Takukuru iieleze jamii namna inavyoshughulikia rushwa kubwa
Gloria Tesha
Daily News; Thursday,September 25, 2008 @20:00
HIVI karibuni, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea alizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema kuwa kazi ya kupambana na rushwa ni ngumu na inahitaji uangalifu mkubwa.
Pia alisema hakuna faida ya kuwa fisadi wakati unamchunguza fisadi kutokana na tuhuma mbalimbali alizozipata kupitia vyombo vya habari, kwamba yeye ni fisadi.
Maneno hayo aliyasema baada ya kuulizwa maswali na waandishi hao wakitaka kujua kazi alizozifanya katika kipindi cha miaka miwili cha ukurugenzi katika chombo hicho na namna anavyoshughulikia kesi kubwa za rushwa.
Aidha, wakati akitoa ufafanuzi wa maswali hayo pamoja na mengine mengi, Hosea alisema jamii inashindwa kuelewa kuwa sheria haibagui rushwa ndogo na kubwa, bali rushwa ni rushwa mbele ya sheria isipokuwa tofauti inakuwapo katika namna uchunguzi unavyofanyika na hatua zinavyochukuliwa.
Namna mkurugenzi huyo alivyofafanua kuhusu uchunguzi wa kesi kubwa za rushwa unavyofanyika, ikiwa ni pamoja na muda wa kukamilika, ni dhahiri kwamba mafanikio ya kushughulikia kesi kubwa tano kati ya 10 zilizopangwa kuchunguzwa na Takukuru kwa mwaka ni ya kujivunia.
Nikinukuu maneno ya Dk. Hosea, kesi hizo ambazo hakuwa tayari kuzitaja, zipo kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) na mbili kati yake zimerudishwa Takukuru kwa ajili ya marekebisho madogo, kesi hizo zinahusu rushwa katika mikataba ya madini, kutumia mamlaka vibaya na kushindwa kusimamia sheria.
Pamoja na mafanikio hayo yaliyoelezwa na Dk. Hosea bado elimu na uwazi zaidi kuhusu namna kesi hizo zinavyoshughulikiwa unahitajika kwa jamii.
Ule ufafanuzi kwa wanahabari wale kuwa kesi za rushwa kubwa zinaitwa kubwa kutokana na kuvuka mipaka ya nchi, suala husika kupigiwa kelele sana katika jamii pamoja na kumhusu mtu maarufu na endapo imehusisha kiwango kikubwa cha fedha na inaangaliwa namna ilivyoathiri uchumi wa nchi, hautoshi, kwa suala hilo kueleweka kwa jamii.
Nadhani somo alilolitoa Hosea linahitajika kwa jamii nzima, siyo wakati wa kusubiri kuandikwa katika vyombo vya habari ndiyo kutoa ufafanuzi wa namna kesi hizo zinavyoshughulikiwa, ni wazi kama utaratibu wa kuwaelimisha watu namna wanavyoshughulikia kesi hizo wangeutoa mapema, jamii isingekuwa na sababu ya kudhani mafisadi hawashughulikiwi.
Muda wa kutafuta vielelezo na kujiridhisha kwamba kuna kesi ya kupeleka mahakamani ni wazi unahitajika, lakini pia ikumbukwe kuwa jamii inapaswa kuelewa hatua zinazochukuliwa ili kuepuka kudhaniwa visivyo, mambo haya yaende pamoja.
Sipingani na alichosema mkurugenzi wa Takukuru, kwamba upo ugumu wa kushughulikia masuala ya rushwa hata kufikia wanaoshughulika kudhaniwa kuwa nao ni mafisadi, kwa kuwa mafanikio hayaonekani mapema.
Malalamiko ya wengi ni kwamba Sheria ya Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 katika vifungu vyake bado inabana, lakini kama akina Zephania Musendo walidaiwa kubainika, vipi hayo mapapa?
Ni wakati sasa umefika kwa Takukuru pamoja na kauli nzuri kwamba kuna faida gani ya kuwa fisadi wakati unachunguza mafisadi, wakimaanisha kwamba wao siyo mafisadi, ionekane kwa vitendo. Watanzania wanatamani kuona na kusikia wanaoliingizia taifa hili hasara wanafikishwa mahakamani na wanashughulikiwa ipasavyo. Kila la heri Takukuru.