SEHEMU YA 3
Waheshimiwa Majaji,
Sasa baada ya kueleza sheria inavyosema, swali muhimu ni hili:
Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kila kipengele cha kosa hili kwa ushahidi gani?
Kwa sababu siyo kila ushahidi unaowasilishwa Mahakamani unathibitisha kosa linaloshtakiwa.
Kosa hili lina vipengele maalumu. Na kila kipengele lazima kiunganishwe na ushahidi wa kutosha.
Jambo la kwanza ni allegiance, yaani utii kwa Jamhuri ya Muungano.
Kwanza, sheria inaanza na mtu ambaye yuko chini ya allegiance kwa Jamhuri ya Muungano.
Hili si jambo la kupuuzwa.
Mahakama inapaswa kujiuliza: Je, upande wa mashtaka umeonyesha kwa ushahidi kwamba kipengele hiki kimetimizwa?
Ikiwa ni jambo lisilopingika kwamba mshtakiwa ni raia wa Tanzania, basi suala linalofuata ni kama vipengele vingine vya kosa vimeonyeshwa kwa kiwango kinachotakiwa na sheria.
Jambo la pili ni nia inayotakiwa na sheria.
Waheshimiwa Majaji, hapa ndipo kiini cha kesi hii kilipo.
Kifungu cha 39(2)(d) hakisemi tu kwamba mtu amesema jambo fulani.
Kinazungumzia mtu ambaye anaunda nia ya kusababisha au kuhamasisha mtu au kundi la watu kutekeleza lengo lililotajwa katika kifungu hicho, na kisha anaonyesha nia hiyo kwa maandishi, uchapishaji au kitendo cha wazi.
Kwa hiyo, Mahakama inapaswa kutenganisha mambo mawili.
Kwanza, maneno yaliyosemwa.
Pili, nia ambayo sheria inataka ithibitishwe.
Maneno yanaweza kuthibitishwa kwamba yalisemwa. Lakini swali la kisheria ni: Maneno hayo yanaonyesha nia gani?
Na zaidi, je, yanaonyesha nia mahsusi inayotakiwa na kifungu cha 39(2)(d)?
Jambo la tatu ni kitu kilichokusudiwa kutokea.
Waheshimiwa Majaji, lazima kuwe na jibu la wazi kuhusu swali hili:
Mshtakiwa alikusudia nini kitokee?
Upande wa mashtaka unasema kulikuwa na nia ya kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025.
Lakini Mahakama lazima itenganishe nia ya kutaka uchaguzi usifanyike, nia ya kutaka mabadiliko ya kisiasa, nia ya kushinikiza Serikali, nia ya kuhamasisha maandamano, nia ya kuhamasisha uasi na nia mahsusi inayotakiwa na kifungu cha 39(2)(d), ya kutishia Executive, Legislature au Judiciary.
Si kila moja ya mambo hayo ni kitu kimoja kisheria.
Kwa hiyo, swali si tu kama maneno yalitamkwa.
Swali ni kama upande wa mashtaka umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya maneno hayo na nia mahsusi inayounda kosa chini ya kifungu cha 39(2)(d).
Jambo la nne ni nani aliyetishiwa.
Waheshimiwa Majaji, kifungu kinataja taasisi maalumu: Executive, Legislature au Judiciary.
Kwa hiyo, Mahakama inapaswa kujiuliza:
Ni taasisi ipi hasa iliyokusudiwa kutishiwa?
Na kitendo gani hasa kilikuwa tishio dhidi ya taasisi hiyo?
Ikiwa jibu ni Serikali, basi ni lazima ionyeshwe ni kwa namna gani kitendo hicho kilifikia kiwango cha intimidation kinachotakiwa na kifungu.
Ikiwa ni Bunge, ni lazima lionyeshwe.
Ikiwa ni Mahakama, ni lazima lionyeshwe.
Hatuwezi kuchukua neno moja au sentensi moja na kuliondoa kwenye mazingira yake bila kuonyesha uhusiano wake na kipengele cha kosa.
Jambo la tano ni kwamba masharti ya kifungu hayaishii kwenye maneno.
Waheshimiwa Majaji, kifungu cha 39(2)(d) kinahitaji nia hiyo idhihirishwe kwa kuchapisha maandishi, uchapishaji au overt act or deed whatsoever.
Kwa hiyo, ushahidi kuhusu video, maandishi, machapisho ya mitandao ya kijamii au hotuba haupaswi kuangaliwa tu kwa swali la:
Je, mshtakiwa alisema haya?
Bali:
Je, chapisho au kitendo hicho kinaonyesha nia mahsusi inayotakiwa na kifungu cha 39(2)(d)?
Hapo ndipo tofauti kati ya ushahidi wa tukio na ushahidi unaothibitisha kila kipengele cha kosa inapojitokeza.
Kuhusu mashahidi 17 wa upande wa mashtaka, Waheshimiwa Majaji, upande wa mashtaka uliita mashahidi 17 na kuwasilisha vielelezo mbalimbali.
