NIANZE kwa kuwatakia wasomaji Krismasi njema na Mwaka Mpya 2009 wenye mafanikio.
Wote watakaofanikiwa kusherehekea Krismasi ya mwaka huu na kupata bahati ya kuuanza Mwaka Mpya wa 2009, wana wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuwaruhusu kuendelea kuishi.
Tunaishi na kuwapo kwa huruma na upendeleo wa Mwenyezi Mungu. La msingi ni kukumbuka kwamba tunaishi ili kutekeleza mpango wa Mwenyezi Mungu, wa kusimika ufalme wa Haki, Wema na Huruma duniani.
Katika makala iliyopita nilitoa ahadi ya kuiendeleza kwa kutoa mifano hai ili kuonyesha jinsi viongozi wetu wa dini na hasa wakatoliki, wanavyotutawala badala ya kutuongoza. Mtu anayeishi chuki, hawezi kukemea chuki, mtu anayeshindwa kutenda haki, wema na huruma, hawezi kuwakemea wanaoshindwa kama yeye.
Ni lazima mtu kutoa kibanizi ndani ya jicho lake ndipo atoe vibanzi kwenye macho ya wengine. Ni lazima kwanza viongozi wetu wa dini wajifunze kuongoza na kuonyesha njia, ndipo waingize ushawishi wao ndani ya jamii yetu. Wakikazania kutawala hawawezi kutoa mchango wowote!
Siandiki makala hii kutafuta haki, siandiki makala hii kumshitaki mtu yeyote, siandiki makala hii kutafuta kushinda ama kushindwa, siandiki makala hii kushindana na mtu yeyote yule.
Nijuavyo mimi, katika mfumo wa Kanisa Katoliki, mnyonge hawezi kupata haki wala kusikilizwa. Haki ni ya wakubwa: Maaskofu, Makardinali na Baba Mtakatifu. Hivyo kufikiri utamshinda Askofu, hata kama amekukosea ni ndoto. Ninaandika makala hii kuelezea ukweli. Nina imani kubwa kwamba ukweli hata ukipindishwa namna gani, kuna siku utajitokeza. Ukweli ni ukweli siku zote. Na hasa kama ukweli umeandikwa, inasaidia zaidi, maana kuna msemo: Kilichoandikwa kimeandikwa!.
Ninaandika makala hii kuwashawishi waumini, ili waanze kuwashinikiza viongozi wao, kuachana na utawala. Wajifunze kuongoza, wajifunze majadiliano, wajifunze kushirikisha, wajifunze kusikiliza na kutoa haki bila upendeleo, waache tabia ya uchu wa madaraka, waache tabia ya kupenda utukufu wajifunze kutumikia, maana Bwana Yesu hakuja kutumikiwa bali kutumikia. Marekani na Ulaya wamefanikiwa kufanya hivyo na kuliweka Kanisa mikononi mwa waumini, kwanini sisi Afrika tusifanikiwe?
Lakini pia ninaandika makala hii kujibu maswali mengi ninayoulizwa kila siku. Ninapokea simu, ujumbe mfupi na barua pepe, watu wakitaka kujua kama kweli mimi ni padri wa Kanisa Katoliki au ni kujipachika tu kama wale wanaojiita madaktari bila kuisomea fani ya udaktari.
Nilipadrishwa Desemba 27, 1981parokiani Itahwa-Bukoba. Marehemu Askofu Christoher Mwoleka, ndiye aliyenipatia daraja la upadri, maana nilipadrishwa kulitumikia Jimbo Katoliki la Rulenge. Kati ya watu walioshuhudia upadrisho wangu ni (sasa) Askofu Severine NiweMugizi, wakati huo akiwa bado mwanafunzi. Wengine walioshuhudia upadrisho wangu ni waumini, mapadri wa Bukoba na Rulenge na Askofu Nestory Timanywa, wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
Nilipadrishwa baada kumaliza masomo yote ya upadri, falsafa nilisomea Seminari ya Ntungamo, Bukoba (1975-1976) Rector wangu alikuwa Askofu Damian Kyaruzi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Askofu Anthony Banzi, wa Jimbo Katoliki la Tanga, alikuwa mwalimu wangu pale Ntungamo. Teolojia, nilisomea Kipalapala Tabora (1977-1981). Rector wangu alikuwa Padre Alfons Ndekimo, wa Jimbo Katoliki la Moshi. Mwadhama Policap Kardinali Pengo, alinifundisha mwaka wa kwanza wa Teolojia. Askofu Agapitus Ndorobo, Askofu wa Mahenge, alikuwa mwaka mmoja mbele yangu. Askofu Thadeus Ruwaichi, Askofu wa Dodoma; Askofu Almachius Rweyongeza, Askofu wa Kayanga; tulikuwa darasa moja. Askofu Msonganzila, Askofu wa Musoma, alikuwa nyuma yangu miaka miwili. Mimi ni padri, sikujipachika upadri.
