Swali zuri sana Da Hustla! Unajua kwa Marekani ilikuwa ni kama "kumtupa jongoo na mti wake kabisa!!!" Weusi wa Marekani waliuona Ukristo ni kama dini ya mkandamizaji, dini ya mbaguzi na hivyo wanamapinduzi wa mrengo mkali waliususa na kutafuta mbadala wake. Waliokuwa mstari wa mbele wakaanza kuukimbia kwanza utamaduni wa mtu mweupe na kuyachukua majina ya Kiafrika. Leroi Jones akawa Imamu Amiri Baraka, zikazuka shule kwa mfano mmoja iliitwa "Ujamaa Shule" (iliyoko1554 8th Street, NW, Washington, DC 20001) , weusi wakabuni sherehe yao iliyoitwa "Kwanzaa" (inayotumia falsafa ya Kiafrika tena kwa Kiswahili - kwa mfano kudumisha umoja, kujichagulia, imani, nia); na mengine kundi kubwa la Wamarekani weusi likahamia Ghana moja kwa moja. Nakumbuka hata lilikuwepo genge la wahuni Wamarekani weusi likijiita "Mau Mau." Hapo ndipo Elijah Muhammad naye akaanzisha dini ya Weusi tofauti na ile ya wababe wao (Ukristo) na kuuiita Taifa la Kiislamu (Nation of Islam), wakiuona Uislamu kama ni dini ya watu wengineo zaidi ya Wazungu wa kwao. Ndipo akina Cassius Clay wakajiunga na Taifa la Kiislamu na kubadili majina na kuwa Muhammad Ali, Malcolm X akawa Abdul Malik Al Shabbaz wengi wakafuata na kuyaacha majina yao na kuyachukua ya Kiislamu. Tukawasikia akina Maulana Karenga (zamani Ronald McKinley Everret), hata NBA ikawapata akina Kareem Abdul Jaabar (zamani akiitwa Ferdinand Lewis Alcindor). Kwangu huo ulikuwa ni ususaji wa mambo ya mkandamizaji katika nyanja ya kidini na utamaduni. Tumeiona hiyo India wakati Mohandas Karamchand Gandhi alipowaongoza Wahindi kususia nguo kutoka Uingereza na kuanza kufuma za kwao hadi leo wanapendeza sana wakivaa nguo zao. Unaweza kuyaita mapinduzi ya kiutamaduni na ya kiimani. Uislamu ulikuwa karibu sana kama dini mbadala isiyokuwa na mizizi ya kimagharibi. Kule Afrika Kusini aliishi mwanaharakati na mwandishi aliyeitwa Peter Abrahams. Ameandika vitabu kama vile "Mine Boy," "Tell Freedom" na "A Wreath for Udomo." Huyu aliususia Ukristo baada ya kuingia kanisani katika mji mmoja ukubwani mwake na kuhamishwa asikae viti vya mbele kwani vilitengwa kwa ajili ya weupe wa huko. Alipoinuka na kutoka nje hakurudi tena kanisani akawa Mkomunisti mpaka alipokufa muongo mmoja ama miongo miwili iliopita. Naye aliususa Ukristo wa Kaburu na kuupokea Ukomunisti uliokuwa ukikataa imani ya kidini. Ni ile ile kutupa jongoo na mti wake kabisa.