukagua eneo lenye RVF badala ya kuongozana na wataalaamu na kufuatilia kisayansi kwa ukaribu anawasikiliza wahusika au wamiliki wa mifugo na hadi kupelekea kudanganywa kwamba hakuna ugonjwa ilihali ugonjwa umetapaka kwenye hiyo Ranchi.
 
Someni hapa chini. Ni yeye JK aliyeruhusu uhuni huu, au manyang'au wanamzunguka. Lawama zitakwenda kwake kwa vyovyote. Huyu si raisi makini; japo anaweza kuwa na nia nzuri, hana uwezo DOT


Safari za Kikwete nje zazua shutuma tena

Na Kizitto Noya

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameitupia lawama Ofisi ya Rais kwa matumizi makubwa ya fedha za umma na kuitaka ipunguze matumizi yake ili kulipunguzia taifa mzigo wa kujiendesha.

Shutuma hizo zimetokana na taarifa ya matumizi ya ofisi hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya bajeti ya Ikulu na ile ya kulipia madeni (Consolidated Fund Services) kuwa kubwa mara mbili ya fedha iliyotakiwa kutumika.

Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa katika kipindi hicho, Ofisi ya Rais iliyopangiwa na Bunge kutumia Sh23.4 bilioni, imetumia Sh54 bilioni.

Alisema kutokana na hali hiyo, takwimu za matumizi katika kipindi cha robo ya pili ya bajeti ya ofisi hiyo, inatarajiwa kuongezeka mara dufu endapo hakukuwa na jitihada za makusudi katika kupunguza matumizi katika ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa Lipumba, Ofisi ya Rais inatakiwa kupunguza matumizi yake ikiwa ni pamoja na safari za rais zisizo za lazima nje ya nchi na kujipangia malengo ya utekelezaji wa majukumu yake kulingana na bajeti iliyotengewa.

"Ofisi ya Rais inaongoza kwa ukosefu wa nidhamu katika matumizi ya fedha za umma. Matumizi katika robo ya kwanza ya consolidated fund services, ambayo inajumuisha bajeti ya Ikulu na bajeti ya kulipa madeni, yalikuwa Sh54 bilioni badala ya Sh23.4 bilioni zilizotengwa," alisema Lipumba.

Alisema katika hali ya kawaida, fedha hiyo ilitumika isivyo halali kwani matumizi hayo hayakurudi tena bungeni kuidhinishwa, na kwa kwamba utaratibu huo, Tanzania inajiongezea mzigo wa kuendesha serikali yake bila sababu za msingi.

Lipumba ameishauri Ofisi ya Rais kupunguza safari za rais nje ya nchi, akidai kuwa ndizo zinazoongeza matumizi ya serikali bila kuangalia faida ambayo taifa linapata kwa rais wake kuzifanya mara kwa mara.

"Kuwe na udhibiti wa maana wa matumizi ya fedha za serikali, rais anaweza kukaa ofisini na bado akafanya mazungumzo na wawekezaji kuja nchini, siyo lazima awafuate," alisema Lipumba.

Hata hivyo, jithada za kuwapata wasemaji wa Ikulu na Wizara ya fedha kuzungumzia shutuma hizo hazikuzaa matunda jana. Simu ya Waziri wa Fedha, Zakia Meghji ilikuwa imefungwa wakati Mwananchi ilipojaribu kumpigia ili atoe ufafanuzi jana jioni.

Lakini mtu aliyepokea simu katika Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alisema bosi wake alikuwa ameitwa na Waziri Mkuu kwa ajili ya mazungumzo ya kiofisi jana jioni.

Hata hivyo, Rais Kikwete aliwahi kujibu katika siku za nyuma kuwa safari zake nje ya nchi zina manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa mbali na kuwavuta wawekezaji, zinasaidia kujenga uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali anayoyatembelea.

Katika hatua nyingine, Lipumba ameubeza mpango wa kuondoa umaskini nchini kwa kuwapa mikopo wajasiriamali kupitia benki na saccos, akidai kuwa utekelezaji wake umefanyika kisiasa zaidi kuliko kitalaam.

