DODOMA: Tundu Lissu ajeruhiwa kwa risasi, akimbizwa Hospitali

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,493
2,000
Wakuu,

Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, ajeruhiwa kwa risasi.

Kwa sasa wapo hospitali ya Mkoa, mjini Dodoma.

Ameshambuliwa kwa risasi wakati akishuka nyumbani kwake Area D Mjini Dodoma, alikuwa akitokea Bungeni na alienda Nyumbani kula chakula cha mchana.

Lissu amepigwa risasi 5, miguuni na tumboni.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema hali ya Mbunge huyo aliye hospitalini sasa ni mbaya!


56d494001b8e52eca1b71490ff9635e4.jpg


9f94cea0e0708e5fafb57915caf1dd27.jpg

abc21fedd617180297c6247f403b7362.jpg


=======

UPDATES:

=======

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini ameeleza jinsi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyopigwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Selasini amesema kuwa maelezo aliyopata ni kuwa alikuwa akifuatiliwa na gari tangu anatoka bungeni na dereva wake alilishtukia. Amesema kuwa alivyoona wanamfutilia alipofika nyumbani, dereva alimsihi Lissu asishuke ndani ya gari.

"Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo ni tinted na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu." amesema.

Selasini amesema, “Risasi zilimpata mguuni, mkononi na tumboni lakini daktari anasema anaendelea vizuri."

Lissu amepigwa risasi leo Alhamisi na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wabunge na viongozi wengine wa ulinzi wa Bunge wamefika katika hospitali hiyo kujua kinachoendelea.

Baadhi ya ndugu na wagonjwa wamefurika katika chumba cha upasuaji cha hospitali ya mkoa wakitafakari huku wengine wakilia.

UPDATE: Ndege imeshawasili Dodoma ili kumchukua Tundu Lissu kumpeleka Muhimbili kwa matibabu zaidi

Katibu wa Bunge amethibitisha kufika kwa ndege Dodoma kumchukua Tundu Lissu kumpeleka hospitali ya Muhimbili ili kuokoa maisha yake

DODOMA: RPC amesema watu waliomshambulia Tundu Lissu walikuwa wakitumia gari aina ya Nissan la rangi nyeupe

Freeman Mbowe: Ndugu Lissu kwa sasa yuko katika chumba cha upasuaji anajaribu kuokoa maisha yake, nitazungumza baadaye.

lissu1.jpg

UPDATES: Miongoni mwa waliofika hospitali kumuona Lissu ni Spika Job Ndugai, Waziri Ummy Mwalimu na katibu mkuu wa bunge, Dkt. Thomas Kashilila

Rais Magufuli ametoa pole na kutaka Vyombo vya Dola kuchukua hatua:

CCM imetoa pole

Waziri wa zamani, Mark Mwandosya naye ametoa pole
IMG_3724.JPG


UPDATES: 2235HRS
Ndege iliyokuja kumchukua Tundu Lissu ndo inatua Uwanja wa Dodoma. Ni ndege binafsi, imetoka Dar Es Salaam na itampeleka Mh. Lissu Nairobi Kenya kwa matibabu zaidi.
6a0df0d4014896f500bc344cb3ddcb26.jpg

TunduLissu akipakiwa kwenye ndege usiku huu tayari kwa safari ya Nairobi kwa matibabu zaidi
3c38765220348b8a8712fc343f512797.jpg


*Rais wa Chama cha Mawakili Kenya(LSK), Isaac Okero amesema Lissu amelazwa Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Lissu awasili Nairobi salama lakini Ubalozi wa Tanzania haujatoa ushirikiano

Mbowe: Hali ya Lissu ni mbaya na yupo kwenye chumba cha upasuaji

TAARIFA YA AWALI KUHUSU SHAMBULIO LA KUPIGWA RISASI MHE. TUNDU LISSU

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kupigwa risasi Mwanasheria Mkuu wa Chama ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Tundu Antipus Lissu baada ya kikao cha Bunge mchana wa leo.

Shambulio hilo limetokea majira ya mchana nyumbani kwake Area D Dodoma na kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hosiptali ya Mkoa wa Dodoma.

