UKWELI LAZIMA UJULIKANE
Na. M. M. Mwanakijiji
Hatimaye sakata la ununuzi wa rada liko karibu kuwatokea watu puani! Kampuni kubwa zaidi ya uundaji wa silaha na zana za kijeshi ya Uingereza BAE systems imedaiwa imemlipa dalali wa Uingereza malipo ya zaidi ya shiling bilioni 12 kwa kufanikisha kwake kuiwezesha serikali ya Tanzania kununua rada ya kijeshi ijulikanayo kama Plessey Commander Fighter Control System kutoka kwenye kampuni hiyo kwa gharama za shilingi Bilioni 40. Dalali huyo Bw. Sailesh Vithlani amekiri kuwa licha ya kulipwa malipo ya kawaida ya udalali ya shingili milioni mia tano sawa na asilimia moja ya mauzo hayo kitu ambacho kinakubalika katika biashara hiyo, alipokea pia malipo ya shilingi Bilioni 12 kupitia akaunti yake iliyofunguliwa huko Uswisi na alilipwa na kampuni tanzu ya BAE systems ili kuficha uhusiano wa malipo hayo na kampuni hiyo.
Siri hii imefichuliwa baada ya maofisa wa serikali ya Uingereza kwenda Tanzania na kufanya mahojiano na dalali huyo pamoja na mshirika wake wa kibiashara, mfanyabiashara mwingine wa Kitanzania Bw. Tanil Somaiya ambaye pia amekiri malipo hayo.
Bila ya shaka unashangaa kwanini nimesema Bw. Vithlani na dalali wa uingereza wakati vyombo vingine vya habari vinamuita ni Mtanzania? Ukweli wa mambo ni kuwa Vithlani siyo Mtanzania yeye ana passport ya Uingereza na kwa vile Tanzania haina uraia wa nchi mbili, mtu huyo ni raia wa Uingereza! Ukweli wa mambo mfanyabiashara huyo hakuhusika na ununuzi wa rada tu bali pia ununuzi wa ndege ya kisasa ya Gulfstream 550 inayotumiwa na Rais na pia manunuzi ya hivi karibuni ya helikopta na malori ya kijeshi!
Kwa mujibu wa Somaiya aliyezungumza na gazeti la The Guardian lililotoboa habari za uchunguzi huo kampuni ya BAE ilipanga malipo ya aina mbili, moja ni malipo ya asilimia moja ya bei ya mauzo na ya pili ni malipo ya siri ya asilimia 30! Hapa ndipo penye tatizo! Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali malipo ya asilimia moja ya mauzo katika biashara ya silaha ni ya kawaida ila hayo ya 30 yananuka rushwa iliyo dhahiri!!
Penye utata zaidi ni kukataa kwa Bw. Vithlani kukiri kama baada ya kupata malipo hayo huko Uswisi alimlipa mtu yeyote huko nyumbani Tanzania. Bw. Vithlani alikataa kufanya hivyo, na alipoulizwa kama alimlipa mtu yeyote kutoka kwenye akaunti hiyo nje ya nchi Bw. Vithlani alikataa kusema lolote. Kukataa kwa Bw. Vithlani kusema kama kuna mtu alilipwa nje ya nchi (awe ni mtanzania au vinginevyo) kunaishara mbaya kwa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa! Hapa ndipo wananchi wa Tanzania hatuna budi kupiga kelele ili ukweli ujulikane!
Jinsi mambo yalivyo, kampuni ya BAE imechunguzwa mara kadhaa kwa tuhuma za kutoa malipo kwa viongozi wa serikali na maafisa mbalimbali wa serikali duniani ili iweze kupata tenda za kuuza silaha au vyombo vya kijeshi. Zaidi ya kuchunguzwa kuhusiana na Tanzania Shirika hilo la BAE linachunguzwa pia kwa tuhuma za kulipa wanasiasa na maofisa wa serikali katika nchi za Chile, Cheki, na Romania na Afrika ya Kusini.
Kampuni hiyo ya BAE inadaiwa pia kuhusika na mipango ya aina hiyo na serikali ya Wasaudi, lakini Wasaudi wakaipiga mkwara serikali ya Tony Blair na uchunguzi dhidi yao ukafutwa.
Licha ya pingamizi toka Benki ya Dunia na vyombo mbalimbali ya kijamii ikiwemo Oxfam, na licha ya maombi ya Bunge la Uingereza kutaka kampuni ya BAE kupunguza bei ya rada hiyo, shirika hili lilishikilia uamuzi wake wa kuiuza kwa bei ya juu rada hiyo kwa Tanzania. Cha kushangaza zaidi ni kuwa serikali ya Tanzania ikiongozwa na Rais Mkapa walitetea kwa nguvu haja ya nchi yetu kuwa na rada hiyo ya kijeshi ambayo kwa kweli haikuhitajia au kuongeza usalama katika sekta ya kiraia. Kampuni ya BAE walipata kibali tarehe 20, 2001 toka Wizara ya Biashara na Viwanda ya Uingereza.
Kwa vile siri hii ndo imeanza kufichuka, tunapenda kwa niaba ya Watanzania wengi kusema yafuatayo.