Nilisimamishwa huduma tangu mwaka 2000, baada ya kutumikia miaka 19. Kusimamishwa kwangu ni mfano mzuri wa wanavyotutawala badala ya kutuongoza. Askofu Severine NiweMugizi, aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Rulenge Februari 16, 1997. Tarehe hii ni muhimu sana kuelewa ninachotaka kuelezea.
Askofu Severini, akiwa bado padre na anafundisha Seminari Segerea, wakati wa likizo yake ya mwaka 1993, alilizunguka jimbo zima la Rulenge, akiwahoji mapadre kuhusu maisha yao kwa kile alichokiita yeye Matatizo ya mapadre.
Kama alikuwa ametumwa na TEC au na Balozi wa Baba Mtakatifu au kwa juhudi zake binafsi haina maana yoyote kwangu. Ninalotaka kueleza ni kwamba alizunguka na kati ya watu aliowahoji mimi ni mmoja wao. Alinikuta Bushangaro-Karagwe, kwa vile nilishapata habari zake na kazi yake nilijiandaa vilivyo kumpokea.
Ushahidi wa maongezi yetu hayo - mimi na Padre Severini, wakati huo- haukanushiki kwa lolote lile. Ushahidi unatosha na ni mzito!!
Niliongea na Padre Severini na kujifunua kwa yote aliyotaka kuyajua juu yangu: maisha ya kiroho, misimamo yangu juu ya ukristo na teolojia na mambo mengi tu. Nilijifunua bila woga wowote maana yeye alikuwa rafiki yangu wa karibu sana. Katika kitabu ninachokiandika kuelezea tukio hili, nitaweka barua alizokuwa akiniandikia tulipokuwa marafiki. Baada ya maongezi yetu hayo ya Bushangaro, nilimwomba maongezi yetu tuyafanye maungamo. Niliungama kwake na akaniondolea!
Jambo la kusikitisha sana na kukatisha tamaa na kupunguza imani ni kwamba baada ya Askofu Severini, kupata daraja la Uaskofu wa Jimbo la Rulenge Februari 17, 1997, hata kabla ya miezi miwili kupita nilipata barua kali kutoka kwake ikiwa inataja pamoja na mambo mengine yale tuliyoongea pamoja siku za nyuma kule Bushangaro, wakati akizungukazunguka kuwahoji mapadre na maungamo yangu kwake.
Barua hiyo ya Machi 29, 1997, kumbukumbu 0037/27 yenye kichwa cha habari : KUTOKUAMINI UKRISTU. Akinitaka kuthibitisha au kukana mambo ambayo niliungama kwake mwaka 1993. Jambo hili sikulielewa kabisa na lilinivuruga na kupunguza imani yangu kwake. Niliijibu barua yake kwa unyenyekevu mkubwa. Yeye akajibisha tena kwa Onyo la kwanza nililolipata Aprili 18, 1997 - miezi miwili kamili baada ya Uaskofu wake!
Askofu wangu kwa vile ni mtawala aliamua kutumia maungamo yangu kuninyanyasa, kuharibu imani yangu na wito wangu.
Canon Law, inamzuia kiongozi wa Kanisa kufanya hivyo: Can.984:1 . The confessor is wholly forbidden to use knowledge acquired in confession to the detriment of the penitent, even when all danger of disclosure is excluded.
2. A person who is in authority may not in any way, for the purpose of external governance, use knowledge about sins which has at any time come to him from the hearing of confession. Unaweza kuangalia pia na Can 1388!!
Mimi ninasema alitumia maungamo yangu. Anaweza kukataa kwa kujitetea. Lakini hoja kubwa ni je, alifahamu vipi mwenendo wangu kwa muda wa mwezi mmoja akiwa ofisini? Sheria ya Kanisa inamzuia kiongozi kutumia Previous knowledge ya watu walio chini yake anapoingia madarakani.
Baada ya onyo hili la kwanza ambalo lilitokana na maungamo yangu, maonyo mengine yaliendelea kunyesha kama mvua. Yalikuwa yamepangwa vizuri, ili kila mwaka nipate onyo moja, ili apate msingi wa kunisimamisha huduma za upadri.