CHADEMA tunalaani vikali kitendo hicho, na tunafuatilia kwa karibu hali yake.

Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Imetolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje.

CHADEMA MAKAO MAKUU

DAR ES SALAAM.

=====

Preliminary Press Statement on the incidence of Hon. Tundu Lissu being shot

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) has received with great shock the report on the shooting of the Attorney General of the Party who is also the Chief Whip of the Official Opposition in Parliament and MP of Singida East, Hon. Tundu Antipus Lissu just after a Parliamentary session today.

The attack took place at his Dodoma residence at midday and was seriously wounded and had been rushed to the Dodoma Regional Hospital.

CHADEMA strongly condemns this act, and we are following up closely on his condition.

We will continue to update as we get more information.

Issued by the Directorate of Ideology, Publicity, Communications and Foreign Relations.

=====

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 hadi 32, huku tano zikimpata mwilini.

Lissu alishambuliwa jana Alhamisi kabla hajashuka kwenye gari baada ya kumaliza kikao cha Bunge na alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa saa sita usiku, kuelekea Hospitali ya Aga Khan ya Nairobi, Kenya.

Akitoa taarifa ya tukio hilo kwenye kikao cha Bunge leo Ijumaa, Ndugai amesema risasi mbili zilimpata Lissu kwenye miguu, mbili tumboni na moja kwenye mkono.

Amesema watu wasiofahamika wakiwa kwenye gari aina ya Nissan ambalo halijajulikana walimpiga risasi kisha kutoweka.

“Baada ya tukio hilo watu hao walikimbia,” amesema Ndugai. Alisema Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kuwa wanaishi jirani.

“Alipofika hospitali aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji ili kuzuia damu kuendelea kutoka katika majeraha aliyokuwa ameyapata,” amesema Ndugai.
Amesema upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya akishirikiana na madaktari wengine.

“Baada ya upasuaji tulielezwa kuwa hali yake iliendelea kutengemaa na anaweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi,” amesema.

Ndugai amesema ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ilishaandaa ndege saa 10:30 jioni kwa ajili ya kumchukua mgonjwa na kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hata hivyo, amesema baada ya kushauriana na familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe waliona ni vyema mgonjwa huo apelekwe katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

“Hivyo kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge ilipatikana ndege nyingine ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa saa sita usiku, kuelekea Nairobi,” amesema.

Amesema tukio hilo liliripotiwa polisi ambako waliahidi kufanya msako kuwatafuta wahalifu hao na Serikali itatoa taarifa kamili kwa kuzingatia utaratibu wa kibunge.

Spika Ndugai amesema tukio hilo ni la kwanza la aina yake tangu Bunge lilipohamia Dodoma na kwamba, haijawahi kutokea mbunge akashambuliwa kwa risasi.

Amesema pia haijawahi kutokea tukio la aina hiyo wakati Bunge likiendelea na vikao, hivyo amewaomba Watanzania kuwa na subira wakati vyombo vya dola vikiendelea na kazi.

“Utaratibu wetu wa kibunge wa matibabu ambao ndiyo utaratibu wa Watanzania wote, baada ya mwenzetu kupata tatizo hili tulikuwa tumeshaagiza ndege kumpeleka Muhimbili,” amesema.

Amesema ingekuwa anatakiwa kusafirishwa nje, Serikali ina mkataba na Hospitali ya Apollo ya India na kwamba, Lissu amepelekwa Nairobi kwa sababu familia imeomba.

“Lakini kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi, ni kwa sababu familia iliomba. Nimnukuu Mheshimiwa Mbowe kwa niaba yake si kwamba wana shaka na umahiri na uwezo wa madaktari wetu,” amesema.

Amewataka Watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo katika kipindi hiki kigumu.

Amewashauri wabunge walioanza kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kutumia maneno ya hekima badala ya kuendelea kuchonganisha pande mbili.

Habari zaidi, soma=>Ubelgiji: Tundu Lissu aruhusiwa kutoka Hospitalini
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom