kuhusu ilivyokusudiwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haimaainishi kuwa tunamswalia yeye kama vile tunavyoswali kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye Swalaah zetu kwa kusimama na kurukuu na kusujudu na kuomba na kadhalika. Bali inapotajwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inakusudiwa kumuombea du’aa za Rahmah na amani zimshukie .
Tambua ndugu yetu kwamba lugha ya Kiarabu ni pana mno, kwa mfano maana ya neno moja linaweza kuwa na maana nyingi kabisa. Ukitaka kujua maana ya neno la Kiarabu kwanza ujue maana yake ya kilugha, kisha ujue maana yake ki-Shariy’ah (katika Dini ya Kiislamu) ambao huwa inatofautiana na maana ya asili. Na katika maana ya Swalaah kilugha inamaanisha ni du’aa. Ama katika Shariy’ah inaamanisha ni ‘ibaadah (kumwabudu Allaah)
Chukulia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab 33: 56]
Ni kwamba: Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maana yake ni kumsifia kwa Malaika, kumteremshia rahmah na baraka, fadhila n.k.
Ama Malaika Wake kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) du’aa Amghufurie na Amteremshie baraka.
Na ndio sisi Waumini tumeamrishwa pia kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Aayah hiyo na maana yake ni hiyo ya kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) du’aa ya rahmah na amani.
Na alipoulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) jinsi gani kumswalia alijibu kuwa ni kumswalia kama vile tunavyomswalia ndani ya Swalaah katika kikao cha Tashahhud pale kwenye du’aa inayoitwa Swalaatu Ibraahimiyyah (Swalaah ya Ibrahiym) ambayo imekuja katika matamshi mbali mbali yanayotofautiana kidogo; mojawapo ni kama ifuatavyo:
Allaahumma Swalli ‘alaa Muhammadin, wa ‘alaa aali Muhammadin, kamaa Swallayta ‘alaa Ibraahiyma, wa ‘alaa aali Ibraahiyma, Innaka Hamiydun Majiydun, Allaahumma Baarik ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa aali Muhammadin kamaa Baarakta ‘alaa Ibraahiyma wa ‘alaa aali Ibraahiyma Innaka Hamiydun Majiydun
Ee Allaah! Mswalie Muhammad, na ahli wa Muhammad kama Ulivyomswalia Ibraahiym na juu ya ahli zake Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa, Mwenye utukufu. Eee Allaah! Mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na juu ya ahli zake Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa, Mtukufu.