1. Kwanza serikali ya Tanzania ione aibu kuwa hatimaye chombo cha nje kinaonesha kujali maslahi ya nchi yetu au hali yetu zaidi kuliko viongozi wetu tuliowachagua. Inakuwaje wazungu waoneshe kutujali zaidi yetu na kufunga safari kuhoji watu wetu kuhusu ununuzi wa rada hii. Hili linasikitisha. Inakuwaje tuweze kutumia shilingi bilioni 80 kununua vitu ambavyo kwa kweli si vya lazima na tungeweza kupata mbadala wake au ndio tunajaribu kununua gari la aina ya Maybach wakati gari linapoegeshwa ni kwenye nyumba ya kibanda cha nyasi! Gari linagharimu zaidi kuliko nyumba!!!
2. Serikali ya Rais Kikwete ialike wachunguzi toka nje ili waje kuendesha uchunguzi wa kwanini tulinunua rada hii, ni nani walihusika, na watu hao walinufaika vipi kwa manunuzi ya rada hiyo. Rada tuliyonunua haiangalii nchi nzima isipokuwa theluthi moja tu ya nchi yetu, wakati tungenunua rada ya kiraia kwa bei ya chini tungeweza kufanikisha lengo la usalama wa anga! Ni nani aliyeshawishi serikali kuendelea na manunuzi ya rada hii na mtu huyo alinufaika vipi? Je ni Bw. Vithlani? Kama yeye ni dalali bila ya shaka kuna mtu toka serikalini aliyempa ofa hiyo, ni nani huyo?!
c. Tunaitaka serikali ya Uingereza kufuatilia (monitor) akaunti za Bw. Vilathni na Somaiya ili kujua kama kuna malipo yaliyofanyika kwa mtu yeyote mwingine na hususan afisa au kiongozi wa serikali ya Tanzania. Habari ambazo KLH News imezipata na bado hazijathibitishwa ni kuwa kuna baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa serikali iliyopita na wengine waliopo madarakani hivi sasa ambao mara baada ya ununuzi wa rada hiyo walifunga safari kwenda nje ya nchi ambako walikatiwa gawiwo lao baada ya kufanikisha dili hilo. Inadaiwa watu hao wamefungua na wenyewe akaunti Uswisi na sehemu nyingine offshore ambako mifumo ya kodi ni ya siri. Watu wafuatao tunapenda wajitaje hadharani jinsi walivyoshiriki na kunufaika na mipango hiyo na kama wao, familia au jamaa zao wa karibu hawakupokea malipo yoyote yale toka BAE kupitia dalali huyo. Viongozi niwatajao wawe tayari kuruhusu akaunti zao za nje zichunguzwe na SFO na pesa zozote zilizoingizwa kwenye akaunti hizo zijulikane zimetoka wapi.
1.Rais Benjamin William Mkapa ambaye chini ya uongozi wake rada hii ilinunuliwa.
2.Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo na Rais wa sasa Bw. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alitetea ununuzi wa rada hiyo. Na hata jana ametetea.
3.Mwanasheria Mkuu wa Wakati huo Bw. Andrew John Chenge ambaye ni Waziri wa Miundo Mbinu wa sasa ambaye ofisi yake ilisimamia mkataba kati ya serikali na Bw. Saileth Vithlani
4.Prof. Mark Mwandosya aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi ambaye sasa ni Waziri wa Mazingira.
5.Maafisa (wanasheria na washauri) wa Wizara husika ambao walihusika na mikataba hiyo.
6.Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa wakati huo kwani rada hiyo ni ya matumizi ya kijeshi zaidi kuliko ya kiraia.
7.Maafisa na Wanasheria waliohusika katika majadiliano hayo. Na hasa kama ni maofisa hao hao walioshiriki katima manunuzi ya Ndege ya Rais, Helikopta za Bell na Malori ya kijeshi.
d. Siku hiyo kilipopatikana kibali cha kununua rada hiyo (yaani Disemba 20, 2001), Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania alidai kuwa upatikanaji wa rada hiyo utachangia katika ukusanyaji wa kodi kwa ndege zinazoruka katika anga la Tanzania na pia na utasaidia katika mapato ya utalii. Waziri huyo wa wakati huyo Bw. Jakaya Kikwete ambaye leo ndiye ni Rais atuambie je tumefanikiwa katika mambo hayo mawili? Yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alihusika vipi katika upatikanaji wa rada hiyo, alinufaika kwa namna yoyote ile binafsi?
e. Waziri wa Miundo Mbinu Bw. Andrew Chenge alikataa kuwa Tanzania inachunguzwa kuhusika na rushwa akidai kuwa taratibu zote za ununuzi wa rada hiyo zilifuatwa. Alidai kuwa maneno hayo ni "maneno ya wazungu". Ukweli wa mambo ni kuwa wakati rada hiyo inanunuliwa yeye alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tungependa tuelezwe yeye Bw. Chenge anawajua vipi kina Vithlani na Somaiya, na mkataba wa serikali kununua rada hiyo ulikuwa unawalipa watu hao kiasi gani? Pia atuambie maofisa walioshiriki katika majadiliano na madalali hao walilipwa kiasi gani? na Je kiongozi yeyote wa serikali akiwemo yeye mwenyewe walilipwa na madalali hao mara baada ya rada kununuliwa? Je ushahidi ukiletwa na kuoneshwa kuwa Bw. Chenge, Maafisa wa serikali na familia zao za karibu zilifungua akaunti nje zenye kiasi kikubwa cha fedha wako tayari kutueleza fedha hizo zimetoka wapi?
f. Uchunguzi wowote utakaofanywa matokeo yake yatangazwe hadharani, tumechoka na ripoti za ki spika!