Lakini idadi ya mashahidi si kipimo cha kama kosa limethibitishwa.
Mashahidi 17 hawawezi kuchukua nafasi ya kipengele cha sheria ambacho hakijathibitishwa.
Mahakama inapaswa kuangalia kila shahidi kwa swali hili:
Ushahidi wa shahidi huyu unathibitisha kipengele gani cha kosa?
Ikiwa shahidi anathibitisha tu kwamba mkutano ulifanyika, hilo halitoshi peke yake kuthibitisha treason.
Ikiwa shahidi anathibitisha kwamba hotuba ilitolewa, hilo peke yake halitoshi.
Ikiwa shahidi anathibitisha kwamba video ilirekodiwa, hilo peke yake halitoshi.
Ikiwa shahidi anathibitisha kwamba video ilichapishwa mtandaoni, bado Mahakama inapaswa kujiuliza:
Chapisho hilo linaonyesha nia mahsusi inayotakiwa na kifungu cha 39(2)(d)?
Waheshimiwa Majaji, kuna tofauti kati ya shahidi anayesema “Niliona au nilisikia” na ushahidi unaothibitisha “Hiki ndicho kilichokusudiwa kisheria.”
Mahakama ndiyo yenye jukumu la kutafsiri ushahidi huo kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, ushahidi wa mashahidi kuhusu mazingira ya kisiasa, uchaguzi, mikutano ya CHADEMA, machapisho ya mitandao ya kijamii au kauli zilizotolewa lazima hatimaye uunganishwe na kipengele mahsusi cha kosa.
Kuhusu kauli ya tarehe 3 Aprili 2025, Waheshimiwa Majaji, upande wa mashtaka umejenga sehemu kubwa ya kesi yake kuzunguka kauli zinazodaiwa kutolewa tarehe 3 Aprili 2025 katika mkutano wa CHADEMA.
Lakini Mahakama haipaswi kuishia kwenye swali la kama kauli hizo zilitolewa.
Inapaswa kujiuliza:
Kauli hizo, zikisomwa kwa ukamilifu na katika mazingira yake, zinathibitisha kila kipengele cha kosa linalodaiwa?
Na hasa:
Zinaonyesha nia ya kutisha Executive, Legislature au Judiciary kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 39(2)(d)?
Waheshimiwa Majaji, maneno hayawezi kutenganishwa na mazingira ambayo yalitamkwa.
Ikiwa ushahidi unaonyesha kwamba kulikuwa na mjadala kuhusu uchaguzi, marekebisho ya uchaguzi, Katiba, maandamano au shinikizo la kisiasa, Mahakama inapaswa kuangalia mazingira hayo yote.
Hii si kusema kwamba mazingira hayo yanaondoa moja kwa moja kosa.
Bali hoja ni kwamba mazingira hayo yanaweza kuwa muhimu katika kuamua nia ya mshtakiwa ilikuwa nini.
Na hilo ndilo jambo ambalo kifungu cha 39(2)(d) kinahitaji Mahakama ilitathmini.
Waheshimiwa Majaji, baada ya mashahidi 17 kusikilizwa, swali si:
Je, Serikali imeleta mashahidi wengi?
Swali sahihi ni:
Je, ushahidi wao, kwa pamoja na kila mmoja kwa nafasi yake, umeprove kila ingredient ya offence beyond reasonable doubt?
Kwa sababu kama kuna kipengele kimoja muhimu ambacho hakijathibitishwa, basi wingi wa mashahidi hauwezi kuziba pengo hilo.
Na kama ushahidi wa mashahidi 17 unaonyesha kwamba maneno yalitamkwa lakini hauonyeshi nia mahsusi inayotakiwa na kifungu cha 39(2)(d), basi Mahakama lazima itenganishe kati ya kitendo kilichothibitishwa na kosa linalotakiwa kuthibitishwa.
Waheshimiwa Majaji, msingi wa utetezi wangu ni huu:
Kesi hii haipaswi kuamuliwa kwa kuangalia ukubwa wa ushahidi, bali ubora wa ushahidi katika kuthibitisha kila kipengele cha kosa.
Si idadi ya mashahidi inayounda kosa.
Si idadi ya vielelezo inayounda kosa.
Ni sheria na ushahidi unaokidhi kila kipengele cha sheria.
Na pale ambapo kipengele cha kosa hakijathibitishwa, haiwezekani kukamilisha kosa kwa kuunganisha ushahidi usiohusika moja kwa moja na kipengele hicho.
Ndiyo maana, baada ya kupitia mashahidi 17 na vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka, hoja yangu ni kwamba Mahakama inapaswa kujiuliza kwa kila kipengele:
Where is the evidence?
What element of the offence does this evidence prove?
Na mwisho:
Has that element been proved beyond reasonable doubt?
Hapo ndipo Mahakama itakapoweza kuamua kama ushahidi uliopo unathibitisha kosa linaloshtakiwa chini ya kifungu cha 39(2)(d).