SoC02 Tujenge mtazamo chanya na kubadilisha fikra juu ya ushabiki wa soka la Simba na Yanga kwa maendeleo ya Taifa

Stories of Change - 2022 Competition

Impimpi

JF-Expert Member
Jan 7, 2019
464
949
Historia ya mpira wa miguu katika nchi hii imetoka mbali sana , tunacho cha kujivunia tunapoona maendeleo na uwekezaji mkubwa katika soka letu.

Mathalani, vuta picha enzi za chama cha soka cha Tanzania enzi hizo kikiitwa FAT hali ilikuaje kiuchumi kwa timu zetu? Ni ,mara ngapi timu zetu zilikosa nauli ya kusafiri kwenda michuano ya kimataifa ya CAF?

Sasa hivi tunao uwekezaji mkubwa kutoka benki ya NBC kama mdhamini wa ligi na AZAM media kama mdhamini wa haki ya matangazo ya runinga swali linabaki kuwa je?

Kuna kilicho badilika kimtazamo kwa mashabiki na viongozi wa soka hususani katika vilabu hivi viwili katika nchi hii kinachoweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi kilichopo na kijacho?

Toka vilabu hivi vimeanzishwa ni miaka mingi sana kiasi kwamba kama angekuwa binadamu basi sasa hivi angekuwa mzee sana lakini cha kusikitisha timu hizi hazina viwanja vyao wenyewe licha ya kuwa na mashabiki wengi na mianya ya vyanzo vingi vya mapato.

1661459257865.png
1661459322208.png


Chanzo: Binzubeiry.co.tz, 2021 Chanzo: Binzubeiry.co.tz, 2021

Nimekaa chini na kung’amua baadhi ya mambo ambayo vilabu hivi viwili vinachangia katika kuzoretesha maendeleo ya nchi hususani nguvu kazi ya Taifa ambayo ni vijana;

1.Ushabiki wa vilabu hivi unatengeneza kizazi kisichokuwa na mantiki katika kufikiri katika mambo ya msingi katika nchi. Ukitaka kujiuliza maswali mengi na ukakosa majibu basi kaa chini na fikiria namna mashabiki wa timu hizi wanavyotumia akili zao katika kufikiri utagundua kama taifa bado tuna safari ndefu sana katika kupiga hatua katika maendeleo. Mawazo mengi ya mashabiki hawa sio tu yanaishia katika ushabiki wa mpira pia yana akisi hali halisi ya maisha ya kila siku huku mitaani , katika siasa, muziki, uchumi na mambo kadha wa kadha yanayohitaji fikra pana kuyatatua ila yamebaki kutatuliwa kiushabiki na sio uhalisia ulivyo. Hii ni hatari kama taifa kama tunataka kufika mbali.

2. Ushabiki huu pia unatengeneza kizazi kisichotaka mabadiliko hata kama ni ya msingi na ya lazima kutokea kulingana na maendeleo ya kiteknolojia ,kiuchumi na kijamii kiujumla. Fikiria ni mara ngapi vilabu hivi vimeshindwa kupia hatua katika maendeleo ya msingi kisa tu kung’ang’ania mila na utamaduni wa vilabu? Mabadiliko katika maisha hayana budi kutokea hata katika michezo na sheria za mpira wa miguu tunashuhudia mara kadhaa wakifanya mabadiliko katika sheria na teknolojia zinazosaidia mchezo huu mfano VAR (kisaidizi cha mwamuzi kwa kutumia video). Hapa kwetu kilabu ikitaka kufanya mabadiliko basi utatokea mvutano mkubwa sana na sababu kubwa ni ile ile kukumbatia mila na tamaduni za kilabu wanazofaidi wachache . Hii ni mbaya kama taifa kama tunataka kupiga hatua katika maendeleo.

3.Ushabiki huu unatengeneza kizazi kinachopenda propaganda na uzushi na mbaya zaidi mizaha inayokusudia kudhalilisha utu na haiba ya watu katika jamii. Hii inajenga jamii kupenda zaidi habari za uongo na umbeya kwani ndizo zinazopendwa masikioni mwa mashabiki na sio ukweli mchungu utakao wafanya wapate mabadiliko ya kweli. Watoto wetu hawatakua na kurithi kutoka kwenye huu ushabiki wa namna hii zaidi ya kuharibika kifikra. Kilabu hizi ningependa zitumie na kuzingatia taaluma hasa za habari na si propaganda katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku hii itachochea taarifa sahihi katika maendeleo binafsi nay a taifa kwa ujumla.

4.Tunatengeneza na kuandaa kizazi kinacopenda uvivu na kutowajibika. Kwani habari kubwa kila siku midomoni mwa mashabiki hawa kutoka asubuhi hadi usiku ni Simba na Yanga tu iwe vijiweni au maofisini kitu kinachoondoa ufanisi wa kazi na kutowajibika kama taifa. Angalia idadi ya vipindi vya michezo nchini vingi vinaendeshwa asubuhi muda amabao kimsingi ni wa kuwajibika. Hili linatakiwa kufanyiwa kazi na wizara husika ili kuandaa jamii inayopenda kufanya kazi na kuwajibika ipasavyo ili kuinua uchumi wetu na maendeleo ya taifa hili kwa ujumla.

5. Imani za kishirikina pia ni moja ya fikra mbaya ambazo zinaenezwa na ushabiki wa vilabu hivi kwani ni vitenedo vingi vinavyoashiria imani hizi zimeshuhudiwa katika michezo inayohusisha timu hizi mara zinapokutana. Hali hii isipobadilika itaadhiri jamii kwani vilabu hivi kama vioo vya jamii inatakiwa kuonesha mfano wa kuigwa na jamii na sio kuendekeza imani hizi kwani zina mchango mbaya katika jamii kwa kurudisha maendeleo ya kiuchumi nyuma na kusababisha umasikini katika jamii, hivyo endapo mashabiki na vilabu hivi vikibadilisha mitazamo na fikra katika hili itachangia kujenga jamii inayoamini katika kufanya kazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya katika uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Endapo vilabu na mashabiki hawa wakibadilisha fikra na mitazamo katika ushabiki wa mpira wa miguu tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na jamii inayopenda kufanya kazi, amani na upendo, jamii inayofikiria vyema na tutakuwa na jamii inayochukua hatua stahiki na zenye mantiki katika maaamuzi yake kutatua changamoto katika jamii.

Asanteni sana wadau na karibuni kwa michango, maoni na kunipigia kura.
 
Back
Top Bottom