Lipumba alisema mpango huo una kasoro nyingi na umeanzishwa kuifanya serikali ionekana kuwa inawajali wananchi wake, badala ya kuanzishwa katika misingi ya kuwasaidia watu waondokane na umaskini.

Alisema inashangaza kuona Rais anajigamba kupambana na umaskini kwa kutoa Sh21 bilioni kuwakopesha wajasiriamali wakati fedha hiyo itawasaidia wajasiriamali 60,000 kati ya nguvu kazi katika sekta isiyo rasmi yenye Watanzania milioni 17.

"Hili ni tone dogo sana katika bahari ya umaskini wa Watanzania, isitoshe masharti yanayoambatana na upatikanaji wa fedha hiyo ni ya kisiasa na yameleta ubaguzi mkubwa katika jamii," alisema Lipumba.

Alisema kwa kuwa zimetokana na fedha za walipakodi, fedha hizo hazikutakiwa kutolewa kwa masharti ya kupitishwa na serikali ya mtaa au kata, ofisi ambazo chama chake kimepokea taarifa kuwa imewabagua mashabiki na wapenzi wa vyama ambavyo havina mwakilishi katika serikali inayohusika na uchambuzi wa mikopo hiyo.

Alisema kushindwa kwa benki za NMB na CRDB kufikia malengo ya kutoa mikopo hiyo, kumetokana na urasimu uliojitokeza katika zoezi la upatikanaji wa fomu na mikopo yenyewe na akataka kufanyiwe marekebisho ya msingi kutoa mwanya kwa wananchi wengi kunufaika na mikopo hiyo.

"NMB inayotarajiwa kutoa mikopo ya Sh15.5 bilioni mpaka sasa imeshatoa chini ya asilimia 9.2 ya fedha hizo na ikienda kwa kasi hiyo, bajeti ya 2007/2008 itapitishwa na NMB itakuwa haijatoa hata robo ya mikopo inayotarajiwa kutoa," alisema Lipumba.

Kuhusu mlipuko wa homa ya bonde la ufa, Lipumba aliilaumu serikali kwa kushindwa kuudhibiti ugonjwa huo kabla haujaingia nchini wakati taarifa zake zilianza kupatikana tangu mwaka 2002.

Alisema bonde la ufa ni ugonjwa ambao serikali ilijua uwezekano wa kuingia nchini tangu wakati huo baada ya Shirika la Chakula Duniao (Fao) kusambaza waraka kuzitaka nchi za pembe ya Afrika kujihadhari nao.

"Mara baada ya tahadhari hii kulitokea mlipuko wa ugonjwa huo kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa kuzingatia yaliyotokea mwaka 1997/1998, serikali ya Tanzania ilipaswa kutambua kwamba Tanzania pia inaweza kuathirka na kuchukua tahadhari za kujikinga," alisema Lipumba.

Alisema mlipuko wa ugonjwa wa bonde la ufa unashughulikiwa kisiasa badala ya kisayansi kwani hata wazairi wa mifugo Anthony Diallo aliwataka wananchi wasifadhaike kutokana na mlipuko wake akidai kuwa serikali imeshachukua hatua madhubuti wa kuutokomeza jambo ambalo siyo sahihi.

Lipumba amewataka wanasiasa hasa walioko katika serikali ya awamu ya nne kujifunza kuwasikiliza na kutekeleza ushauri wa wataalamu badala ya kung'ang'ania utaratibu wa kutunga sera kwenye majukwaa ya siasa jambo ambalo linaididimiza nchi

Source: Mwananchi Communication Limited 4/4/2007
 
Utangulizi
Ndugu Wananchi;

Leo katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi huu wa Machi, nitazungumzia mambo mawili. Nayo ni: Utoaji mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo na hali ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa na jitihada tunazozifanya kukabiliana nao.

Ndugu Wananchi;

Kabla ya kufanya hivyo, napenda kuitumia nafasi hii kutoa mkono wa heri na pongezi kwa ndugu zetu Waislamu na Wakristo hapa nchini. Kwa Waislamu nawatakia heri na fanaka tele katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W. Na kwa ndugu zao Wakristo nao nawatakia heri na fanaka tele katika sikukuu ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya mateso, kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo.

