Uchaguzi 2020 Yaliyojiri kwenye kampeni za Mgombea Urais wa CHADEMA, Tundu Lissu mkoani Iringa & Njombe, atoa pole kwa Vifo 10, Kwanini Chato ni agenda ya Uchaguzi

CHADEMA

Verified Member
Apr 13, 2013
468
1,000
Wakuu kumekucha tena, na kwa kweli muda ni mfupi mno, tuendelee kuvumiliana kwa kero zetu za kampeni. Leo tena kipenzi cha Watanzania Rais mtarajiwa Mh Tundu Lissu anawasili Mkoani Njombe kwa lengo la kueneza sera nzuri mno za CHADEMA , ikiwa ni pamoja na kuomba kura kwa mabosi wake ambao ni wananchi , basi kwa heshima na taadhima nakuombeni tuendelee kubaki hapa hapa kwa taarifa zaidi.

=========

LISSU: Naomba nizungumze habari ambayo leo Rais wetu ameizungumza pale kijijini kwake Chato. Amesema kwamba huyo mtu aliokula ugali akashiba anachikiona ni Chato tu, kwanini hahoji viwanja vingine ambavyo tumevijenga akataja Singida, Songea, Shinyanga, Dodoma na vingine vingi.

Nimezungumza Chato sana, naomba nifafanue kwanini Chato lazima iwe kelele.

Uwanja wa Chato ni tofauti na viwanja vingine vyote, tofauti yake ni hii, Chato ni kijiji wala sio mji. Karibu na Chato kuna kamji kakubwa kanaitwa Katoro hakana uwanja wa ndege, mbele kuna mji mkubwa wa Geita, hakuna uwanja wa ndege.

Sasa kwanini Chato? Ni kwa sababu mija tu, Magufuli ni Rais ndio maana kuna uwanja wa ndege Chato. Mwaka 97 wakati Mkapa akiwa Rais ilitungwa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, inasema kiongozi wa umma hapaswi kutumia mamlaka yake ya umma kwa manufaa yake binafsi.

Kiongozi wa umma wa kwanza ni Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, tujiulize manufaa ya umma ya uwanja wa ndege wa Chato ni yepi?

Hizi ndege nyingi alizonunua anazotutambia nazo hakuna hata moja inayokwenda Chato. Hakuna abiria hata mmoja anaekwenda Chato, mtu pekee anaekwenda Chato ni Rais Magufuli na nimesema na mama yake wala sio uongo, na ndugu zake.

Uwanja wa Chato umeharibu mabilioni ya shilingi za kitanzania, ni mfano wa kwanza wa jinsi ambavyo watu wenye mamlaka ya umma wanaweza kutumia mamlaka yao vibaya.

Instagram media - CFGqBANpYup ( 741 X 640 ).jpg

=======
UPDATES
Hapa ni jimbo la Makambako Mkoa wa Njombe


LISSU IRINGA & NJOMBE; SALAAM ZA POLE VIFO VYA WANAFUNZI 10, MWAROBAINI WA MATATIZO YA WATANZANIA NA KWANINI ‘CHATO’ NI AGENDA KATIKA UCHAGUZI MKUU 2020

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mhe. Tundu Antiphas Lissu ametoa salaam za pole na rambirambi kufuatia vifo vya wanafunzi 10 wa Shule ya Byamungu Islamic, iliyoko Kyerwa, mkoani Kagera, kwa ajali ya moto iliyotokea usiku wa kuamkia leo, huku akitoa wito kwa vyombo vinavyohusika na masuala ya uchunguzi wa matukio ya namna hiyo, kufanya kazi yake kwa haraka ili kubaini sababu ya moto huo ambao pia ulijeruhi wanafunzi wengine kadhaa.

“Natoa pole kwa wote walioguswa na msiba huo mkubwa wa vifo vya wanafunzi wetu 10. Taarifa za awali zimesema wengine kadhaa pia wamejeruhiwa. Pole sana kwa wazazi. Tuwaombee pumziko la amani watoto hao. Tumezoea kusema kusema kuwa Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa…lakini kuna vitu vingine vinahitaji uchunguzi ili tujue. Wakati mwingine unakuta ni mikono au uzembe wa binadamu. Hivyo vyombo vilivyopewa mamlaka ya kuchunguza matukio ya namna hii vifanye uchunguzi wa haraka, visaidie kupatikana kwa majawabu sahihi,” amesema Mhe. Lissu.

Aidha, Mhe Lissu amesema mwarobaini wa matatizo mengi yanayowasumbua Watanzania, kuwanyima uhuru wao, haki zao na kukwamisha maendeleo yanayohusu maisha na hali zao ni mfumo mpya wa utawala na siasa ambao msingi wake utakuwa Katiba Mpya ya Nchi, kazi ambayo ameahidi ataanza nayo ndani ya siku 100 za uongozi wake, akichaguliwa kuwa Rais, Oktoba 28, mwaka huu.

Amesema mfumo huo mpya wa utawala unaozungumziwa kwenye Ilani ya Chadema ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, utahusisha ugatuaji mkubwa wa madaraka ili kuwapatia mamlaka wananchi ya kujitawala na kuongozwa katika kujiamulia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa rasilimali zinazopatikana mahalia, ili utajiri unaotokana nazo, uwanufaishe kwanza wao na kuboresha ustawi wa maisha yao ya kila siku, badala ya mfumo wa sasa ambao umetoa fursa ya watawala kuhodhi na kujilimbikizia nguvu za kuamua kila kitu kinachomgusa mwananchi mmoja mmoja na kuwahusu Watanzania wote, kutokea makao makuu ya nchi.

Mhe. Lissu ameyasema hayo leo alipozungumza na wananchi wa maeneo ya Mdabulo (Mufindi), Mafinga mjini, mkoani Iringa na Mji wa Makambako, Mkoa wa Njombe, akiwa katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu ambapo amesema mfumo mpya wa utawala na siasa ambao msingi wake utawekwa katika Katiba Mpya, utawasaidia wao kunufaika na utajiri wa rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao, hasa mazao ya chai na mbao ambayo, kutokana na utaratibu mbovu wa utawala wa sasa, hawanaufaiki nazo na wala hazijawa nyenzo imara za kuboresha fursa za kujiletea maendeleo.

“Leo nimeanzia mikutano yangu huko Mdabulo, Mufindi kisha nikaenda Mafinga na sasa niko hapa Makambako, mojawapo ya suala kubwa ambalo nimebaini ni namna ambavyo wananchi wa maeneo haya hawajanufaika kabisa na rasilimali na utajiri mkubwa unaopatikana katika maeneo haya, hasa mazao ya mbao na chai. Nimepita katika maeneo hayo na kushuhudia utajiri mkubwa lakini watu wake ni maskini. Barabara tu ni mbovu kweli kweli na hata bila kuambiwa ninaweza kusema kuwa wakati wa mvua, barabara zile hazipitiki kabisa. Chai na mbazo kutoka Mufindi zingetosha kusaidia wananchi hao kuwa na barabara nzuri, hospitali, zahanati, shule bora na huduma zingine mbalimbali katika ubora unaotakiwa kuboresha maisha ya watu wetu.

“Nimewaambia kwa utaratibu wa mfumo mbovu wa utawala na siasa wa sasa ambapo kila kitu kinaamuliwa kutoka Dar es Salaam au Dodoma, mnaletewa Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi wa Maendeleo hapa ambaye hamna mamlaka naye, hamwezi kumwajibisha, hamkumchagua. Mapato ya mbao na chai zenu na hata matumizi yake hampangi ninyi huku, yanapangiwa Dar es Salaam au Dodoma, kwa utaratibu huu hatuwezi kufika na wala hamwezi kunufaika na rasilimali zenu. Serikali ya Chadema, nitakayoiunda mkinichagua Oktoba 28, itaweka mfumo mpya wa utawala na siasa ambao utatokana na Katiba Mpya, ili wananchi wawe na mamlaka ya kujitawala na kuongozwa kuamua hatma ya maendeleo yao, rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao uwe msingi wa kwanza wa maendeleo hayo. Tutaondoa huu ukiritimba wa kila kitu kinaamuliwa na Rais na wananchi wamegeuka kuwa ombaomba kwa mtu mmoja aliyeko makao makuu ya nchi,” amesema Mhe. Lissu.

