BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,376
- 8,118
Picha: Nusura Abdala enzi za uhai wake
Vumbi la kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdalah bado linazidi kutimka baada ya ndugu kutilia mashaka uharaka wa mazishi yake huku baba mkubwa wa marehemu akija na maswali matano.
Wakati umma ukiendelea kupaza sauti ukitaka majibu juu ya kifo cha mwanafunzi huyo, mwanamume anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Salim Kundyah (47) na ndiye aliyempeleka Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, ameruka viunzi kulizungumzia.
Kwa nyakati tofauti jana, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Elimu ya Juu (Tahliso), Maria John alisema wanasubiri taarifa ya uchunguzi huo huku Rais wa Serikali ya wanafunzi UDOM (UDOSO), Tryphone Mwinuka akisema hawezi kulizungumzia.
Taarifa kutoka hospitali hiyo zilizomkariri daktari aliyemhudumia, Peter Minja zilieleza mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Mei 1, mwaka huu kati ya saa 2 na 3 usiku na mpenzi wake huyo, wakati huo akiwa ni mgonjwa mahututi.
Kwa mujibu wa daktari huyo, vipimo vya awali vilionyesha sukari ilikuwa juu katika kiwango kisicho cha kawaida huku akiwa na upungufu wa damu na kwamba alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea na jitihada za kukokoa maisha yake.
Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo, mitandao ya kijamii imekuwa ikihusisha kifo hicho na ajali ya Naibu Waziri Tamisemi, Dk Festo Dugange iliyotokea usiku wa Aprili 26, mwaka huu jijini Dodoma huku wengine wakikihusisha na kipigo.
Tayari Jeshi la Polisi nchini kupitia kwa msemaji wake, David Misime wametangaza kuanza uchunguzi kutokana na utata huo, uchunguzi utakaoshirikisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Misime alipotafutwa tena jana ili kufahamu maendeleo ya uchunguzi huo, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho uchunguzi unaendelea na uchunguzi ukikamilika umma utajulishwa matokeo.
Juzi, Ofisi ya Rais Tamisemi ilitoa taarifa kwa umma kukanusha Dk Dugange kuwa amejizulu wadhifa wake ili kupisha uchunguzi.
“Taarifa hiyo ni uzushi na wananchi wanaombwa kuipuuza kwani Dk Dugange hajajiuzulu wadhifa wake huo. Bado ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi na Mbunge wa Wang’ingombe mkoani Njombe anaendelea na matibabu Hospitali ya Benjamin Mkapa,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Nteghenjwa Hosseah, Msemaji wa Ofisi hiyo
Msingi wa madai hayo ya kujizulu ni baada ya baadhi ya watu mitandaoni kumtaka naibu waziri huyo ajiuzulu ili kupisha uchunguzi wa sakata hilo analotuhumiwa nalo la ajali hiyo na Nusura ambayo hata hivyo imekwisha kanushwa na Polisi.
Maswali 5 ya baba mkubwa
Baba mkubwa wa marehemu aliyejitambulisha kama Ali Seleman alisema kifo hicho kina utata na yeye ana maswali matano yanayomuumiza kichwa na kueleza siku ya mazishi yalikuja magari matano yakiwa na mwili na waombolezaji.
“Mmmm, kuna utata. Ukiniuliza naweza kusema kifupi hapa ndipo alipozikwa, lakini maswali mengi nitashindwa kuyajibu. Baba wa huyu mtoto ni mdogo wangu tumbo moja, lakini msiba ulivyofika hadi tunazika bado sielewi,” alisema Ali.
Ali (67) anayeishi Kitongoji cha Mtakuja kijijini hapo kwenye eneo la familia huku mdogo wake (Baba wa Nusura) yeye akiishi Mtaa wa Kiwanja cha ndege Singida mjini ambako msafara wa kusindikiza mwili wa Nusura ndiko ulikoanzia.
Mzee Ali anaeleza yapo maswali matano ambayo angetamani kuyajua kuhusu msiba wa binti wa mdogo wake lakini kwa namna ilivyo ameshindwa na amekosa mtu wa kumjibu kwani yeye na mdogo wake walikaa muda usiozidi saa moja walipofika hapo kuzika kisha wakaondoka na msafara wote.
Miongozi mwa maswali yanayomtatiza ni je, Nusura alikuwa na mchumba? Alitokaje Dodoma ghafla kwenda Kilimanjaro? Kwanini hawakusachi nguo zake wapate tiketi aliyosafiria? Kwanini ahusishwe na ajari nyingine Dodoma? Kwa nini mdogo wake alikubali kumzika bila kufanya uchunguzi?
“Hili la kufanya uchunguzi wa mwili lilikuwa muhimu, lakini hadi tunamzika mimi sikuwa najua kuhusu utata baadae ndiyo wanakijiji nasikia wanasema,mwanzo nilipokea taarifa kwamba Nusura amefariki ghafla na baadae mdogo wangu akasema tuandae malalo wanakuja kuzika huku,” anasema.
“Lakini siku ya kumsitiri ulikuja msafara wa magari kama matano hivi, walifikia eneo la kaburi kama unavyojua mdogo wangu hana mji hapa, ile wamemaliza kuzika akasema hakuna arobaini na msiba ndiyo umekwisha hapo, mimi sina simu nizungumze naye kwa hiyo hadi nitafute nauli nikamhani huko mjini,”alisema.
Hata hivyo anasema taarifa za msiba aliambiwa kuwa ulitokea Moshi ambako anakiri kuwa wapo ndugu wachache huko lakini kwamba mdogo wake (baba mzazi wa marehemu) alifanya kazi kwa miaka mingi kiwanda cha sukari TPC.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja, Omari Said ambaye anaishi jirani na lilipo kaburi la binti huyo, alisema mazingira ya msiba tangu awali yalishaonyesha utata na hata mazishi yake kwa wenyeji bado yaliwaacha na sintofahamu.
Said anasema mara baada ya kupokea taarifa za msiba, hakukuwa na maelezo zaidi wala mtu aliyetoka mjini ambaye angeweza kuwasimulia mkasa mzima isipokuwa waliombwa kutafuta vijana wachimbe kaburi kwa ajili ya maziko.
“Basi niliita vijana na Mzee Ali akatuonyesha mahali pa kuchimba, wale wenzetu walikuja na magari kama matano au sita hivi wakazika na muda huo huo wakaondoka wote tukabaki sisi ambao tangu mwanzo hatukuwa tunajua kitu,”
Hata hivyo anakiri kumfahamu binti huyo katika kipindi cha uhai wake kwani amewahi kufika hapo mara kadhaa kwa shangazi yake ambayo ni nyumba ya tatu kutoka anapoishi Mwenyekiti huyo na kwamba alikuwa na taarifa kuwa anasoma Dodoma ingawa hakujua anasoma chuo gani na fani gani.
Kiongozi huyo anakiri kuna mkanganyiko wa taarifa kwani awali waliambiwa alifikwana mauti akiwa Dodoma lakini ghafla wakapata taarifa alikuwa Moshi kwa hiyo hawajafahamu mazingira halisi ukizingatia kuwa wahusika wote wapo mjini.
Mpenzi wa Nusura apiga chenga
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Salim Kundyah (47) anayetajwa na uongozi wa hospitali kuwa ndiye mpenzi wa Nusura na ndiye aliyempeleka hospitali ya Faraja ziligonga mwamba baada ya kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Mei 7, mwaka huu mwanaume huyo aliahidi kuonana na Mwandishi wa Gazeti hili Mjini Moshi lakini alipotafutwa siku hiyo alisema amebanwa kikazi hivyo hawataweza kuonana naye licha ya kusisitiza hataki kuzungumzia suala hilo kwenye simu.
Hata hivyo alimuahidi mwandishi hiyo kuwa atatoka Arusha na kwenda Moshi ili kuonana naye ana kwa ana kwa kile alichodai kuwa hawezi kumpa taarifa kwa njia ya simu kwa kuwa hana uhakika kwamba ni mwandishi kweli au la.
Mei 8, 2023 alipotafutwa tena kwa njia ya simu kujua alipo ili wakutane kama alivyoahidi, napo ilishindikana kwa kuwa alidai amebanwa na kazi na hawezi kutoka na kumuahidi wataonana siku inayofuata ambayo ni jana Jijini Arusha.
Mwandishi hakukata tamaa alimfuata hadi Arusha na alipofika alimpigia simu kujua alipo ili amfuate kwa ajili ya mahojiano lakini alipofika Arusha alimweleza kuwa hayupo Arusha anaelekea Singida kupeleka ndugu wa waliofiwa.
Tahliso, UDOSO wafunguka
Gazeti hili lilipomtafuta Rais wa Tahliso, Maria John Thomas kuhusu sakata hilo na ukimya wao katika suala hilo alisema kwa kifupi “Tunasubiri uchunguzi (wa Polisi, DPP na mkemia mkuu wa Serikali) na hatuwezi kutoa kauli yoyote kwa sasa”
Rais wa UDOSO, Mwinuka alipoulizwa jana kuhusu kutoa tamko kuhusiana na kifo cha mwanafunzi Nusura Abdallah alisema hawawezi kutoa tamko tofauti na lililotolewa na Makamu mkuu wa Chuo UDOM, Profesa Lughano Kusiluka.