Wakati nikiwatakia heri katika sikukuu hizi muhimu kwetu sote Watanzania, napenda kusema kuwa naungana nanyi katika sherehe hizo. Ni matumaini yangu kuwa sherehe hizo zitakuwa tulivu na salama. Napenda kuwahakikishia kuwa vyombo vyetu vya usalama vitafanya kila linalowezekana kulinda usalama wa Watanzania na mali zao wakati wote wa sherehe hizi.



Mikopo ya Uwezeshaji Wajasiriamali
Ndugu Wananchi;

Mwezi Januari mwaka huu Serikali ilianza kutekeleza mpango wake wa mikopo ya uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo wadogo nchini. Mpango huo unalenga kuwasaidia wananchi wa kawaida waweze kupata mikopo kwa masharti nafuu.

Shabaha yetu ni kuwa, kupitia mikopo hiyo wakopaji wataweza kuanzisha au kuendeleza shughuli za uzalishaji mali na huduma ambazo zitawapatia kipato zaidi na hivyo kuinua hali zao za maisha na kupunguza umaskini. Mikopo hiyo itawasaidia wananchi vijana na wanawake waweze kupata ajira kwa njia ya kujiajiri wenyewe.

Ndugu Wananchi;

Katika utekelezaji wa mpango huu, tuliamua kuwa kazi ya kutoa mikopo kwa niaba ya Serikali itafanywa na Mabenki ya Biashara, Benki za Wananchi na Asasi zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo. Kwa ajili hiyo Benki za Biashara za NMB na CRDB ziliteuliwa pamoja na Benki za Wananchi za Dar es Salaam, Mwanga na Mufindi na Benki ya Posta. Kadhalika asasi zinazotoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wadogo wadogo nazo zitahusishwa. Mpaka sasa shilingi bilioni 10.5 zimekwishatolewa kwa mabenki ya NMB na CRDB, kila moja ikipata shilingi bilioni 5.25. Shilingi bilioni 10.5 zilizosalia za kupewa Benki za Wananchi, Benki ya Posta na asasi zinazotoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wadogo bado hazijatolewa. Benki Kuu inaendelea kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wa fedha zilizopokelewa benki za NMB na CRDB maelewano yalikuwa kwamba benki hizo zitatoa na kukopesha fedha yao ambayo itakuwa mara tatu ya zile walizopewa na Serikali. Kwa ajili hiyo basi benki hizo zitakopesha shilingi bilioni 31 badala ya zile shilingi bilioni 10.5 tu zilizotolewa na Serikali. Zile fedha za Serikali zitabakia kama dhamana kwa mikopo itakayotolewa na mabenki hayo.



Mafanikio Yameanza Kupatikana

Ndugu Wananchi;

Tayari Benki za NMB na CRDB zimeanza kutoa mikopo kwa wananchi mmoja mmoja na vyama vya kuweka na kukopa. Kwa mfano, hadi kufikia tarehe 23 Machi, 2007 benki ya NMB ilikwishatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.419 kwa mikoa yote ya Tanzania Bara isipokuwa Ruvuma na Rukwa. Katika zoezi hilo waombaji 2,013 nchini kote wamepatiwa mikopo.

Kwa upande wa Benki ya CRDB kiasi cha shilingi 397,660,000 kilikuwa kimeshakopeshwa kwa SACCOS nane zenye wajasiriamali 1,160. Wakati huo huo shilingi 725,660,000 za kukopeshwa SACCOS tatu zenye wajasiriamali 1,441 zilikuwa zinasubiri kibali cha Makao Makuu ya Benki hiyo.

Ndugu Wananchi;

Watu wengi binafsi, vikundi vingi na SACCOS nyingi zimejitokeza kuomba mikopo. Benki ya NMB imepokea jumla ya maombi 59,974 yenye thamani ya shilingi bilioni 105.2. Benki ya CRDB nayo imepokea maombi yenye thamani ya shilingi 8,070,382,,000 kutoka SACCOS 42 zenye wajasiriamali 17,454.