Aidha, Mhe. Lissu amesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2020, una agenda nyingi ambazo lazima zijadiliwe kwa uwazi kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Watanzania, akisema kuwa kitendo cha Rais John Magufuli ambaye ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, kujenga kiwanja cha ndege kijijini kwao Chato, mkoani Geita, ambacho hakitumiwi na Umma wa Watanzania, ni mojawapo ya agenda hizo kwa sababu ni mojawapo ya kielelezo cha wazi cha matumizi mabaya ya madaraka, kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1997s, ambayo inazuia viongozi kutumia nafasi zao kujipendelea, kwa maslahi yao binafsi.

“Leo nimemsikia Rais Magufuli akiwa Chato akinijibu kuhusu Uwanja wa Ndege wa Chato, anasema kwanini ninahoji kuhusu uwanja huo tu na sioni viwanja vingine vya ndege ambavyo vimejengwa maeneo mengine nchini. Sasa ninamwambia Chato ujenzi wa uwanja huo lazima upigiwe kelele na kila Mtanzania mzalendo, mpenda nchi yake, kwa sababu ni uwanja tofauti na viwanja vingine vyote. Uwanja ule umejengwa huko kijijini kwa sababu tu Magufuli ni Rais. Ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka na mfano hai wa ufisadi katika awamu hii ya tano. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1997, ilitungwa wakati wa Rais Mkapa, ilizuia viongozi kutumia madaraka yao kwa maslahi au manufaa yao binafsi. Uwanja ule anautumia Rais Magufuli na mama yake.

“Tujiulize manufaa na maslahi ya umma ya Uwanja wa Ndege wa Chato. Hauna manufaa yoyote kiuchumi, kiutalii. Uwanja wa Chato unatumiwa na umma gani zaidi ya Rais Magufuli na mama yake niliwahi kuona amepelekwa pale. Zaidi yake hakuna abiria mwingine anapita uwanja huo. Uwanja huo umejengwa kwa namna isiyoeleweka kwa kutumia mamilioni ya Watanzania. Miji mikubwa iliyoko jirani na kijiji hicho, Katoro, Geita, Biharamulo haina uwanja wa ndege. Tujiulize mbona Nyerere hakujijengea uwanja wake, wala Rais Mwinyi, wala Rais Mkapa, wala Rais Kikwete. Yeye hata hajamaliza miaka mitano ameshajijengea uwanja wa ndege kijiji kwake. Ndani ya miaka hii michache kila kitu kimekuwa Chato, Chato, Chato. Ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka ya umma, ndiyo maana ni agenda muhimu uchaguzi huu,” amesema Mhe. Lissu.

Akisisitiza hoja zake kuhusu mjadala wa agenda za Uchaguzi Mkuu, Mhe. Lissu alikumbushia wito wake kwa Mgombea Urais wa CCM, Mhe. Magufuli kuhusu mdahalo wa Wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisema kuwa itakuwa jukwaa sahihi kujadili matendo, mipango na mikakati ya utawala wa Rais Magufuli kwa miaka 5 iliyopita na kuwaambia Watanzania maono yao kwa miaka mitano mingine ya uchaguzi na vizazi vijavyo. Alizitaka mamlaka na vyombo vinavyohusika, ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), kuandaa mdahalo huo kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Alitumia mikutano hiyo mitatu na mingine midogo ya njiani katika maeneo ambayo alikuwa na ratiba ya mikutano, kuwaombea kura wagombea wa udiwani na ubunge wa Chadema, huku akirejea tena kusisitiza kauli yake kuitaka NEC iwarejeshe bila masharti wagombea ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali ambao wameenguliwa kugombea au wamekatiwa rufaa, ili wote wakashindane kwenye sanduku la kura kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Mhe. Lissu ataendelea na ratiba ya mikutano yake ya kampeni siku ya kesho, Jumanne, Septemba 15, 2020 katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Mikoa ya Njombe na Mbeya.

Imetolewa leo Jumatatu, Septemba 14, 2020 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Chadema
Umati wa watu waliojitokeza kumskiliza mgombea urais wa Chadema Mhe. @tunduantip ( 640 X 640 ).jpg


 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom