Wakati wangu wote niliokuwa hapa Nairobi Kenya kwa mapumziko ya sikukuu, nimekuwa mzito kumtembelea Tundu Lissu mara kwa mara. Naona soni. Soni ya kumtazama steringi wa demokrasia, siasa, na utawala wa sheria akiwa amelala kitandani. Anazungumza hadi anaumiza. Anauliza hadi analiza. Nimekwenda mara mbili tu tangu nifike tarehe 20 mwezi huu.
Amini nawaambia, Lissu ni steringi wa mambo ya siasa, demokrasia na utawala wa sheria. Amesema kwa kukosoa walipokosea. Ameonya hatari za mambo mbalimbali ya kisheria na kidemokrasia jkwa mustakabali wa nchi yetu. Amesema waziwazi hadi kuitwa mnazi. Amesema nje na ndani ya Bunge. Ametetea, ameunga mkono na kupigania anachokiamini. Who else?
Tarehe 20 Januari, 1968 alizaliwa. Akakua. Akapambana kimaisha, kimasomo, kisiasa na kadhalika. Mwaka huu, akashambuliwa. Akaanguka asijitambue. Akabebwa asijijue. Akatibiwa asigundue. Akalala kitanda cha wagonjwa hapa Nairobi kwa siku 101. Hatimaye, amesimama tena. Amesimama kuelekea kutembea. Kutembea kwenda mapambanoni tena. Stay alive!
Lissu atatikisa, atayumbisha na kugeuza mambo. Wanaoonekana kusambaratika, wataimarika. Kuanzia mapokezi yake atakaporejea (ambayo tayari yameshaanza kuratibiwa huku akiendelea kutibiwa), mambo yatanoga hadi kutia woga. Ataimarisha panapomuhitaji na kupandisha kujiamini, kusema na kujenga hoja kwa wale wanaomuamini. Steringi wa siasa za kisasa atarudi kumalizia picha yake.
Lissu ananihuzunisha, ananiimarisha na, kama mwanaCCM, ananitisha. Haachi kusoma hata kitandani. Haachi kusema mtu akiingia ndani. Haachi kufikiri na kukariri. Haachi kutafiti ili kujiweka fiti. Haachi kuponda na kupenda. Haachi kupanga na kupangua kwa kujua. Haachi kutabiri kwa umahiri. Ni wa kipekee.
Nawatakieni mwaka mpya mwema wa 2018 ambao utakuwa na Lissu tena!
Mzee Tupatupa wa Lumumba (kwasasa Nairobi, Kenya)