Ni wazi kuwa thamani ya maombi yaliyopokelewa na Benki ya NMB ni kubwa zaidi, kwa takriban mara saba, ikilinganishwa na shilingi bilioni 15 zilizotengwa na benki hiyo kwa ajili ya mikopo ya uwezeshaji katika awamu ya kwanza ya utekelezaji.

Ndugu Wananchi;

Kutokana na maombi kuwa makubwa kuliko uwezo uliopo Benki hiyo imeamua kusitisha upokeaji wa maombi mapya ya mikopo. Wameamua kuwa kwa sasa wafanye kazi ya kushughulikia maombi yaliyokwishapokelewa ambayo nayo hawataweza kuyatosheleza yote.

Naamini sababu zao ni za msingi kabisa kwani hakuna maana kuendelea kupokea maombi mapya wakati hata yale waliyonayo yamekwishazidi uwezo wao. Benki ya CRDB ndiyo bado ina uwezo wa kuendelea kupokea mikopo. Wao hawajafikia ukomo wa fungu lao walilotenga.

Ndugu Wananchi;

Taarifa zinaonyesha kwamba baadhi ya mikoa imeweza kuwasilisha maombi mengi na kuna baadhi ya wilaya hakuna maombi yaliyowasilishwa kabisa. Wakati mabenki yanaendelea kupitia maombi waliyopokea Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu zoezi hili ili kuhakikisha kuwa malengo yetu kwa kila mkoa kupata mgao wake wa mikopo yanatimizwa.

Vile vile, tutazungumza na mabenki ili kutafuta njia za kuhakikisha kuwa wananchi wa zile wilaya ambazo wanachelewa kuwasilisha maombi hawapotezi kabisa fursa hii. Serikali pia, itajaribu kuzungumza na mabenki ili kuona namna ya kuhudumia SACCOS katika wilaya ambazo benki ya CRDB haipo na NMB haitakuwa tayari kufanya hivyo.



Malalamiko na Matatizo

.Ndugu Wananchi;

Natambua kuwepo malalamiko na matatizo kadhaa kuhusu mikopo ya wajasiriamali ambayo ningependa kuyazungumzia leo. Kwa mfano, nilipokuwa wilayani Ngorongoro wiki chache zilizopita wananchi wa wilaya hiyo walitaka kujua hatima yao itakuwaje kwani watu wote wamechelewa kuwasilisha maombi ya mikopo wakati Benki ya NMB inasimamisha kupokea maombi mapya. Nilitoa majibu ambayo ningependa kuyarudia tena leo kwa manufaa ya wilaya zenye matatizo kama haya.

Ni makusudio ya Serikali kuona kuwa watu wa kila mkoa na kila wilaya nchini wanapata mikopo hiyo. Hivyo basi, pamoja na Benki ya NMB kusimamisha kupokea maombi kwa sasa, hapana budi utaratibu ufanywe ili, wilaya ambazo wananchi wake hawakuwahi kuwasilisha maombi ya mikopo nao wapate fursa hiyo.

Haiwezekani na wala haikubaliki kuwepo wilaya hata moja nchini ambayo watu wake hawatapata fursa ya kupata mikopo hii. Ikitokea hivyo dhamira ya kuanzisha mpango wa mikopo hii nchini itakuwa haikufikiwa.

Ndugu Wananchi;

Kumekuwepo pia malalamiko kuhusu utaratibu wa kupokea maombi, kuyashughulikia na kutoa mikopo. Zipo hisia kuwa utaratibu ni mgumu mno, mlolongo ni mrefu na kwa sababu hiyo kuna usumbufu na inachukua muda mrefu mno kwa mtu kupata mkopo.

