Leta andiko japo moja tu niliposema nilifurahia kifo cha JPM.
Tena nakumbuka kabisa niliandika kuwa kuna mambo ambayo sikukubaliana kabisa na marehemu, na wala siyo yote. Lakini nilieleza kuwa pamoja na yote, kifo kile kilinisikitisha. Kwa mambo yalivyokuwa yanaenda, ningefurahi asiendelee kuwa Rais, lakini siyo asiendelee kuishi.
Siandiki haya kwaajili ya kumfurahisha yeyote. Usiku ule nilikuwa nimelala, nikapigiwa simu na mtu ambaye hajawahi kunipigia simu usiku. Ndipo akanipa taarifa hiyo. Ilinishtua sana, nikaduwaa kwa muda, kisha sikulala, nikakaa kwa karibia masaa 3 kabla ya kulala tena. Japo kulikuwa na minong'ono kuwa alikiwa anaumwa lakini kichwani mwangu hakukuwa na fikra kuwa alikuwa katika hatari ya kifo.
Na siku ya pili yake nikaambiwa na ndugu yangu kuwa mke wangu aliwaambia baadhi ya watu kuwa kumbe nilikuwa namkritisaizi tu Magufuli mdomoni, moyoni nilikuwa nampenda sana, mbona inaonekana nimehuzunika. Na kwa kweli nilihuzunika, na nakumbuka neno langu la kwanza, nilipopewa taarifa nilisema tu, 'my God!'. Na ufahamu kuwa JPM kabla ya kuwa Rais, niliwahi kuongea naye mara 4 kwa simu. Na kuna mengine, kwa vile hayupo Duniani, siwezi kuyaweka hapa.
Mimi ninachoamini ni kuwa wanadamu tuna uwezo wa kusema tendo hili na lile ni mabaya, lakini hatuwezi kuhukumu. Ndiyo maana huwezi kuona japo mara moja mimi Bams eti nikaandika, oh JPM yupo jehanamu, anaungua moto, JPM ni mzoga. Yesu alisema, njooni kwangu nyote msumbukao na kuelemewa na mizigo ya dhambi, nitawapumzisha, hata kama muwe na dhambi nyekundu kama damu, nitawatakasa. Sasa mimi mwanadamu nitajuaje nyakati za mwisho za marehemu na Mungu wake, hata nitoe hukumu kuwa JPM yupo jehanamu?
Bado naamini kwa kiongozi kuwaua, kuwateka, kuwatesa au kuwabambikia kesi watu unaowaongoza ni ushetani, lakini kamwe siwezi kushangilia kifo cha mwanadamu yeyote. Nitashangilia kama mtu mwovu akikoma kuwa mwovu iwe kwa hiari au kulazimishwa. Lakini pia nimewahi kuandika hapa kuwa mimi naamini kuna baadhi ya mambo mabaya yalifanyanyika bila ya kuwa na maelekezo ya moja kwa moja toka kwa marehemu. Baadhi ya wasaidizi wake, naamini walifanya baadhi ya mambo ya hovyo sana kwa nia ya kumfurahisha. Kosa lake ni kutowakemea. Niliwahi kueleza kuwa mathalani hela yangu, ilikuwa kidogo tu, hela ya mshahara wangu toka UK wakati nafanya kazi nje ya nchi TRA wakaifungia, lakini baada ya kupambana nao kwa siku 2, wakaifungulia. Sikulipa chochote, sikumhonga mtu. Sasa niamini kuwa ile pesa aliifungia Magufuli? Kama angeifungia Magufuli au angekuwa ameelekeza pesa yangu ifungiwe, kuna mtu TRA angeweza kuiachia?
Mimi siyo mnafiki, hakika ningefurahi utawala wa Magufuli kukoma, lakini siyo kukoma kwa kifo. Mimi kama mtu binafsi, sikuwahi kuguswa na chochote kibaya ambacho kilifanywa dhidi yangu kama mtu binafsi, hakuna kabisa lakini unahuzunika na wenzako ambao wanaumia kwa kuonewa. Nina uhakika walioguswa moja kwa moja kwa mabaya na utawala wa JPM, hawawezi kufika hata 10%, lakini hata wangekuwa 5% ni binadamu wenzetu, wanapoonewa au kutotendewa haki ni lazima tupaze sauti zetu.
Lakini pia kuna watu wanajifanya walimpenda sana JPM lakini ukweli ni wanafiki wakubwa, ndio wanaomfanya marehemu kutukanwa na kusemwa vibaya wakati wote kwa maana hawatulii kila siku ni kuanzisha mada za kumkejeli Samia, Mbowe, CAG Asad, Zito, Kikwete; na kuwasema kuwa si chochote wakilinganishwa na JPM. Hawa watu wanaosemwa vibaya nao wana wafuasi wao na wana wanaowaunga mkono na kuwakubali kwa yale wayatendayo, unadhani watakaa kimya? Nao watakutukania yule wanayeamini wewe ulimpenda. Hao hawana tofauti na mzee Makamba ambaye aliropoka, na sasa kauli yake inawafanya baadhi ya watu wamtukanie watu wanaoamini Makamba anawapenda.
Ukweli unabakia pale pale, utawala wa marehemu kuna mambo mabaya kabisa uliyatenda na kuna mazuri pia. Niliwahi kutamka, kwangu mimi, utawala wa marehemu, ungeacha kujihusisha na mambo ya kuua, kuteka na kupoteza watu, mengine yote ni madogo. Uhai wa binadamu mwenzako una thamani kama wa kwako. Uhai wangu una thamani sawa na wa JPM, Membe, Sanane, Azory na mwingine awaye yeyote. Kama sifurahii uhai wangu uondoke kwa nini nikafurahie wa JPM, Membe au Lisu kuondoka? Kama hakuna awezaye kumwongezea mwanadamu mwenzake hata siku moja ya kuishi, basi tuogope kabisa kumwondolea mtu mwingine siku za kuishi.
Wanaofurahia na kushangilia vifo vya wanajisumbua bure maana hao watu wamelala. Tafakari ya maisha yao ni jambo jema. Mema yaendelezwe, mabaya wazikwe nayo.