Hatuna shida na Kingunge - Kanisa Katoliki
na Joseph Sabinus
KANISA halina shida na Kingunge na wala halitaki malumbano naye kwa kuwa limetimiza wajibu wake na sasa ni wajibu wa wananchi kutafakari maudhui ya waraka wake, amesema Msemaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Kupitia msemaji huyo ambaye ni Ofisa Habari wa TEC, Padri Modest Katonto, kanisa hilo limesema kwa kuwa tayari viongozi wake wakiwamo maaskofu wamekwishatoa ufafanuzi na maelekezo mengi, sasa linasikiliza maoni ya watu na endapo itaonekana kuna haja zaidi, basi litatoa taarifa na maelekezo zaidi kwa kile kitakachoonekana kutoeleweka vizuri au kuwakwaza wengine.
Msimamo huo umetokana na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Kingunge Ngombale- Mwiru, kupinga hadharani waraka uliotolewa hivi karibuni na Kanisa Katoliki ukiwaelekeza waamini na wananchi kwa jumla, namna nzuri ya kupata viongozi bora wa taifa hili.
Katika moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vilivyomalizika hivi karibuni, Kingunge alitaka Kanisa Katoliki kuondoa waraka huo kwa madai kuwa unaweza kuifanya nchi kuwa mithili ya Lebanon.
Hata hivyo, Kingunge hajaonyesha kauli au kipengele chochote katika waraka huo kinachomfanya ailinganishe Tanzania na Lebanon akihofia kuibuka tatizo la udini.
Baada ya kauli hiyo bungeni, baadhi ya maaskofu walitoa ufafanuzi kuhusu waraka huo wakisema haulengi kugawa watu kwa misingi yoyote ama ya kidini, kisiasa au kikabila, bali kutoa elimu ya uraia hivyo, kuupinga ni sawa na kutetea ufisadi.
Agosti 12, mwaka huu, mzee Kingunge ambaye ni mkongwe wa siasa nchini, alifanya mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake ambapo aliutumia kuwashambulia maaskofu hao akitaka wamuombe radhi kwa kumhusisha na ufisadi.
Katika mkutano huo, Kingunge alisema ni makosa viongozi wa dini kutoa ilani kwa kuwa ilani za uchaguzi hutolewa na vyama vya siasa pekee.
Hata hivyo, watu wengi wameshindwa kutambua kuwa iweje siasa itenganishwe na dini kwa kuwa viongozi wa dini wanao wajibu wa kumjenga mtu kiroho na kimwili.
Hata hivyo, watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na madhehebu mengine, wanasiasa na wasomi mbalimbali wamenukuliwa wakishangazwa na uamuzi wa Kingunge.
Wengi wao wamelitaka Kanisa Katoliki kumpuuza Kingunge na kutofanya malumbano naye, lakini wakasisitiza kuwa waraka huo wa kanisa ni elimu ya uraia hivyo, hauna budi kupongezwa na wote wenye mapenzi mema kwa taifa. Kutokana na hali hiyo, ofisa habari huyo wa TEC alisema: Kwetu kanisa si muda wa kuendelea na malumbano na wala kanisa halina shida na Kingunge kwani suala la msingi ni hoja iliyo mbele yetu. Akaongeza: Waziri Mkuu (Mizengo Pinda), alishauri kanisa lisipuuze maoni ya watu; basi wakati ukifika na tukajua hoja za watu hasa kinachowatatiza, tutatoa maelekezo kwa hicho kinachoweza kuwa kinaonekana kikwazo kwa wengine.