Ni jambo jema kuwa na utaratibu wa kufanya mambo lakini ni vyema utaratibu ukawa rahisi na kwamba haichukui muda mrefu kutekeleza jambo. Hatuna budi basi kuuangalia upya utaratibu wetu wa sasa na kufanya marekebisho pale panapostahili ili mambo yaende vizuri. Yaani, iwe rahisi kwa waombaji kuomba na ichukue muda mfupi kwa waombaji kupata majibu na kupewa mikopo kwa wale watakaokubaliwa.



Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;

Pamoja na kusema hayo sina budi kusisitiza kuwa baadhi ya taratibu zilizowekwa ni muhimu kuwepo. Zina manufaa yake. Kwanza, zinasaidia kuhakikisha kuwa mikopo inawafikia walengwa. Hii ni mikopo ya raia Watanzania na ni mikopo ya maskini ili kuwawezesha wainue hali yao ya maisha. Si mikopo ya matajiri, wao mabenki yapo, tena yamejaa mabilioni ya fedha zinazosubiri wakopaji kama wao wawapatie.

Pili, taratibu hizo zinasaidia kuhakikisha kuwa fedha zilizokopeshwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na mikopo inalipwa. Mathalan, itasaidia kuhakikisha kuwa mtu aliyeomba mkopo wa kulima bustani ya nyanya hatatumia pesa hizo kumalizia nyumba yake au kulipia ada ya mwanae. Ni mambo ya maana, lakini siyo makusudio ya mkopo. Kama watu wataachwa wafanye hivyo mikopo haitalipwa na mtaji huu wote utakufa. Tukifikia hali hiyo dhamira yetu ya kuwa na utaratibu endelevu haitafikiwa. Itakuwa ni hasara kubwa ambayo ni lazima tuhakikishe kuwa hatufiki hapo.



Utaratibu Uzingatiwe

Ndugu Wananchi;

Utaratibu wa kuomba na kutoa mikopo unasisitiza mambo makuu yafuatayo: Kwanza, sharti muombaji awe na mradi unaokopesheka. Mwombaji awe na shughuli ya uzalishaji mali au utoaji huduma anayoiombea mkopo. Shughuli hiyo lazima ithibitike kuwa inafaa kupewa mkopo kwa kupitia taratibu zilizowekwa.

Pili, muombaji apitishe fomu zake za maombi kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa au Kijiji atakapofanya hiyo shughuli ili wamtambue na wautambue mradi.

Tatu, maombi yachambuliwe na Kamati ya Maendeleo ya Kata. Kamati hiyo itatoa maombi yake kabla maombi hayo hayajawasilishwa Benki kwa uamuzi wa mwisho.

Kwa upande wa SACCOS wanachama wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa uongozi wa SACCOS yao kwa uchambuzi. Uongozi wa SACCOS ukiridhika huwasilisha maombi hayo kwa Afisa Ushirika wa Wilaya ambaye huthibitisha uhai wa SACCOS hiyo. Baada ya hapo uongozi wa SACCOS huwasilisha maombi hayo benki kwa uamuzi.

Ndugu Wananchi;

Wamekuwepo pia watu wanaolalamika kuwa kiasi cha fedha kinachotolewa katika mikopo hii ni kidogo mno na kwamba riba ya silimia 10 ni kubwa mno. Ni kweli kiasi kinachokopeshwa, yaani kati ya shilingi 50,000 na 5,000,000 si kikubwa lakini imefanywa hivyo kwa makusudi. Hii ni mikopo ya watu wenye kipato cha chini ambao katika hali ya kawaida benki haziwakopeshi. Maskini hakopesheki benki. Hana dhamana ya kukubalika na benki na wala hana uwezo wa kulipia gharama za kuombea mkopo.

Ndugu Wananchi;

Kwa kutambua ukweli huo na kwa nia ya kutaka kuwawezesha wananchi wenye vipato vya chini kupata mikopo ili na wao waanze safari ya kuelekea kwenye maisha bora, ndipo Serikali ilipoamua kuanzisha mpango huu wa mikopo. Hakuna sharti la kuwa na dhamana kwa wakopaji na wala hawalipi ada ya kuomba mkopo. Serikali imebeba mzigo huo. Fedha iliyotolewa na Serikali kwa benki ndiyo dhamana, na ndiyo inayofidia gharama za kuchukua fomu za maombi na za kushughulikia maombi.