Mwinuka alisema Chuo kina idara maalum ya kutoa taarifa nje ya Chuo na hana mamlaka ya kutoa tamko kwa mujibu wa taratibu wa Chuo chao.
“Taarifa zozote zinazohusiana na masuala ya uhusiano na matangazo kuna idara maalum ambazo zinatoa taarifa kwa umma lakini msemaji mkuu ni Mkamu mkuu wa Chuo na tamko lake lilishaonekana kupitia barua ya Afisa uhusiano, hata taarifa zetu sisi wanafunzi nazipeleka kwa Makamu,”alisema Mwinuka.
Simulizi ya mwandishi kutoka kijijini
Ni umbali wa kurusha jiwe kutoka katika nyumba ndogo iliyojengwa kwa matofari ya udongo upande wa Magharibu, kuna kitu mfano wa tuta pembeni kukiwa na miti minne iliyochomekwa kila kona.
Haihitaji kuambiwa lakini kwa mila za Kiafrika hili ni kaburi, tena ni la muda usiozidi wiki moja tangu shughuli za mazishi zilipofanyika katika eneo hilo ambalo lina kaburi moja pekee chini ya mti unaojulikana kwa lugha ya wenyeji ‘msugala’.
Safari ya kufika hapo ilikuwa ni kushuhudia mahali ulipolala mwili Nusura, watu wawili wamenifika hapa ambao ni Baba mkubwa wa Marehemu na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja kijiji cha Kikonge wilaya ya Iramba mkoani Singida.
“Ni hapa hapa ndipo tulipomsitiri binti yetu, inaumiza mioyo lakini kwenye ukoo bado kuna maswali makubwa matano hayana majibu, hata hivyo mtoaji ni Mungu na anayetwaa ni yeye kwa wakati wake, acha iwe hivyo,” anasema mmojawao.
Siyo rahisi kumaliza utata wa maswali ya namna kifo kilivyotokea na mazingira yake, kwani fumbo hilo ameondoka nalo binti huyo aliyekuwa anasubiriwa na familia na Taifa kutumika miongoni mwa wasomi.
Miongoni mwa utata wa maswali kwenye msiba huo ambayo hata Polisi wameona kuna haja ya kufanya uchunguzi ni hatua ndefu za kutoka Dodoma kwenda mkoani Kilimanjaro na hata mauti kumfika akiwa Hospitali ya Faraja, Kilimanjaro.
Ugumu kumpata Baba
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumpata Mzee Hassan Abdallah, baba mzazi wa marehemu au mama yake kwa nyakati tofauti ikiwemo kufika nyumbani kwake, mjini kati eneo maarufu la stendi ya zamani, mkoani Singida bila mafanikio.
Kabla ya kwenda, mwandishi alipata taarifa kwa siku mbili mfululizo baadhi ya watu walikwenda na kukutana naye lakini hakuwa tayari kuzungumza jambo ambalo hakuliamini.
Nilipofika hapo nilipokewa na mtu ambaye alikuwa anaingia ndani ya nyumba aliyeomba nikaribie wakati anakwenda kuwaita wenyeji ambao hata hivyo alitoka msichana anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 19 hadi 20 aliyenidadisi kwa maswali mengi.
Msichana huyo alikwepa kujibu yale niliyomuuliza ndipo akasema,"sasa kama si ndugu huwezi kumuona mzee kwani anatakiwa kutosema jambo lolote kuhusu msiba,". Licha ya kugoma kuingia ndani kumuita baba mwenye nyumba, lakini alieleza marehemu ni dada yake.
Kuhusu watu waliofika kwenye mazishi hayo, anasema Shekh aliyeongoza mazishi hayo ni Athuman Hussein (Shekh Ulaya) alitoa shukrani akiwatambua wageni kutoka Moshi waliosindikiza mwili na wengine aliwataja kutoka Dodoma licha ya kuwa hakuna waliosimama kusema neno bali walitajwa hivyo hajui walikuwa akina nani.
Nyumbani kwao singida
Katika Mtaa wa Kiwanja cha Ndege kwenye nyumba ya kawaida, masufuria yamejaa nje kuashiria kulikuwa na pilika za chakula cha kusanyiko,hata hivyo inakuwa vigumu kuwapata wazazi wa Nusura kwani sharti la hapo ni kutokusema kitu kwa sasa kwa madai kuna vyombo vinachunguza.