Onyo la pili ni kichekesho. Padre Emmanuel Mutabazi, kaka yangu, mwalimu wangu, msomi na mtaalamu wa Biblia, na leo hii bado anafundisha Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki kule Nairobi, aliingia chumbani mwangu pale Bushangaro, na kuiba kutoka chumbani kwangu kitabu nilichokuwa ninakisoma kwa wakati huo chenye jina : Jesus The Man kilichoandikwa na Barbara Thiering, na kukipeleka kwa Askofu, kunishitaki kwamba ninasoma vitabu vinavyopotosha. Mtaalamu wa biblia badala ya kunielekeza ananishitaki kwa Askofu, kwa kosa la kusoma kitabu.
Hivyo onyo la pili nililolipata Mei 7, 1998, kumbukumbu 0037/31, ni la kusoma kitabu cha Jesus The Man. Hii sheria ya kuwazuia watu kusoma vitabu inatumika wapi katika Kanisa Katoliki?!
Onyo la tatu nililipata kwa sababu ya kuchelewa Ujerumani. Nilikwenda Ujerumani kumwangalia Mzee Mwoleka, wakati anaumwa. Askofu Severini, anadai alinipatia ruhusa ya juma moja! Juma moja kwenda Ujerumani kumwona mgonjwa! Lakini hata kabla juma moja alilonipatia kumalizika alishaniandikia barua ya onyo kana kwamba alijua nitachelewa. Onyo liliandikwa Machi 29, 1999, kumbukumbu 0037/37 na kutumwa parokiani kwangu wakati ruhusa yangu ilikuwa inakwisha Aprili 4, 1999! Ushahidi upo maana maandishi hayafutiki.
Kama nilikosa kwa kuchelewa na kwa vile alikuwa anajua kwamba nilikwenda kumwona mgonjwa basi angenisubiri nilirudi nijieleze. Badala yake nilikuta barua ya onyo juu ya kitanda changu!
Kisa cha kusimamishwa huduma (suspension): Askofu Severini, aliniandikia hivi: On the 13th of June 2000 you wrote to me just informing me about your plans to meet the doctors from the USA and a friend from Holland coming to visit you. It is a fact beyond doubt that for more than two months up to the day I passed by the parish premises on the 7th of August, you were out of your place of work without permission......
I am now suspending you from the priestly ministry for one year from the day you receive this decree..
Hivyo suspension, kisa chake ni kuwapokea wageni na kuwa nje ya kituo kwa kipindi cha mwezi, ingawa yeye labda kwa kupitiwa anasema miezi miwili. Ushahidi upo na wageni waliokuwa wamenitembelea wapo na watanisaidia kulieleza hili vizuri .
Ukiangalia kosa na adhabu unaona kuwa hakuna uwiano. Nikumbushe kwamba maonyo yote matatu na suspension ni vitu nilivyopokea bila majadiliano wala kuzungumza na Askofu Severini. Hakunipatia nafasi ya kujieleza. Ni mambo ambayo inaonekana wazi alikuwa ameyapanga hata kabla ya kushika utawala wa Jimbo la Rulenge.
Hivyo nimekuwa kwenye suspension miaka kumi. Bila matunzo ya kimwili na kiroho kutoka kwa Askofu wangu. Nimenyimwa haki za msingi za binadamu:Chakula, malazi na matibabu, vitu ambavyo hata majambazi, magaidi wanapofungwa wanavipata.
Niliandika barua kwa rafiki yake mkubwa Mheshimiwa Askofu Methodius Kilaini, kulalamikia uonevu wa Askofu Severine, lakini sikupata jibu hadi leo hii. Niliandika barua tatu kwa Balozi wa Baba Mtakatifu Tanzania, kulalamikia uonevu wa Askofu wangu, lakini sikupata jibu. Niliandikia barua mbili kule Roma na kuhakikisha kwamba zimefika, lakini sikupata jibu lolote. Huu ni ushahidi wa kutosha kwamba ndani ya mfuno wa Kanisa Katoliki, wanyonge hawasikilizwi. Nimetoa mfano wangu, ili kulielezea vizuri hili, lakini mifano iko mingi sana, na nitaendelea kutoa mmoja baada ya mwingine.
Swali la kujiuliza ni je, kwanini mtu aliyekuwa rafiki wa karibu, anigeuke kiasi cha kutumia maungamo yangu kuninyanyasa na kuniharibia imani yangu na wito wangu? Haya ndiyo nitakayoyaeleza kwenye makala inayofuata. Lengo kubwa likiwa ni kuonyesha jinsi viongozi wetu wa dini wanavyotutawala badala ya kutuongoza.