Ndugu zangu;

Ni kweli kabisa kwamba ingekuwa vizuri kama mikopo hii ingekuwa haina riba yoyote. Tena lingefurahisha wengi na hususan wale ambao kiimani riba ni jambo haramu. Suala la kutokuwepo riba, lilizungumzwa kwa kina lakini lilikuwa gumu kulitekeleza. Sababu ya msingi ni gharama nyingine za kibenki zilizobaki hata baada ya Serikali kubeba mzigo wa dhamana na gharama za kuomba mkopo.

Ndiyo maana mikopo hii ina riba. Hata hivyo, ndugu zangu, ukilinganisha na riba ambazo kwa kawaida huwa zinatozwa na mabenki haya kwa mikopo ya namna hiyo riba inayotozwa kwa mikopo hii bado ya chini.

Vile vile unapolinganisha na riba inayotozwa na asasi za fedha zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, riba inayotozwa kwa mikopo hii bado ni nafuu sana. Nyingi ya asasi hizo hutoza riba ya zaidi ya asilimia 30 na nyingine hufikia hata asilimia 40 au zaidi.

Ndugu Wananchi;

Nimeyaeleza haya kujaribu kufafanua baadhi ya mambo yanayoleta utata katika utaratibu mzima wa mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo. Sikuyamaliza maswali yote waliyokuwa nayo wananchi, naamini tutapata fursa siku zijazo kuyafafanua. Lakini pia, viongozi wenzangu taifani, mikoani na wilayani watasaidia kuyafafanua. Waendeeni, waambieni. Watafurahi kuwasaidia kwani ni wajibu wao.

Ndugu Wananchi;

Nauona mpango wa mikopo ya wajasiriamali kuwa ukombozi wa wanyonge. Kila kitu kina changamoto zake. Kuwepo kwa changamoto kusitukatishe tamaa bali kutuongezee ari ya kutafuta mbinu na maarifa ya kuzishinda. Maombi yangu kwa wadau wote ni kuwepo na ushirikiano miongoni mwetu. Pawepo na mawasiliano ya urahisi miongoni mwa wadau ili tatizo linapotokea habari ziwafikie wahusika kwa wakati. Naomba sote tushirikiane na tushikamane kwa dhati katika kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa kutimiza malengo yake.

Tuhakikishe kuwa taratibu zilizowekwa zinafuatwa lakini urasimu na ucheleweshaji usiokuwa wa lazima unaepukwa. Pia tuhakikishe kuwa mikopo inatumika kwa shughuli iliyokusudiwa na inarejeshwa kwa wakati ili na wengine nao waweze kukopeshwa. Tukiyazingatia na kuyafanya haya tutakuwa tumejenga msingi mzuri wa kuwapatia Watanzania wa kawaida fursa ya kubadili maisha yao kuwa mazuri zaidi kuliko yalivyo hivi sasa.

Ndugu Wananchi;

Naomba nimalizie mazungumzo yangu kuhusu mikopo kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu tunaotaka mikopo kuwa na moyo wa subira. Muda utahitajika tangu mtu awasilishe maombi mpaka atakapopata. Hatuna budi kulitambua hilo na kuwa na subira nalo.

Lakini, kubwa zaidi ni ule ukweli kwamba si kila mmoja aliyeomba mkopo atapata wakati huo huo. Kama tulivyoona maombi ni makubwa kuliko fedha iliyopo. Kwa vyovyote vile, wapo watakaopata mwanzo na wapo watakaopata baadaye baada ya wale wa mwanzo kuanza kulipa.

Nawasihi Watanzania wenzangu tuutambue ukweli huo na kuukubali, ndiyo maana nawasihi tuwe na moyo wa subira. Kutaka wewe uwe wa mwanzo ndiyo ubinadamu, lakini ni vyema kutambua kuwa kwa hali ilivyo unaweza usiwe wa mwanzo. Ikitokea hivyo kubali na endelea kusubiri. Utaratibu huu ni endelevu. Si wa mara moja.



Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa

Ndugu Wananchi;

Nchi yetu hivi sasa imekumbwa na tatizo la ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa yaani kwa Kiingereza Rift Valley Fever au kwa kifupi RVF. Ni ugonjwa hatari unaoua wanyama na binadamu pia.

Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa wa mifugo na mwanadamu hupata maradhi hayo kwa kula nyama ya mnyama aliyeathirika.

Vile vile mnyama na mwanadamu wanaweza kupata maradhi kwa kuumwa na mbu wa aina ya Aedes mwenye wadudu wa maradhi hayo.

Mbali ya kuua mifugo mingi ugonjwa huu pia umesababisha vifo vya wananchi wenzetu katika baadhi ya mikoa hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 28 mwezi huu watu 33 walikuwa wamepoteza maisha yao na wengine 119 walikuwa wameambukizwa.

Kwa upande wa mifugo mikoa ambayo imekumbwa na ugonjwa huu ni Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Singida na Mbeya. Mikoa ambayo watu wameathirika na hata baadhi yao kufariki dunia ni pamoja na Manyara, Tanga, Dodoma na Morogoro. Mikoa ya Dar es Salaam na Singida pia inao wagonjwa wachache wenye kuonyesha dalili za ugonjwa huo ambao wanaendelea kuchunguzwa.



Ndugu Wananchi;

Napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole Watanzania wenzetu wote walioathirika na ugonjwa huu hatari. Kwa wale waliotangulia mbele ya haki, tunawaomba ndugu na jamaa zao wapokee mkono wetu wa rambirambi na pole zetu nyingi. Tunaelewa machungu ya kupotelewa na wapenzi wao. Tunajumuika nao na kuomboleza nao katika wakati huu mgumu wa machungu mengi na majonzi tele. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu wetu hao rehema na azilaze roho zao mahali pema peponi.

Kwa wagonjwa wanaoendelea kupata matibabu tunawaombea wapone haraka ili wajiunge tena na familia zao na jamii nzima ya Watanzania katika ujenzi wa Taifa. Kwa wenzetu waliopoteza mifugo tunawapa pole kwa kupoteza rasilimali muhimu. Wasivunjike moyo, ndiyo mitihani ya dunia. Kuteleza si kuanguka.



Hatua Zinazochukuliwa na Serikali

Ndugu Wananchi;

Serikali inatambua uzito wa tatizo linalotukabili na inafanya kila iwezalo kutokomeza ugonjwa huu. Katika mkakati tuliouandaa hadi sasa tumechukua hatua zifuatazo:

Kwanza, tumezuia kufanyika kwa minada ya mifugo kote nchini. Hatua hii ni ya muda inayolenga katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa. Minada itaruhusiwa tena kufanya kazi pindi hali itakaporejea kuwa nzuri.

Pili, tumeimarisha utoaji wa chanjo za mifugo dhidi ya ugonjwa huu kwenye maeneo yote yenye mifugo. Hadi sasa tumeshatumia kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kununulia chanjo na vifaa vingine vya kukabiliana na ugonjwa. Tayari tumeagiza dozi milioni mbili za chanjo ya RVF. Kati ya hizo, dozi 736,600 zimeshapokelewa na kusambazwa kwenye wilaya zilizoathirika na zile zilizo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa.

Tatu, tumeandaa chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mpango wa dharura wa kitaifa wa kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa. Mpango huu utagharimu dola za Kimarekani takribani milini 12.3. Tunaendelea kuwasiliana na marafiki zetu wa nje kuhusu uwezekano wa kutusaidia kugharamia mpango huu mapema iwezekanavyo ili kunusuru mifugo yetu na maisha ya watu.

Wajibu wa Kila Mmoja Wetu

Ndugu Wananchi;

Jukumu la kupambana na ugonjwa huu ni letu sote. Kila mmoja wetu pale alipo anao wajibu wa kuhakikisha kuwa anachukua tahadhari zote muhimu zitakazosaidia katika kukabiliana na ugonjwa huu. Hivyo nawaomba tuzingatie mambo yafuatayo:

Kwanza, tuhakikishe kwamba mifugo yote inapata chanjo. Hii ndiyo kinga yetu ya kwanza ya kupambana na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa. Serikali inafanya jitihada ili kuhakikisha kwamba dozi za kutosha za chanjo zinapatikana. Hivyo nawaomba watu wote wapeleke mifugo yao ikachanjwe mapema iwezekanavyo.

Pili, tuache tabia ya kuhamisha mifugo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kiholela. Uhamishaji holela wa mifugo unachangia katika kueneza ugonjwa. Aidha, unarudisha nyuma jitihada zetu za kudhibiti ugonjwa huu hatari.

Tatu, tuepuke kuchinja wanyama na kuchuna ngozi bila kuchukua tahadhari za kujikinga. Vile vile tujiepushe na kushika damu, majimaji na nyama ya mnyama anayehofiwa kuwa na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa.

Nne, tusile nyama ya mnyama aliyekufa kwa ugonjwa huu. Inashangaza sana kusikia kuwa baadhi ya wenzetu wanadiriki kufukua mizoga iliyozikwa na kula nyama yake. Ndugu zangu, ni uchu wa kiasi gani huo unaotufanya hata tupuuze tishio kubwa kwa maisha ya mwanadamu kama hili la ugonjwa huu. Nawasihi tusikilize ushauri. Wahenga wamesema �asiyesikia la mkuu huvunjika guu�.

Tano, tuepuke kunywa maziwa yasiyochemshwa vizuri. Siku zote tuchemshe maziwa vizuri kabla ya kuyanywa.

Sita, wataalam na watendaji kwenye ngazi ya wilaya na vijiji wasimamie kwa ukamilifu utekelezaji wa Sheria ya Magonjwa ya Mifugo ili kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu.

Saba, wananchi watumie vyandarua hasa vile vilivyowekwa dawa ili kujikinga na mbu. Ndugu zangu, tukumbuke kuwa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unaenezwa pia na mbu aina ya Aedes. Hivyo kinga dhidi ya mbu ni jambo muhimu sana.

Na nane, tuongeze juhudi za kudhibiti mbu ili tupunguze kushamiri kwa mbu kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Watu wafukie mazalia ya mbu na pale inapowezekana wanyunyizie dawa.

Ndugu Wananchi;

Katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huu, vyombo vya habari vinalo jukumu kubwa la kusaidia kuelimisha umma kuujua ugonjwa na jinsi ya kujikinga nao. Nawaomba mtimize wajibu wenu huo wa msingi kwa ukamilifu. Nawashukuru kwa hatua tuliofikia sasa naomba waendelee kufanya vizuri zaidi. Nawaomba wawe na ushirikiano na mawasiliano ya karibu na mamlaka husika na hasa wataalamu husika ili kuepuka kuandika au kutangaza habari ambazo hazijathibitika.



Hitimisho

Ndugu Wananchi;

Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu atazingatia mambo ya msingi katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huu. Hususan naomba tuzingatie ushauri wa wataalam utakaoendelea kutolewa mara kwa mara. Mimi naamini kuwa kama tukiyazingatia hayo tutaweza kuzuia kuenea na hatimaye kuutokomeza ugonjwa huu hatari mapema iwezekanavyo.

Watanzania tunayo sifa moja kubwa. Nayo ni kuwa pale tunapokabiliwa na adui siku zote huwa wepesi sana katika kuunganisha nguvu zetu na kupambana nae.

Ndugu zangu, ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa ni adui hatari anayetaka kutudhalilisha na hata kutuangamiza. Naamini kama ilivyo kawaida yetu tutaunganisha nguvu zetu ili tuweze kumtokomeza adui huyu mapema iwezekanavyo.

Na, katika vita hii kila mmoja wetu analo jukumu lake la kufanya. Naomba basi kila mmoja wetu atekeleze jukumu lake ipasavyo ili tuweze kuushinda na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Homa ya Bonde la ufa. Inawezekana Timiza Wajibu Wako.



Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa Kunisikiliza.
 
Back
Top Bottom