Hata hivyo mdogo wake anayeitwa Ummukulthum anatoka nje na kuzungumza kwa ufupi “Tumempoteza mtu muhimu ambaye tulimtarajia kuwa msaada kwa siku za usoni, ni dada yangu tumezaliwa pamoja yeye akiwa mtoto wa tatu, baba hawezi kusema hadi hapo vyombo vya uchunguzi vitakapomaliza kazi yao.”
Binamu wa marehemu Seleman Segu ambaye ni mtoto wa shangazi ya marehemu Nusura, anasema kuwa kilichoficha ukweli wa msiba wa dada yake siyo aliyefariki bali uharaka wa kumzika.
Seleman anaeleza kuwa taarifa za msiba zilitolewa kwa haraka wakati huo naye alikuwa Moshi, lakini alipokwenda kufuatilia kwa ndugu wakasema tayari wamesafirisha na siku ya pili anafunga safari kurudi nyumbani akaambiwa wamezika mchana huo.
“Muulize mtu yeyote, mimi nilianza kulala toka siku hiyo nikamwambia mjomba kwamba tulichofanya si chema, hili jambo tungejua ukweli wake kama pangefanyika uchunguzi kidogo wa mwili kabla ya kuzika, haya maswali tusingeulizwa lakini mjomba wangu dini imemkaa sana ndiyo maana kila kitu kwake ni ndiyo tu,” anasema.
Seleman anasema taarifa zilimkuta akiwa TPC Moshi akifuatilia haki zake baada ya kupunguzwa kazini, lakini anasema mbali na mahusiano mazuri yaliyokuwepo baina yake na dada yake huyo, hakuwahi kusikia kama alikuwa na mchumba.
Safari ya kufika Kikonge
Ili uweze kufika katika kijiji hiki ambacho ni kikubwa, yakupasa kujifunga mkanda na hasa ukiwa mgeni na mazingira ya usafiri wa eneo husika.
Anzia Singida mjini, popote ulipo waulize wenyeji wakupeleke stendi ya Mkombozi, imeitwa hivyo kwa sababu ukuta wake unapakana na shule kongwe ya msingi ya Ukombozi. Usafiri wa hapa ni gari ndogo aina ya Noha.
Kwa hakika jifunge mkanda, ni mateso na adhabu kwa mgeni, lakini ni wanaishi sawa na msemo wa wahenga hiyari yashinda utumwa kwani burudani ya muziki inatosha kuwaburudisha na kuwariwaza.
Watu wazima ndani ya Noah tulikuwa 17, watoto wawili,juu mizigo usipime, safari inaanzia Mkombozi tunazunguka kupitia Sekondari ya Senge kisha kutokeza Uhasibu. Kumbuka njia hiyo inatusaidia kuwakwepa Polisi wa usalama barabarani.
Mbele kidogo anapanda anaongezeka abiria ambaye anakwenda kukaa juu ya mizigo kukamilisha idadi ya watu 20 kwenye gari hiyo yenye uwezo wa kubeba watu 8 wanaomjumlisha dereva.
Sikiliza, tunakaa hivi, dereva mbele amekaa na watu wazima wawili na mtoto mmoja ambayo jumla yao ni wanne, yeye akiendesha kwa kukaa upande,sehemu ya pili wamekaa wanne, sehemu ya tatu wanne wakimpaka kijana wa darasa la nne au tano lakini viti vyao vimelazwa ili kupisha watu wanne kukaa nyuma sehemu ya mizigo, mtu mmoja amejikunja akisimama sehemu ya kati ya kulalia mwegemeo wa viti vya nyumba ndipo mwingine anakaa juu ya gari kulinda mizigo.
Ni kweli kuwa barabara si ya lami lakini haina mashimo kama maeneo mengine, lakini mwendo wa gari hiyo unaweza kuomba maji. Tunatumia dakika 87 kufika kituoni na anayeshuka ni mimi peke yangu gari ikielekea Ndola ambako ndiko mwisho wa safari.
Ili usijazane hivyo, yakupasa kupanda pikipiki hadi Kaselya (mahali alipozikwa Dk Sima aliyeuawa kwa mapanga wiklayani Tarime) ambako Noha zinabeba watu 10 tu lakini gharama yake ukijumlisha na usafiri wa pikipiki ni sawa na nauli ya basi kutoka Singida kwenda Mwanza.
MWANANCHI